Kisima chagharimu Sh22 milioni


Gasper Andrew, Singida  
MBUNGE wa Jimbo la Singida mjini, Mohammed Gullam Dewji, ametumia zaidi ya Sh 22 milioni, kugharamia uchimbaji wa kisima kirefu cha maji cha kitongoji cha Mtisi, kata ya Mtamaa. 
  
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kisima alisema, fedha hizo zimetumika pamoja na mambo mengine,kufanyia  utafiti wa eneo lenye maji,uchimbaji  na ununuzi wa pampu ya mkono. 
  
“Hapa naomba niweke mambo wazi, gharama hii inajumuisha pia uchimbaji wa kisima ambacho kwa bahati mbaya baada ya uchimbaji kina kirefu sana, kikawa hakina maji.  Pamoja na kukosekana huko kwa maji, lakini fedha nyingi  ilitumika”,alifafanua. 
  
Dewji alisema, ameamua kutumia fedha zake binafsi kugharamia uchimbaji huo wa kisima, kwa lengo la kuwapatia maji safi na salama wakazi wa kata ya Mtamaa. 
  
“Mimi binafsi naamini kwamba maji safi na salama, yatasaidia kuondoa uwezekano wa kutokea kwa magonjwa ya mlipuko ikiwamo, ugonjwa wa kuharisha”,alisema. 
  
Aidha, mbunge huyo aliwataka wakazi wa kijiji cha Mtamaa na vijiji jirani, kukitunza kisima hicho ili kiweze kutoa huduma endelevu. 
  
Dewji alisema kazi ya uchimbaji wa  visima, ni ya gharama kubwa mno, hivyo ni muhimu kisima hicho kikatuzwa  vizuri na kila mkazi wa eneo hilo, awe mlinzi ili kisiharibiwe. 
  
Awali diwani wa kata ya Mtamaa (CCM), Mbua Chima, alitumia fursa hiyo kumshukuru mbunge huyo kwa msaada wa kuwachimbia kisima wakazi wa kata hiyo.
Chanzo: Mwananchi

‘Acheni kuvamia migodi yenye leseni’


Gasper Andrew, Shelui 
OFISI ya madini Kanda ya Kati imewataka wachimbaji wadogo wa dhahabu katika mgodi wa Sekenke Halmashauri ya Wilaya ya Iramba mkoani Singida, kuacha tabia ya kuvamia maeneo yenye leseni na kuanza kuendesha shughuli zao kinyume cha sheria.

Tamko hilo la ofisi ya madini, limekuja kufuatia mgogoro uliotokana na wachimbaji wadogo kugoma kuondoka wala kuingia ubia na mwenye leseni katika eneo hilo kwa madai kuwa wapo kwa muda mrefu na leseni husika kutaja Kijiji cha Mgongo badala ya Sekenke.

Akizungumza mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Iramba juzi, Kamishna msaidizi wa madini Kanda ya Kati, Manase Mbasha alisema kitendo cha wachimbaji hao kuvamia eneo lenye leseni na kugoma kuondoka kinakiuka sheria ya madini namba sita ya mwaka 2010 na walipaswa kushtakiwa.

Kutokana na hali hiyo, Mbasha aliwataka wachimbaji hao kukaa na mwenye leseni kufikia mwafaka badala ya kuendelea kufanya shughuli zao kinyume cha sheria na kuikosesha Serikali mapato.

Hata hivyo alimtaka mmiliki wa leseni ya eneo hilo, John Bina na wenzake kuhakikisha kuwa wanalipa fidia kwa wote wanaostahili kwa mujibu wa sheria.Inakadriwa kuwa zaidi ya wachimbaji wadogo 1,000 wamejiajiri kwenye sekta ya madini katika eneo la Sekenke mkoani Singida.
Chanzo: Mwananchi

RC apiga marufuku walanguzi wa alizeti


na Hillary Shoo, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone amepiga marufuku wanunuzi binafsi wa alizeti kununua moja kwa moja zao hilo kutoka kwa wakulima kuanzia sasa.
Badala yake amewataka wakulima kuuza mazao yao kwenye vyama vya ushirika vya msingi kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani ili kunufaika na zao hilo.
Aliyasema hayo jana ofisini kwake alipokuwa akizungumza na viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi 81 vya mkoani hapa.
“Kuanzia leo na kuendelea vyama vya ushirika vya msingi ndiyo pekee vitaruhusiwa kununua zao la alizeti kutoka kwa wakulima na wanunuzi binafsi watanunua kwenye maghala kwa maelekezo ya chama kikuu cha ushirika (SIFACU) na kwa bei watakayokubaliana.” Alisisitiza Kone.
Kone alisema wanunuzi binafsi wamekuwa wakinunua zao hilo kwa wakulima kwa bei ndogo kwa sababu ya kutumia wanunuzi wa kati licha ya halmashauri kukosa ushuru wa zao hilo na kuzinyima mapato ya kuweza kujiendesha.
“Udhibiti na ubora wa zao la alizeti umekuwa mdogo hivyo kutokuwa na soko lililo bora, mkoa unakosa takwimu  sahihi za uzalishaji wa zao hili na zaidi ya hili wanunuzi wamekuwa wakitorosha zao hili kwa njia za panya hivyo mkoa kukosa pato litokanalo na alizeti,” alisema.
Alieleza kwamba mfumo wa stakabadhi ghalani unaotumiwa na vyama vya msingi vya ushirika ndiyo pekee unaoweza kumsaidia mkulima mdogo kupata pato linalolingana na jasho lake.
Chanzo: Tanzania Daima

Atalikiwa kwa kuzaa ‘nyani’


na Jumbe Ismailly, Singida
MWANAMKE mmoja, Mwanaharusi Juma (34) mkazi wa Kijiji cha Ndulungu Wilaya ya Iramba mkoani hapa, amekimbiwa na mumewe kutokana na kujifungua watoto wawili wanaofanana na nyani.
Mama huyo mwenye familia ya watoto wanne wenye baba wawili tofauti, aliolewa na mume wa kwanza na kuzaa naye mtoto mmoja, Fadhila Juma (15) mwaka 2007 - mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Ndulungu, kabla ya kuolewa na Sadick Selemani ambaye amemkimbia baada ya kumzalia watoto hao wawili wenye kasoro kimaumbile.
“Niliolewa na Sadick mwaka 2008 na nimeishi naye kwa miaka kumi nikampatia watoto watatu, wakiwemo wawili wanaofanana na nyani, na mmoja alikuwa kawaida kama binadamu wengine,” alisema.
Alisema kuwa watoto hao licha ya kuwa binadamu, lakini wamekuwa na sura za wanyama.
Mama huyo aliwataja watoto watatu aliozaa na Sadick kuwa ni Alhaji Sadick (10), Ramadhani Sadick (6) wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Ndulungu na Abdulatifu Sadick (5).
Alibainisha kuwa, watoto hao wenye matatizo wamekuwa wakishindwa kutembea mwendo mrefu bila kupumzika na kupumua kwa shida sana na matumbo yao ni makubwa.
“Matumbo ya watoto wangu wawili wenye matatizo ni makubwa, macho yao ni mekundu kama mnavyoyaona, na hupumua kwa shida sana kiasi cha kuwafanya washindwe kutembea umbali mrefu bila kupumzika,” alisisitiza Mwanaharusi.
Alisema kuwa, watoto hao walizaliwa wakiwa katika hali ya kawaida kabisa, lakini walianza kuugua mara kwa mara na kutoongea tena hadi hivi sasa.
“Mimi ni mke mdogo katika ndoa ya wake wawili, na mume wangu alipoona nimeanza kumbana sana kuhusu matibabu ya watoto hao, aliondoka mwaka 2010 na kuhamia kwa mke mkubwa,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima

Dewji kutoa mamilioni kusaidia kilimo


Mwandishi Wetu, Singida
MBUNGE wa Jimbo la Singida mjini (CCM),  Mohamed  Dewji, ameahidi kuwapa wananchi wa jimbo lake Sh250 milioni, lengo likiwa ni kugharamia mradi wa kilimo katika eneo hilo.

Akizungumza jimboni kwake katika hafla ya uzinduzi wa kisima cha maji cha kitongoji cha Mtisi, Kijiji cha Mtamaa alisema,  fedha hizo zitatumika kununua tani 60 za mbegu za choroko, dengu na mbaazi katika msimu ujao wa kilimo.

Dewji alisema  lengo la mradi huo  ni kuwajengea mazingira mazuri wakulima wa jimbo lake ili waweze   kuboresha hali zao  kiuchumi.

Alisema pia kuwa, kila kikundu cha wakulima 25, kitapewa jembe la kukokotwa na wanyama (plau).
“Mimi, madiwani pamoja na watendaji, tutawahamasisha wakulima kila kaya ilime ekari moja ya mazao hayo ya mbaazi, dengu na choroko.  Mazao hayo yana soko la uhakika na bei zake zipo juu zaidi ya zao la mahindi”, alisema na kuongeza:

“Binafsi nitanunua mazao hayo kwa bei ambayo itakuwa na faida kubwa kwa mkulima wa mazao hayo”.
Katika hatua nyingine,  Dewji alisema Mtaalamu wa Kilimo katika ofisi yake kwa ushirikiano na wataalamu wa manispaa, watasimamia mradi huo kwa karibu, ili wakulima waweze kuzingatia ushauri wa kilimo bora.

“Lengo ni kwamba mavuno katika ekari hiyo moja ya aidha, dengu, choroko au mbaazi, yakidhi mahitaji ya kuweza kumkomboa mkulima kiuchumi,”  alisema kwa kujiamni.

Wakati huo huo, mbunge huyo  alitumia nafasi hiyo kuwataka wakulima kubadilika na kuachana na kilimo cha mazoea na kuanza kulima kilimo kinachozingatia ushauri wa taalamu.

Aidha, alisema kutokana na misimu ya mvua za miaka hii kutokueleweka vizuri, njia pekee ya kunufaika na kilimo, ni mkulima kuwahi kuandaa mashamba na mbegu bora kabla msimu haujaanza.
Chanzo: Mwananchi

MKAZI WA SINGIDA JELA MIAKA 30 BAADA YA KUKIRI KULAWITI MVULANA WA MIAKA 9.


Bango la mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida.Picha  na Nathaniel Limu.
Na Nathaniel Limu.
Kijana mkulima wa kijiji cha Ihanja jimbo la Singida Magharibi Samwel Simon (22) amehukumiwa kutumikia jela miaka 30 baada ya kukiri kosa la kumlawiti kijana wa kiume mwenye umri wa miaka tisa (jina tunalo).
Mvulana huyo mdogo ni mkazi wa kijiji cha Nkhoiree tarafa ya Ihanja jimbo la Singida Magharibi.
Awali mwendesha mashitaka inspekta msaidizi wa polisi Shukurani Magafu, alidai mbele ya hakimu wa mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida Terrysophia Tesha kuwa mnamo juni 12 mwaka huu katika muda ambao haujafahamika, mshitakiwa Samwel alimlawiti mvulana huyo mdogo na kumsababishia maumivu makali katika sehemu yake ya kutolea haja kubwa.
Magafu amesema siku ya tukio, mshitakiwa alimlaghai kijana huyo wa kiume na kisha kuingia naye ndani ya chumba chake cha kulala na baada ya kumvua kaptura, alimkaba kwa nguvu na kuanza  kumwingilia kinyume na maumbile.
Amesema wakati mshitakiwa akiendelea na unyama wake, kijana huyo alikuwa akipiga kelele ambazo zilichangia majirani na watu waliokuwa karibu na eneo la tukio kufika haraka kwa lengo la kujua kinachomsibu kijana huyo.
“Watu walipofika eneo la tukio, walimkuta mshitakiwa bado anaendelea kuvaa suruali yake na ndipo walipomkamata na kumfunga kwa kamba ya katani inayotumika  kufungia ng’ombe na kumpeleka kituo kidogo cha polisi Ihanja”, alisema mwendesha mashitaka huyo.
Amesema mshitakiwa alipofikishwa kituo cha polisi Ihanja, bila kusumbua, alinyoosha maelezo na kukiri kuwa ni kweli amemwingilia kimwili kinyume na maumbile kijana huyo wa kiume.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mwendesha mashitaka Magafu alisema pamoja na mshitakiwa kutokuwa na rekodi yo yote ya makosa ya uhalifu,l akini kitendo alichomfanyia mtoto huyo mdogo hakivumiliki mbele ya jamii.
Kwa upande wake mshitakiwa, aliiomba mahakama hiyo imwonee huruma na kumwachia huru kwa vile amefanya kosa hilo kwa kusukumwa na pombe nyingi aliyokuwa ameitumia siku hiyona pia hajaisumbua mahakama na hilo ni kosa lake la kwanza toka a
Habari kwa hisani ya MO BLOG

Mtoto Wa Afrika Ilivyokuwa Singida

Watoto wa Kompasheni, Kanisa la Moravian Singida Mjini wakifuatilia moja ya tukio, maadhimisho ya mtoto wa Afrika,
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Tumaini, Mjini Singida iliyo maalumu kwa wasiosikia, wakifuatilia kwa makini hotuba ya mgeni rasmi
Mkurugenzi wa Manispaa Singida, Mathias Mwangu(katikati), Afisa maendeleo jamii, Daffi Imanuel(kushoto), na mmoja wa ofisa kati
 Wanafunzi wa Shule ya Msingi Tumaini, Mjini Singida iliyo maalumu kwa wasiosikia, wakifuatilia kwa makini hotuba ya mgeni rasmi

Na Elisante John, Singida
Juni 17, 2012:ZAIDI ya watoto 2,900 wanaishi mazingira hatarishi Manispaa ya Singida, hivyo kuchochea vitendo viovu, kwa kukosa malezi bora.
 
Hali inayosababishwa na watoto wengi kukosa msingi imara wa malezi, wakati wote wa makuzi yao.
 
Kati ya watoto hao Wasichana ni 1,454 na wavulana 1,472 ambao baadhi yao hulazimika kujiigiza katika kwenye vitendo viovu, ili kujikimu maisha ya kila siku.
 
Mkurugenzi wa Manispaa Singida, Mathias Mwangu, amesema hayo kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika, yaliyofanyika juzi, katika viwanja vya Utamaduni, mjini Singida.
 
Mwangu amesema, licha ya watoto hao kujihusisha na tabia hizo mbaya katika jamii, pia wanalazimika kukosa haki za msingi, kama vile elimu, huduma za afya, chakula na malazi bora.
 
Amesema, Manispaa yake kwa kushirikiana na wadau wake, inaangalia uwezekano kuandaa utaratibu maalumu, utakaowezesha watoto hao kuungana na familia zao, kwa faida yao na Taifa kwa ujumla.
 
Siku ya mtoto wa Afrika huadhimishwa Juni 16 kila mwaka, kukumbuka mauaji ya Soweto,nchini Afrika Kusini, wakati wakidai elimu bora; Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Haki ya watoto walemavu ni jukumu letu kuzilinda,kuziheshimu, kuzidumisha na kuzitimiza’

MBUNGE WA SINGIDA MJINI(CCM)MOHAMMED DEWJI AWAKABIDHI PIKIPIKI ZENYE THAMANI YA MILION 20 WAFANYA BIASHARA YA BODABODA SINGIDA.

 Mbunge wa jimbo la Singida mjini Mh. Mohammed Gullam Dewji akizungumza na wafanyabiashara wa bodaboda (hawapo kwenye picha) muda mfupi kabla hajawakabidhi msaada wa pikipiki kumi zenye thamani ya shilingi milioni 20.Kushoto ni katibu wa umoja wa wafanyabiashara wa bodaboda, Maulid Mpondo.Kulia wa kwanza ni Kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Singida,Williamu Haaly na anayefuata,ni katibu wa CCM manispaa ya Singida.
 

 Mo akizungumza na waumini wa kanisa la Pentekosti la kijiji cha Ititi muda mfupi kabla hajakabidhi msaada wa mifuko 25 ya saruji na shilingi laki tano taslimu.
 Mmoja wa wafanyabiashara wa bodaboda akisoma risala yao kwa mbunge wa jimbo la Singida mjini Mh. Mohammed Gullam Dewji.
Mbunge wa jimbo la Singida mjini Mh. Mohammed Gullam Dewji akimkabidhi katibu wa umoja wa wafanyabishara wa bodaboda msaada wa pikipiki 10.
 

 Mbunge wa jimbo la Singida mjini,Mohammed Gullam Dewji akimkabidhi Mchungaji Daud Elia mifuko 25 ya saruji kwa ajili ya kujengea kanisa.
  Baadhi ya Wafanyabiashara Wa Bodaboda wakimsikiliza mbunge wao.
 Pikipiki 10 aina ya sanlag CC150 zilizotolewa msaada ya mbunge wa jimbo la Singida mjini, Mohammed Gullam Dewji kwa vikundi 10 vya wafanyabiashara wa bodaboda mjini Singida.
Baadhi ya wafanyabiashara wa bodaboda wa mjini Singida wakiserebuka na kucheza 'KIDUKU' na mbunge wao Mohammed Gullam Dewji muda mfupi kabla ya mbunge huyo kuwakabidhi wafanyabiashara hao msaada wa pikipiki.
 Jengo la kanisa la Pentekoste la kijiji cha Ititi jimbo la Singida mjini.
---
Na Geofrey Mwakibete na Nathaniel Limu




Wafanyabiashara wa bodaboda jimbo la Singida mjini,wamehimizwa kuunda/kuanzisha  vikundi ili pamoja na mambo mengine, kujijengea mazingira mazuri ya kukopesheka.
Wito huo umetolewa na mbunge wa jimbo la Singida mjini,Mohammed Gullam Dewji,wakati akizungumza kwenye hafla iliyofana, ya kukabidhi pikipiki 10 aina ya sanlag CC 150 zenye thamani ya shilingi milioni 20 kwa vikundi vya wafanyabiashara wa bodaboda.


Alisema faida za kujiunga kwenye vikundi ni nyingi ikiwemo ya kuwa nafasi nzuri ya kupata mikopo mbalimbali kutoka kwenye taasisi za kifedha.Mtu mmoja mmoja akitaka kukopa fedha benki ni ngumu, kuotokana masharti yaliyowekwa na taasisi za kifedha. 


“Siku zote umoja ni nguvu,utegano unachangia kuleta ulegevu unaozaa udhaifu.Mahali pana ulegevu,kwanza hakuna maendeleo ya kweli na pia kutetea haki,inakuwa ngumu mno”,alifafanua Dewji ambaye pia ni mjumbe wa NEC CCM mkoa wa Singida.


Kuhusu pikipiki hizo alizotoa msaada, alisema lengo lake ni kwamba kila kikundi kitaitumia pikipiki yake kwa ajili ya kukiongezea kikundi mapato ambayo endapo yatatunzwa vizuri,ipo siku kila mwanakikundi anaweza akamiliki pikipiki yake binafsi. 


Aidha, amewataka wakati wote kuzingatia sheria halali zilizowekwa na mamlaka husika, ili shughuli zao ziweze kuendelea bila matatizo.


“Pia napenda kutumia fursa hii, kuomba mamlaka zinazohusika na sheria za usalama barabarani na utozaji wa kodi na ushuru, kujipanga kwa ajili ya kutoa elimu kwa wafanyabiashara wa bodaboda,ili waweze kuzifahamu sheria husika”,alisema na kuongeza;


“Nina imani kwamba wafanyabiashara wa boda boda wakifahamu kwa kina sheria za usalama barabarani,kutapunguza mno ajali na pia wakifahamu mambo ya kodi na ushuru,hawatakwepa kulipa”.


Katika hatua nyingine, Dewji amewahimiza waumini wa madhehebu ya dini, kuongeza kasi ya utoaji sadaka,ili kuimarisha ustawi wa madhahebu yao.


Alisema waumini wanao wajibu mkubwa wa kuchangia kwa hali na mali madhehebu yao kwa lengo  yaweze kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi zaidi.


“Sadaka inayotolewa kwa moyo mkujufu,licha ya kusaidia ustawi wa dhehebu la dini husika,mtoaji anakuwa amejiwekea thawabu mbele ya mwenyezi Mungu”,alisema Dewji.
Akiijengea nguvu hoja yake hiyo,mbunge huyo, alisema ustawi wa kweli wa dhehebu la dini,utaletwa na waumini wenyewe,watu wengine/taasisi zingine,kazi zao ni kusaidia mahali waumini wanapokuwa wamepelea.  


Katika siku yake ya pili ya ziara yake ya kikazi jimboni kwake,Dewji alitoa msaada wa mifuko ya saruji 40 kwa msikiti wa kijiji cha Manguamitogho na mifuko mingine 25 ya saruji na shilingi laki tano taslimu, kwa kanisa la Pentekoste la kijiji cha Ititi.


Katika siku yake ya mwisho ya ziara yake (17/6/2012),Dewji alitarajiwa kuwa na kikao maalum na madiwani wa kata za Singida mjini,kuzindua kisima cha maji cha kijiji cha Mtisi,kuzungumza na wanachama wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Singida na kukagua kituo cha afya cha Sokoine mjini Singida

Wakulima washauriwa kuunda mtandao kukabiliana na athari za ukame


Nathaniel Limu, Singida
Wataalam wa kilimo kwenye maeneo ambayo ukame umekithiri hapa nchini, wameshauriwa kuunda mtandao wa mawasiliano, utakaosaidia kubadilishana uzoefu wa namna ya kukabiliana na athari zinazosababishwa na ukame.
Changamoto hiyo imetolewa juzi na katibu tawala mkoa wa Singida, Liana Hassan wakati akifungua semina ya siku tatu iliyohusu  kilimo bora cha mtama iliyohuduriwa na wataalamu 47 kutoka wilaya nane za hapa nchini.
Alisema hivi sasa ukame unaosababishwa na uhaba wa mvua, unasababisha pamoja na mambo mengine, uhaba mkubwa wa mavuno ya mazoa ya chakula.
Akifafanua, Liana alisema uhaba huo wa mavuno ya chakula unasababisha baadhi ya maeneo kuwa na njaa kali na hivyo wakazi wake, kushindwa kujiletea maendeleo endelevu.
Aidha, Katibu tawala huyo, amewataka wananchi waishio kwenye maeneo kame, kuacha tabia ya kuchagua vyakula.
Awali ofisa mwandamizi wa shirika lisilo la kiserikali la International Crops Research Institute for the Semiarid Tropics (ICRISAT), lenye makazi yake Nairobi nchini Kenya, Dk. Mary Mgonja, alisema shirika lao limejikita kaitka kuhimiza wananchi kujenga utamaduni wa kulima mazoa yanayostahimili ukame likiwemo zao la mtama, kwa madai kuwa mtama ni zao la chakula na  biashara.
 “Zao la mtama ni muhimu katika maeneo yanayokabiliwa na ukame na pia sehemu ambazo udongo una rutuba ya wastani.  Utafiti wa zao hili umeweza kutoa kenlojia mbali mbali ambazo zinaweza kutumiwa ili kuongeza tija katika uzalishaji”,alisema.
Dk.Mary alisenma kuwa shirika la ICRISAT limepewa msaada wa zaidi ya dola za kimerikani milioni mbili kwa ajili ya kugharamia na kuratibu mradi wa kuhima kilimo bora cha mtama ambao amedai kuwa licha ya kuwa ni chakula bora,kwa sasa lina soko la uhakika.
Alisema wilaya ya Same,Mwanga,Moshi,Kongwa,Singida vijijini,Iramba,Serengeti na Kondoa,kila moja imepatiwa shilingi milioni kumi kwa ajili ya kugharamia mafunzo kwa wakulima na wataalam wa kilo katika hatua ya kwanza ya mradi.
Chanzo: Mo Blog

Askari Magereza aua fundi kwa risasi



Na Jumbe Ismailly, Singida

MKAZI wa mjini Singida, Muna Abubakari (37) ambaye ni fundi ujenzi, amefariki dunia juzi baada ya kupigwa risasi na askari wa Jeshi la Magereza mkoani hapa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Linus Sinzumwa, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi, majira ya saa saba mchana.
Alisema askari aliyehusika na tukio hilo ametambuliwa kwa jina la CPL Abdalla Kabwe (31) na kwamba baada ya kutekeleza azma yake hiyo alitoroka na haijulikana alikokwenda.
Alisema kabla ya tukio hilo, Abubakar alikuwa na askari wa gereza huyo wakijenga katika jengo la ofisi mpya ya jeshi hilo iliyopo maeneo ya Mtaa wa Bomani.
Alieleza kuwa wakati wakiendelea na ujenzi huo ndipo askari wa kawaida wa magereza aliyetambulika kwa jina la Fred John (24) alimkabidhi bosi wake, CPL Kabwe bunduki aina ya SAR yenye namba 1123457 ikiwa na risasi 10 naye aliondoka kwenda kufuata vifaa vingine vya ujenzi.
Kwa mujibu wa msemaji huyo wa jeshi, inadaiwa Abubakari na askari huyo alikuwa marafiki na kwamba ghafla walisikia mlio wa risasi.
“Watu wengine waliokuwa ndani ya jengo hilo na majirani waliposikia mlio huo walianza kukimbilia kwenye eneo la tukio na kumkuta Abubakari akiwa amelala chini huku akibubujikwa na damu nyingi huku bunduki iliyotumika ikiwa imeachwa pembeni ya mwili wake na askari Kabwe akiwa ametoweka,” alisema.
Kamanda huyo alisema jeshi hilo limeanzisha msako wa kumtafuta askari Kabwe na wakati huohuo wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha mauaji hayo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Singida, Dk. Suleiman Muttani, alisema kuwa fundi ujenzi huyo amefariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu.

Chanzo: Tanzania Daima

MBUNGE WA IRAMBA MAGHARIBI MH. MWIGULLU LAMECK KUWASILISHA HOJA BINAFSI.




Mbunge wa jimbo la Iramba magharibi na katibu wa uchumi na fedha CCM taifa Mwigullu Lameck Nchemba,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) juu ya kusudio  lake la kuwasilisha hoja binafsi ya kuundwa kwa baraza maalum la kushughulikia makosa ya uhujumu uchumi na rushwa.Picha na Nathaniel Limu.
MBUNGE wa jimbo la Iramba magharibi (CCM) mkoani Singida, Mwigulu Nchemba, anakusudia kuwasilisha hoja binafsi wakati wa bunge la bajeti lijalo, juu ya kuanzishwa kwa baraza maalum litakaloshughulikia makosa ya uhujumu uchumi na vitendo vya rushwa.
Amesema amefikia uamuzi huo ambao amedai utasadia kwa kiasi kikubwa wananchi kuendelea kuiamini serikali yao , baada ya kubaini kuwa kesi zinazohusu vitendo hivyo, huchukua muda mrefu, mno kumalizika na kitendo hicho,huchangia watuhumiwa wengi kuachiliwa huru.
Akifafanua zaidi, amedai kwamba kuchelewa kumalizika kwa kesi hizo, hutoa mwanya kwa watuhumiwa kutoa rushwa ili sheria iweze kupinduliwa kwa manufaa yao .
Mwigulu ambaye pia ni Katibu wa fedha na uchumi wa CCM taifa, alisema kuachiwa kwa watuhumiwa wa makosa ya rushwa na uhujumu uchumi, kunachangia mno kuporomoka kwa maadili ya viongozi na wakati huo huo, wananchi kuichukia serikali yao.
Alisema mazingira ya usikilizaji wa kesi hizo yalivyo hivi sasa katika mahakama hizi za kawaida, yanachangia kupunguza ufanisi wakati wa kuzishughulikia, kutokana na msongamano wa kesi katika mahakama hizo za kawaida.
“Nadhani umefika wakati makosa haya mazito, yatengewe chombo chake maalum ili yashughulikiwe kwa umakini wa hali ya juu zaidi, na maamuzi yaweze kupatikana mapema iwezekanavyo”,alisema.
Akiijengea nguvu hoja yake hiyo, alisema baada ya serikali kuondoa kesi zinazohusu migogoro ya ardhi na kuanzisha baraza maalum linaloshughulikia makosa/malalamiko ya ardhi tu, kwa sasa migogoro ya ardhi imepungua kwa kiwango kikubwa.
“Maandalizi yote muhimu kwa ajili ya kuwasilisha hoja hii nzito kwenye kikao kijacho cha bunge la bajeti, yanakwenda vizuri kama itaafikiwa hoja hii, basi pamoja na mambo mengine, yafanyike marekebisho ya sheria ya upelelezi iliyopo hivi sasa na kuupa umuhimu ushahidi wa mazingira kwa kuwa kutolea ushahidi makosa ya rushwa, ni mgumu”,alifafanua Nchemba.
Mwigulu alisema pia upo umuhimu mkubwa wa kuongeza adhabu ya makosa hayo ambayo itakuwa fundisho la kweli kwa wakosaji na kuwaogofya viongozi/wananchi wanaotarajia kutoa rushwa ua kuhujumu uchumi.

HALMASHAURI YA SINGIDA KUWEKA TARATIBU NA SHERIA ZITAKAZOHIMIZA WANANCHI KUCHANGIA MIRADI YA MAENDELEO.


   Mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Vicent Kone,akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC),  Kulia ni katibu tawala mkoa wa Singida,Liana Hassan. Baadhi ya wajumbe wa kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Singida walioshiriki Kikao kwenye ukumbi wa mikutano wa kanisa katoliki mjini singida.Picha zote na Nathaniel Limu.
IMEELEZWA kwamba halmashauri ya wilaya ya Singida,imeshindwa kufikia malengo yake ya ukusanyaji wa mapato ya ndani,kwa kile kilichodaiwa kuwa wananchi wa jimbo la Singida mashariki,kuzuiwa kuchangia maendeleo yao.
Hayo yamesemwa juzi na mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Illuminata Mwenda,wakati akitoa taarifa yake ya kushindwa kukusanya mapato ndani kama inavyokusudiwa, kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kanisa katoliki mjini Singida.
Alisema wananchi wa jimbo hilo,wamezuiwa kuchangia na kutekeleza miradi yao ya maendeleo na pia wasilipe ushuru wala  kodi kama inavyoelekezwa na sheria ndogo za halmashauri hiyo.
Mwenda alisema siasa za aina hiyo,zimechangia ukusanyaji wa mapato ya ndani kuwa mgumu mno na vile vile zimedumaza maendeleo kwa ujumla katika jimbo hilo.
Hata hivyo, mkurugenzi huyo alisema wanaangalia utaratibu wa kisheria utakaosaidia kuwahimiza wananchi wa jimbo hilo kushiriki kuchangia na kutekeleza miradi yao ya maendeleo, kama ambavyo wananchi wengine wa majimbo mengine ya halmashauri,wanavyochangia.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Mkalama,Mussa Chang’a alisema serikali ya mkoa isiruhusu siasa uchwara kuendelea kwa vile zitapunguza kasi ya kuwaletea wananchi maendekeo endelevu.
“Ni afadhali kulaumiwa kuliko kuacha wanasiasa uchwara wanaharibu au wanadumaza maendeleo ya wananchi, yaliyofikiwa na yanayotarajiwa kufikiwa”,alisema.
Taarifa iliyotolewa kwenye kikao hicho, ni kwamba halmashauri ya wilaya ya Singida ni ya mwisho katika ukusanyaji wa mapato ya ndani katika kipindi cha kuanzia julai mwaka jana hadi machi mwaka huu.
Halmashauri hiyo, imekusanya asilimia 18.4 tu,wakati manispaa ya Singida,imekusanya asilimia 37,Iramba 71.4 na Manyoni 54.
Mbunge wa jimbo la Singida mashariki (CHADEMA) Tundu Lissu, ameapa kwamba wananchi wa jimbo lake watakuwa kwenye likizo ya kuchangia maendeleo yao,hadi hapo ubunge wake utakapokoma.
Kwa hisani ya Mo Blog

NAPE AKAGUA UJENZI WA HOSPITALI YA RUFANI SINGIDA


Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Nape Nnauye akizungumza na
viongozi wa CCM mkoa wa Singida baada ya kuwasili kwa ziara ya kikazi ya
siku moja leo Juni Mosi, 2012.

Katibu tawala wa mkoa wa Singida, Liana Hassan (wapili kulia) akionyesha
ramani ya jengo la utawala la hospitali ya rufani ya Singida ambayo
ujenzi unaendelea. Kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Singida, Jerome Alute

Nape akikagua ndani ya majengo ya hospitani ya rufani Singida

Ofisa Tawala wa mkoa wa Singida, Liana Hassan (kushoto) akimpa maelezo
Nape kuhusu ujenzi wa hospitali hiyo ulipofika. Kulia ni Alute
Nape na ujumbe wake wakikagua jengo la Wazazi la hospitali ya Rufani Singida

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa