Wajumbe baraza la katiba wataka nafasi ya mgombea binafsi iondolewe kwenye katiba mpya

WAJUMBE wa baraza la maoni ya Katiba mpya katika Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, wamependekeza kuondolewa kwa kipengele cha mgombea huru katika nafasi za udiwani, ubunge na Raisi.
Wajumbe  hao wamesema kuwa ni vyema wagombea wote wa nafasi hizo wakatokana na vyama vya siasa, ili kupunguza uwezekano wa kumuingiza madarakani kiongozi ayesiyekuwa na maadili mazuri.
Wakizungumza kwenye kikao cha  baraza  la maoni ya katiba mpya wilaya ya Ikungi mkoani Singida leo,  baadhi ya wajumbe wamesema  wagombea wanaotokana na vyama vya siasa hupigiwa kura za  maoni na kuchunjwa kwenye vikao kabla ya  kuwepewa tiketi ya kuwania nafasi husika.
Wamesema kitendo cha kuruhusu mgombea huru,  kinaweza kusababisha watu wenye ushawishi mkubwa wa kifedha kutumia vibaya fursa hiyo kununua uongozi  na kuingiza nchi kwenye  utawala wa kiditeta.
Hata hivyo Mwenyekiti wa kikao hicho Ali Salehe amesema kuwa  kuondolewa kwa kipengele hicho,  pia kunaweza kuwanyima fursa baadhi ya wagombea  wazuri wanaoshindwa kupambana na wenye  fedha katika ngazi za vyama.
Baraza la maoni  ya katiba mpya Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida lenye wajumbe zaidi ya 100 limemaliza vikao vyake  vya siku mbili kwa kutoa mapendekezo mbalimbali katika rasimu hiyo ya Katiba.

Nyara za Serikali zawafikisha polisi



JESHI la Polisi Mkoa wa Singida, linawashikilia watu wawili kwa tuhuma ya kumiliki nyara za Serikali kinyume na sheria. Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwela aliwataja watu wanaoshikiliwa kuwa ni Esinasi Stephano (36) mkazi wa Kijiji cha Chikuyui. Alisema mtuhumiwa alikamatwa kwa kosa la kumiliki meno mawili ya tembo yenye uzito wa kilo tano na thamani ya zaidi ya Sh milioni 4.4.

Alisema mtuhumiwa huyo, alikamatwa juzi jioni baada ya raia wema kutoa taarifa polisi.

Alimtaja mtuhumiwa wa pili kuwa ni, Mwanandi Amani (34) mkazi wa Kijiji cha Mitundu ambaye alikamatwa na mkia wa tembo, meno mawili ya ngiri, mafuta ya samba na sare moja ya Jeshi la Polisi.

Alisema mtuhumiwa huyo, alikamatwa baada ya raia wema kutoa taarifa juu ya umilikaji wake wa nyara za serikali kinyume na sheria.

Katika hatua nyingine, alisema wameanzisha msako mkali wa kusaka watu wanne waliomvamia mmiliki wa duka Miraji Abdallah (45) mkazi wa Kijiji cha Mtunduru na kupora simu 15 za kiganjani.

Alisema watu hao, wanaodhaniwa ni majambazi, kabla ya kupora simu hizo ambazo thamani yake bado haijajulikana, walimjeruhi vibaya Miraji na watu wengine Hamisi Hamisi (30) na Hatibu Idde (18) kwa kutumia visu.

CHANZO HABARI LEO

HABARI YA KUSIKITISHA: MWANAFUNZI WA DARASA LA TATU AUAWA KIKATILI






Mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Kizega wilayani Iramba Bi. Mariamu Alphonce mwenye umri wa miaka kumi ameuwawa kikatili kwa kukatwa shingo na kucharangwa kwa panga sehemu mbalimbali za mwili wake na kaka yake bwana Elibariki  Alphonce. 

Akieleza kwa uchungu baba wa mtoto huyo bwana Alphonce Msengi amesema alipofika nyumbani kwake majira ya saa kumi na moja jioni alikuta damu nyingi na alipo angali vizuri alimuona mtoto wake Mariamu Alphonce akiwa amekatwakatwa kwa mapanga na tayari alikuwa ameshafariki.

Bwana Msengi baada ya kuona hivyo alipiga yowe na walikuja majirani na watoto na wakamwambia tumemuona mtoto wako Elibariki akiwa na mapanga mawili akikimbia huku akiwa hana nguo. 


Wakieleza mwenyekiti wa kitongoji Bi Vailet Mbigu na mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kizega bwana Elisante Gyuzi wamesema pamoja na shule kuandaa taratibu zote za mashishi , kijana aliyefanya unyana huo huwa anavuta bangi na mara nyingi alikuwa akisikika kumtishia kumuuwa baba yake kwa kumkata kwa panga.




Kwa upande wake  kaimu mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Iramba daktari Timoth Sumbe amesema wamempokea Mariamu Alphonce akiwa ameshafariki huku mwili wake ukiwa na majeraha ya kukatwakatwa sehemu ya shingoni,kichwani.




Akiongea kwa simu kamanda wa jeshi lapolisi mkoani Singida bwana Godfrey Kamwela amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na jeshi lake lina endelea kumsaka mtuhumiwa bwana Elibariki Alphonce ambaye alitoweka baada ya mauaji ili aweze kufikishwa mahakamani. 



SOURCE: ITV

Magunia ya mkaa 311 yaliyovunwa kinyemela yakamatwa Singida

WAKALA wa huduma za Misitu  nchini  katika  halmashauri ya wilaya ya Singida,amefanikiwa kukamata magunia ya mkaa 311 yenye thamani ya zaidi ya shilingi 5.2 milioni, ambayo yamevunwa kinyume na sheria.

Meneja wa wakala huyo wilayani Singida bwana Hashimu Kativo, amesema magunia hayo wameyakamata  mapemawiki hii katika msako mkali unaoendelea wa kuwakamata wafanyabiashara na watu wengine wanaouza  mazao ya misitu na nyuki kinyume na sheria za  nchi.

Amesema  magunia hayo yamekamatwa katika kijiji cha Tupendane kata ya Mang’onyi baaada ya kukuta magunia hayo yakiwa yamekusanywa  bila kuwa na kibal cha kuvuna wala leseni ya kununua na kuuza mkaa.

Hata  hivyo amefafanua kuwa wamiliki wa mkaa huo waliweza kutoroka kwenda kusikojulikana.

Bw Katiyo amesema katika ukamataji huo, pia wameharibu matanuru sita makubwa ambayo yalikuwa yakitumika kuchoma mkaa kwa ajili ya kuuza.

Yunde ashinda kwa kishindo kugombea Uenyekiti wa halmashauri ya Ikungi mkoani Singida.

DSC01915
Katibu wa CCM wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida, Joseph Rudisha akitoa mwongozo kwenye mkutano wa uchaguzi wa kuchagua mwenyekiti na makamu wake wa halmashauri ya wilaya hiyo mpya.Wa kwanza kulia ni mgombea pekee wa nafasi ya uenyekiti Celestine Yunde.
DSC01919
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ikungi, Hassan Tati akizungumza kwenye mkutano wa uchaguzi wa nafasi za mwenyekiti na makamu wake wa halmashauri ya wilaya mpya ya Ikungi. Mkutano huo ulifanyikia kwenye ukumbi wa mikutano wa chuo cha maendeleo ya wananchi mjini Singida.Wa kwanza kulia ni mgombe wa nafasi ya mwenyekiti Celestine Yunde na kushoto ni mgombe wa nafasi ya makamu mwenyekiti, Alli Nkhangaa.
DSC01926
Mgombea wa nafasi ya mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ikungi, Celestine Yunde akiomba kura kwa wajumbe (hawapo kwenye picha) wa mkutano wa uchaguzi wa kuchagua wagombea watakaopambana na wagombe kutoka CHADEMA. Kulia ni katibu wa CCM wilaya ya Ikungi, Joseph Rudisha na kushoto ni mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ikungi, Hassan Tati.
DSC01917
Baadhi ya madiwani waliohudhuria mkutano wa uchaguzi wa CCM wilaya ya Ikungi wanaowania nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti katika halmashauri ya wilaya hiyo.Mkutano huo ulifanyikia katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha maendeleo ya wananchi mjini Singida.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Celestine Yunde wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) halmashauri ya wilaya ya Ikungi, amechaguliwa kwa kishindo kuwania nafasi ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo.
Yunde ambaye alikuwa mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Singida kabla ya wilaya hiyo kuzaa halmashauri mpya ya Ikungi, alipata kura 29 za ndio na moja ilimkataa.
Kwa ushindi huo mnono, Yunde atapambana na mgombea kutoka CHADEMA iwapo chama hicho cha upinzani, kitaamua kutoa mgombea.
CHADEMA ina madiwani wawili katika wilaya ya Ikungi.
Nafasi ya makamu mwenyekiti imenyakuliwa na Alli Nkhangaa ambaye naye alipata kura 29 za ndio na moja ilimkataa.
Mapema akizungumza kwenye mkutano huo wa uchaguzi, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ikungi Hassan Tati, amewahimiza madiwani hao kuhakikisha wanaimarisha umoja wao ili chama kiendelee kuwa na nguvu za kushinda chaguzi mbalimbali.
Wakati huo huo, Katibu wa CCM wilaya ya Singida vijijini Mwanamvua Kilo, amesema mkutano wa uchaguzi wa nafasi ya mwenyekiti na makamu wake katika halmashauri hiyo umeahirishwa hadi hapo baadae.
Amesema mkutano huo uliokuwa ufanyike juzi, pamoja na madiwani wote wa halmashauri hiyo kuhudhuria, haukufanyika kutokana na hitilafu zilizojitokeza mara tu baada ya mkutano huo kuanza.
Amesema hawezi kwa sasa kusema ni nini kilichotokea kwenye mkutano wao, ila ifahamike tu kwamba uchaguzi huo utarudiwa baadae katika siku itakayopangwa.
KWA HISANI YA MO BLOLG
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa