Home » » 'Kupanda bodaboda bila helmeti ni kudhamiria kujiua'

'Kupanda bodaboda bila helmeti ni kudhamiria kujiua'



Kutovaa helmeti kwagharimu maisha ya wapanda bodaboda Baadhi wapata ulemavu wa kupoteza kumbukumbu Polisi watangaza kiama kwa wasiovaa helmeti Na Shadrack Sagati BRUNO Sigala (24) amelazwa katika Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI) kwa miezi mitatu tangu alipoanguka na bodaboda mkoani Singida.
Katika ajali hiyo alivunjika mikono yote, mguu moja na alitikisika ubongo na sasa hana kumbukumbu. Ingawaje huu ni mwaka 2016. Lakini Sigala kwa kukosa kumbukumbu, anasema ni mwaka 2018.
Hali kadhalika, wakati amelazwa wodini hapo kwa takribani miezi mitatu hadi sasa, yeye anadai kwamba ana miaka mitano tangu afikishwe katika wodi hiyo ya wagonjwa wa mivunjiko! Wauguzi wanaomhudumia wanaeleza kuwa Sigala anasubiri kufanyiwa upasuaji wa mikono na mguu baada ya kuhamishwa kutoka katika wodi inayoshughulika na majeraha ya kichwa.
"Alipoanguka na bodaboda aliumia vibaya kichwani, migugu pamoja na mikono. Alipofikishwa hapa madaktari waliangalia kipaumbele kwanza ni ubongo, baada ya kupata ahueni katika majeraha yake ya kichwa ndipo alipohamishiwa katika wodi hii ili aendelee na matibabu ya miguu na mikono," anasema Ofisa Uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi.
Bruno Sigala ni kielelezo cha waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda ambao wanaanguka na kuumia vibaya kichwani kutokana na kutovaa kofia ngumu ya kinga yaani helmeti kwa kimombo.
Kijana huyo alikuwa anafanya biashara ya kubeba abiria kwa pikipiki na aligongwa na gari katika ajali iliyomfikisha Muhimbili. Katika ajali hiyo, Sigala aliumia kichwani, akajing’ata ulimi na kuvunjika mikono yote na mguu mmoja. Akijieleza kwa kubabaisha anakiri kuwa hakuwa amevaa kofia wakati anaendesha pikipiki.
"Sikuwa najua umuhimu wa kofia hiyo, kwani mafunzo yenyewe ya kuendesha nilijifunzia tu mitaani, nikaanza biashara ya kubeba abiria."
Kofia ngumu zimetengenezwa kwa lengo la kumlinda mwendesha bodaboda asiumie kichwa pale apatapo ajali. Baadhi ya kofia hizi zinatengenezwa zikiwa na sehemu ya kupitishia hewa, kufunika uso usiathirike kwa kioo maalumu ambacho hata kikivunjika hakileti madhara kwa mvaaji pamoja na kulinda masikio.
Mwendesha pikipiki yuko hatarini kupoteza maisha pale apatapo ajali kama hakuvaa kofia ngumu. Tafiti zinaonesha kuwa kofia ngumu hupunguza hatari ya mwendesha pikipiki kuumia kichwa pale apatapo ajali kwa asilimia 69 na inapunguza kifo kwa asilimia 42.
Takwimu zilizopo katika Taasisi ya Mifupa (MOI) ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambazo zinahusisha miezi sita, Machi 15 hadi Septemba 15, 2011, zinaonesha kwamba wapanda bodaboda wengi wanaojeruhiwa vibaya pale ajali za pikipiki zinapotokea, ni wale wasiovaa helmeti.
Wengi wao wanajeruhiwa vibaya kichwani. Daktari bingwa wa Magonjwa ya Mifupa katika Taasisi ya MOI, Dk Bryson Mcharo, anasema katika utafiti wake wa miezi 6 ukihusisha majeruhi wapatao 722, amebaini kuwa nusu ya majeruhi hao walipanda pikipiki bila kuvaa helmeti.
"Katika utafiti huo nilibaini kuwa madereva pikipiki ambao wanaona umuhimu wa helmeti ni wale ambao angalau wamepitia mafunzo ya udereva na wana leseni, lakini wengi wa majeruhi ambao hawakuvaa kofia hawana leseni na pia hawana mafunzo ya kuendesha pikipiki,” anaeleza Dk Mcharo.
"Karibia nusu ya majeruhi hao, asilimia 46, waliumia kichwani jambo linaloonesha kwamba madereva wengi na abiria wao hawazingatii uvaaji wa helmeti," anasema Dk Mcharo.
anasema kati ya majeruhi hao madereva wa pikipiki ndio wengi na zaidi ya nusu, asilimia 51.8, hawakuvaa helmeti.
Kwa mujibu wa Dk Mcharo, nusu ya majeruhi hao, walipata ajali baada ya kugongana au kugongwa na magari na asilimia 7 waligongana kati ya pikipiki na pikipiki huku asilimia 27 ni majeruhi waligongwa na pikipiki.
Mkuu wa Kitengo cha Dharura katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Juma Mfinanga, anasema mwaka 2015 walipokea majeruhi 8,400 waliotokana na ajali za barabarani kiwango ambacho ni asilimia 61 ya majeruhi wote wa ajali waliofikishwa katika kitengo hicho.
Dk Juma anafafanua kuwa kati ya majeruhi hao asilimia 71 walikuwa ni madereva, asilimia 46 walikuwa ni abiria wakati asilimia 39 walikuwa ni waenda kwa miguu. Anasema kwa mwaka huu kuanzia Januari hadi Julai pekee, majeruhi wa pikipiki waliofikishwa kwenye kitengo hicho ni 4,900 kiwango ambacho ni sawa na asilimia 64 ya majeruhi wote wa ajali za barabarani.
Anasema nusu ya ajali hizo (asilimia 51) ni majeruhi waliotokana na ajali za pikipiki, huku idadi ya wanaume ni mara tatu ya wanawake ya majeruhi wote waliofikishwa hospitalini hapo.
Dk Juma anasema majeruhi walioumia kichwani walikuwa ni asilimia 42 na kati ya hao asilimia 8 hadi 10 ni wagonjwa waliojeruhiwa vibaya na kupona kwao ni kwa kudra za Mwenyezi Mungu, huku asilimia 85 hadi 88 ni wale ambao wameumia kwa kiwango cha kati na asilimia 61 ya majeruhi hao walivunjika mifupa mirefu ambayo ni mikono na miguu.
Majeruhi waliohamishiwa katika taasisi ya mifupa ni asilimia 89.1 ya majeruhi wa pikipiki waliopokelewa kituoni hapo mwaka 2015. Kuhusu gharama, Dk Juma anasema gharama zinatofautiana kulingana na hali ya mgonjwa, lakini akasema kwa wastani hospitali inatumia zaidi ya Sh 650,000 kwa mgonjwa mmoja anayefikishwa katika kitengo cha tiba ya dharura kwa ajili ya kumtibia wakati wa dharura.
Uvaaji wa helmeti kwa dereva na abiria wa pikipiki ni moja ya masharti yaliyowekwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) wakati wa kutoa leseni kwa dereva wa pikipiki.
"Lazima awe na helmeti na abiria wake pia atatakiwa kuvaa kofia ya kujikinga wakati wote na kwamba kofia hiyo inatakiwa kuwa na alama ya eneo la utoaji huduma ya usafiri," inasema kanuni ya usafirishaji ya pikipiki za magurudumu mawili na matatu ya mwaka 2010.
Kanuni hiyo inatoa masharti kwamba dereva wa pikipiki ya magurudumu matatu kwamba haruhusiwi kubeba idadi ya abiria zaidi ya mmoja, dereva wa pikipiki anatakiwa kuvaa kofia ngumu ya kujikinga wakati wote yeye na abiria wake.
Lakini jambo hilo halifanyiki. Pikipiki nyingi zinazobeba abiria zinatisha, unaweza kukuta dereva na abiria wake hawajavaa helmeti, au dereva anayo lakini abiria hana. Wakati mwingine unaweza kukuta dereva kavaa na abiria kaishikilia mkononi au kuipakata.
Hili limechangia dereva na abiria kupoteza maisha pindi inapotokea ajali.
Hili ndilo limemfanya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kutahadharisha kwamba kupanda pikipiki bila kuvaa kofia ngumu ni dhamira ya kujiua, kwa sababu dereva na abiria wakipata ajali ni rahisi kupoteza maisha kwa kupigiza kichwa chini.
Makonda anawataka madereva wa bodaboda na abiria wao kuvaa helmeti. “Nimeshawasiliana na kamati yangu ya usalama barabarani mkoa. Hili nitalisimamia kikamilifu lazima wote wawe na helmeti,” anasema Makonda.
Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara wa Sumatra, Johansen Kahatano, anasema sheria ya Sumatra ya pikipiki inamtaka dereva wake avae helmeti wakati wote, kushindwa kufanya hivyo ni kuvunja sheria kwa makusudi. Kuhusu madai ya abiria kutopenda kuvaa hizo kofia, Kahatano anasema kwamba amekuwa anawashauri waendesha pikipiki wasipakie abiria ambao hawataki kuvaaa kofia ngumu.
"Usimamizi ni mgumu. Lakini tunaendelea kutoa elimu kwamba abiria akipanda pikipiki aone umuhimu wa kuvaa helmeti na kuthamini maisha yake. Hilo ni jambo la lazima. Sisi kama mamlaka tuna kazi ya kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuvaa kofia ," anasema Kahatano.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, hataki kumung’unya. Uvaaji wa kofia ngumu helmeti kwa waendesha pikipiki na abiria wao ni lazima. Yule ambaye atakaidi agizo hilo atakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria. Itaendelea kesho. Inserts "Karibia nusu ya majeruhi hao, asilimia 46, waliumia kichwani jambo linaloonesha kwamba madereva wengi na abiria wao hawazingatii uvaaji wa helmeti" “Majeruhi walioumia kichwani walikuwa ni asilimia 42 na kati ya hao asilimia 8 hadi 10 ni wagonjwa waliojeruhiwa vibaya na kupona kwao ni kwa kudra za Mwenyezi Mungu.” “Kupanda pikipiki bila kuvaa kofia ngumu ni dhamira ya kujiua, kwa sababu dereva na abiria wakipata ajali ni rahisi kupoteza maisha kwa kupigiza kichwa chini.”

Chanzo Gazeti la Habari leo

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa