IMG_2067
Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama,akizungumza na kamati ya maafa mkoa wa Singida na za wilaya zake zote sita kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa mjini hapa. Waziri Mhagama ameziagiza kamati zote za maafa kuanzia ngazi ya kijiji kujenga utamaduni wa kufanya tafiti zitakazosaidia kupambana na maafa katika maeneo yao.
Na Nathaniel Limu-Mo Blog
[Singida] Waziri wa  Nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, amezikumbusha halmashauri za wilaya,manispaa na majiji kutenga maeneo maalum kwa ajili ya vijana kufanyia shughuli zao za kiuchumi.
Mhagama ametoa wito huo wakati akizungumza na kamati ya maafa ya mkoa na zile za wilaya sita kwenye mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa mjini hapa.
Alisema kundi la vijana ambalo ndilo kubwa zaidi,linategemewa na familia,wilaya,mkoa na taifa kwa ujumla katika jukumu la upatikanaji wa maendeleo yakiwemo ya kiuchumi,hivyo linapaswa kujengewa mazingira mazuri na rafiki, kwa ajili ya shughuli zao.
Aidha, alisema halmashauri pamoja na kuwajibika kuwatengea  vijana maeneo maalum ya kufanyia shughuli zao,pia zinapaswa zitenge fedha za kutosha kwa ajili ya kuwakopesha viana na wanawake waweze kuboresha mitaji yao.
Katika hatua nyingine, waziri huyo ameagiza ukaguzi ufanyike viwandani na sehemu za kibiashara kubaini iwapo vijana/watu walioajiriwa,wana mikataba ya kazi na wanalipwa kiwango kilichowekwa na serikali.
“Hili jukumu nalitoa kwa wakuu wa mikoa, hakikisheni kila mwajiriwa kwenye sekta binafsi, wanakuwa na mikataba ya ajira na wanalipwa kwa mujibu wa maelekezo ya serijkali. Serikali haiwezi kuvumilia vijana au watu wengine wanaendelea kunyonywa nguvu zao na waajiri wasiofuata maagiza ya serikali”,alisisitiza Mhagama.
Katika hatua nyingine,waziri huyo alisema katika juhudi za serikali za kuhakikisha hakuna Mtanzania atakaye kufa kwa njaa, imeongeza tani zingine zaidi ya elfu tatu za nafaka kwa mkoa wa Singida, ili kupunguza makali ya njaa.
“Huu msada wa chakula kwa watu wenye upungufu wa chakula,utatumwa mkoani kwenu wakati wo wote kuanzia sasa,Natoa onyo,chakula hiki kiwafikie walengwa tu,ikibainika msimamizi amekwenda kinyume,huyo atakuwa hajipendi”,alisema.
Awali Katibu Tawala msaidizi, uchumi na uzalishaji sekretarieti ya mkoa wa Singida,Aziza Mumba,alisema mkoa una upungufu wa chakula tani 104,672.
Alisema kati ya tani hizo,tani 100,897 ni za kuuza kwa ajili ya kupunguza makali ya bei,na tani 4,275 ni kwa ajili ya wananchi wasiojiweza.
Aidha,Mumba alisema katika awamu ya mwezi huu,serikali kuu imetoa tani 328.7 za chakula bure kwa watu wasiojiweza na tani zingine 2,958.3 kwa ajili ya kupunguza makali ya bei ya chakula.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Singida magharibi (CCM) Elibariki Kingu, pamoja na kuipongeza serikali kuu kwa kuwajali wananchi wake ili wasife njaa,ameiomba awamu hii ya tani zaidi ya elfu tatu, itumwe mapema iwezekanavyo iweze kunusuru baadhi ya kaya ambazo hazina kabisa chakula.
IMG_2048
Mbunge wa jimbo la Singida magharibi (CCM), Elibariki Kingu, akisisitiza jambo kwenye mkutano ulioitishwa kwa ajili ya Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, kuzungumza na kamati za maafa ya mkoa na za wilaya zote sita.
IMG_2034
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya mkoa na za wilaya sita za mkoa wa Singida,wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama (hayupo kwenye picha).(Picha zote na Nathaniel Limu).
IMG_2032