Home » » Barabara, kilimo vyainua kipato cha wakazi wa Singida

Barabara, kilimo vyainua kipato cha wakazi wa Singida

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Ukibahatika kuutembelea Mkoa wa Singida na kurejesha kumbukumbu zako miaka 10 nyuma unaweza usiamini yanayotokea hivi sasa kwenye mkoa huo. Unaweza kushangaa na kujiuliza maswali mengi jinsi mkoa huo unavyobadilika na kuvutia watu wengi sasa.
Singida sasa wamejenga nyumba za kisasa, barabara za lami na wakazi wake wameongeza uzalishaji wa zao la alizeti, karanga na vitunguu na hivyo kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja.
Uzalishaji wa mazao ya biashara; alizeti, pamba na vutungu umeongezeka kwa kasi ukilinganisha na miaka minane iliyopita kwa mfano, mwaka 2007 Mkoa wa Singida ulivuna tani 28, 000 za alizeti wakati mwaka 2012 Singida ilivuna tani 202,000 za zao hilo.
Ukuaji na kuwapo kwa mabadiliko ya kiuchumi katika mkoa huo hasa kuongezeka kwa pato la mtu mmoja mmoja kunachangiwa na shughuli za kilimo, ufugaji na ujenzi wa barabara ya lami ambayo imekamilika mwaka 2007.
“Pato la mtu mmoja, mkoani Singida, kabla ya mwaka 2007 lilikuwa Sh280,000 kwa mwaka, sasa ni Sh650,000 kwa mwaka,” anasema Liana Hassan, Katibu Tawala wa mkoa huo.
Mabadiliko yalivyotokea
Mabadiliko hayo hajatokea kirahisi kwenye mkoa huo bali mambo mengi yamebalika kutokana na juhudi za Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone na Benki ya Dunia (WB) ambayo imetoa mkopo wa Sh44.506 bilioni kwa Serikali ya Mkoa wa Singida.
Mradi wa ujenzi wa kilometa 109 ya barabara kuanzia Singida mpaka Shelui kupitia Mlima wa Sekenke, uko chini ya Central Transport Corridor Project (CTCP). Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Mhandisi Yustaki Kangolle anasema Barabara ya Singida hadi Shelui imejengwa katika awamu tatu; kuanzia Singida hadi Iguguno, awamu ya pili Iguguno hadi Sekenke na Sekenke hadi Shelui.
Ujenzi wa barabara hiyo umewavutia wakazi wa mkoa huo kuongeza bidii katika kilimo cha alizeti na kununua na kuanzisha viwanda vidogo vya kukamua mafuta kutokana na fursa ya kusafirisha kwa wingi mafuta hayo jijini Dar es Salaam, Arusha na mkoani Kilimanjaro.
Mwitikio wa wananchi wa Singida kupenda kulima na kutekeleza maagizo ya Serikali ya Mkoa wa Singida chini Dk. Kone wameleta mabadiliko kilimo cha alizeti na kusababisha kuongezeka kwa viwanda vya kukamua mafuta.
Kutokana na juhudi za wakulima, Ofisa Mtendaji wa TCCIA wa mkoa huo, Calvent Nkulu anabainisha kuwa miaka saba iliyopita kulikuwa na viwanda 50 vya kukamua mafuta, lakini sasa kuna viwanda 120 mkoani Singida.
“Kutokana na kipato cha wananchi kuongezeka, tumewahamasisha wajenge nyumba za kisasa badala ya nyumba za tembe. Wananchi wanapata urahisi wa kusafirisha vifaa vya ujenzi kutoka Singida mjini hadi vijijini,” anaeleza mkuu wa mkoa huo.
Mazao ya biashara yanasafirishwa hadi nchi za jirani; Rwanda, Kenya, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na mazao ya chakula kwa mfano, samaki, maparachichi yanasafirishwa na kuuzwa jijini Dar es Salaam kutoka mkoani Mwanza na Rwanda.
“Biashara imekua hapa Singida, wafanyabiashara wanatoka Kenya kwa ajili ya kununua vitungu na kuku, Singida ya leo siyo ile ya zamani,” anasema Julius Madebwe ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kitengo cha Biashara mkoani Singida.
Mkoa huo sasa umekuwa na maendeleo makubwa ya shughuli za ujenzi wa nyumba za kisasa kutokana na kuwapo kwa barabara hiyo na kukua kwa shughuli za kilimo baada ya kuwapo kwa mvua za kutosha.
Biashara ya mafuta ya alizeti imepata soko kubwa nchini na kuwavutia watu wengi kuifanya akiwamo Mhandisi Mstaafu wa Wakala wa Barabara nchini, John Shailla ambaye ananunua mbegu za alizeti Wilaya ya Bariadi na kuzikamua kwenye mashine yake na kuuza kwa walaji.
Jambo kubwa la kujivunia kwa wakazi wa Singida ni bidhaa mbalimbali zinazosafirishwa kutoka nchini Rwanda kwa mfano, maparachichi na maharagwe hivi sasa yanauzwa sokoni mkoani Singida tofauti na awali magari ya mizigo yalikuwa yakikwama njiani.
Baada ya kukamilika kwa barabara hiyo, mkazi wa Shelui katika mkoa huo, Mohamed Hassani anasema kuwa ajali zimeongezeka kwenye Mlima wa Sekenke na baadhi ya wananchi wameiomba Serikali iwaruhusu madereva watumie barabara ya zamani wakati wa kuteremka mlima huo.
Baadhi ya wakazi wa Kata ya Iguguno, Misigiri, Ulemo na Kijiji cha Kyengege akiwamo dereva wa malori ya mizigo, Henry Michael na mkulima wa Kata ya Iguguno, Hatibu Sambai wanapendekeza kuwekwa kwa alama za barabarani katika maeneo muhimu ya pembezoni mwa barabara ambako kuna shule, hospitali na miji midogo ili kupunguza ajali.
Wakazi wa wengi wa kata hizo wameshangazwa na barabara hiyo kuharibika mapema na kuwa mashimo mengi huku wakiitupia lawama Tanroads kwa kuitengeneza barabara hiyo chini ya kiwango na kutoweka mitaro ya kupitisha maji wala barabara za waendesha baiskeli, pikipiki na barabara ya waenda kwa miguu.
“Matatizo ni mengi kwenye barabara hii, haina mitaro ya kupitisha maji na matokeo yake maji yanaingia kwenye makazi ya watu,” anabainisha Nikodemmonti Maigai, mkazi wa Kijiji Kyengege.
Hata hivyo mkazi wa kijiji hicho, Josephat Mginza anawalaumu Tanroads kwa kuwa hawawashirikishi wakazi wa Singida wakati wa kutengeneza barabara na matokeo yake kusababisha wananchi wengi kulalamika kutokana na kupoteza fursa za biashara zilizokuwapo pembezoni mwa barabara.
Kutokana na kuwapo kwa kasoro hizo Meneja wa Tanroads mkoani Singida, Mhandisi Kangole alikiri kwamba barabara hiyo imejengwa chini ya kiwango kwa kuwa fedha walizopata hazikutosheleza kujenga barabara ya kiwango cha juu.
“Barabara hii imejengwa kwa kiwango cha TLC 10- ni aina ya barabara ya kiwango cha chini. Sasa tunafikiria kuweka lami juu ya hii ya sasa na kilometa moja ya barabara ya milimita 50 inaweza kugharimu Sh600 mpaka Sh800 milioni,” anabainisha Mhandisi Kangole.
Kutowekwa kwa alama za barabarani na vibao, Mhandisi Yonennes Mbegalo anabainisha kwamba ni tatizo linalosababishwa na baadhi wananchi ambao wanaviiba na hivyo amewataka kuvilinda vibao hivyo.
Wakati Mhandisi Kangole akisema hayo Mhandisi Masige Matari anatoa sababu za kuharibika kwa barabara hiyo kwamba wingi wa magari ya mizigo umesababisha kuwapo mashimo.
“Kabla ya Barabara ya Singida hadi Shelui kuwekwa lami, malori ya mizigo 117 yalikuwa yakitumia barabara hii kwa siku, leo yanapita malori 1,135 kwa siku kwenda Rwanda, DRC, Kagera na Mwanza.
Baadhi ya wananchi wanapongeza jitihada hizo wakisema kuwa ikiwa harakati za maendeleo zitaendelea mkoa huo unaweza kuwa na maendeleo ya kasi zaidi.
Chanzo;mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa