DK.KITILLA AFICHUA SIRI YA ZITTO KWENDA MAHAKAMANI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Dk. Kitilla MkumboMHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kitilla Mkumbo, amefichua siri ya kwenda mahakamani kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), kwamba ni baada ya jopo la wasomi kumshauri kufanya hivyo.
Dk. Kitilla alisema kabla ya hapo, mbunge huyo alikuwa tayari kuwaachia viongozi wa chama chake wamvue uanachama kama alivyofanyiwa yeye na aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Alitoa kauli hiyo juzi wakati akiendesha mafunzo ya siku moja kwa viongozi wa mikoa na wajumbe wa Chama cha ACT–Tanzania juu ya historia, misingi, itikadi na falsafa ya chama hicho.
Alisema kwamba jopo la wasomi walimuelezea Zitto umuhimu wa kuangalia maslahi ya watu waliomchagua na njia inayotaka kutumika kufikia uamuzi wa kumvua uanachama wake katika chama hicho.
“Sisi tuliridhia kuvuliwa uanachama kwa kuwa hakukuwa na maslahi ya moja kwa moja yanayoweza kuathiri maisha yetu na familia zetu, lakini kwa Zitto hilo lingetokea na kumuathiri kwa mazingira yote mawili,” alisema.
Kuhusu kuandaa waraka unaodaiwa kuwa ni wa usaliti ndani ya CHADEMA, Dk. Kitilla alisema katika utatu wao wakiwa wanachama wa CHADEMA wakati huo walikuwa na nia ya mabadiliko ya muda mrefu ndani ya chama hicho baada ya kubaini baadhi ya mambo hayaendi sawa.
“Mimi, Mwigamba na Zitto tumekuwa na nia ya muda mrefu ya kuleta mabadiliko ndani ya CHADEMA, matamanio yetu ya mabadiliko yalihitimishwa kwa kuandika waraka wa mabadiliko, ukiainisha sababu za mabadiliko na mikakati yetu ya kushinda uchaguzi ndani ya chama,” alisema Dk. Kitilla.
Aliongeza baada ya Mwigamba kukutwa na waraka wa mabadiliko uliodhaniwa kuwa ni uhaini, walifukuzwa ndani ya chama hicho na kwamba hawakuona sababu ya kujiunga na chama kingine chochote cha siasa katika vyama vilivyopo.
Kwamba baada ya hali hiyo, vyama mbalimbali viliwafuata na kutaka wajiunge navyo, ikiwamo CCM, na waliwakatalia kwa kuamini kujiunga na chama hicho ni usaliti wa dhamira zao katika kufikia mabadiliko, na kuwa nchi ilipofika sio muda wa kukisaidia kuendelea kubaki madarakani.
Alisema matatizo yaliyopo katika vyama vya upinzani ni ya asili na yanafanana kwa kiasi kikubwa, ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa umakini, kuwepo kwa hisia umiliki pamoja na kukosekana kwa demokrasia.
Dk. Kitilla ambaye kwa sasa ni mshauri wa ACT-Tanzania, alisema iwe ni marufuku kwa mwanachama wa chama hicho kuzungumzia vyama vingine badala ya kuwazungumzia wananchi na matatizo yao.
Chanzo:Tanzania Daima

MFUGAJI ATISHIA KUMBURUZA MAHAKAMANI DIWANI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

MFUGAJI na mkulima wa Kijiji cha Ufana, Kata ya Mgungira, Tarafa ya Sepuka, wilayani hapa mkoani Singida, Sawaka Kujelwa, ametishia kuwafungulia mashtaka mahakamani viongozi wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kata hiyo kwa madai ya kuuza zaidi ya ekari 500 anazozitegemea kwa ajili ya makazi, kilimo na malisho.
Kujelwa, aliwataja viongozi hao kuwa ni Mwenyekiti wa CCM wa Kata, Nhende Shija na Diwani Mussa Ng’imba, ambao alidai waliamua kuvamia maeneo yake baada ya yeye kuugua ugonjwa wa kushindwa kwenda haja ndogo, Desemba 21, 2009.
Alisema baada ya kuugua ndipo alilazimika kwenda kwenye matibabu ambako alipita hospitali ya misheni ya Mtakatifu Gasper mjini Itigi, Makiungu, Puma na hatimaye hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi, mkoani Kilimanjaro mwaka 2010 alikopona.
“Baada ya kupata matibabu KCMC, madaktari walinishauri kukaa karibu na hospitali hiyo kwa uchunguzi zaidi, ambapo nilikaa hadi mwaka 2012 ndipo niliporudi nyumbani, lakini nikilazimika kufuata masharti ya madaktari ya kutofanya kazi ngumu,” alisema.
Aliongeza kuwa wakati akiwa kwenye matibabu Moshi KCMC, ndipo diwani kwa kushirikiana na mwenyekiti wa chama wa kata, walipoanza kuyavamia maeneo yake aliyokuwa akiyategemea kwa kilimo na malisho ya mifugo, na mwaka jana wakati anaendelea na mapumziko ya matibabu, watu walizidi kuvamia.
Alisema kuwa baada ya kuona hali hiyo, aliandika barua kwa Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, kumjulisha, lakini bila mafanikio na ndipo mwaka jana alimwandikia mwenyekiti wa kijiji kumfahamisha juu ya uvamizi huo.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Matinje, Elius Milekwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Ufana, Machiya Nyorobi, walipotakiwa kuzungumzia malalamiko hayo, walikiri eneo lililovamiwa ni la Kujelwa na kwamba wanaoendesha shughuli za kilimo na malisho kwa sasa ni wavamizi na hawataki kuyaachia.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mgungira, Nhende Shija alipoulizwa sababu za kuvamia maeneo hayo, alidai hakuvamia bali ni mali yake.
Diwani Ng’imba alisema kuwa, malalamiko hayo hayana ukweli wowote ila ni mali yake na mwenyekiti huyo, na kwamba Sawaka ni tapeli tu.
 Chanzo;Tanzania Daima

DALADALA NAMBA 'T111 BRN'

 

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Nani atabisha kwamba hakuna jambo linalogusa Wabongo kama elimu? Au labda tuseme hakuna jambo linalogusa Wabongo kama matokeo ya mitihani. Ndiyo maana sikushangaa kupokea mapepe kibao wiki hii. Hebu niwaonyeshe mbili tu.
Yes, Serikali yetu bunifu. Kwa nini tuhangaike kuinua uwezo wakati tunaweza kushusha viwango? Achana na hawa wanaharakati wote, ambao kazi yao ni kupinga tu utadhani wanaamka na kula malimau tu kila asubuhi. Mimi nasema, hongera sana wote waliofaulu mwaka huu. Hongera kwa kuzaliwa mwaka mwafaka, mwaka wa neema, mwaka wa mafanikio. Hongera zaidi kwa wizara yetu ya shule pamoja na Baraza la Vyakihuni kwa kuonyesha njia. Kwa njia hii tunajua Bongo yetu itasonga mbele kwa kasi sana.
Kwanza kwenye mpira. Miaka mingapi tumelalamika kuhusu kiwango cha mpira hapa petu? Uongozi mbovu huzaa mpira mbovu. Na kutokana na ubovu huo, tumepata matatizo sana ya uhaba wa magoli mara kwa mara. Tunajitahidi kuwafundisha washambuliaji wetu jinsi ya kufunga, lakini ukweli ni kwamba magoli ni madogo mno. Hivyo, kuanzia msimu ujao wa ligi kuu na ligi zote chini yake, magoli yatapanuliwa kwa mita tano zaidi. Nadhani kwa njia hiyo tutaweza kushangilia magoli mengi, potelea mbali iwapo kwenye mashindano ya kimataifa goli itakuwa dogo, lazima wajue kwamba mabadiliko ni sisi, sisi ni wabongo na tutabonga na kuboronga kwa njia zetu wenyewe.
Haya, upande wa fedha pia. Hawa watu wa Hazina watumie ubunifu badala ya ubanifu. Kama pesa hazitoshi, chapa pesa nyingi zaidi. Kwa njia hiyo, kila mtu atajisikia akibeba marundo ya manoti. Hata kama haina thamani ni lazima tushindane na wenzetu wa Zimbabwe, ambao hatimaye walitumia dola zao milioni moja kwa ajili ya kununua kilo moja ya sukari. Kila mtu milionea au hata bilionea, wataka nini zaidi?
Kwa kweli katika sayansi inaitwa sheria ya utapiamlo ni sheria ya Mungu kabisa. Mlo ukipungua kwa mtoto, tumbo linaongezeka, linatuna, linang’aa. Na elimu inaweza kuwa vivyo hivyo.
Tena ingawa tunafanya kwa mtindo wetu mwenyewe, tunaendeleza vizuri sana umoja wa Afrika. Wale wenye sifa ya uaminifu na kutokomeza utapeli walionyesha njia siku nyingi, yaani Nigeria lakini wapumbavu wa vyuo vikuu mwisho walikataa kuamini matokeo hayo, hivyo waliotaka kuingia vyuo vikuu vyao walilazimika kufanya mtihani wa ziada. Kufuru kabisa na ole wake profesa atakayejaribu huo upuuzi hapa. Kama mtu amepata cheti, wao ni nani kukihoji?
Baraza la Vihuni juuuuuu! Viwango ziiiiii, kidumu na kudumu.
Duh! Barua hii ilinishtua kidogo, lakini kabla sijaweza kuachana na mshangao wangu, ikaja nyingine.
We Makengeza,
Mimi sijui nifurahie ya mwaka huu au niomboleze ya mwaka jana. Yaani, baada ya kuletwa hapa kwenye shule ya walimu wawili na kitabu kimoja, nimejitahidi kwa nguvu zangu zote kuwapatia vijana wetu angalau misingi michache ya elimu, lakini haiwezekani. Wanapata kitu labda, lakini mbele ya mitihani lazima wafeli kwa sababu hatuna uwezo wa kuwapatia zaidi. Sasa mwaka huu, tupo walimu walewale na kitabu kilekile na hata notisi zilezile, maana utapata wapi zingine lakini ghafla shule nzima imefaulu. Haiyumkiniki. Sijaongeza juhudi wala maarifa, maana tangu niombe ualimu nimejitahidi vilevile. Na sioni kwamba wanafunzi wangu wamebadilika pia. Tena wa mwaka huu walikuwa na hasira zaidi wakijua watapigwa muhuri wa ujinga tu. Je, wanastahili kusonga mbele? Labda kwa kuwa na akili, ambayo ikikutana na mazingira ya kweli ya elimu, lakini kwa hayo waliyoyapata kutoka kwangu na mwenzangu, mmmmh! Tunaelekea wapi?
Basi kutokana na hayo, nikajikuta natafakari kwa kina wakati nimefunikwa na giza nene ya eneo letu. Wakati asilimia sitini ya shule za Kenya zina umeme, kwetu ni asilimia mbili tu ya shule za vijijini. Ndiyo maana elimu iko hoi kwa koroboi. Lakini angalau tuna nafasi ya kutafakari.
Sasa, uzee wako lazima unakumbuka enzi zile za kupiga deki resepsheni. Sijui inaitwaje siku hizi, lakini nimegundua kwamba tabia za mtu mmoja mmoja zinaakisi tabia za wakubwa wetu na mifumo yao ya kutufuma bila sisi kuwafumania. Angalia watoto wanavyohaha barabarani kutafuta wafadhili kwa ajili ya timu yao ya mpira au mahafali wa darasa la saba. Nani kawafundisha kwamba dunia ni kuombaomba siyo kufanya kazi? Elimu ya Kujitegemea siyo kujiegemea iliishia wapi? Hata ule mpango wa maskauti wa kufanya kazi ndogondogo ili walipwe kwa ajili ya mipango yao iliishia wapi? Nani kawatonya umatonya?
Haya, hata katika elimu mambo hayo ya kuwangia viwango yalianza leo? Tangu zamani sote tumethamini sura ya elimu, badala ya elimu yenyewe. Zamani ilitosha kunawa vizuri kwa uso wa kawaida, yaani kusoma kwa bidii chini ya uangalizi wa walimu wanaofundisha kwa bidii ndani ya mazingira wezeshi. Nakumbuka, maana hata mimi nilisoma wakati ule. Lakini hata wakati ule, bado wanafunzi wengi walijali sura ya elimu tu, siyo elimu yenyewe maana lengo lilikuwa cheti siyo zaidi ya hapo.
Haya, sura ya elimu ikaanza kuota vipele kutokana na sababu mbalimbali. Maarifa ikapungua na wengi walikosa vyeti ndipo ilibidi kutafuta sabuni za kuua vijidudu vilivyoanza kujitokeza. Badala ya kuoga vizuri, watu walitegemea sabuni itafanya kazi peke yake. Sabuni hii kwa lugha ya kitaalamu iliitwa sabuni twisheni. Na wengine walibuni sabuni kali zaidi iliyoitwa sabuni akademiki. Ndiyo maana tulisikia kwamba watu wengine walipata fasticlasi ya vidato, kisha wakala disko baada ya mwaka mmoja chuoni kutokana na kukosa sabuni hiyo (ingawa nasikia hata kule siku hizi sabuni hizi zimetapakaa).
Kutokana na sabuni hizo pia, Serikali yetu kufuru iliweza kubuni mpango wa viwango panuka, badala ya viwango pandisha. Kila mtu alitakiwa kuoga hata maji yakiwa machafu namna gani au hata kukosekana kabisa, ili mradi wanakubali kununua sabuni twisheni na wao. Wasipokuwa na uwezo wa kupata hiyo sabuni potelea mbali. Wenye sabuni ndiyo wenye zabuni za kujaza nafasi za juu.
Lakini mambo siyo rahisi kivile. Wasio na sabuni walianza kuwashwa sana, ngozi zao zikaharibika hadi wakaanza kudai elimu ya kweli na wao. Ndipo hapo tumekuja na mikorogo kabisa. Mtu anaweza kuwa hana maji, hana sabuni, hana chakula bora, lakini ili mradi resepsheni inapigwa deki. Nani atajua na ataweza kwenda kujinadi popote? Cheti ni mkorogo, ndiyo maana unaona watu wana sura ya Mirinda, lakini akili ya Pepsi.
Ndiyo maana nawahurumia wanafunzi wangu wa huko nyuma. Kama suala ni mkorogo tu, kwa nini pepa zao zisisahihishe upya ili na wao waingie katika ufalme wa mbingu.
Lakini mwisho, nawapa pole wanafunzi wa mwaka huu pia. Muwe mmebebwa na daladala ya ‘T111BRN’ au la, mustakabali wa nchi yetu uko mikononi mwenu.
Ndiyo. Siyo tu kwa sababu ambazo tumezizoea kwamba sura ya elimu itajenga sura ya ghorofa au daraja au kutibu sura ya magonjwa. Bali vizazi vitakavyofuata vitaweza kupata au kukosa nafasi kutokana na maisha yenu. Kwa matokeo kama haya, wengi mtaweza hata kuomba masomo ya nje. Iwapo nyinyi na Fasticlasi yenu (siyo First Class) mtaonekana katika vipimo vingine kwamba hamjui, mitihani ya Bongo itadharauliwa moja kwa moja. Na hata humu, nani atawaajiri mkorogo ukitambulika?
Mwalimu mkereketwa.
Na mimi pia nikabaki natafakari ndani ya giza nene. Twafunga goli au twajifunga? Kupanua goli ndiyo suluhisho. Tukichapa pesa nyingi, mwisho si itaonekana feki? Sura ya Mirinda itaficha daima akili ya Pepsi?
Chanzo:Mwananchi

WATAKAO URAIS CCM MTEGONI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 

KAMATI ya Usalama na Maadili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Agosti mwaka huu, itafanya mapitio ya mwenendo wa wanachama wake waliopewa onyo kwa kosa la kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu 2015, kabla ya wakati kinyume na Kanuni za Uongozi na Maadili ya CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i).

 

Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya kile kilichozungumzwa kwenye kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM iliyofanya kikao cha siku moja jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.

 

Alisema pamoja na mambo mengine, kikao hicho kilipokea taarifa ya mazungumzo yanayoendelea kati ya CCM kwa upande mmoja na vyama vingine vya siasa ambavyo ni CHADEMA, NCCR-Mageuzi na CUF ambayo yanasimamiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi.

Bw. Nnauye alisema, lengo la mazungumzo yaliyokutanisha vyama hivyo ni kuangalia kwa kina sababu za baadhi ya wajumbe wachache wa Bunge Maalumu la Katiba, kususia na kutoka nje katika awamu ya kwanza ya vikao vya Bunge hilo.

Lengo lingine ni kuangalia namna ambavyo wajumbe hao watarudi bungeni ili kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba ambapo Kamati Kuu ya CCM, imeridhishwa na mwenendo wa mazungumzo hayo, kupongeza juhudi zinazofanywa na Jaji Mutungi pamoja na vyama husika vinavyoshiriki mazungumzo.

 

"Kamati Kuu pia ilipokea taarifa za harakati za baadhi ya wanachama wa CCM walioonesha nia ya kuomba ridhaa ya chama kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu 2015...baada ya kutafakari kwa kina, Kamati hii inapenda kuwakumbusha wote kuwa ili wasipoteze sifa za kugombea ni muhimu wakazingatia katiba, kanuni na taratibu za chama.

"Wanachama waliopewa adhabu na Kamati Kuu kutokana na kukiuka taratibu za chama katika suala hili, Kamati ya Usalama na Maadili ya chama itafanya mapitio ya mwenendo wao na utekelezaji wa adhabu hiyo Agosti mwaka huu.

"Ikibainika hawatekelezi ipasavyo masharti ya adhabu zao, itapendekeza kwa Kamati Kuu iongeze adhabu kwa kuzingatia taratibu za chama," alisema Bw. Nnauye.

Aliongeza kuwa ni muhimu wanachama wote wakatambua kuwa, chama ni pamoja na Katiba, kanuni na taratibu zake hivyo kutoziheshimu na kuzifuata ni kuvuruga jambo ambalo haliwezi kuvumilika.

Alisema dhamira ya CCM kusimamia Katiba, kanuni na taratibu za chama ni kuhakikisha chama hicho kinakuwa na umoja, mshikamano ambao ni wa muhimu sana hasa wanapokwenda kukamilisha kazi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2010/15.

Februari mwaka huu, CCM ilifanya vikao vya kitaifa ambavyo vilishughulikia suala la maadili ndani ya chama vikihusisha Kamati Ndogo ya Udhibiti, Tume ya Udhibiti na Nidhamu na Kamati Kuu.

Vikao hivyo viliwahoji baadhi ya wanachama wa chama hicho ambao ni Bw. Frederick Sumaye, Bw. Edward Lowasa, Bw. Bernard Membe, Bw. Stephen Wassira, Bw. January Makamba na Bw. William Ngeleja.

Baada ya wanachama waliohojiwa, ilithibitika kuwa baadhi ya tuhuma dhidi yao ni za kweli hivyo kamati zilipendekeza adhabu na mapendekezo hayo yalipelekwa kwenye Tume ya Udhibiti na Nidhamu na hatimaye Kamati Kuu ya CCM ambayo ilitoa adhabu kwa wahusika.

Ilithibitika wanachama hao walifanya makosa mawili, mosi la kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea Urais kabla ya wakati kinyume na Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM, Toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i).

Kosa la pili ni kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii kinyume na Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM, Toleo la Februari 2010, Ibara kadhaa za kanuni hizo.

Kwa mujibu wa Bw. Nnauye ambaye alitoa tamko la CCM Februari 18 mwaka huu juu ya adhabu zilizochukuliwa kwa wanachama hao, alisema Kamati Kuu baada ya kuthibitisha makosa hayo imewapa watu hao adhabu ya onyo kali na kuwataka wajiepushe na vitendo vinavyokiuka maadili na iwapo wataendelea na vitendo hivyo, chama kitawachukulia hatua kali zaidi.

Alisema tafsiri ya adhabu ya onyo kali kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM, Toleo la Februari 2010, Ibara ya 8(ii) (b) ni mwanachama aliyepewa adhabu ya onyo kali, atakuwa katika hali ya kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi 12, ili kumsaidia katika jitihada zake za kujirekebisha.

Aliongeza kuwa, Kamati Kuu iliitaka Kamati Ndogo ya Udhibiti kuwachunguza na kuchukua hatua kwa wote waliohusika kwa namna moja au nyingine (mawakala na wapambe) kufanyika kwa vitendo hivyo ambavyo vilivunja kanuni za chama.

Pia Kamati Kuu iliwaonya vikali viongozi na watendaji wa chama ikiwataka wajiepushe kujihusisha na matendo ya wanaowania urais yanayovunja na kukiuka maadili ya chama badala yake wazingatie kanuni na taratibu za chama.

Chanzo:Majira

WAKAMATWA NA NYARAZA MIL.200/-

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

WATU sita wakazi wa wilayani ya Manyoni mkoani Singida, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kukutwa na nyara za serikali zenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 200.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Fatma Toufiq, bila kuwataja watuhumiwa hao, alisema kuwa tukio hilo lilitokea Julai 8, mwaka huu, kwenye nyumba ya kulala wageni iitwayo Matunda.
 Alizitaja nyara hizo kuwa ni vipande 28 vya meno ya tembo ambavyo ni sawa na tembo wanane, singa za tembo bando sita, ngozi ya simba moja, mkia wa pofu, kucha nne za simba, silaha aina ya SMG mbili, risasi 48 na magazine tatu.
Toufiq alisema nyara hizo zote zina thamani ya sh. 202,560,000 na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ambapo ukikamilika watuhumiwa hao watapelekwa mahakamani.
Katika hatua nyingine, Toufiq alisema baada ya Operesheni Tokomeza matukio ya ujangili wa tembo yaliendelea kwenye maeneo mbalimbali ya Ikolojia.
Alisema kuwa katika matukio matatu, askari wa Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Kati (KDU) na polisi Manyoni waliwakamata watuhumiwa wanne wakiwa na meno ya tembo sita na vipande 37 ambavyo ni sawa na tembo 15.
Kwa mujibu wa Toufiq watuhumiwa hao ni George James maarufu kama Maige aliyekamatwa Februari 12, mwaka huu, katika Kijiji cha Mgandu, akiwa na vipande 21 vyenye uzito wa kilo 39.5 ambavyo thamani yake ni sh. 34,760,000.
Mtuhumiwa mwingine ni Ally Hamadi aliyekamatwa Februari 16, mwaka huu, katika Kijiji cha Mgandu, akiwa na vipande 16 vyenye uzito wa kilo 19.4 vyenye thamani ya sh. 17,072,000.
Wengine kwa mujibu wa mkuu wa wilaya, ni David Makasi na Joseph Malima waliokamatwa Machi 29, mwaka huu, wakiwa na nyara mbalimbali zenye kilo 31.1 ambazo thamani yake ni sh. 27,368,000 na kwamba nyara zote hizo zina thamani ya sh. 79,200,000.
Alifafanua kuwa tembo wote waliuawa kwenye mapori ya akiba ya Rungwa/Kizigo/Mhesi na kwamba Ikolojia ya Rungwa–Ruaha bado ina tembo wengi ambao huzunguka kwenye mapori ya akiba ya Rungwa/Kizigo/Muhesi, Swagaswaga na Mkungunero.
Toufiq aliongeza kuwa mapori mengine ni hifadhi za taifa za Ruaha, Tarangire, Mikumi na Manyara na hujumuisha pia na mapori ya wazi ya Mgori, Itiso, Pawaga, Pwaga Rumuma, Mtera, Chaya, Mwamagembe, Shelui na Sambaru/Londoni.
Kwa kutambua changamoto hiyo, mkuu huyo wa wilaya alibainisha kuwa ofisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori ilifanya mawasiliano na wakuu wa taasisi za Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa).
 Alisema mawasiliano hayo yalifanyika ili kuwezesha wakuu wa kanda dhidi ya ujangili (KDU-Arusha na Manyoni) katika kupambana na ujangili kushirikiana na kikosi kazi cha Ikolojia ya Ngorongoro, Manyara-Tarangie ambacho kimekuwa kinafuatilia mitandao ya ujangili sehemu mbalimbali na tayari wanayo kanzi data (Data Base).
Chanzo:Tanzania Daima

ABIRIA WA TRENI WAKWAMA MANYONI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 

ZAIDI ya abiria 700 waliokuwa wakisafiri na treni ya abiria wakitokea Kigoma kuelekea Dar es Salaam, wamekwama kwa siku mbili wilayani Manyoni, baada ya treni ya mizigo kuanguka.
Wakizungumza na waandishi wa habari waliofika eneo hilo jana, abiria hao wamelilalamikia Shirika la Reli kutokana na kutokuwa na utaratibu mzuri wa kusafirisha abiria wake pindi tatizo linapojitokeza.
Walisema walipofika Manyoni majira ya mchana, walielezwa kuwa treni ya mizigo ilikuwa imeanguka kituo kinachofuatia cha Saranda, hivyo wasubiri utaratibu.
“Lakini cha kushangaza mabasi ambayo yalikuwa yakiletwa na Shirika la TRL yalikuwa machache kwa sababu abiria tulikuwa wengi,” alisema mmoja wa abiria hao, Anton Beni.
Walisema kutokana na hali hiyo walilazimika kulala nje huku wakiwa na watoto wadogo na wengine wagonjwa, kwani mabasi yalipokuwa yakifika kuwachukua hakukuwa na utaratibu na kusababisha watu kugombea na kusema hadi sasa baadhi ya abiria hawajui hatima yao ya kufika Dar es Salaam.
Meneja wa Kanda wa TRL kutoka Dar es Salaam, Philipo Rutizibwa, alisema suala la abiria waliokwama Manyoni wameshafanya utarabu wa mabasi na yameshaanza kuwachukua kuwapeleka wanakokwenda
 Chanzo:Tanzania Daima

WAZIRI NYALANDU AMWAGA MSAADA WA MILIONI 10 WA MABATI 420 SHULE ZA SEKONDARI KWA AJILI YA MAABARA


diwani
Diwani wa Kata ya Kinyeto, Francisco Ng’eni akipokea msaada wa mabati 200 kutoka kwa Mwenyekiti Hanje kwa niaba wa Mbunge wa Jimbo hilo Mhe, Lazaro Nyalandu.
kabidhi
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Singida Vijijini, Narumba Hanje (kulia) akimkabidhi mabati 220 yenye thamani ya shilingi milioni tano Afisa Mtandaji wa Kata ya Mtinko Jimbo la Singida Kaskazini, Eliufoo Mkanga katika hafla fupi iliyofanyika jana katika shule ya Sekondari ya Kata ya Mtinko , mabati hayo yametolewa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maabara na Mbunge wa Jimbo hilo Mhe,Lazaro Nyalandu.
maabara
Hili ni jengo la maabara ya sekondari ya Kinyeto likiwa katika hatua ya lenta.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

DC Iramba ahamia kijijini kufanikisha Ujenzi wa Zahanati

2
Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Yahaya Nawanda.
Na Mwandishi wetu-Mo Blog
MKUU wa wilaya ya Iramba mkoa wa Singida,Yahaya Nawanda, ameahidi kuishi kwa siku tano katika nyumba za kabila la kisukuma kijiji cha Kizonzo tarafa ya Shelui, ili kuhakikisha zoezi la kukusanya michango ya ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho linafanikiwa.
Nawanda ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa uhamasishaji wananchi kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF),uliofanyika kwenye kijiji cha Kizonzo.
Alisema katika kipindi hicho atasimamia kwa karibu uchangiaji huo,ili ujenzi wa zahanati hiyo uweze kufanyika mapema iwezekanavyo.
“Ninyi ndugu zangu, mmekuwa mkipata taabu sana kufuata huduma ya afya kwenye zahanati ya kijiji cha Mgongo kwa kutembea umbali wa kilomita nane kwenda na kurudi. Akina mama wajawazito ndio wanaotaabika zaidi”, alifafanua Nawanda 
“Sasa tunasema hatutakubali kabisa ninyi muendelee kutaabika kufuata matibabu umbali mrefu kiasi hicho.Tunataka kipindi kifupi kijacho,matibabu muyapate hapa hapa kijijini kwenu”.
Kutokana na hali hiyo Nawanda amewataka wananchi kujiandaa mapema kwa zoezi hilo la uchangiaji wa ujenzi wa zahanati yao unaotarajiwa uanza mapema iwezekanavyo.
Kuhusu mfuko wa afya ya jamii (CHF),mkuu huyo wa wilaya,alisema suala la kujiunga na mfuko huo ni la lazima kwa madai kwamba afya bora ni mtaji wa mwili wa binadamu ye yote.
“Wilaya yetu ya Iramba, ni wilaya ya kwanza nchini kwa vituo vyake vyote vya afya kuwa na dawa za kutosha wakati wote.Kwa hiyo mwanachama wa CHF, nawahakikishia kuwa mtapata tiba wakati wote pindi watakapougua”,alisema DC huyo.
Kwa mujibu wa Dc Nawanda, kuku moja wa kienyeji mwenye thamani ya shilingi 10,000 tu, anatosha kugharamia ada ya kaya moja yenye mume, mke moja na watoto wanane, kupata matibabu kwa kipindi cha mwaka moja bila kuongeza kiasi kingine cha fedha.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa