Home » » TAMISEMI YAZUNGUMZIA VURUGU UCHAGUZI WA MITAA

TAMISEMI YAZUNGUMZIA VURUGU UCHAGUZI WA MITAA

Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Khalist Luanda.
Imeelezwa kuwa uwazi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, ndiyo kiini cha vurugu zinazotokea wakati wa kuapisha viongozi waliochaguliwa kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Khalist Luanda, wakati akizungumza na NIPASHE kuhusu vurugu zilizojitokeza wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa Desemba, mwaka jana.

“Mfumo wa sasa katika chaguzi unawezesha mtu kujumlisha kura za kila kituo na kufahamu nani ameshinda, kwahiyo ni vigumu kufanya hujuma,”
alieleza Luanda.

Luanda aliagiza maofisa watendaji wote wanaobainika kuwa wazembe au wenye udhaifu wa aina yoyote, inayosababisha vurugu kiasi cha kuahirisha au kusimamisha shughuli za kuapisha viongozi hao, achukuliwe hatua kama mhalifu yeyote wa jinai, kama kanuni za uchaguzi zinavyoelekeza.

Alisema hali hiyo inatakiwa kuwa fundisho kwa wote watakaohusika kwenye zoezi la kupiga kura ya maoni, kuidhinisha au kubatilisha.

Katiba inayopendekezwa na kwenye uchaguzi mkuu wa viongozi, unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Hata hivyo, Luanda alifananisha wanaofanya vurugu hizo na ‘Panya Road’ (mtandao wa wahuni), akisema Tanzania hakuna mfumo wa kisheria unaoelekeza mtu akidhulumiwa haki yake kufanya fujo.

Alihusisha wanaofanya vurugu hizo na waliokuwa wakifanya vurugu kwenye vituo vya uchaguzi, kwamba baada ya kushindwa wameweka mikakati ya kuvuruga shughuli za kuwaapisha waliowashinda.

Alipoulizwa matukio ambayo wananchi walibana maafisa watendaji wakidaiwa kuchakachua matokeo na kutangaza waliokuwa wagombea wa CCM kuwa washindi badala ya washindi halisi, alisema hakuna kitu kama hicho.

Luanda aliombwa kuzungumzia tukio la Kijiji cha Nduoni, Kirua Vunjo Magharibi,  Kilimanjaro ambako mgombea wa NCCR-Mageuzi alishinda lakini Afisa Mtendaji akatangaza kuwa mshindi ni mgombea wa CCM.

Baada ya wananchi kumbana, mtendaji huyo alibatilisha tangazo hilo na kurejesha ushindi kwa mgombea wa NCCR-Mageuzi baada ya wananchi
kumbana, akatangaza matokeo yaliyompa ushindi mgombea wa NCCR-Mageuzi.

Alisema hakuwa na taarifa ya tukio hilo na kama hivyo ndivyo, basi matatizo mengine yanatokana na udhaifu wa watendaji husika na kwamba hapo kinachohitajika ni wahusika kushughulikiwa kwa mujibu wa kanuni.

“Mtendaji anapokuwa na udhaifu binafsi, siyo sawa kuhusisha kasoro anazosababisha na serikali au chama chochote bali Msimamizi wa Uchaguzi, ambaye ni Mkurugenzi wa eneo husika anatakiwa kutumia kanuni za uchaguzi kumshughulikia,” alieleza Luanda.

Katika tukio la Vunjo, wananchi walijikusanya wakiwa na mabango yaliyoeleza masikitiko yao juu ya kuapishwa Joseph Msaki (CCM) aliyepata kura 158 kama Mwenyekiti wa kijiji ilhali Thomas Ngowi (NCCR-Mageuzi) aliyepata kura 163 akiachwa bila kuapishwa.

Wananchi hao walifikia uamuzi wa kufunga ofisi za Serikali ya Kijiji hicho, wakikataa kuongozwa na mwenyekiti asiye chaguo lao hali
iliyosababisha Afisa Mtendaji wa Kirua Vunjo Magharibi, Reginald Mlay,kumtangaza Thomas kuwa ndiye mwenyekiti halali.
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa