MJUE MGOMBEA URAIS ANNA MGHWIRA KUPITIA CHAMA CHA ACT-WAZALENDO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Anna Mghwira ni Mwenyekiti wa kitaifa wa chama kipya cha siasa, ACT – Wazalendo. Alizaliwa Januari 23, 1959 katika hospitali ya Mkoa wa Singida, Kata ya Mungumaji, Kitongoji cha Irao Manispaa ya Singida Mjini. (Januari mwaka huu alitimiza miaka 56). Baba mzazi wa Anna alikuwa diwani na kiongozi wa Tanu kabla ya CCM hadi mwaka 1985, mama yake alijishughulisha na kilimo na ufugaji na wazazi hawa kwa ujumla walipata watoto tisa, akiwamo Anna.

Mgwira alianza safari ya kielimu katika Shule ya Msingi Nyerere Road mwaka 1968 – 1974 akaendelea na sekondari kwenye Shule ya Ufundi Ihanja kati ya mwaka 1975 – 1978 kabla ya kuhitimisha masomo ya juu ya sekondari (kidato cha V na VI) Lutheran Junior Seminary kati ya mwaka 1979 – 1981. Aliendelea na masomo ya chuo kikuu mwaka 1982 baada ya kujiunga Chuo Kikuu cha Thiolojia (Chuo Kikuu cha Tumaini) na kuhitimu Shahada ya Thiolojia mwaka 1986. Mwaka huohuo, alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kusomea shahada ya Sheria.

Kati ya mwaka 1987 – 1998, aliendelea na shughuli za ujenzi wa Taifa, akifanya kazi ndani na nje ya nchi na kupata uzoefu mkubwa. Safari ya elimu ya Mghwira ilikamilikia Chuo Kikuu cha Essex, Uingereza ambako alianza Shahada ya Uzamili ya Sheria (LLM) mwaka 1999 na kutunukiwa mwaka 2000.

Licha ya kuwa mwanasheria na mtheologia aliyebobea, pia amefanya kazi za maendeleo kwa muda mrefu na ana uzoefu katika uendeshaji wa Serikali za Mitaa, utumishi katika mashirika ya kimataifa, kitaifa na mashirika ya dini ambamo amejihusisha na masuala ya wanawake, watoto, wakimbizi, utawala na haki za binadamu. Mghwira ana historia ya kupenda siasa, masuala ya jamii na michakato ya maendeleo kama inavyojidhihirisha katika maandiko yake mbalimbali katika majarida na magazeti ya hapa ndani ya nchi.

Alianza siasa tangu wakati wa Tanu akiwa mwanachama wa Umoja wa Vijana wa Tanu (Tanu Youth League) na aliwahi kushinda tuzo mbalimbali kutokana na ushiriki wa juu katika Tanu lakini baadaye ilipoanzishwa CCM alipunguza ushiriki wake ili ajipe muda katika masomo na baadaye ndoa na malezi ya watoto.

Kwa kipindi kirefu, hakuwa anajihusisha na siasa hadi alivyoamua kujiunga na Chadema mwaka 2009 ambako alishika nafasi mbili tu za uenyekiti wa baraza la wanawake ngazi ya wilaya na katibu wa baraza la wanawake mkoa. Machi mwaka huu alijiunga rasmi na ACT – Wazalendo na katika Mkutano Mkuu wa kwanza wa chama hicho, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa ACT.
Aliolewa na Shedrack Maghwiya tangu mwaka 1982 na walibahatika kupata watoto watatu wa kiume: Fadhili, Peter na Elisha. Hata hivyo, kwa bahati mbaya, mumewe hivi sasa ni marehemu.

Mbio za ubunge

Mghwira alijitosa katika mbio za ubunge kwa mara ya kwanza Januari 2012 baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza uchaguzi mdogo katika Jimbo la Arumeru Mashariki baada ya kifo cha Solomon Sumari. Alishiriki kura ya maoni ndani ya Chadema akihitaji kupewa ridhaa. Hata hivyo, chama hicho kilimpitisha Joshua Nassari (Josh) na Mghwira alikuwa na kazi ya kuendelea kumuunga mkono hadi ushindi ulipotangazwa kwa chama hicho. Pia, amewahi kugombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki, kupitia Chadema japokuwa hakuchaguliwa kushikilia wadhifa huo.

Mbio za urais

Mghwira hajatangaza kuwa atagombea urais. Ila, tafiti kadhaa na maoni ya Watanzania zinaonyesha kuwa yeye ni miongoni mwa viongozi wa kisiasa ambao wamejipambanua hivi karibuni na kuonyesha uwezo mkubwa katika uwanja wa kisiasa na hivyo anapewa nafasi kubwa kuwa anaweza kupewa majukumu makubwa na anaweza kuyahimili.

Nguvu yake

Jambo la kwanza linalompa nguvu mwanamama huyu ni umahiri katika elimu. Yeye ni msomi nguli wa masuala ya sheria lakini ana shahada tatu za vyuo vikuu. Nchi yoyote ingependa pamoja na sifa nyingine, iongozwe na Rais ambaye elimu si kikwazo kwake. Kwa nchi kama Tanzania ambayo mfumo dume umewakandamiza wanawake kwa kipindi kirefu, Mghwira anakuwa mmoja wa wanawake wachache wenye uwezo mkubwa.

Kwa sababu Mghwira ni mwanamke imara na anayepambana kwa muda mrefu sasa. Kitendo tu cha yeye kuwa mwanamke ni baraka tosha kwa siasa za kisasa ambazo zinaanza kuchangamkia, kukubali na kutafuta mchango wa wanawake katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Jinsia yake inampa fursa ya kuendelea kuaminiwa zaidi katika jamii ambayo inazidi kupoteza imani na uaminifu wa wanaume.

Lakini nguvu ya tatu ya Mghwira ni uthubutu. Ameniambia kuwa hata alipoingia katika ndoa bado alithubutu kujiendeleza kielimu bila kuchoka. Alipambana na changamoto za ndoa na shule. Wanawake wengi huchagua kufanya jambo moja na kuacha mengine, yeye alikwenda nayo yote na kuyakamilisha salama. Uwezo na uthubutu huu vinamfanya kuwa mwanamama imara anayeweza kukabidhiwa uongozi wa taasisi kubwa.


Mghwira ni mtu wa kuhoji kila jambo, si mwanamama “Ndiyo Mzee”. Wakati natafuta maoni ya watu waliowahi kufanya naye kazi katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, mtendaji mmoja aliniambia kuwa ukimpa Mghwira kazi ya harakati iliyo kwenye maandishi, hataondoka kwako hadi umpe taarifa za kina za kila jambo na atakuhoji hadi utachoka. Hata mtaalamu mshauri wa chama hicho Profesa Kitila Mkumbo ameniambia kuwa wakati wanafanya marekebisho ya katiba ya chama cha ACT walikabidhi kazi hiyo kwa jopo maalumu la wataalamu akiwemo Mghwira.

Profesa Kitila ananiambia kuwa kwa kiasi kikubwa katika timu hiyo, Mghwira ndiye aliyehoji na kutoa mapendekezo ya masuala mengi kuliko hata wataalamu wengine wa sheria ambao walikuwa wanaume.

Nilipojaribu kumfikia Mghwira kwa ajili ya kupata taarifa zake za kina na maisha binafsi, nilijikuta nashushiwa maswali matano mfululizo kiasi kwamba nilirudi kujipanga na kumtafuta tena. Huyu ni mwanasiasa wa kisasa ambaye anahoji kila jambo lililoko mbele yake, sifa hii wanaikosa wakuu wengi wa nchi.

Pamoja na kuwa na elimu kubwa, uzoefu wa kutosha wa kukaa nje ya nchi na kufanya kazi na taasisi za kitaifa na kimataifa, Mghwira ni mwanamama wa kawaida sana. Watu wa karibu naye wanamtaja hivyo. Si mtu wa kupoteza muda na mambo yasiyo na tija, anapenda kuandika makala za kuelimisha jamii, kufanya kazi na jamii na kujitolea na kujichanganya na wananchi wasio na uwezo na wenye kuhitaji msaada. Sifa zote hizi ni nguvu muhimu kwa binadamu yeyote ambaye anahitaji uongozi mkubwa wa nchi.

Udhaifu wake

Udhaifu mkubwa nilioubaini na hata kujulishwa na watu wa karibu naye ni kuwa yeye ni mwanasiasa mpole sana. Nimeambiwa kuwa ni mpole kupita kiasi na mara nyingi huwa anakuwa msikilizaji mzuri kabla hajaanza kuhoji mambo mfululizo. Moja ya sifa muhimu za Rais ajaye ni uwezo wa kuwa mpole na mkali kutegemeana na mazingira.

Kiwango cha upole cha mwanamama huyu kinazidi kiwango cha ukali alionao na naliona kama ni jambo linalopaswa kufanyiwa kazi kwa sababu Taifa letu lilipofikishwa, mara kadhaa nimesisitiza kuwa tunahitaji kiongozi anayeweza kumudu hali zote mbili.

Lakini udhaifu wa pili mkubwa wa Mghwira ni kutojijenga kisiasa ndani ya nchi. Katika siasa, bado namuona kama mchanga, hajakomaa na kuwa na uwezo mkubwa kiasi cha kujipa jina kubwa kwa jamii.

Mchango wake katika jamii ni mkubwa kwa sababu amewahi kusimamia masuala mengi ya kijamii na kisheria yanayoonekana, lakini ninachokisema hapa ni kuwa, chama chochote kile kina jukumu la kusimamisha kiongozi ambaye anajulikana katika tasnia za siasa. Kutojijenga na kuwa juu tokea alipokuwa Chadema nakuchukulia kama udhaifu ambao anahitaji kuufanyia kazi.

Nini kinaweza kumfanya apitishwe?

Kama ACT - Wazalendo kitampitisha mwanamama huyu kuwa mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, sababu ya kwanza ya kufanya hivyo inaweza kuwa ni ile dhana ya kumpa mwanamke nafasi. Chama anachotoka ndicho peke yake kimeweza kumpa mwanamke nafasi ya juu ya uongozi, nadhani pia bado chama hicho kinaweza kumpa jukumu kubwa zaidi ya hilo kwa sababu tayari kimeshajijengea misingi ya kuwajenga kina mama.
Lakini ikiwa Mghwira atapitishwa, uzoefu wake kimataifa na katika masuala ya haki za binadamu na kushughulika na masuala ya kijamii kunaweza kuwa moja ya sababu. Mwanamama huyu amefanya kazi mbalimbali za kitaaluma na kijamii hapa Tanzania, Sweden, Marekani, Uingereza na nchi nyingine za Afrika. Amekuwa mwalimu wa vyuo vikuu hapa Tanzania na msimamizi wa miradi mbalimbali ya kitaifa ya mashirika ya ndani na nje ya nchi. Uwezo na uelewa wake vinampa fursa ya juu ya kuteuliwa kugombea urais na kuonyesha kuwa kina mama wanaweza ikiwa wanapewa fursa sawa na wanaume.

Nini kinaweza kumwangusha?

Dhana ileile ya kijinsia inayombeba, pia ndiyo inayoweza kumuangusha. Ikiwa ACT kitadhani kuwa vyama vingine washindani vitasimamisha wagombea wanaume imara ambao wanaungwa mkono na mfumo dume uliotawala nchi hii, chama hicho kinaweza kumuweka nje Mgwira na kutafuta mwanachama mwingine “mwanamume” ambaye atakuwa na fursa ya kupambana na wanaume wengine kutoka vyama vingine na kuangaliwa na jamii “ambayo kwa kiasi kikubwa bado inatawaliwa na wanaume”.

Lakini jambo la pili linaloweza kumwangusha ni ugeni wake katika masuala ya kisiasa. Kama nilivyoeleza, Mghwira hana uzoefu wa uongozi wa juu wa kisiasa katika vyama, nadhani nafasi aliyonayo ndani ya ACT - Wazalendo ndiyo inayompa uzoefu wa kwanza wa siasa za kitaifa.

Lakini uzoefu wa jumla unaonyesha kuwa vyama mbalimbali hapa Tanzania huteua wagombea urais wake miongoni mwa wanachama wazoefu au wale waliowahi kushika madaraka muhimu katika chama kwa muda mrefu. ACT ikipiga hesabu hizi inaweza kabisa kumuweka nje mwanamama huyu.

Asipochaguliwa (Mpango B)

Ikiwa hatapewa fursa ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama chake, anaweza kuwa na mipango mitatu mezani:

Mpango wa kwanza ni kugombea ubunge katika jimbo mojawapo Tanzania. Bahati nzuri nimejulishwa kuwa moja ya majimbo anayojipanga kugombea ni pale Singida. Ikiwa ndivyo basi, mpango huu unaweza kumfaa kwa maana ya kuzidi kujifunza na kupata uzoefu wa siasa za Tanzania kwa upana.

Lakini mpango wa pili ni kuendelea kufundisha vijana katika vyuo vikuu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri kwa wanafunzi na wa kisheria katika jamii. Katika masuala haya ana uzoefu mkubwa nayo na itakuwa tu ni kiasi cha kuendelea pale alipoishia.

Nadhani mpango wa tatu ni kuendelea kuongoza chama cha ACT - Wazalendo. Nimeambiwa kuwa uongozi (Uenyekiti wake) unapaswa kuisha Februari, 2020. Ikiwa ndivyo nadhani ana fursa njema ya kuendelea kufanya uongozi.


Hitimisho

Mgwira ni mwanasiasa na kiongozi wa chama kipya ambacho kimeanzishwa na wanachama wengi waliotoka Chadema. Safari yake kisiasa na hata ugombeaji wa nafasi nyingine kubwa za nchi kwa namna moja au nyingine, lazima utaathiriwa na ustawi au uzorotaji wa Chadema. Ikiwa Chadema kitazidi kukubalika kwa Wwatanzania na kuwa chama kinachoimarika zaidi kuishinda ACT, ndiyo kusema kuwa yeye na wenzake watakuwa na wakati mgumu kujipambanua kisiasa na hivi ndivyo siasa za Afrika hutizamwa.

Pamoja na sintofahamu hizo, namuona Mgwira kama mmoja wanasiasa watulivu na wenye maono mapana katika Taifa hili. Kwa maneno yake yeye mwenyewe amenieleza kuwa “Natamani siku moja nchi hii iongozwe kwa misingi ya udugu na kusaidiana, kwa misingi ya malezi ya maadili bora kama alivyofanya Mwalimu Nyerere. Mimi nimekulia kwenye familia kubwa sana lakini wazazi wetu walitulea sote kama ndugu na tuliishi kwa furaha kubwa, nina ndoto kuwa Tanzania ijayo ipite katika njia hiyo.”

Ninachoweza kusema kwa sasa ni kumwombea mama huyu nguli wa upinzani na kumtakia safari njema katika nia zake za kisiasa ikiwamo hii ambayo ametajwa kwamba ana sifa za kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Julius Mtatiro: Ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii; ana uzoefu mkubwa wa uongozi wa kisiasa hapa Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi na Lugha, Shahada ya Sanaa (B.A) katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (LLB) – Anapatikana kupitia +255787536759.
Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni yake binafsi.

Chanzo: Mwananchi, Mei 18, 2015

MO AMPIKU DANGOTE MFANYABISHARA BORA AFRIKA‏

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. MO dewji
Vinara wa biashara Afrika walipewa tuzo mbalimbali za African Business katika picha ya pamoja. Kuanzia kushoto ni Daphne Mashile Nkosi, Strive Masiyiwa, Helen Hai na Mohammed Dewji . hafla ya utoaji wa tuzo hizo ilifanyika hoteli ya Four Seasons Hotel mjini New York.(Picha na African Business).
Na Mwandishi wetu, New York
MTANZANIA Bilionea Mohamed Dewji amepata tuzo ya Mfanyabiashara Bora wa Afrika wa mwaka 2015, katika kinyang’anyiro cha tuzo za wafanyabiashara bora wa Afrika (African Business Awards 2015).
Dewji maarufu kama Mo alikabidhiwa tuzo hizo usiku wa kuamkia jana mjini New York.
Katika hafla hiyo iliyofanyika katika hoteli ya Four Season mkabala na jengo la Umoja wa Mataifa (Baraza Kuu) watu wengine waliopata tuzo ni Aliko Dangote, Daphne Mashile Nkosi, Strive Masiyiwa na Helen Hai.
MO alimshinda Aliko Dangote ambao walikuwa kwenye Kategori moja wakiwania tuzo hiyo ya mfanyabiashara bora wa Afrika, huku wengine walioshindanishwa kwenye kategori hiyo ni CEO wa Paramount Group, Ivor Ichikowitz, CEO wa Groupe Loukil, Groupe UADH, Bassem Loukil, na Oscar Onyema DG wa Nigerian Stock Exchange.
Tuzo hizo zimeandaliwa na jarida la African Business .
Pia katika tuzo hizo taasisi kadhaa zinazofanya vyema bara la Afrika zilitambulika. Taasisi hizo ni pamoja na kiwanda cha sementi cha Dangote , Guaranty Trust Bank, Abellon Clean Energy, Nigerian Stock Exchange na taasisi ya bima kwa masoko yanayochipukia ya BIMA.
Akielezwa wasifu wake katika hafla hiyo, Mo ameelezwa kama mfanyabiashara aliyefanikiwa kutokana na kuongeza kipato na ukubwa wa kampuni ya Mohammed Enterprise toka aitwae kutoka kwa baba yake.
Akiwa mtendaji wa kampuni hiyo, akiwa katika miaka ya 40 amefanya mabadiliko makubwa katika makampuni mbalimbali ya umma yaliyoshindwa kujiendesha katika sekta ya kilimo, viwanda na maeneo ya makazi na viwanda.
Uongozi wake uliwezesha kampuni hiyo ya MeTL kufanya makubwa kiasi cha kumfanya aingie katika jarida la Forbes la matajiri wa Afrika.
Majaji waliompa tuzo kwa mwaka huu walisema kwamba uongozi wake umewezesha biashara katika kampuni hiyo kuchupa kutoka dola za Marekani milioni 30 hadi bilioni 3.
Akipokea tuzo hizo Dewji alisema kwamba tuzo hiyo ni ishara muhimu kwa waafrika wote na uwakilishi wa uhakika wa vijana katika masuala ya ujasirimali.
DSC_0310
Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya MeTL Group, Mohammed Dewji.
Tuzo ya Biashara ya Mwaka ilienda kwa kiwanda cha saruji cha Dangote kinachoongozwa na bilionea wa Afrika, Aliko Dangote.
Kiwanda hiki kilichopo Nigeria kimejipanga kusambaza uzalishaji katika nchi nyingine za Afrika, hatua ambayo imeifanya tuzo hiyo kuwa ya kwao.
Akipokea tuzo hiyo Aliko alisema amefurahishwa sana na tuzo hiyo ya thamani kubwa na kwamba imetolewa wakati ambapo kiwanda hicho kinatanua shughuli zake kuhakikisha ukombozi wa uchumi kwa nchi za Afrika unafanyika kwa dhati.
“Tunaamini katika Afrika. Tunaamini kwamba katika kuhakikisha kuna uwekezaji mkubwa wa miundombinu Afrika itaweza kusonga mbele katika uchumi wake”.
Daphne Mashile Nkosi, Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya manganisi ya Kalagadi ya Afrika Kusini alipokea tuzo mwanamke bora katika biashara. Majaji walimpa tuzo hiyo kwa kuwa ameonesha mafanikio makubwa katika sekta ambayo kwa kawaida huendeshwa na wanaume.
Mdada huyo anatambulika kwa kuwezesha kupatikana kwa ajira 30,000 huko Northern Cape, na ni muasisi wa mgodi wa aina yake katika kipindi cha miaka 30.
Mfanyabiashara wa Zimbabwe, mjasiriamali, anayependa kusaidia watu wenye mahitaji Strive Masiyiwa alipata tuzo ya mafanikio katika maisha.
CPoF_XCWcAAyCO6
Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya MeTL Group, Mohammed Dewji akipokea tuzo yake.
Strive ambaye ni mmoja wa waanzilishi na Mwenyekiti Mtendaji kwa kampuni ya kimataifa ya mawasiliano ya simu Econet Wireless amepewa tuzo hiyo kwa mafanikio yake na pia kwa misaada mingi aliyotoa kwa vijana.
Masiyiwa ametumia utajiri wake kusomesha vijana zaidi ya laki moja wa Afrika katika kipindi cha miaka 20.
“Ni heshima kuu kupata nafasi ya kuthaminiwa na jarida lako, Ni heshima kuwa miongoni mwa marafiki… tafadhali endelezeni kazi hii njema,” alisema akizungumza kwa njia ya video.
Tuzo ya mfanyabiashara wa Mfano imeenda kwa Helen Hai, Mtendaji mkuu wa Made in Africa Initiative.
Tuzo hii kwa kawaida hutolewa kwa mtu aliyetoa mchango mkubwa katika kuboresha hali ya ufanyaji biashara barani Afrika.
Helen ambaye ana asili ya China amewezesha mabadiliko makubwa katika biashara ya viatu ya Ethiopia baada ya kuanzisha kiwanda cha viatu cha Huajian Oktoba 2011 baada ya kuwa na mkutano na rais wa nchi hiyo Meles Zenawi mwaka huo huo.
Imeelezwa kuwa kiwanda hicho mara baada ya kuanzisha katika kipindi cha miezi sita tu waliweza kuongeza pato la mauzo ya nje ya nchi hiyo kwa mara mbili na katika kipindi cha miaka miwili kiliajiri waethiopia 4000.
Sasa hivi mdada huyo amefungua kiwanda cha nguo nchini Rwanda.
“Sekta binafsi haikuja Afrika kutoa msaada, tumekuja afrika kufanyabiashara. KLakini katika biashara tunatekeleza maelengo ya maendeleo. Nina imani kubwa na Afrika, naamini kupitia simulizi za mafanikio tunashawishi wengine kujiamini kutwaa uongozi na kuliwezesha bara hili kutambua fursa zake,” alisema Helen.
Guaranty Trust Bank, iliwashinda wengine kadhaa waliotajwa na kushinda tuzo ya utawala bora wakati Abellon Clean Energy ilipata tuzio ya ubinifu wakati Nigerian Stock Exchange ilipata tuzo ya urejeshaji kwa jamii faida ikiwa ni huduma bora za jamii.
Akizungumzia tuzo hizo ambazo ni za sab, Omar Ben Yedder alisema hafla hiyo imwezeshwa na Zenith Bank, GTBank, Agility na Cofina .
Washindi wa 2015
AFRICAN BUSINESS OF THE YEAR
-Dangote, Nigeria
BUSINESS LEADER OF THE YEAR
-Mohammed Dewji, CEO, Mohammed Enterprise, Tanzania
MOST OUTSTANDING WOMAN IN BUSINESS
-Daphne Mashile Nkosi, Executive Chairperson, Kalagadi Manganese, South Africa
AWARD FOR GOOD CORPORATE GOVERNANCE
-Guaranty Trust Bank, Nigeria
AWARD FOR BEST CORPORATE SOCIAL RESPONSIBILITY
-The Nigerian Stock Exchange, Nigeria
AWARD FOR INNOVATION
-Abellon Clean Energy, Ghana
INSURANCE COMPANY & INITIATIVE OF THE YEAR
-BIMA ( bimamobile.com )
LIFETIME ACHIEVEMENT AWARD
-Strive Masiyiwa
AFRICAN BUSINESS ICON
-Helen Hai

Chama cha ACT WAZALENDO chazindua kampeni zake za Ubunge jimbo la Manyoni

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
SAM_0108baadhi ya wagombea ubunge wa chama cha ACT Wazalendo waliohudhuria mkutano wa uzinduzi katika jimbo la Manyoni-Singida.
Na, Jumbe Ismailly, Manyoni       
CHAMA Cha ACT Wazalendo wilaya ya Manyoni Mkoani Singida kimezindua kampeni za ubunge wa jimbo la Manyoni mashariki kwa kumnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo,Muttee John Henry na kuwatisha watendaji wa idara ya afya wanaouza madawa kwenye vituo vya kutolea huduma na hivyo kusababisha wananchi kukosa huduma katika vituo vya kutolea huduma hizo.
Akiwahutubia wananchi wa mji wa Manyoni na vitongoji vyake,mgombea ubunge wa jimbo la Manyoni mashariki kupitia tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo,Henry amesema vituo vingi vya kutolea huduma za afya vimekuwa vikikabiliwa na uhaba mkubwa wa madawa jambo linalowafanya wagonjwa wanaofuta huduma kutakiwa kwenda kununua dawa kwenye maduka ya madawa yaliyopo karibu na vituo hivyo.
Hata hivyo mgombea huyo alifafanua kwamba kutokana na kuwepo kwa tatizo kubwa la upatikanaji wa dawa,ni asilimia sita tu ya watanzania ndiyo wanaonufaika na mfuko wa afya ya jamii (CHF),hali inayoonyesha bado kuna idadi kubwa ya watanzania wanaopoteza maisha kwa kukosa huduma hizo za afya kwenye maeneo ya vijijini.
‘Ndugu zangu nchi hii asilimia sita tu ya wananchi wa Tanzania ndiyo wanaonufaika na mfuko wa afya ya jamii na asilimia 98 ya wakulima,wafugaji,bodaboda,mama lishe na wafanyakazi katika sekta isiyokuwa rasmi hawanufaiki na mfuko wa afya ya jamii(CHF)’’alifafanua Henry.
Kwa mujibu wa Henry,licha ya wananchi hao kupigania kuongeza uchumi kwa nguvu zote kwa kipindi cha miaka 35,wanapofikia umri wa miaka 60 huwa wamechoka na hivyo kujikuta wakisahaulika katika taifa lao walilolitumikia kwa kipindi kirefu katika maisha yao.
Aidha alisisitiza kwamba taifa linalowasahau wananchi waliolitumikia kwa miaka mingi ikilinganishwa na watumishi wa serikali ambao wanapostaafu hulipwa mafao yao ya kustaafu,hilo siyo taifa jema ambalo baba wa taifa alikuwa akijivunia.
Alisisitiza mgombea huyo kijana kwamba ni wakati muafaka sasa wa kuweka utaratibu wa kuwasaidia watanzania wanyonge  hao pale wanapochoka.
 Ili kukabiliana na hali hiyo ya ukosefu wa madawa kwenye vituo vya kutolea huduma,Henry alisema chama cha ACT Wazalendo kimetafakari sana na kuja na mpango mpya wa kuanzisha mfuko utakaowasaidia watanzania wanyonge.
“Najua fedha zetu tunazokusanya ni chache sana lakini mfuko wa wanyonge ambao utaweza kuhifadhi fedha kidogo kidogo ndiyo kimbilio la wanyonge wanaopata majanga ya kuugua basi wanapona kwa mfuko wa afya ya jamii”alifafanua.
Naye katibu wa Mkoa wa Chama Cha ACT Wazalendo,Lipu Loti Robert alisema idadi kubwa ya watendaji wamebainika kulihofia azimio la Arusha lililoachwa na baba wa taifa marehemu,Mwalimu Julius Nyerere na ndiyo maana waliamua kulivunja kwenye moja ya vikao vilivyofanyika Zanzibar.
Hata hivyo Roberti aliweka wazi kuwa ACT baada ya kubaini kutokuwepo kwa azimio la Arusha ndipo walipozindua azimio la Tabora ambalo lina mambo manne,ambayo ni pamoja na Hifadhi ya jamii,suala la uchumi shirikishi,sekta ya afya na sekta ya elimu.  
SAM_0105katibu wa ACT Mkoa wa Singida,Bwana Lipu Loti Robert akifungua mkutano wa uzinduzi wa kampeni kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Manyoni mashariki.
SAM_0106
Mmoja wa wakereketwa wa chama hicho akipeperusha bendera kwenye mkutano wa uzinduzi
SAM_0109
baadhi ya viongozi wa ACT waliohudhuria mkutano wa uzinduzi kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Manyoni mashariki.Picha zote na Jumbe ismailly
NA MO BLOG

LOWASSA ASIMIKWA KUWA KIONGOZI WA WANYATURU, MKOANI SINGIDA‏

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Mmoja wa wazee wa Kimila wa Kabila la Wanyaturu, Mzee Semani Nyambia akimvisha Mgombea Urais wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa, vazi la kimila (mgololi) ikiwa ni ishara ya kusimikwa kuwa mlezi wa Wanyaturu, wakati wa Mkutano wake wa Kampeni, uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Ilongero, Jimbo la Singida Kaskazini, leo Septemba 13, 2015.PICHA NA OTHMAN MICHUZI, SINGIDA.
Mgombea Urais wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa, akihutubia Mkutano wa hadhara wa Kampeni, uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Ilongero, Jimbo la Singida Kaskazini, leo Septemba 13, 2015. katika hotuba yake, Mh. Lowassa amesema iwapo atapata ridhaa ya wananchi kuwa Rais wa Tanzania, ataanzisha viwanda vya kusindika zao la alizeti, ili wakulima wa zao hilo waweze kufaidika na pia atakabiliana na kero zote za Mkoa wa Singida kwa ujumla. Mh. Lowassa, kesho Septemba 14, 2015 ataendelea na ziara yake ya Kampeni katika Mkoa Shinyanga, baada ya leo kumaliza katika Mkoa wa Singinda, kwenye Majimbo ya Manyoni Magharibi, Singida Kaskazini, Iramba Mashariki na Iramba Magharibi.
Mgombea Urais wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa, akimnadi Mgombea Ubunge wa UKAWA kupitia CHADEMA katika Jimbo la Singida Kaskazini, David Djumbe,  wakati wa Mkutano wake wa Kampeni, uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Ilongero, Jimbo la Singida Kaskazini, leo Septemba 13, 2015.
Mgombea Urais wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa, baadhi ya wagombea wa Udiwani wa maeneo mbalimbali ya Jimbo la Singida Kaskazini, wakati wa Mkutano wake wa Kampeni, uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Ilongero, Jimbo la Singida Kaskazini, leo Septemba 13, 2015.

Hawa wote wameahidi kuwapakura.
Vijana wa Ilongero wakifatilia kwa makini Mkutano huo.
Wananchi wa Ilongero, Singida Kaskazini wakifatilia kwa makini hotuba ya Mgombea Urais wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa.

Wakiperuzi picha za Mgombea wao.

Kina Bibi Mkutanoni.
Furaha toka moyoni.
Mzee Msindai akizungumza.
Chopa ikitua.































 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa