Home » » Kaimu Msimamizi wa uchaguzi Singida mjini atupilia mbali pingamizi la CHADEMA dhidi ya mgombea wa CCM

Kaimu Msimamizi wa uchaguzi Singida mjini atupilia mbali pingamizi la CHADEMA dhidi ya mgombea wa CCM

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

DSC01221
Kaimu msimamizi wa uchaguzi jimbo la Singida mjini, Gerald Muhabuki Zephyrin,akizungumza na Modewjiblog juu ya uchaguzi ubunge jimbo la Singida mjini.(Picha na Gasper Andrew).
Na Nathaniel Limu, Singida
PINGAMIZI lililowekwa na Chama Cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA),jimbo la Singida mjini, dhidi ya mgombea wa CCM Mussa Ramadhan Sima kuwa fomu zake haziko sawa kwa mujibu wa kanuni,taratibu na sheria za uchaguzi,limetupiliwa mbali kwa madai kwamba halina mashiko.
Akizungumza na mwakilishi wa Modewjiblog ofisini kwake, kaimu msimamizi wa uchaguzi jimbo la Singida mjini,Gerald Muhabuki Zephyrin, alisema kuwa CHADEMA iliwasilisha pingamizi kwamba barua ya kumthibitisha Sima kugombea ubunge kupitia tiketi ya CCM, imesainiwa na mtu ambaye hakubaliki kisheria.
Akifafanua, alisema mgombea wa jimbo la Singida mjini kupitia CHADEMA, Msindai Mgana Izumbe, amelalamikia barua hiyo kuwa imesainiwa na  Mary Maziku, kwa madai sio katibu halisi wa mkoa wa Singida.
Gerald alisema katika  kujiridhisha kama kweli Maziku sio mtu stahiki wa kumuthibitisha mgombea wa CCM kwenye nafasi ya ubunge jimbo la Singida mjini,aliwasiliana na makao makuu CCM Lumumba jijini Dar-es-salaam,na kujibiwa kwa barua kwamba Maziku ndiye katibu wa CCM mkoa wa Singida.
“Mgombea Msindai ambaye alikuwa mwenyekiti CCM mkoa hadi kumalizika kwa mchakato wa kura za maoni,katibu wake wa mkoa kwa wakati huo, alikuwa Mary Chatanda ambaye nafasi yake imechukuliwa na Mary Maziku kipindi cha mchakato wa kura za maoni unaendelea.Maziku ndiye aliyesaini barua ya kumthibitisha Sima”,alifafanua zaidi.
Katika hatua nyingine,Gerald ambaye ni mkuu wa idara ya utumishi na utawala manispaa ya Singida,amesema kuwa aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Singida mjini,Victoria John Msusu kupitia UPDP,ameeguliwa kwenye kinyang’anyiro hicho baada ya kushindwa kutimiza masharti ikiwemo kushindwa kuwasilisha fomu kwa wamadai na kushindwa kulipa ada ya fomu shilingi 50,000.
Msimamizi amewataja wagombea wa ubunge wa jimbo la Singida mjini waliopitishwa na chama kwenye mabano kuwa ni ni pamoja na Sima (CCM),Jeremia Paulo Wandili (ACT Wazalendo),Msindai Mgana Izumbe (CHADEMA) na Mwanamvua John Haji (CUF).
Alisema kampeni zimeishaanza vizuri kwa amani na utulivu mkubwa na amewaoomba wagombea kufanya kampeni kwa ustarabu na kuzingatia kanuni,taratibu na sheria za uchaguzi.
“Matarajio ya wananchi wa jimbo la Singida mjini,ni kwamba oktoba 25 mwaka huu,wapige kura kuwachagua viongozi wanaoamini watawaletea maendeleo ya kweli na si vinginevyo”, alisema Gerald.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa