Home » » CHIKAWE ATOA HOFU UCHAGUZI WA 2015

CHIKAWE ATOA HOFU UCHAGUZI WA 2015

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

 Kuanza kufuta vyama Jumatatu Vipo vya kiraia, dini.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe.
 Serikali imetishia kuchukua hatua kali kwa watu binafsi, vyama vya siasa, kijamii na vya kidini vitakavyobainika kuvuruga usalama na utulivu wa nchi katika kipindi cha Kura ya maoni kwa Katiba inayopendekezwa na uchaguzi mkuu, huku ikitishia kufuta asasi kadhaa kuanzia wiki ijayo.
 
Imetangaza kwamba kuanzia wiki ijayo itavifuta katika daftari la usajili vyama vya kijamii na vya kidini ambavyo vitakiuka katiba za kuanzishwa kwake.
 
Hatua hiyo ilitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mustakabali wa nchi kuelekea Kura ya Maoni kwa Katiba inayopendekezwa na Uchaguzi Mkuu.
 
VYAMA KUFUTWA JUMATATU
Waziri Chikawe alisema kuanzia Jumatatu ijayo, wizara hiyo itaanza kuvifuta vyama vyote vilivyosajiliwa chini ya Sheria ya Vyama, Sura 337, ambavyo havifuati matakwa ya kisheria ya kuwasilisha taarifa zao za mwaka za ukaguzi wa hesabu na kulipa ada kisheria.
 
Alisema kazi hiyo itaanza kwa vyama vilivyopo jijini Dar es Salaam na itaendelea nchi nzima na kwamba vyama hivyo havitaruhusiwa kuendelea na shughuli zake.
 
“Serikali inapenda kuwataka wananchi mmoja mmoja au vikundi, zikiwamo taasisi za dini kuepuka kushiriki katika vitendo ambavyo vinaashiria kuvuruga amani na utulivu nchini na itachukua hatua za kisheria kudhibiti hali hiyo,” alisema Waziri Chikawe.
 
Waziri Chikawe alisema kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio ambapo baadhi ya viongozi wa taasisi za dini wanatoa matamko yanayoashiria kuingilia masuala ya kisiasa kinyume cha sheria na katiba zinazosimamia uendeshaji wa taasisi hizo.
 
Mathalani, alisema viongozi wa dini wanapokutana na kutoa matamko yanayolenga kuwashawishi waumini wao wafuate maelekezo yao kuhusiana na masuala ya Katiba inayopendekezwa au kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao, matamshi hayo yanakiuka sheria za usajili wa taasisi hizo.
 
“Ni kweli kuwa viongozi wa taasisi za dini wana haki ya kushiriki katika masuala ya kisiasa kama watu binafsi ila ni kinyume cha sheria kutumia uongozi wao kushawishi waumini wao watekeleze matakwa yao ya kisiasa,” alisema.
 
Alisema serikali inatambua kuwa waumini wa dini mbalimbali wana haki ya kuamini mafundisho ya dini zao, lakini wanapaswa kutekeleza masuala yao ya kisiasa na kijamii kwa utashi wao wenyewe bila ya kushawishiwa na mtu yeyote kama sheria za nchi zinavyosema.
 
“Mfano mwingine ni pale kiongozi au viongozi wa dini wanapochangisha fedha na kuandamana au kukutana na wanasiasa kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kuwashawishi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi…hii siyo kazi ya taasisi za dini na ni kinyume cha sheria,” alifafanua.
 
Hata hivyo, hakutaja viongozi wa dini waliokwenda kumshawishi mgombea wa urais, lakini mwezi uliopita, kundi la watu wanaodaiwa kuwa ni Masheikh kutoka Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, lilikwenda mjini Dodoma kumshawishi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, achukue fomu kugombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
 
Pia kundi la Wachungaji wa Makanisa ya Pentekoste kutoka maeneo kadhaa nchini, yalikwenda Dodoma kumshawishi Lowassa kugombea nafasi hiyo.
 
Chikawe alisema uzoefu unaonyesha kuwa kila inapofikia wakati wa kuelekea katika chaguzi mbalimbali, hutokea matukio ambayo mengine yakiashiria uvunjifu wa usalama na utulivu wa nchi.
 
Alisema matukio hayo yanasababisha hamasa za kisiasa au baadhi ya watu kutumia muda kutekeleza ajenda zao za kihalifu kwa kisingizio cha vuguvugu la kisiasa.
 
Waziri huyo alikumbushia matukio ya hivi karibuni Visiwani Zanzibar kulikuwa na matukio ya baadhi ya ofisi za vyama vya kisiasa kuchomwa moto na watu wasiojulikana pamoja na wanachama wa vyama hivyo kuvamiwa na kujeruhiwa wakati wakitoka katika mikutano ya kisiasa.
 
“Kwa vyovyote vile matukio kama haya yanaashiria uvunjifu wa amani na utulivu na ni lazima serikali ichukue hatua kuhakikisha kuwa yanadhibitiwa ili kila mwananchi awe huru kufanya shughuli zake za kisiasa, kijamii na kiuchumi bila hofu ya kufanyiwa uhalifu,” alisisitiza.
 
Aidha, alivishauri vyama vya siasa kuepuka kufanya ushabiki wa kubeba wanachama wao kutoka sehemu moja kwenda nyingine wanapoandaa mikutano na badala yake washirikishe wanachama waliopo sehemu husika kufanya mkutano.
 
Alisema utekelezaji wa jambo hilo utapunguza ushabiki wa kisiasa na tatizo la uvamizi wa wanachama wanapokuwa wanatoka kwenye mikutano ya mbali na maeneo yao pamoja na kupunguza mzigo wa ulinzi kwa askari.
 
MATAMKO YA VIONGOZI WA DINI NA JUKWAA
Tamko la serikali limekuja siku chache baada ya Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, kutakiwa kupeleka vielelezo 10 Polisi, ikiwamo hati ya usajili wa kanisa hilo, nyaraka za idadi ya makanisa anayomiliki, muundo wa uongozi wa kanisa lake na nyaraka za helikopta anayomiliki.
 
Vingine ni idadi ya nyumba na mali ambazo Kanisa linamiliki, muundo wa Bodi ya Wadhamini wa Kanisa pamoja na majina yao na makusanyo ya Kanisa.
 
Machi, mwaka huu, Jukwaa la Wakrsto Tanzania, lilitoa tamko la kuwataka waumini wake kujiandikisha kwa wingi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, kuisoma Katiba inayopendekezwa na kujitokeza kuikataa kwa kupiga kura ya hapana. Jukwaa hilo linaundwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (Tec), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT).
 
Pia, Taasisi za Kiislamu nchini zimetoa matamko mbalimbali ya kuwataka waumini kutoshiriki kura ya maoni kutokana na serikali kutopeleka bungeni Muswada wa Mahakama ya Kadhi.
 
Kwa sasa Tanzania ina vyama vya siasa 22 vyenye usajili wa kudumu na kimoja chenye usajili wa muda huku chama tawala ni CCM na vyama vikuu vya upinzani ni Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi, ambavyo wakati wa Bunge Maalum la Katiba, waliunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
 
UGAIDI 
Waziri Chikawe alisema serikali imejizatiti kiusalama katika kupambana na vitisho vya ugaidi kwa kuweka maofisa usalama hasa nyumba za ibada, ikiwa ni pamoja na kutumia mashine za kielektroniki zenye uwezo wa kutambua watu waliobeba vitu vya kusababisha milipuko.
 
Aidha, aliwatoa hofu Watanzania kuwa ulinzi umeimarishwa, hivyo waendelee na shughuli zao za kila siku.
 
Kauli ya Waziri Chikawe inakuja huku kukiwa na taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa kikundi cha kigaidi cha Al Shaabab kinalenga kushambulia mikoa ya Arusha, Mbeya, Mwanza na Dar es Salaam na baadhi ya vyuo vikuu.
 
Kuhusu kukamatwa kwa raia wa Tanzania, Rashid Mberesero, kwa tuhuma za kuhusika na tukio la mashambulizi katika Chuo Kikuu cha Garissa, nchini Kenya, alisema anachojua ni kuwa amefikishwa mahakamani, lakini serikali haijapewa taarifa rasmi.
 
Chikawe alisema ugaidi ni tatizo la kidunia na kuwaomba wazazi kuwa karibu na watoto wao ili wasijiingize katika makundi au kushawishiwa kwa namna moja au nyingine kuingia katika makundi mabaya hasa kupitia mitandao ya kijamii. Aidha, akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua hatua zinazochukuliwa dhidi ya wageni wanaodaiwa kuingia kwa wingi nchini, alisema kila mgeni anayeingia nchini wizara hiyo ina taarifa zake na wanaoingia kinyume cha sheria hurudishwa nchini kwao.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa