Home » » Singida yazindua huduma tembezi za madaktari bingwa

Singida yazindua huduma tembezi za madaktari bingwa

 
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe amezindua huduma tembezi za madaktari bingwa humo na kuwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma hizo za kibingwa.

Huduma zilizozinduliwa Wilayani Iramba katika hospitali ya Kiomboi zitahusisha huduma za za upasuaji, meno, macho, upasuaji wa mifupa, huduma za kibingwa za magonjwa ya watoto, wanawake na huduma za mionzi.

Mhandisi Mtigumwe amesema matarajio ya mkoa huo ni kuwa huduma tembezi za kibingwa zitasaidia kutambua na kutibu magonjwa mbalimbali kabla hayajafikia hatua ya usugu na kupunguza gharama za rufaa za wagonjwa kwenda nje ya mkoa.

“Huduma tembezi za kibingwa zitawasaidia wananchi kutambua uwepo wa huduma za kibingwa katika mkoa wa singida na kupata matibabu kwa gharama nafuu” alisema Mhandisi Mtigumwe.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. John Mwombeki akisoma taarifa ya hali ya afya Mkoa wa Singida amesema wazo la kuanzisha huduma tembezi za kibingwa limetokana na idadi kubwa ya operesheni zilizofanyika kwa mwaka 2015/2016 na pia mkutano wa wadau wa afya mkoani hapa kuafiki wazo la kuanzisha huduma hiyo.

"Kwa kipindi cha mwaka 2015/2016  jumla ya operesheni kubwa na ndogo 4,836 zimefanyika katika hospitali mbalimbali mkoani hapa, aidha Idara ya macho katika hospitali ya Mkoa imefanya jumla ya operesheni kubwa na ndogo 2,020" ameongeza Dkt. Mwombeki.

Dkt. Mwombeki amesema uwepo wa madaktari bingwa 11 mkoani Singida pia umekuwa chachu ya utekelezaji wa huduma hiyo huku Mkoa ukifanya jitihada za kuazima madaktari wengine katika mikoa jirani ya Dodoma na Manyara.

Baadhi ya wagonjwa waliohudhuria katika siku ya kwanza ya zoezi hilo huku huduma hiyo ikitarajiwa kufanyika kwa muda wa siku tano wilayani hapo wameeleza shauku na furaha yao ya kusogezewa huduma za kibingwa katika halmashauri zao.

"Nilikuwa naumwa jino ambalo limeota vibaya, niliambiwa nitaweza kufanyiwa operesheni katika hospitali kubwa kama Muhimbili lakini hawa madaktari wametusaidia , nimepata huduma haraka na kwa gharama nafuu, nawasihi wenzangu waje kwa wingi" amesema Bi Neema Josseph Mkazi wa Kijiji cha Kizaga Wilayani Iramba.

 Naye Mzazi wa mtoto Jonas Masaka amesema huduma za kibingwa zitamsaidia mtoto wake mwenye matatizo ya macho na hiyo kumpunguzia gharama ya kumpeleke katika hospitali kubwa kutibu tatizo la macho linalomsababisha mtoto huyo kushindwa kusoma vizuri.

Huduma  ya tembezi za kibingwa Mkoani Singida zitafanyika katika Wilaya zote tano za Mkoa nwa Singida na hvyo kupunguza wagonjwa wa rufaa watakaopelekwa hospitali za Bugando, KCMC na Muhimbili.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa