Home » » SERIKALI YARIDHISHWA WAHADZABE KUACHANA NA UJIMA.

SERIKALI YARIDHISHWA WAHADZABE KUACHANA NA UJIMA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SERIKALI wilayani Mkalama mkoani Singida imeridhishwa na kasi inayofanyika kuibadili jamii ya Wahadzabe kutoka kutegemea maisha ya ujima na kuanza kuishi maisha ya kawaida yanayoambatana na mabadiliko ya mazingira yaliyopo sasa.
Akizungumza na gazeti hili, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Christopher Ngubiagai kuhusu jamii hiyo ambayo chakula chao kikuu ni nyama, mizizi, matunda na asali ikiendelea kuishi kwenye viota katikati ya pori, alisema Halmashauri ya wilaya hiyo inafanya mapinduzi makubwa hasa kwa kufikisha elimu kwa watoto wao.
Wahadzabe ni miongoni mwa makabila madogo zaidi nchini linalopatikana kaskazini mwa Tanzania kando ya Ziwa Eyasi kwenye Bonde la Ufa na kupakana na uwanda wa Serengeti pia wapo katika wilaya ya Mkalama.
Jamii hiyo inayoaminika kuwa ni ya mwisho kabisa barani Afrika inayotegemea uwindaji kwa ajili ya kuishi, inatakiwa kubadilika taratibu kutokana na muingiliano wa kasi unaojitokeza na jamii ya wakulima na wafugaji wanaowazunguka.
Katika kuwezesha elimu kwa vijana, Halmashauri ya wilaya ya Mkalama inatoa chakula, nguo na kuendesha programu maalumu kwa ajili ya kuhudumia wanafunzi wa jamii hiyo waliopo katika shule ya msingi Munguli, kata ya Mwangeza iliyotengenezwa mahsusi kwa ajili ya watu wa jamii hiyo.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya alisema pamoja na kuwapo kwa wanafunzi wa jamii hiyo, shule hiyo pia hutumiwa na watu wengine ambao wapo hapo wa jamii ya Kisukuma, Wamang’ati na Wabarbaig.
Pamoja na halmashauri hiyo kutoa mambo hayo muhimu, taasisi za kijamii ikiwamo Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (Haydom - Mbulu) na asasi ya kiraia ya FFCC hutoa mchango wa chakula kuongeza nguvu kwa jamii hiyo kushiriki kikamilifu katika kupata elimu ya kawaida.
Ngubiagai alisema watoto wa jamii hiyo wana akili sana kutokana na jinsi wanavyoweza kushika kwa haraka kusoma, kuandika na kuhesabu na kwamba katika mtihani wa darasa la tatu, watoto wa jamii hiyo walishika namba moja hadi 10 huku Wahadzabe wengine wakifanya vyema katika stadi mbalimbali.
CHANZO ; HABARI LEO.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa