Home » » Basi la Mtei lataifishwa kwa kubeba wahamiaji

Basi la Mtei lataifishwa kwa kubeba wahamiaji


WATU 12 raia wa Ethiopia wamehukumiwa na mahakama ya Wilaya ya Singida, kulipa faini ya Sh100,000 kila mmoja baada ya kukiri makosa mawili ya kuingia na kuishi ndani ya ardhi ya  Tanzania bila ya kuwa na kibali halali.
Pia mahakama hiyo, imeamuru basi la Kampuni ya Mtei ya mjini Arusha lililokuwa limebeba Waethiopia hao kukamatwa na kutaifishwa kuwa mali ya Serikali.
Waethiopia hao ambao wote bado vijana wadogo na wengine ni wanafunzi wa shule na vyuo, ni pamoja na Ahmed Mohammed Mahamud, Tazana  Walao, Mohammed Osman, Abraham Nirato Shango, Adinan Abdalah na Alamu Gabresekesie.
Weingine ni Muhidini Sufiani Ahmed, Tasfai Sutatu  Kidisu, Yassin Mohammed Hassan, Afandi Aden Suleiman, Ayele Liranso Gafuche na Pakala Agore Mancha.
Baada ya mwendesha mashtaka mwanasheria wa Serikali Ahmed Seif kuwasomea makosa hayo mawili ya kuingia na kuishi  nchini bila ya kuwa na kibali, washtakiwa wote kila mmoja kwa nafasi yake, walikiri kutenda makosa hayo.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Mwanasheria wa Serikali, Seif, aliiomba mahakama hiyo  iwape adhabu kali washtakiwa ikiwa ni njia moja wapo ya kukomesha vitendo vya wahamiaji haramu kuingia na kuishi nchini bila ya kuwa na kibali chochote halali.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mfawidhi Kiongozi wa Mahakama ya Wilaya ya Singida, Flora Ndale alisema mahakama yake imezingatia yale yote yaliyoombwa na upande wa mashtaka na utetezi na kufikia uamuzi wa kutoa adhabu ya kulipa faini ya Sh100,000 kila mshtakiwa.
Washtakiwa wote 12 walilipa faini hiyo.
Kwa mujibu wa Mwanasheria wa Serikali Seif, washtakiwa hao walikamatwa Januari 17, mwaka huu alasiri katika eneo la Kijiji cha Kititimo nje kidogo ya Mji wa Singida wakiwa wametokea mkoani Arusha wakidai kwenda Afrika Kusini.
Mwananchi


0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa