Home » » MASWALI YA TUNDU LISSU YAMPA KIGUGUMIZI KATIBU WA CCM.

MASWALI YA TUNDU LISSU YAMPA KIGUGUMIZI KATIBU WA CCM.




Mbunge wa jimbo la Singida Mashariki, Mh.Tundu Lissu akiwa na wapambe wake nje ya mahakama ya mkoa, mahali kesi yake ya kupinga matokeo yaliyompa ubunge inasikilizwa.
Badhi ya wasikilizaji wa kesi ya Mh. Tundu Lissu wakiwa wamejazana katika madirisha ya mahakama ya mkoa wa Singida kusikiliza kesi hiyo.(Picha zote na Nathaniel Limu).
Na. Nathaniel Limu
‘MVUA’ ya maswali katika kesi ya mlalamikiwa wa kwanza  Tundu Lissu  ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi wa ubunge wa jimbo la Singida Mashariki, yamesababisha aliyekuwa Katibu wa CCM Singida vijijini, Cosmas Kasangani, kupandwa na hasira na  kushindwa kujibu maswali ipasavyo.
Ilimlazimu Wakili  Godfrey Wasonga aliyewasilisha maombi ya kupinga ushindi wa Tundu, aiombe mahakama kuu inayosikiliza kesi hiyo, imruhusu ampe mteja wake ushauri nasaha ili aweze kuacha woga na hasira,kitendo ambacho kingeharibu lengo lao la kutaka matokeo ya uchaguzi  ushindi huo utenguliwe.
Baada ya Mahakama Kuu kukubali ombi hilo, Wasonga alimfuata Kasangani kizimbani na kumpatia ushauri nasaha  ambao ulizaa matunda kwa shahidi huyo, kutulia na kuanza kujibu maswali ya Tundu Lissu.
Aidha, Jaji Mosses Mzuna anayesikiliza kesi hiyo, alimtoa hofu Kasangani ambaye kwa sasa ni Katibu wa CCM Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, kwamba endapo atachoka kusimama, anaweza akawa anajibu maswali akiwa ameketi na pia anaruhusiwa kunywa maji, wakati wo wote.
Kasangani ambaye ni shahidi wa  10 katika kesi hiyo inayovuta hisia za wakazi wengi wa Mkoa wa Singida, katika kikao cha juzi alianza kutoa ushahidi wake akiongozwa na wakili wa CCM, Wasonga.
Kasangani ambaye alikuwa akitoa ushahidi wake kwa kujiamini, aliiomba mahakama kuwa mlalamikiwa wa kwanza Tundu Lissu alikuwa na mawakala 10 kila kituo cha kupigia kura, jambo ambalo ni kinyume na taratibu za uchaguzi.
Akifafanua zaidi,alisema katika vituo 124 vya jimbo la Singida mashariki, Tundu alikuwa na mawakala watano ndani ya kila kituo na wengine watano nje ya kituo.
Kasangani alisema katika barua za wakala hao wa Tundu ambazo alifanikiwa kuzinasa, zilikuwa za kutoka vyama vya TLP, NCCR – Mageuzi, APPT maendeleo, CUF na CHADEMA.
Alisema barua hizo zilikuwa zinafanana mno karibu kwa kila kitu na kuonekana dhahiri zimeandaliwa na kuandikwa na mlalamikiwa wa kwanza, Tundu Lissu
Katibu hyo wa CCM  aliiambia mahakama hiyo iliyofurika wasiklizaji, kuwa vyama vya siasa vya TLP, NCCR – Mageuzi, APPT maendeleo havikuwa na mgombea ubunge katika jimbo la Singida mashariki, kwa hivyo havikustahili kuweka mawakala.
Barua hizo zilizoandikwa kwa anuani ya vyama vya TLP, APPT maendeleo, NCCR Mageuzi, CUF na CHADEMA, zilisababisha mabishano makali ya kisheria kati ya mlalamikiwa kwa kwanza Tundu Lissu akisaidiwa na mawakili watatu, ambao wanasimamia mwanasheria mkuu wa serikali na msimamizi wa uchaguzi na wakili wa waleta maombi.
Tundu na wenzake walikuwa wanapinga barua hizo kupokelewa na mahakama kuu kama vielelezo katika kesi hiyo, kwa madai hazikubaliki kisheria.
Hata hivyo, wakili wa waleta maombi, Wasonga aliweza kushinda katika mabishano hayo na mahakama kuu ikazipokea barua hizo na kuwa vielelezo halali katika kesi hiyo.
Katika hatua nyingine wakati kesai hiyo inaendelea, jaji Mzuna alikemea tabia iliyojitokeza kwa mawikili hao  kuanza kutupiana vijembe kwa kutumia lugha ambayo haikubaliki kisheria.
Baada ya hapo, Tundu Lissu alianza kumuuliza shahidi Kasangani maswali kama ifuatavyo:-
Tundu, Shahidi katika barua hizo ulizo nazo, hebu angalia ya kwanza kama imeandikwa kwa kalamu au imeandikwa kwa mashine.
Kasangani; zimeandikwa kwa mashine na sio kwa mkono.
Tundu, Je barua ya kwanza ni ya chama gani na ina jina la Tundu Lissu mahali popote au saini yake?
Kasangani; barua hii ni ya APPT maendeleo, haina jina lako wala saini yako.  Isipokuwa ina saini ya Selemani Alli Ntandu, Katibu wa chama hicho.
Tundu; shahidi hebu angalia vizuri barua ya pili inayofuata, mwambie jaji ni ya chama gani na imeandikwa kwa kalamu au mashine.
 Kasangani, mheshimiwa jaji, barua hii ni ya TLP, imeandikwa kwa mashine na imesaini na katibu wa TLP wilaya Athumani Nkii.
Tundu; Je shahidi, barua hiyo ya TLP ina jina au saini yangu mahali popote?
Kasangani, Haina.
 Barua zote zilizokuwa zinalalamikiwa na Kasangani kuwa ziliandikwa na Tundu Lissu kwa lengo la kujipatia ushindi, hazikuwa na jina la Tundu na zote ziliandikwa kwa mshine/kompyuta.
 Aidha, katika ushahidi wake Kasangani,alisema askari polisi D. 9979 Paulo aliyekuwa anasimamaia kituo kimoja katika kijiji cha Ikungi, aliacha kazi yake na kuanza kumpigia kampeni Tundu siku ya kupiga kura (31/10/2010).
 Tundu alimpatia Kasangani shahada kutokakwa mkuu wa polisi nchini Saidi Mwema na ya Kamanda wa polisi mkoa wa Singida, Celina Kaluba ambazo zote zinampongeza polisi huyo, kwa utumishi wake uliotukuka.
 Baada ya Kasangani kuzisoma kwa sauti, Tundu alimuuza, je kati yako na  mkuu wa polisi nchini Saidi Mwema, nani anamfahamu au anafahamu zaidi utendaji kazi wa askari D.9979 Pulo?.
Kasangani, alinyamaza kwa muda na baada ya kukazaniwa na Tundu, alijibu kwa kifupi,‘sijui’.
Wakati Tundu akiendelea kuporomosha mvua ya maswali ya Kasangani, Kasangani alimwomba jaji Mzuna kwamba amechoka na hawezi tena kuendelea kujibu maswali.
Jaji Mzuna, alimwambia kuwa avumilie na kuendelea na kazi ya kujibu maswali ili kazi hiyo iishe siku hiyo.Alimtaka akae kwenye fomu kama amechoka kusimama.
Hata hivyo, Kasangani amabye kwa wakati huo alionyesha wazi kuishiwa pumzi, alisisitza kuwa hana nguvu tena nguvu ya kuendelea kujibu maswali.
Kesi hiyo iliahirishwa na (jana) (30/3/2012) saa tatu asubuhi, ilitarajiwa kuendelea kwa Kasangan kujibu maswali yaTundu Lissu.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa