Home » » WATUMISHI 3 WASIMAMISHWA KAZI IRAMBA.

WATUMISHI 3 WASIMAMISHWA KAZI IRAMBA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KAIMU Mkuu wa Wilaya ya Iramba, mkoani Singida, Christopher Ngubiagai, ameagiza kusimamishwa kazi na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watumishi watatu wa halmashauri hiyo kwa tuhuma mbalimbali, ikiwamo matumizi mabaya ya madaraka.
Ngubiagai ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, mkoani humo alitaja tuhuma nyingine kuwa ni kushindwa kutoa ushauri makini na kusababisha upotevu wa fedha na nguvu za wananchi katika ujenzi wa bweni la wasichana la shule ya sekondari Kinyangiri wilayani Mkalama.
Aliwataja watumishi hao kuwa ni David Malegi, Mhandisi Msaidizi Ujenzi, Hashim Ndwata (Fundi Sanifu) na aliyekuwa Mratibu wa Mradi huo, Jeremiah Lubeleje ambaye kwa sasa amehamishiwa wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.
Alieleza kuwa mradi huo wa ujenzi wa bweni la wasichana ulianza Septemba 6, mwaka 2011 wakati wilaya ya Mkalama ikiwa haijagawanywa kutoka wilaya mama ya Iramba.
Ngubiagai alisema wafadhili wa mradi huo, Ubalozi wa Japan walitoa hundi ya Sh milioni 133.7 kwa ajili ya ujenzi wa bweni hilo ambapo halmashauri ilipewa jukumu la kusimamia, kutoa ushauri wa kitaalamu, kununua na kuweka vitanda na magodoro ujenzi utakapokamilika.
“Ujenzi wa hosteli hiyo ulikuwa ukamilike Aprili 18, mwaka 2012 lakini hadi hivi leo ( zaidi ya miaka minne) haujakamilika na jengo limekaa bila kutumika, huku wasichana waliopaswa kulitumia wakitembea kilometa 14 kwenda na kurudi hali inayowaathiri kitaaluma,” alisema Ngubiagai.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa licha ya ujenzi huo kutokamilika kama ambavyo mkataba ulielekeza, uongozi wa halmashauri ya Iramba pia umeshindwa kukabidhi bweni hilo kwa halmashauri ya wilaya ya Mkalama.
Kutokana na hali hiyo, alisema njia pekee ni kuwasimamisha kazi wahusika wa mradi huo ili uchunguzi wa kina ufanyike na ikithibitika wamehusika na tuhuma hizo hatua za ukiukwaji maadili ya utumishi wa umma zichukue mkondo wake.
Kusimamishwa kwa watumishi hao watatu kunafanya idadi ya waliosimamishwa katika halmashauri hiyo hadi sasa kufikia tisa. Februari mwaka huu watumishi sita wa Idara ya Afya nao walisimamishwa kwa tuhuma ya upotevu wa zaidi ya Sh milioni 145.2 za Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
CHANZO: HABARI LEO

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa