MH. TUNDU LISSU AFANANISHA KESI YAKE NA MKASA WA YOHANA MBATIZAJI.


Mbunge wa jimbo la Singida Mashariki kupitia Chama cha CHADEMA Mh. Tundu Lissu (mwenye fimbo) akiingia kwenye viwanja vya kituo cha zamani cha mabasi mjini Singida kwa kuhutubia wananchi.
Mbunge wa jimbo la Singida Mashariki (CHADEMA) muda mfupi kabla hajaanza kuhutubia wakazi wa jimbo la Singida mjini. Wa kwanza kulia ni mke wake.
Mbunge wa viti maalum kupitia Chama cha CHADEMA na ambaye ni mdogo wake Tundu Lissu Christina Mughwai, akisalimia mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara ulioitishwa kwa ajili ya Tundu.
Mbunge wa jimbo la Singida Mashariki (CHADEMA) Mh. Tundu Lissu akihutubia wakazi wa jimbo la Singida mjini.
Mbunge wa jimbo la Singida Mashariki (CHADEMA) Mh. Tundu Lissu (waliosimama mwenye kofia) akitoa salamu ya CHADEMA ya ‘peoples power’. (Picha zote na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Mbunge wa jimbo la Singida Mashariki (CHADEMA) Mh. Tundu Lissu, amedai kwamba zaidi ya shilingi milioni 200, zimetumika kugharamia kesi ya ‘kuunga unga’ ambayo ililenga kutafuta kichwa chake kama ilivyokuwa kwa Yohana Mbatizaji.
Bila kufafanua kuwa kichwa chake kilikuwa kikitafutwa kikiwa kimetenganishwa na kiwiliwili au kikiwa hakijatenganishwa na kiwili wili chake, amesema kati ya kesi 14 zilizofunguliwa katika mahakama tofauti nchini, kwa ajili ya kutengua matokeo ya wabunge wa CHADEMA ya kwake ilikuwa kubwa zaidi na ndio maana haikupewa umuhimu unaostahili  na vyombo vya habari.
Hata hivyo, hakufafanua au kueleza iwapo hivyo vyombo vya habari navyo vilinufaika na kiasi hicho cha shilingi milioni 200 ambazo zililenga kumwangamiza kisiasa.
Tundu amesema wana-CCM hao ambao ni wakulima wa kawaida, wametumiwa na wahusika walikuwa wakimwaga fedha ili kufanikisha azma zao ya kumng’oa katika nafasi yake  ya ubunge, lakini fedha zote zimeliwa bila kufanikisha lengo.
Aidha, alisema kuwa aliyekuwa katibu mkuu wa CCM Yusufu Makamba, aliwahi kutoa waraka kuwa katika majimbo yote yaliyochukuliwa na vyama vya upinzani,wahusika walioshindwa,wafungue kesi mahakamani.
Habari kwa Hisani ya Mo Blog

PICHA NA HABARI: CHADEMA KUPITIA MH. TUNDU LISSU YAIBUKA KIDEDEA KESI YA UBUNGE SINGIDA MASHARIKI.


Wakili wa waleta maombi Wanaccm Godfrey Wasonga akitafakari kwa hisia kali muda mfupi kabla ya kesi ya kupinga matokeo yaliyompa ubunge Tundu Lissu hayajatangazwa.

Mbunge wa jimbo la Singida mashariki CHADEMA),Tundu Lissu,muda mfupi baada ya mahakama kuu kutupilia mbali maombi yaliyotolewa na Shaban Selema na Pascal Halu wa CCM,kupinga matokeo yaliyompa ushindi wa ubunge.
Mbunge wa jimbo la Singida mashariki (CHADEMA) Tundu Lissu akifutwa machozi na mke wake wakati wakitoka nje ya mahakama baada ya mahakama kuu kutangaza kuwa ushindi wake huo,ni halali.
Baadhi wa watu waliohudhuria kusikiliza kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Tundu kuwa mbunge muda mfupi baada ya maamuzi hayo kutolewa.(Picha zote na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Mbunge wa jimbo la Singida mashariki (CHADEMA)Tundu Lissu imeigaragaraza vibaya CCM baada ya mahakama kuu kutupilia mbali hoja 11 zilizowasilishwa na waleta maombi wawili wanachama wa CCM za kutaka kutengua ushindi wake wa ubunge kwa madai kuwa, alikiuka sheria na taratibu za uchaguzi na kusababisha uchaguzi huo kutokuwa huru na wa haki.
Shabani Selema na Pascal Halu wote wanachama wa CCM na wakazi wa kijiji cha Makiungu tarafa ya Mungaa jimbo la Singida Mashariki, walifungua kesi ya kupinga matokeoa yaliyompa ushindi Tundu kwenye uchaguzi mkuu uliopita.
Jaji Mosses Mzuna wa makahama kuu Moshi mjini mkoa wa Kilimanjaro, katika kutoa hukumu hiyo, amesema ushahidi uliotolewa na upande wa waleta maombi, umeshindwa kuthibitisha bila kuacha shaka yo yote kuwa, mlalamikiwa wa kwanza, wa pili mwanasheria mkuu wa serikali na wa tatu msimamizi wa uchaguzi, kuwa walivunja/kiuka  sheria, taratibu na kanuni za uchaguzi na kusababisha uchaguzi huo kutokuwa huru na wa haki.
Akitoa maamuzi ya makahama, amesema kuwa katika hoja zote 11 zilizoletwa na waleta maombi hao, ushahidi wote ni wa kuhisi, kusikia  na kushuku, ambao hauna uhalisia wa mambo yaliyowasilishwa.
Jaji Mzuna amesema kuwa mahakama yo yote haiwezi kutegua matokeo ya uchaguzi kwa kuambiwa maneno matupu bila ya maneno husika kuthibishwa kwa ‘document’ husika.
Amesema ushahidi wa upande wa walalamikaji pia umekuwa ni kama kinyonga, mara kwa mara ulikuwa ukukigeuka geuka.
Akifafanua zaidi, Mzuna ametaja  baadhi ya hoja ambazo zililetwa na waleta maombi kuwa ni mlalamikiwa Tundu kuandaa barua tano zinazofanana kwa mawakala wa CUF, TLP, AAPT Maendeleo, NCCR -Magezui na CHADEMA, kwa lengo la kujinufaisha katika zoezi la uchaguzi mkuu.
Ametaja hoja nyingine kuwa Tundu aliwapa chakula mawakala wa chama chake na wa vyama vingine isipokuwa wa chama cha CCM, kitendo ambacho kiliashiria ni hongo ili mawakala wasiokuwa wa chama chake nao wampigie kura.
HABARI KWA HISANI YA MO BLOG

TUNDU LISSU ASHINDA KESI YA KUPINGA UBUNGE WAKE

 

  • Hoja zote za upande wa mlalamikaji zatupwa.
  • Maofisa Jeshi pamoja na kikosi maalum waudhulia maakamani.

Mbunge
wa Singida Mashariki kwa tiketi ya CHADEMA, Tundu Lissu, ameshinda kesi
iliyofunguliwa dhidi yake mjini Singida kupinga ushindi uliomweka
madarakani

Hukumu
imetolewa na Jaji Moses Mzuna anayetoka mahakama kuu kanda ya
Kilimanjaro, iliyofunguliwa na makada wawili wa CCM, Shabani Itambu na
Pascal Hallu.
 
Leo
mahakamani wafuasi wa vyama mbalimbali vya siasa, wananchi wa Singida,
na waandishi wa habari walijitokeza kwa wingi sana katika eneo la
mahakama.


Idadi
ya Polisi pia ilikuwa kubwa, ndani na nje ya mahakama.Kilicho kuwa cha
ajabu kidogo leo getini maofisa wote wakubwa wa jeshi la polisi
walikuwepo pale na kikosi maalumu kwa ajili ya kukagua kila anayeingia
mahakamani,  kila mtu aliyekuwa anaingia mahakamani alipekuliwa hadi
wabunge waliokuja kusikiliza kesi hiyo.


Akisoma
hukumu Jaji Moses Mzuna alisema “HOJA YA TISA, Kama Mgombea wa
walalamikaji (CCM) alikataa kusaini matokeo. Hoja hii haipaswi
kunipotezea muda sana. Njau hakuhudhuria, aliwakilishwa na mlalamikaji
wa kwanza ambaye alikataa kusaini matokeo.


Wakili
wa serikali alisema, kukataa pekee kusaini matokeo hakusaidii kutengua
matokeo. Hivyo hata hoja ya tisa naitupilia mbali. Haikuwa sahihi.

Hoja
ilitolewa hapa, kuwa mawakala walikula kiapo kwa hakimu. Walalamikaji
walisema kuwa walipaswa kula kiapo kwa msimamizi wa uchaguzi. Je
kuapishwa na hakimu kunabatilisha matokeo?


Hoja
zilizotolewa na mawakili wa serikali walisema Hakimu ana mamlaka ya
kutoa viapo. Binafsi nasema kuwa waliotunga sheria hawakumaanisha kuwa
Mahakimu hawaruhusiwi kuapisha mawakala, vinginevyo kungekuwepo fomu ya
hakimu tu. Lakini fomu zinaonyesha hakimu, Msimamizi wa uchaguzi na
Msimamizi msaidizi, fomu inatambulika kisheria, kwa sheria ya Uchaguzi.
Hii haihusiani na zoezi la uchaguzi.


Katika kesi ya Prince bagenda Vs Wilson masilingi, katika kesi hii mawakala walifanya kazi bila kuapishwa, na ilichukuliwa kuwa sehemu ya kutengua uchaguzi, angalia pg 240.


Kwa
lugha yake jaji alisema hawakuwa na mamlaka halali, lawful mandate,
lakini ilisaidia kutengua, na mwanasheria wa serikali alihusika katika
hili.


Maelezo
hayo yanatofautiana na kesi iliyo mbele yangu, jimbo la Singida
mashariki mawakala walikula kiapo, na walikuwa na mamlaka halali. Hivyo
hoja hii naitupilia mbali


HIVYO, UCHAGUZI ULIKUWA WA HAKI, NA TUNDU LISSU NI MBUNGE HALALI NA UCHAGUZI ULIKUWA HURU NA WA WA HAKI, HIVYO SIWEZI KUTENGUA.


Walalamikaji
wa kesi hiyo, iliyofunguliwa mahakama kuu kanda ya Dodoma, walikuwa
wanatetewa na wakili Godfrey Wasonga, kutoka mkoani Dodoma, huku Lissu
akijisimamia mwenyewe.


Kesi
hiyo ilianza kusikilizwa Machi 12, 2012, kufuatia makada wawili wa CCM,
kupinga ushindi wa Lissu kwa madai kuwa uchaguzi huo uligubikwa
na dosari nyingi.


Awali
Katika mahojiano na Lissu, alisema vyovyote mahakama itakavyo
hukumu, anajivunia kuimarisha demokrasia na kuwa mbunge wa kwanza
kutoka upinzani, kwenye historia ya mikoa ya kanda ya kati.Habari kwa Hisani ya Media 2 Solution Blog

Hukumu Ya Tundu Lissu leo Ijumaa

 Na Elisante John
Singida,

KESI inayomkabili mbunge wa Singida mashariki kwa tiketi ya CHADEMA, Tundu Lissu, iliyofunguliwa mjini Singida kupinga ushindi uliomweka madarakani, itatolewa leo ijumaa (Aprili 27, mwaka huu).
Hukumu itatolewa na Jaji Moses Mzuna, anayesikiliza kesi hiyo, iliyofunguliwa na makada wawili wa CCM, Shabani Itambu na Pascal Hallu.
Kesi hiyo imekuwa kivutio sana kwa wananchi wengi wa mkoa Singida na nchini kwa ujumla, kutokana na umaarufu wa mbunge huyo machachari.
Jaji anayesikilia shauri hilo mjini Singida, anatoka mahakama kuu kanda ya Kilimanjaro.
Walalamikaji wa kesi hiyo, iliyofunguliwa mahakama kuu kanda ya Ddoma, wanatetewa na wakili Godfrey Wasonga, kjtoka mkoani Dodoma, na Lissu amejisimamia mwenyewe.
Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Machi 12, 2012, kufuatia makada wawili wa CCM, kupinga ushindi wa Lissu kwa madai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na dosari nyingi.
Katika mahojiano na Lissu, amesema vyovyote mahakama itakavyo hukumu, anajivunia kuimarisha demokrasia na kuwa mbunge wa kwanza kutoka upinzani, kwenye historia ya mikoa ya kanda ya kati.
Amesema, kanda hiyo ilijulikana sana kuwa ngome ya CCM, lakini amefanikiwa kuchaguliwa na wananchi ili awatumikie.

BODI ZA ZABUNI SINGIDA ZATAKIWA KUZINGATIA SHERIA YA UNUNUZI WA UMMA YA MWAKA 2004.


Mwanasheria Mwandamizi wa PPAA Esthery Nyagawa akitoa mada yake kwenye warsha iliyohudhuriwa na wazabuni, wahasibu na maafisa ugavi (hawapo kwenye picha) iliyohusu  utatuzi wa migogoro katika ununuzi wa umma chini ya sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2004 na sheria mpya ya mwaka 2011.
 Baadhi ya wazabuni, maafisa ugavi kutoka serikalini na wahasibu waliohudhuria warsha iliyohusu utatuzi wa migogoro katika manunuzi ya umma. (Picha zote na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Mwanasheria Mwandamizi wa mamlaka ya rufaa za zabuni za umma (PPAA) Esthery Nyagawa, amezihimiza bodi za zabuni kuwa makini wakati wa uteuzi wa zabuni ili kujijengea mazingira mazuri ya kuteua mzabuni ambaye atatoa huduma bora inayofanana na thamani ya fedha atakazolipwa.
Nyagawa ametoa changamoto hiyo wakati akitoa mada yake ya matatizo yaliyiokithiri katika  ununuzi wa umma, ambayo husababisha malalamiko kutoka kwa zabuni.
Amesema baadhi ya bodi za zabuni, zimekuwa zikiteua wazabuni wasiokuwa na sifa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutokuwa makini  na hivyo  kuisababishia serikali au taasisi ya umma, kupoteza fedha nyingi.
Mwanasheria huyo amesema jambo la msingi ni bodi za zabuni kuzingatia sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2004, inayoelekeza jinsi mchakato wa ununuzi wa umma unavyopaswa kuendeshwa.
Katika hatua nyingine, Nyagawa amewataka wazabuni wasikubali kuanza utekelezaji wa mkataba, bila ya kuwa na mkataba.
Aidha, amesema wazabuni wanalo jukumu kubwa lakutoa taarifa juu ya matatizo wanayokumbana nayo wanaposhiriki kwenye zabuni za serikali na taaisisi zake, ili yaweze kufanyika na kushughulikiwa ipasavyo.
Mwanasheria huyo mwandamizi, ametoa mada hiyo kwenye warsha kuhusu utatuzi wa migogoro katika ununuzi wa umma chini ya sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2004 na sheria mpya ya mwaka 2011.
Warsha hiyo ilihudhuriwa na wazabuni wa huduma mbalimbali, wakuu wa taasisi za umma, maafisa ugavi wa serikali na wahasibu. 

WAJASIRIAMALI SINGIDA WANUFAIKA NA MRADI WA KUWEZESHA BIASHARA.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Parseko Kone (kushoto) akitembelea maonyesho ya wajasiriamali mara baada ya kufungua sherehe za utoaji zawadi kwa washindi wa mashindano ya mpango huo zilizofanyika katika ukumbi wa chuo cha FDC mjini Singida.
Na.Mwandishi wetu
Akiongea Mkuu wa mkoa amesema kuwa washiriki hao walinufaika na mtaji wa Sh. 2,800,000, BDG ilitumia kigezo cha ustawi wa biashara na uandishi mzuri wa michanganuo katika kuwapatia wajasiriamali hao fedha hizo.
Aidha amesema tangu mpango huo uanzishwe mwezi Agosti 2008, umewapatia wajasiriamali nchini, mtaji wenye thamani ya Sh. Bilioni 15 hadi kufikia Agosti mwaka jana.
Kone amepongeza wajasiriamali hao ambao jumla yao ni watu 64, kwa kushinda na kufanikiwa kupeleka fedha hizo mkoani Singida, ambazo amesema anaamini zitasaidia kuongeza mzunguko wa fedha.
 Habari kwa Hisani ya Mo Blog

WANANCHI WA SINGIDA WATAKIWA KUJENGA UTAMADUNI WA KUPANDA MITI WAKATI WOTE.



Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Compassion International Tanzania Mchungaji Joseph Mitinje akipanda mti kwenye viwanja vya kanisa la FPCT kisaki nje kidogo ya mji wa Singida.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Compassion International Tanzania (CIT) Mchungaji Joseph Mayala Mitinje, amewahimiza Watanzania kujenga utamaduni wa kupanda miti wakati wote badala ya kusubiri April mosi siku ya upandaji miti.
Mchungaji Mitinje ametoa wito huo wakati akishiriki kupanda miti kwenye viwanja vya kanisa la FPCT la kata ya Kisaki Manispaa ya Singida ambapo amesema kila mtu hivi sasa ni shahidi mzuri wa madhara yatokanayo na uhaba wa miti nchini.
Mitinje amesema baada ya miti kuvunwa ovyo, upatikanaji wa mvua sasa umekuwa adimu huku  vyanzo vya maji vinaendelea kukauka na miti kwa matumizi ya binadamu nayo imekuwa ya shida katika upatikanaji wake.
Katika hatua nyingine, Mchungaji Mitinje, amewataka waumini wa kikristo na wananchi kwa ujumla, kutunza miradi ya maji inayoanzishwa katika maeneo yao na wafadhili, serikali na taasisi mbali mbali ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Amesema lengo la miradi hiyo ambayo inagharimu fedha nyingi mno,ni kuiunga serikali mkono katika juhudi zake za kupunguza/kuondoa tatizo la uhaba wa maji kwa wananchi wake.
Mkurugenzi huyo alikuwa katika ziara ya siku moja ya kikazi ya kuziundua visima virefu viwili vya maji viivyochimbwa katika kanisa la 814 FPCT Kisaki na 901 KLPT Singida mjini.
Kwa mujibu wa Mchungaji Mitinje visima hivyo vimegharimu zaidi ya shilingi 80.6 milioni.

MATAMASHA YA MICHEZO SINGIDA YATAKIWA KUELEKEZWA HADI NGAZI ZA VIJIJINI.


Katibu Tawala mkoa wa Singida Liana Hassan akizungumza kwenye hafla ya kufunga mafunzo ya makocha wa michezo mbalimbali (hawapo kwenye picha) kutoka baadhi ya shule za sekondari za mkoa wa Singida. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) mkoani Singida Allan Jumbe. Wa kwanza kushoto ni Mratibu wa Mradi wa Elimu kupitia michezo (TTU)mkoa wa Singida Anord Bugado na wa kwanza kulia ni Katibu CWT mkoa wa Singida Said Mselemu.
 Katibu Tawala mkoa wa Singida Liana Hassan akimkabidhi cheti mmoja wa walimu wa shule za sekondari waliohudhuria mafunzo ya siku saba ya michezo mbalimbali. (Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Katibu Tawala mkoa wa Singida Liana Hassan ameagiza matamasha ya michezo mbalimbali yaelekezwe hadi ngazi ya vijijini ili pamoja na mambo mengine, wakazi wa maeneo hayo waweze kupata fursa ya kuibua vipaji vyao.
Hassan ametoa changamoto hiyo wakati akizungumza kwenye hafla ya kufunga mafunzo ya makocha wa michezo mbalimbali wa shule za sekondari za mkoa wa Singida.
Amesema kumekuwa na mazoea yasiyopendeza ya kufanyia matamasha ya michezo sehemu za mijini  tu kitendo ambacho kimekuwa kikiwanyima wakazi wa vijijini fursa mbali mbali ikiwemo kuibua vipaji vyao.
Kwa upande wa serikali ya mkoa wa Singida,katibu tawala huyo,alisema imejipanga vizuri kwa lengo la kuhakikisha michezo inautangaza mkoa kikamilifu.
Hassan amesema kupitia uongozi wa mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone, mkoa unaendelea kuiandaa shule ya sekondari ya Mandewa manispaa ya Singida ili ianze kupokea wanafunzi wenye vipaji vya michezo kutoka sehemu mbalimbali za mkoa.
Mafunzo hayo ya siku saba yaliyofanyikia kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya chama cha walimu mkoa wa Singida, yaliandaliwa na mradi wa elimu kupitia michezo kwa shule za sekondari (TTU) za mkoa wa Singida.
Mradi huo unafadhiliwa asilimia 75 na Wizara ya Mambo ya Nje ya serikali ya Finland kupitia shirika lisilo la kiserikali la LiiKe.

Mtumishi wa Usalama Taifa ajinyonga



Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida,
Celina Kaluba
Mtumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa mkoa wa Singida amejinyonga hadi kufa, akiwa kwenye eneo lake la kazi, kwa kutumia shuka.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida, Celina Kaluba, alimtaja mtumishi huyo kuwa ni Azaria Mbaga (47), mkazi wa Sabasaba mjini Singida.

Kamanda Kaluba alisema kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 9, mwaka huu saa 8:30 usiku katika kibanda kinachotumiwa na walinzi wa ofisi hiyo, iliyopo eneo la Bomani, mjini Singida.

Alisema kuwa, muda mfupi baada ya kujinyonga, wenzake walifanikiwa kuuona mwili wake ukiwa umening’inia ndani ya banda hilo, majira ya saa 9:30 usiku, na kutoa taarifa kituo cha Polisi.




Kaluba alisema marehemu katika miaka ya nyuma, aliwahi kuugua maradhi ya akili na kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ambako alipatiwa tiba na kupona.


”Marehemu siku kama tatu au nne hivi, kabla ya kujinyonga, alionekana kama vile amechanganyikiwa, nadhani hali hiyo ilikuwa dalili za kumsababishia ajiue kwa kujinyonga,” alisema Kaluba.


Alisema chanzo kamili cha kujinyonga kwake, hakijafahamika, lakini upelelezi zaidi kuhusiana na tukio hilo unaendelea.

CHANZO: NIPASHE

RAIS JAKAYA KIKWETE ATOA ZAWADI YA PASAKA KWA WAZEE WA KAMBI YA SUKAMAHELA WILAYANI MANYONI.

 Katibu tawala mkoa wa Singida (kulia) akikabidhi mbuzi watatu wakiwa ni zawadi kutoka kwa Rais Kikwete kwa wazee wasiojiweza wa kambi ya Sukamahela wilayani Manyoni.
 Katibu tawala mkoa wa Singida Liana Hassan (kulia) akikabidhi dumu la mafuta ya alizeti moja ya zawadi zilizotolewa na Rais Kikwete kwa wakazi wa kambi ya wazee ya Sukamahela.
 Katibu tawala mkoa wa Singida Liana Hassan (kulia) akimvisha shati mmoja wa wakazi wa kambi ya wazee ya Sukamahela.
 Katibu tawala mkoa wa Singida,Liana Hassan akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi zawadi zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete, kwa wakazi wa kambi ya Sukamahela wilayani Manyoni.Kushoto ni mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Manyoni,Fotunata Malya na anayefuata ni mke wa Ras, Liana Hassani.
Mkazi wa kambi ya wazee wasiojiweza ya Sukamahela wilayani Manyoni Kareudia Madoli akitoa shukurani kwa niaba ya wenzake kwa Rais Kikwete kwa msaada wake kwa ajili ya sherehe ya pasaka.Picha zote na Nathaniel Limu
---
Katibu tawala mkoa wa Singida,Liana Hassan amewahimiza  wakazi mkoani humo kujenga utamaduni wa kusaidia makundi ya watu wenye mahitaji ili pamoja na mambo mengine kuwapunguzia makali ya maisha.
Liana ametoa wito huo wakati akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi zawadi mbalimbali zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete, kwa wakazi wa kambi ya Sukamahela wilayani Manyoni.Msaada huo ni kwa ajili ya wakazi hao, kusheherekea pasaka.



Alisema upo umuhimu mkubwa kwa wakazi mkoani humo, kutambua kwamba wana wajibu wa kusaidia kwa hali na mali,makundi mbalimbali yenye mahitaji wakiwemo wazee wasiojiweza.



“Kwa hiyo ndugu zangu nawaombeni sana tumuunge mkono rais wetu Kikwete katika kuyasaidia makundi haya.Mwaka jana rais Kikwete alitoa msaada kwa watoto waishio kwenye mazingira magumu cha kituo cha Kititimo, na leo hii anawasaidia wakazi wa kambi hii ya Sukamahela”,alisema na kuongeza;“Hebu kila mmoja wetu kwa kadri ya uwezo wake utakavyomuruhusu,tumuunge rais kwa kuyasaidia makundi haya wakati wa sherehe mbalimbali na hata siku za kawaida”.



Awali afisa jamii mfawidhi wa makazi ya Sukamahela,Fredrick Mbyoya alitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili kambi hiyo, kuwa ni uhaba wa maji,wakazi hawajapata mavazi kwa muda mrefu na watoto wanaosoma Day care centre,shule ya msingi na sekondari,hawana viatu,sare,madaftari na kalamu.Kwa mujibu wa Mbyoya, kituo hicho kina wakazi 73 na nyumba za kuishi 54.



Zawadi zilizotolewa na rais kwa wakazi wa kambi ya Sukamahela, ni mchele kilo 112,lita 40 za mafuta ya alizeti na beberu (mbuzi) tatu wakubwa.Pia ofisi ya mkuu wa mkoa wa Singida,imemuunga mkono rais kwa kutoa msaada wa nguo mbalimbali kwa wakazi hao ambao baadhi,ni wagonjwa wa ukoma.Wakati huo huo, tarehe (7/4/2012) mbunge wa jimbo la Manyoni mashariki,John Chiligati,alitarajiwa kuwasaidia wakazi wa Sukamahela mchele kilo 100,mbuzi wawili na mafuta ya alizeti lita 20.


 


Lengo la msaada ni kuwawezesha wakazi hao kufurahia sikukuu ya pasaka.Pia Chiligati,alitarajiwa kuwasaidia wazee wasiojiweza wa Majengo Manyoni mjini,mchele kilo 20,mbuzi moja na mafuta ya alizeti,lita kumi.

BALOZI SEIF IDD APIGA TAFU SKULI YA SEKONDARI YA MASISTA YA MITUNDURUNI MKOANI SINGIDA.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi mchango wa shilingi 1,000,000/- Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki Mh. Dianna Chilolo kwa ajili ya uendelezaji wa Jengo Jipya la Skuli ya Sekondari ya Masista ya Mitundu Mkoani Singida. Mchango huo aliukabidhi VIP Karimjee Mjini Dar es salaam kutekeleza ahadi aliyoitowa wakati alipotembelea Ujenzi huo Tarehe 7/2/2012 Huko Singida akiwa mlezi wa Mkoa huo Kichama.
Othman Khamis Ame – Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amekabidhi mchango wa Shilingi Milioni Moja { 1,000,000/-} kwa ajili ya uendelezaji wa Ujenzi wa Jengo jipya la Skuli ya Sekondari ya Masista iliyopo Mitundu Mkoani Singida.
Mchango huo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa alipotembelea Ujenzi wa Jengo hilo wakati wa ziara yake ya siku tatu Mkoani Singida ya tarehe 7 February mwaka 2012 akiwa Mlezi wa Mkoa huo Kichama.
Balozi Seif amekabidhi Mchango huo kwa Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki Mh. Dianna Chilolo hapo katika Ofisi ya watu Mashuhuri { VIP } iliyopo katika jengo la  Karimjee Mjini Dar es salaam.
Akitoa mchango huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema  amelazimika kutoa mchango huo kutokana na uamuzi wa Uongozi wa Skuli hiyo kutoa upendeleo wa kuwapatia Elimu  bila ya ada Watoto Yatima na wale wanaoishi  katika Familia zenye mazingira magumu.
Akipokea Mchango huo Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki Mh. Dianna Chilolo amempongeza Balozi Seif kwa Jitihada zake za kuunga mkono Maendeleo ya Elimu Mkoani Singida.
Alisema Mchango huo ni moja ya Vitendo vinavyoendelea kuwapa moyo Wananchi wa Singida katika  harakati zao za kupewa msukumo wa Kimaendeleo wakati wanapoanzisha Miradi ya Utawi wa Jamii.
Mh. Dianna Chilolo ameahidi kwamba mchango alioutoa Balozi Seif ataufikisha kwa wakati muwafaka na kutumiwa kwa lengo lililokusudia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliutembelea Mkoa wa Singida mnamo Mwezi wa Pili mwaka huu katika ziara ya siku tatu akiwa mlezi wa Mkoa huo Kichama.
Balozi Seif katika ziara hiyo alibahatika kuweka Mawe ya Msingi pamoja na kuzindua miradi tofauti ya Maendeleo na Kiuchumi ya Wananchi wa Singida ikiwemo pia ile ya Chama Cha Mapinduzi.

Kesi Ya Tundu Lissu:Yaibua Makubwa



Josephat isango- Singida.
Kesi ya kupinga matokeo ya Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya CHADEMA jana iliibua mambo mapya, baada ya mshitakiwa Tundu Lissu kutoa waraka Mahakamani ulioandikwa na John Chiligati kuomba ufafanuzi namna TLP ilivyoshiriki katika uchaguzi Mkuu wa 2010.
Kwa mujibu wa barua hiyo ambayo Tanzania daima inayo, yenye kumbukumbu namba CCM/OND/559 Vol.II/10, ya tarehe 23/03/2011. John Chiligati aliomba kujua kama kweli TLP iliweka mawakala katika Jimbo la uchaguzi wa singida mashariki, au kama mihuri iliyotumika ya TLP ilikuwa ni sahihi au ni ya kughushi,

Kufuatia barua hiyo, barua nyingine ya majibu kwa Chiligati, iliyotolewa mahakamani hapo na Tundu Lissu ilitoka kwa Hamadi R. Tao, aliyekuwa naibu katibu Mkuu TLP, yenye kumbukumbu Namba TLP/HQ/HAB/VOL.V/165, Ilisema Ni kweli mawakala wa TLP hawakuteuliwa au kama waliteuliwa utaratibu wa uteuzi haukufuata taratibu za Chama. Barua hiyo ya TLP ilipingana vikali sana na barua ya Mwenyekiti wa TLP, wilaya ya singida, iliyoandikwa kumjibu Katibu wa taifa wa TLP, ya tarehe 12/04/2011, ilisema kuwa Chama cha TLP kiliweka mawakala kusimamia katika uchaguzi Mkuu bila malipo.
Hata hivyo mjadala wa mahakamani ulikuwa Mkubwa, baada ya Shahidi wa 19, Bw. John Madindilo, ambaye ni Mwenyekiti wa TLP Mkoa wa singida kukubaliana na hoja zote za Lissu, na alimtaja Mtoto wa Augustino Mrema, anayeitwa Michael Mrema kuwa alitumwa singida kama afisa wa Chama kwenda kufuatilia suala hili, na alipopewa taarifa hiyo, hakuridhika nayo badala yake aliwalelekeza wale viongozi wa Singida, kuandika barua kwa Katibu Mkuu kadiri itakavyompendeza Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema.
Baadhi ya mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo: Baina ya tundu Lissu na SHAHIDI, JOHN MADINDILO
T/L Ni kweli au si kweli kuwa ulikasimu madaraka kwa Mwenyekiti wa TLP wa wilaya ya Singida, kwa kuwa wewe ulikuwa Mgombea, na Mwenyekitji wa Wilaya ya singida, ulimwamini, kwa uwezo wake na uadilifu , na uzoefu wake?
P/W:NDIYO NILIFANYA HIVYO LAKINI YEYE PIA YUPO MAKAO MAKUU YA MKOA HAPA MJINI.
T/L Ni kweli au si kweli kuwa mliweka mawakala kulinda maslahi ya Chama,
P/W NI kweli,
T/L Ni sahihi au siyo sahihi, mnapokuwa na Mgombea urais, huwa mnaweka mawakala?
P/W NI KWELI, pale ambapo mawakala wanakuwa tayari kujitolea.
T/L Ni kweli au si kweli kuwa kwa mujibu wa barua ulizo nazo, kesi hii ipo kwa maslahi ya Chiligati na Mrema?
P/W Ni kweli kwa mahusiano ya barua hizi walizoandikiana.
T/L Kama nimekusikia vizuri uliiambia mahakama hii kuwa kuna Afisa wa Chama anakuja toka Mkao makuu, umpokee na umpe ushirikiano?
P/W NI kweli.
T/L Je huyo afisa wa chama alikuwa anaitwa nani?
P/W: Siruhusiwi kumtaja
JAJI: Kama umemtaja Augustino Mrema, Mwenyekiti wa TLP Taifa ni Afisa gani unashindwa kumtaja
P/W: ni Mikaeli Mrema.
T/L. Mikaeli Mrema ambaye ni mtoto wa Augustino Mrema?
W/P.NDIYO
T/L. Mikaeli Mrema alisema nini?
P/w; alisema kuwa kulikuwa na mawakala hewa wa TLP waliwekwa Singida mashariki?
T/L. Hukushangaa kupokea taarifa ya Malalamiko toka makao makuu wakati wewe Mwenyekiti wa Mkoa huna taarifa yeyote?
P/W: NILISHANGAA SANA lakini nilipokea kwa kuwa inatoka kwa Mkubwa wangu wa Kazi.
T/L: Nimeshtakiwa hapa, kwa mujibu wa barua mbalimbali ulizosoma, wanaitaka Mahakam itengue matokeo ya uchaguzi, kwa mujibu wa ufahamu wako, unasemahe juu ya hili?
P/W: watakuwa wanakuonea.
Kesi hiyo haikuendelea mchana, baada ya upande wa walalamikaji kushindwa kuleta Mashahidi mahakamani, kitendo kilichopelekea jaji kuwapiga faini ya kulipa nusu gharama ya siku katika kesi hiyo:
Na mahojiano yalikuwa hivi:
Wakili wa walalamikaji; Mheshimiwa jaji, naiomba Mahakama iahirishe kesi hii hadi kesho kwa kuwa shahidi wetu hajaja, na amefunga simu,
JAJI: Ulichukua hatua kuleta shahidi mmoja tu?
Wakili: huwa tunachelewa kutoka mahakamani, hivyo inakuwa vigumu kuwatafuta kwa siku inayofuata. Hata hivyo kazi ya kutafuta mashahidi sio yangu ni ya wateja wangu.
TUNDU LISSU: Mheshimiwa jaji, uchelewashaji unaofanywa kwa makusudi unaniathiri mimi, kwanza kiuchumi kwa kuwa nakaa hotelini, pili ninashindwa kushiriki kazi za kibunge, na ninashindwa kuwatumikia wanachi wangu walionichagua. Siku nyingine ulinionya nisidai gharama, leo mheshimiwa jaji, naomba upande wa walalamikaji walipe gharama,
Jaji: Mlalamikaji naomba usimame, unajua kuwa katika kesi hii mimi nalipwa na serikali, na hawa wanasheria watatu wa serikali, na katibu wangu?
MLALAMIKAJI: NDIO,
JAJI: mbona hampo ‘serious’ . Kuna uzembe mkubwa unatokea na leo hii sitaki kukubali kirahisi uzembe huu. Kuna uzembe unafanywa na walalamikaji, na tayari nilionya hili tangu mwanzo. Mtumzembe hukumbushwa na leo naamuru mtalipa nusu gharama ya ahirisho la kesi leo kwa uzembe wenu ili mjitume na mjue wajibu wenu sio kutupotezea muda hapa.

PINDA AONGOZA UPANDAJI MITI SINGIDA



 Waziri Mkuu,Mizengo Pinda akipanda mti kwenye chanzo cha maji katika kijiji cha  Ilongero, Singida Aprili 1, 2012 ikiwa ni siku ya kitaifa ya upandaji miti.  Aliyesimama kushoto ni Mkuu wa Mkoa huo, Vincent Perseko Ole Kone.
 Wanafunzi wakipanda  miti katika chanzo cha maji cha kijiji cha Ilongero, Singida ambako waziri Mkuu Mizengo Pinda aliongoza shughuli hiyo Aprili 1, 2012 ikiwa ni siku ya kitaifa ya upandaji  miti
Waziri Mkuu,Mizengo Pinda akikagua kisima  kirefu cha maji baada ya kuongoza upandaji miti katika kijiji cha Ilongero , Singida Aprili 1, 2012 ikiwa ni siku ya kitaifa ya upandaji iti Kushoto ni mkuu wa mkoa huo, Vincent  PersekoOle- Kone. Picha na PMO
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa