Home » » MINYUKANO YA UCHAGUZI TANGU 1958

MINYUKANO YA UCHAGUZI TANGU 1958

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Hayati Mwalimu Julius Nyerere
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imepanga Oktoba 25 mwaka huu kuwa siku ambayo Watanzania watakuwa wanapiga kura kuwachagua viongozi wapya katika nafasi za udiwani, ubunge na urais.
Historia inaonyesha kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa 14 tangu nchi ianze kuwa na mfumo wa kuchagua viongozi wake.
Hata hivyo, tofauti na chaguzi zingine, uchaguzi wa mwaka huu utakuwa na changamoto mpya kwa chama tawala CCM, kutokana na kuwa vyama vinne vya upinzani; Chadema, CUF, NLD na NCCR-Mageuzi, vimeamua kuungana na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vikiwa na lengo la kupambana na CCM kuhakikisha vinaing’oa madarakani.
Ukawa wamekubaliana kumsimamisha mgombea mmoja wa urais, ubunge katika jimbo husika na diwani kupambana na mgombea wa CCM.
 Historia ya uchaguzi
Historia ya uchaguzi nchini inaweza kugawanywa katika makundi matatu; Chaguzi tatu chini ya mfumo wa vyama vingi zilifanyika enzi za Tanganyika, chaguzi hizo mbili zilifanyika kabla ya uhuru mwaka 1958 na 1960  na uchaguzi wa tatu ulizofanyika Novemba Mosi mwaka 1962 baada ya uhuru, kabla ya Tanganyika kuungana na Zanzibar.
Baadaye kukafuatia miongo mitatu ya utawala wa chama kimoja na kulifanyika chaguzi sita; uchaguzi wa mwaka 1965, uchaguzi wa 1970, uchaguzi wa 1975, uchaguzi wa 1980, uchaguzi wa 1985 na uchaguzi wa mwaka 1990.
Mfumo wa vyama vingi ulirejeshwa nchini mwaka 1992 na tangu wakati huo kumekuwa na chaguzi nne; uchaguzi mkuu wa 1995, uchaguzi wa mwaka 2000, uchaguzi wa mwaka 2005 na uchaguzi wa mwaka 2010. Katika historia hiyo, kumekuwa na chama kimoja tu ambacho ndicho kimeendelea kutawala, CCM kilichoundwa mwaka 1977 baada ya muungano wa vyama viwili vya TANU na ASP.
 Uchaguzi wa kwanza uliofanyika nchini 1958 kwa ajili ya kuchagua wabunge ulikuwa ukijulikana kama uchaguzi wa karata tatu. Uchaguzi huo ndio uliopima ukomavu na nguvu ya Tanu kama sehemu ya maandalizi ya kuondokana na utawala wa kikoloni.
 Uchaguzi wa karata tatu
Uchaguzi huo ndiyo uliopima ukomavu na nguvu ya Tanu kama sehemu ya maandalizi ya kuondokana na utawala wa kikoloni.
Katika uchaguzi huo, wapigakura walitakiwa kuchagua mgombea mmoja kutoka kila kundi: Mwafrika, Mhindi na Mzungu, hivyo kupata wagombea watatu. Kwenye kitabu chake cha Modern History of Tanganyika alichotunga 1976, Mwanahistoria wa Kiingereza  John Iliffe alisema, uchaguzi wa aina hiyo ulidhaniwa kuwa ungemaliza migongano. Hata hivyo, serikali ya kikoloni iliweka sifa ya mpigakura kuwa ni pamoja na kipato cha Paundi 150 kwa mwaka, elimu ya miaka minane au kuwa na ofisi inayotambulika.
Mwanzoni sifa hizo zilipingwa na Tanu ambayo ilitishia kujitoa kwenye uchaguzi huo, ikisema kuwa Waafrika wengi maskini, wasiokuwa na ajira wangezuiwa kupiga kura. Lakini baadaye kikundi cha wanasiasa wa Tanu chini ya Mwalimu Nyerere, kiligundua kuwa kugomea uchaguzi huo kungechelewesha uhuru wa Tanganyika au kungetoa mwanya wa ushindi rahisi kwa chama pinzani cha United Tanganyika Party (UTP) kilichokuwa kikiendeshwa na walowezi wa kizungu.
Katika mkutano wake wa mwaka, uliofanyika Januari 1958, Tanu kilikubali kushiriki uchaguzi huo.  Wakati huo pia Tanu ilikuwa na migogoro ya ndani iliyosababisha mmoja wa waanzilishi wake, Zuberi Mtemvu, kujitoa na kuanzisha chama kipya cha African National Congress (ANC).
Pamoja na tofauti hizo, Tanu ilifanikiwa kupata ushindi mnono baada ya kupata viti 28 kati ya viti 30 vilivyokuwa vikishindaniwa.  Mwaka 1960 ulifanyika uchaguzi wa wabunge na Tanu kikaendeleza ushindi wake kwa kupata viti  70 kati ya viti 71 vilivyokuwa vikishindaniwa.
Tanganyika ilipata uhuru wake Desemba 9, 1961 na Mwalimu Nyerere akawa Waziri Mkuu chini ya usimamizi wa Malkia Elezabeth wa Uingereza. Januari mwaka 1962, Mwalimu Nyerere alijiuzulu wadhifa huo na Rashidi Kawawa akachukua nafasi yake. Nchi ikawa Jamhuri na ilianza kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa rais Novemba 1962. Katika uchaguzi huo wa rais, Chama cha Tanu kilikabiliana na Chama cha ANC na wapigakura milioni 1.8 walijiandikisha.  TANU ilishinda kwa asilimia 98.15 na Nyerere akawa Rais wa Tanganyika.
Baada ya uchaguzi huo Tanganyika ikawa taifa la chama kimoja cha siasa na mwaka 1964 iliungana na Zanzibar na kuunda Tanzania.
Wakati wa demokrasia ya chama kimoja, utaratibu wa uchaguzi uliokuwapo ni Kamati ya Utendaji ya Tanu kuchagua watu wawili na kuwapeleka kwa wapigakura kwa ajili ya kumpata mbunge. Lakini katika nafasi ya kiti cha urais, utaratibu huo ulikuwa unamhusisha mtu mmoja aliyechaguliwa na Mkutano Mkuu wa vyama vya Tanu na ASP.  Baada ya mtu huyo kupita, alitakiwa kuthibitishwa na mkutano wa uchaguzi. Wapigakura walikuwa wanapiga kura ya ndiyo au hapana.
Mfumo huo wa uchaguzi, ndiyo uliomchagua Mwalimu Nyerere bila kupingwa katika kipindi chote cha utawala wake yaani mwaka 1965, 1970, 1975 and 1980, akiwa anashinda kwenye chaguzi hizo kwa zaidi ya asilimia 90. Mwalimu Nyerere alistaafu mwaka 1985 na CCM ikamchagua Ali Hassan Mwinyi kuwa rais. Hata hivyo, kulikuwa na mabadiliko makubwa mawili, kabla ya uchaguzi wa mwaka 1985: kuanzishwa kwa mfumo wa ukomo wa uongozi kwa nafasi ya rais na kupungua kwa umri wa mpigakura kutoka miaka 21 hadi 18.
Mwaka 1992 nchi iliingia katika mfumo wa vyama vingi. Mwaka 1995, Tanzania ikaingia rasmi kwenye uchaguzi chini ya mfumo huo wa vyama vingi, ikiwa ni miaka 33 tangu uchaguzi wa kwanza ulipofanyika mwaka 1962. Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 1995, CCM ilimteua Benjamin William Mkapa na akashindana na watu watatu kutoka vyama vya upinzani: Augustine Mrema aliyekuwa anakiwakilisha Chama cha NCCR- Mageuzi. Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF na John Cheyo wa UDP. Katika uchaguzi huo Mrema ndiye aliyeonekana tishio kwa CCM, lakini mwishoni Mkapa alishinda uchaguzi huo kwa kupata wa asilimia 61 ya kura zilizopigwa na Mrema alipata asilimia 27.
Miaka mitano baadaye, Mkapa alishinda tena kwa asilimia 71, akifuatiwa na Profesa Lipumba aliyepata asilimia 16, NCCR haikusimamisha mgombea katika uchaguzi huo na Mrema ambaye wakati huo alikuwa ametoka NCCR na kujiunga na Chama cha Tanzania Labour (TLP) alipata asilimia saba.
Mwaka 2005 CCM ikamteua Jakaya Kikwete kuwa mgombea wake wa urais na alishinda kwa asilimia 80, akifuatiwa na Profesa Lipumba aliyepata asilimia 11. Rais Kikwete alifanikiwa kutetea nafasi yake hiyo mwaka 2010 alipopata asilimia 62, akifuatiwa na Dk Willibroad Slaa wa Chadema ambaye alikuwa wa pili baada ya kupata asilimia 27.
Mwaka huu, Watanzania wanaingia tena katika Uchaguzi Mkuu unaovishirikisha vyama vingi tena kukiwa na ushirikiano wa baadhi ya vyama vya upinzani.
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa