Home » » BILAL AHIMIZA UMUHIMU WAUWEKEZAJI ELIMU

BILAL AHIMIZA UMUHIMU WAUWEKEZAJI ELIMU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. MohamMed Gharib Bilal.
 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. MohamMed Gharib Bilal, amewaasa wadau wa elimu kuwekeza bila kuchoka kwenye elimu kuanzia ngazi za sekondari ili kupata wanafunzi wazuri watakaojiunga vyuo vikuu.
Dk. Bilal aliyasema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa kimataifa wa kupitia masuala ya taaluma na mitaala katika Chuo Kikuu cha Waislamu (MUM) kilichopo mjini hapa jana.

Mkutano huo unahudhuriwa na zaidi ya watu 400 kutoka nchi 13 duniani.

Dk. Bilal aliwaasa waumini wa dini ya Kiislamu kufuata misingi ya dini hiyo kama inavyoelekeza hususan kwa wanafunzi wa elimu juu ambao wana jukumu la kuhakikisha wanasoma kutokana na kile ambacho Mwenyezi Mungu amekieleza katika kitabu chake kitukufu cha Qur`an.

Alisema tatizo lingine ambalo linasababishwa na ufaulu mdogo wa wanafunzi ni vyuo kupata wanafunzi wachache hasa wa masomo ya sayansi, akasema ni vyema vyuo vikashiriki katika kudaili wanafunzi kwa umakini na kuinua kiwango cha elimu.

Dk. Bilal pia alizilaumu baadhi ya taasisi za kidini zinazowashawishi wanafunzi wa kike na kiume kuacha kuchukua masomo ya sayansi na udaktari katika vyuo vikuu vya hapa nchini na hivyo kukosa wataalam wengi wa kutosha katika sekta hiyo.

Alisema wanafunzi wengi waliotoka sekondari wamekuwa na uelewa mdogo.

Aidha, alibainisha kuwa kushuka kwa elimu ya sekondari nchini kunasababisha kupatikana kwa wahitimu wa vyuo vikuu wenye ujuzi na uelewa wa hali ya chini.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu mkoani Mororogo, Mwantumu Malale, kwa upande wake alisema ni vyema vyuo vikuu nchini vikafundisha elimu ya jumla inayozingatia mazingira ya nchi bila kujali elimu ya maghabiri pekee na kuwataka wanafunzi wa Kiislamu kutumia elimu kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Mkutano huo unawashirikisha wahakiki wa kitaaluma na wadau wengine wa elimu kutoka nchi za Burundi, Rwanda, Kenya, Msumbiji, Malawi, Uganda, Afrika Kusini, Sudani Kusini, Malaysia, Saudi Arabia, Nigeria, Indonesia na wenyeji Tanzania.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa