Mfanyabiashara ajiua kwa risasi, mwingine achinjwa

Watu wawili wamefariki dunia katika matukio mawili tofauti yaliyotokea mkoani Singida mwishoni mwa wiki likiwemo la mfanyabiashara kujipiga risasi kichwani na mwingine huchinjwa shingo, kutolewa koromeo na ulimi.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Geofrey Kamwela alisema katika tukio la kwanza, mfanyabiashara Mashaka Omari (30) alikutwa chumbani kwake Mtaa wa Ipembe akiwa amekufa baada ya kujipiga risasi kichwani.
Alisema mfanyabiashara huyo alijiua kwa kutumia bastola yake yenye namba TZ CA 895101 ambapo polisi walikuta ganda moja la risasi iliyotumika lakini magazini ilikuwa na risasi 11," alisema Kamanda Kamwela.
Uchunguzi wa awali unaonesha marehemu alikuwa na mgogoro kati yake na mtu mwingine ambaye hakutajwa kwa ajili ya masuala ya kiusalama hivyo kusababisha ajiue.
"Marehemu aliacha ujumbe huo wa maandishi kwenye gari lake namba T664 EES aina ya Toyota RAV 4 ambalo alikuwa ameliegesha nje ya ofisi yake," alisema na kuongeza kuwa, uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea.
Katika tukio lingine, mkazi wa Kijiji cha Sambaru, Wilaya ya Ikungi, Tatu Selemani (42), alichinjwa shingo na kitu chenye ncha kali na watu wasiofahamika saa 1:30 asubuhi.
Kamanda Kamwela alieleza licha ya kuchinjwa shingo pia marehemu alitolewa koromeo, ulimi, kuchunwa ngozi usoni na kutolewa sikio la kushoto ambapo mwili wake ulikutwa umbali wa mita 80 kutoka nyumbani kwake.
Alisema katika tukio hilo, mtu mmoja Amosi Shenan maarufu kwa jina la 'Babu', mkazi wa kijiji hicho ambaye ni mume wa marehemu, amekamatwa kwa mahojiano zaidi na uchunguzi bado unaendelea

Chanzo;Majira

Padri anayedaiwa kutelekeza mtoto kuburuzwa kortini tena leo

Mahakama ya Mwanzo Utemini iliyopi mjini hapa Mkoa wa Singida, leo inatarajia kuendelea kusikiliza kesi inayomkabili Padri  wa Kanisa Katoliki mjini hapa,  Deogratius Makuri ya kumtelekeza bila  kumhudumia mtoto wake wa kike aliyedaiwa kuzaa na muumini wake.
 Kesi hiyo ilisikilizwa wiki iliyopita na kuahirishwa baada ya kudaiwa mahakamani hapo kuwa padri huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi wa muda mrefu na Maria Boniphance (26) aliyekuwa mhudumu wa kanisa hilo Parokia ya Singida mjini.

 Ilidaiwa mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Ferdnand Njau kuwa wakati wote huo wa mahusiano ya kimapenzi, ndipo mshitakiwa alimpa ujauzito na kuzaa naye mtoto wa kike.

Mlalamikaji (Maria) alidai mahakamani hapo kuwa   baada ya ujauzito huo, aliamua kulifikisha suala hilo kwa wazazi wake ambao walimwendea padri huyo na kukubali kuhusika na mimba hiyo.

Alidai kuwa padri huyo aliahidi kwa maandishi kuwa atamtunza mtoto wake (jina tunalo) hadi hapo atakapokuwa na uwezo wa kujitegemea, kinyume chake ahadi hiyo alitekeleza kwa miezi michache na akasitisha matunzo.

"Pamoja na kuchukua hatua mbalimbali ikiwamo kufikisha suala hilo ofisi ya ustawi wa jamii... aliahidi kupitia hati ya mkataba kuwa atakuwa anatoa kila mwezi Sh. 80,000 na akishindwa afikishwe mahakamani, ndiyo mimi nimeamua kumshitaki, ”alidai mlalamikaji huyo.

Ilidaiwa kuwa pamoja na ahadi hiyo padri Makuri alianza kutoa madai mbalimbali kwamba mtoto huyo siyo wake wa kuzaa, na hapo ndipo aliamua kusitisha matunzo kama alivyoahidi.  .
 
CHANZO: NIPASHE

Ikungi kutumia bil. 25/-

HALMASHAURI ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, inatarajia kutumia shilingi bilioni 25.696 katika mwaka wa fedha 2014/2015 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shughuli za maendeleo.
Akisoma taarifa ya bajeti kwenye kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo jana, Makamu Mwenyekiti Ally Nkangaa, alisema katika kipindi hicho kiasi cha sh bilioni 15.426 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wake.
Hata hivyo alisema katika bajeti iliyopita halmashauri iliomba kuidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 16.953 ambapo hadi kufikia mwezi Desemba mwaka huu, jumla ya shilingi milioni 512.322 zilikuwa zimetumika kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Nkhangaa alisema katika utekelezaji wa bajeti, zipo changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na baadhi ya vijiji na kata kutochangia nguvu kazi na fedha.
Chanzo;Tanzania Dama

Mvua kubwa zaleta madhara Singida, watu watano wahofiwa kufa maji


DSC049001
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida, SACP Geofrey Kamwela, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na tukio la maafa ya mvua kubwa iliyosababisha vifo.
Na Nathaniel Limu, Singida
MVUA kubwa zilizoanza kunyesha mkoani Singida zimeanza kuleta maafa baada ya watu watano kuhofiwa kufa maji kutokana na gari waliolokuwa wakisafiria kusombwa na maji ya mto.
 Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Singida, SACP Geofrey Kamwela amesema tukio hilo limetokea Desemba saba mwaka huu saa 3:30 asubuhi huko katika mto wa Nzalala kijiji cha Kisimba tarafa ya Kisiriri wilayani Iramba.
Amesema siku ya tukio, abiria 16 waliokuwa wakitoka kijiji cha Doromoni kwa kutumia Landrover 110 TDI lenye namba za usajili T.499 ATR, lilisombwa na maji ya mto wakati dereva wake akijaribu kuvuka mto Nzalala.
 Akifafanua, amesema walimpofika kwenye mto huo abiria hao walimwomba dereva huyo asubiri maji ya mto yapungue ili waweze kuvuka lakini dereva huyo alikataa kwa madai maji ni machache.
 “Wakati gari hilo lilipofika katikati ya mto, lilizimika ghafla na wakati huo huo maji ya mto yaliongezeka na kulifunika gari.  Dereva na kondakta waliweza kufanikiwa kutoka na kukimbilia kusikojulikana”
 Aidha, amesema abiria 11 waliweza kuokolewa na wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Iramba na watano hadi sasa haijulikani iwapo wamekufa ndani ya landrover au wamesomba na maji na kupelekwa kusikojulikana.
 Katika hatua nyingine, Kamanda Kamwela, ametoa wito kwa madereva wa vyomba vya moto, baiskeli na watembea kwa miguu kuchukua tahadhari wakati wa kuvuka mito au mabonde kipindi hiki cha mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
 Alitumia fursa hiyo kushauri mamlaka zinazohusika kutengeneza madaraja kwenye mito au mabonde badala ya kuweka zege ambalo husaidia tu katika kipindi cha kiangazi.
 “Aidha nashauri abiria nao wasikubali kujazwa kwenye vyombo vya usafiri tofauti na uwezo hali wa gari” amesema.
Na Mo Blog

MAJAMBAZI WAWILI WAUAWA MKOANI SINGIDA.

TUNAOMBA RADHI KWA HII PICHA


Kamanda wa polisi mkoa wa Singida,SACP Geofrey Kamwela,akionyesha bunduki ya kijeshi aina ya SMG no.34555  iliyokuwa ikitumiwa na watu wawili wanaodhaniwa kuwa majamabazi katika kijiji cha Manga manispaa ya Singida.

WATU wawili wakazi wa manispaa ya Singida ambao majina yao bado hayajajulikana,wakiwa kwenye Jokofu la kuhifadhia maiti baada ya kuuawa wakati wa majibishano ya risasi na polisi.


JESHI  la Polisi mkoani Singida limewauwa watu wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakati wa kurushiana rasasi.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Singida, SACP, Geofrey Kamwela amesema tukio hilo limetokea desemba tisa mwaka huu saa 12:00 jioni, huko katika kijiji cha Manga nje kidogo ya mji wa Singida.
Amesema watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wakiwa na bunduki moja ya kijeshi aina ya SMG, walifika kijijini hapo kwa lengo la kufanya uhalifu.
Kamanda Kamwela, amesema watu hao ambao miili yao imehifadhi kwenye chumba cha mochwari katika hospitali ya mkoa, majina na makazi yao bado hayajajulikana.
Akifafanua, amesema taarifa za siri kutoka kwa raia wema zilifikia jeshi la polisi na ndipo askari polisi walipofika kwenye eneo la tukio.
“Baada ya polisi kufika kijijini hapo watu hao walistuka kuwa wanafuatilwa na askari polisi na hivyo kuanza kukimbia kuelekea kijiji cha Uhamaka kwa kutumia pikipiki yenye namba za usajili T. 634 BTW aina ya Sanlag yenye rangi nyeusi”,amesema Kamwela.
Amesema walipoona Polisi wanawakaribia waliamua kutelekeza pikipiki yao hiyo na kuanza kukimbilia porini kwa miguu.
“Hali ilipokuwa ngumu zaidi, walianza kuwarushia polisi risasi, hivyo polisi nao ikwabidi kujibu mapigo.  Katika majibizao hayo ya risasi, majambazi mawili yaliweza kujeruhiwa huku mmoja akifanikiwa kutoroka”
Amesema majambazi hayo yaliyojeruhiwa yalifariki dunia wakati yanakimbizwa katika hospitali ya mkoa kwa matibabu,lakini yakafia njiani.
Amesema katika eneo la tukio, ilipatikana
bunduki moja aina ya SMG yenye namba 34555 ikiwa na risasi saba kwenye magazine.  Pia pikipiki iliyokuwa iantumiwa na majambazi hayo, iliwezea kupatikana.
Kamwela alitoa wito kwamba wananchi waendelee na moyo huo huo wa kuwafichua watu wanaowatilia shaka ili waweze kudhibitiwa mapema kabla ya kufanya uhalifu.
Kwa hisani ya Mtandao wa Singida Yetu

WATANO WAFA MAJI NA WENGINE 11 WANUSURIKA

WATU watano wanahofiwa kufa maji na wengine 11 wamenusurika, baada ya gari waliyokuwa wakisafiria kusombwa na maji ya mto kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani mkoani Singida.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida Kamishina msaidizi mwandamizi Geofrey Kamwela, tukio hilo limetokea jana majira ya saa 3: 30 asubuhi katika Kijiji cha Kisimba Wilayani Iramba.
Amesema watu hao waliokuwa wakisafiri kwa gari yenye namba za usajili T.499 ATR aina ya Land rover 110 TDI, walikuwa wakijaribu kuvuka mto Nzalala kutoka eneo Doromoni kwenda Kiomboi Mjini.
Kamanda Kamwela amesema wakati dereva ambaye hajatambuliwa jina wala makazi akijaribu kuvusha, gari hiyo ilizimika katikati ya mto kabla ya kosombwa na maji ikiwa na abiria 16 ndani.
Amesema abiria 11 kati yao wameokolewa na kupelekwa hospitali ya Wilaya ya Iramba kwa matibabu, wakati juhudi za kufukua gari hiyo iliyofukiwa kwa mchanga mita chache kutoka eneo la tukio na kutafuta watu wengine watano ambao hawajulikani walipo zinaendelea kufanywa.
Dereva wa gari hiyo na kondakta wake wanasadikiwa kutoweka baada ya tukio hilo na polisi wanaendelea kuwasaka.

Ajali yaua watano

Singida.Abiria watano wamekufa baada ya gari aina ya Landrover 110 waliyokuwa wanasafiria kusombwa na maji katika Kijiji cha Doromoni Wilaya ya Iramba.
Katika ajali hiyo iliyotolea jana, watu wengine 11 walinusurika baada ya kuruka na kuogelea mara baada ya gari hiyo kupinduka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
Kamwela alisema ajali hiyo ilitokea majira ya asubuhi wakati gari hilo likiwa linabeba abiria 16 kutoka Kijiji cha Doromoni wilayani Iramba kuelekea Kiomboi mjini.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni kujaa kwa maji katika Mto Nzalala kiasi cha kulifunika daraja.
Kamwela alisema wakati dereva alipojaribu kuvuka, gari hiyo ilizidiwa nguvu na maji, hivyo kuisomba.
Baadhi ya abiria walionusurika kwenye ajali hiyo walisema kwamba walipofika kwenye daraja hilo walimwambia dereva asivuke, bali asubiri maji yapungue.
Walidai dereva alikaidi agizo hilo na kuamua kuvuka na alipofika katikati alionekana kubabaika na maji kabla ya maji kuizidi nguvu gari.
Habari ambazo pia hazijathibitishwa zilidai kuwa dereva na kondakta wa gari hilo waliruka na kukimbia eneo la ajali.
Chanzo;Mwananchi

Polisi yaua majambazi wawili

JESHI la Polisi mkoani Singida limewaua kwa kuwapiga risasi majambazi wawili waliokuwa wakijiandaa kufanya uhalifu katika Kijiji cha Manga nje kidogo ya mji wa Singida.
Kamanda wa Polisi mkoani Singida, Godfrey Kamwela alisema tukio hilo limetokea juzi, saa 12:00 jioni baada ya polisi kupata taarifa za siri kutoka kwa raia wema.
Kamwela alisema majambazi hayo yalikuwa na bunduki moja aina ya SMG yenye namba 34555 ikiwa na risasi saba kwenye magazine, huku wakitumia pikipiki T 634 BTW Sanlg.
Aidha, Kamanda Kamwela alisema askari polisi walifika katika eneo hilo, na watu hao walistuka kwa kuwa wanafuatiliwa na askari na hivyo kuanza kukimbia kuelekea Kijiji cha Uhamaka kwa kutumia pikipiki hiyo.
Hata hivyo, alisema walipoona polisi wanawakaribia waliitelekeza pikipiki hiyo na kuanza kukimbia porini kwa miguu, lakini hali ilipokuwa ngumu zaidi walianza kuwarushia polisi risasi, hivyo polisi nao walilazimika kujibu.
“Majibizano hayo ya risasi yalipelekea majambazi wawili kujeruhiwa huku mmoja akifanikiwa kukimbia. Majeruhi hao walifariki dunia wakati wakikimbizwa hospitali ya mkoa kwa matibabu. Maiti zimehifadhiwa hospitalini hapo kwa ajili ya kutambuliwa na ndugu zao,” alisema Kamwela.
Alisema kwenye eneo la tukio ilipatikana bunduki moja aina ya SMG ikiwa na risasi saba na pikipiki iliyokuwa wakiitumia kukimbia. Polisi wanaendelea na uchunguzi   ili kubaini kama kuna mtandao wa majambazi pamoja na kumsaka mtuhumiwa aliyekimbia.
Wakati huohuo, polisi mkoani hapa inawashikilia watu wanne akiwemo mhudumu wa nyumba ya kulala wageni ya Lake Hill Singida Motel kuhusiana na tukio la ujambazi lililotokea kwenye hoteli hiyo.
Kamanda Kamwela alisema wizi huo ulitokea juzi, saa 9:30 usiku, ambapo watu ambao idadi bado haijajulikana wakiwa na bunduki walivamia hoteli hiyo na kuwapora wapangaji vitu mbalimbali.
Alisema watu hao walipofika katika hoteli hiyo walifyatua risasi hewani kwa lengo la kuwatisha wapangaji na walinzi na kufanikiwa kuwafunga kamba walinzi wote watatu na kuingia katika vyumba viwili na kuwanyang’anya wapangaji mali pamoja na fedha.
Aliwataja wanaoshikiliwa kwa tuhuma hizo ni walinzi hao wa kampuni binafsi ya ulinzi ya Mass Security ya mjini Singida ambao ni Juma Mwangwi (35), Zakaria Pastory (23) na Donald Samson (19) na Mhudumu wa hoteli hiyo, Alistides Salvatory  (24).
Kamanda Kamwela alitaja vitu vilivyoporwa kuwa ni kompyuta mpakato moja, simu tatu za mkononi zenye thamani ya sh milioni moja, saa mbili za mkononi moja yenye thamani ya dola 500 za Marekani  pamoja na fedha taslimu sh 800,000 na dola 500
Chanzo;Tanzania Daima

Ofisi ya mtendaji Kondoa yafungwa

OFISI ya mtendaji wa kijiji cha Salanka, kata ya Salanka, wilayani Kondoa, imefungwa kwa kukosa mtendaji wa kijiji kwa muda wa mwaka moja sasa.
Hali hiyo imeelezwa kuchangia wananchi kukosa huduma hivyo na kulazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo kwenye ofisi ya kata.
Mtendaji wa kijiji hicho alisimamishwa na mkutano wa kijiji kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za kijiji.
Akizungumza kwenye mkutano wa kijiji, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Khamis Majaliwa, alisema wamekuwa wakifuatilia suala hilo kwa muda sasa huku Ofisi ya Mkaguzi wa Hesabu za Ndani wa halmashauri hiyo akifika mara moja na hadi sasa hajafika kijijini hapo kwa madai ya kukosa usafiri.
Katika mkutano huo, wanakijiji hao waliazimia kwenda kuonana na Waziri Mkuu kutatua tatizo hilo lililodumu kwa muda wa mwaka sasa licha ya viongozi mbalimbali kuulizwa na kukosa majibu.
Alipoulizwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Omar Kwang’, alisema kwa wakati huo alikuwa yuko nje ya ofisi akiwa likizo na kumtaka mwandishi kusuburi hadi atakaporudi ofisini ndipo atatoa majibu.
Chanzo;Tanzania Daima

MSIMAMO WA CHADEMA MKOA WA SINGIDA DHIDI YA MAAMUZI YA KAMATI KUU - TAARIFA KWA UMMA



                     
WILFRED NOEL KITUNDU
MWENYEKITI CHADEMA MKOA SINGIDA
S.L.P 260
3.12.2013
KATIBU WA CHADEMA MKOA
S.L.P 260
SINGIDA
YAH: - KUJIUZURU UENYEKITI MKOA SINGIDA
Somo hapo lahusika,
Ninapenda kukuarifu kuwa nimeamua kujiuuzuru nafasi yangu ya uenyekiti wa mkoa ambayo nimekuwa nikiitumikia kwa kipindi kirefu sasa kama kielelezo cha kuamini na kudai demokrasia ya kweli ndani ya chama.

Ikumbukwe kwamba mimi ndio mwanachama wa kwanza kujiunga na CHADEMA mkoa wa SINGIDA na ni mwanachama wa 300 kitaifa, hiyo ni heshima kubwa sana kwangu na sipo tayari kuipoteza kwa kukubali kuwa sehemu ya udharirishaji huu wa demokrasia uliopitiliza

Maamuzi na vitendo vinavyoendelea ndani ya chama chetu kwa sasa ni ubakaji na udharirishaji wa demokrasia ya kweli tunayoihubiri mbele ya umma.

Kwa barua hii basi, nimeonelea bora upate ufahamu huo kuwa si vema mimi kuendelea kupingana na dhamira yangu inayonituma kuwa mwanademokrasia wa kweli.

Kwa kipindi hiki kifupi mnaweza mkaendelea kuitumia anuani yangu ya posta mpaka hapo mtakapopata anuani yenu tayari.

Ninatanguliza shukrani zangu za dhati kwa wanachadema wote wanaopinga upuuzi huu uliofanywa na kamati kuu ya chama.

Kusimamia haki, katiba na misingi ya chama ni wajibu wangu, hivyo kwa namna yoyote ile sitaweza kuwa tayari kufumba macho pindi ujinga wa namna hii unapoendelea kutekelezwa kwa uwoga wa uchaguzi.


Nakutakia kila la heri kwenye majukumu yako.

………………………………………………….
Wilfred N. Kitundu

MWENYEKITI CHADEMA
MKOA SINGIDA
S.L.P 260
3.12.2013




Wajasiriamali waelezwa umuhimu wa soko la hisa

MKUU wa Mkoa wa Singida, Dk. Parseko KoneMKUU wa Mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone, ameelezea umuhimu wa soko la hisa katika upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu na uwekezaji kuwa haviwezi kuletwa na masoko ya mitaji pekee.
Kwa mujibu wa mkuu huyo, dhima ya kupata rasilimali na kuzitumia kikamilifu kwenye miradi yenye tija, husababisha ukuaji wa uchumi na kuongeza utajiri.
Dk. Kone amebainisha hayo juzi mjini Singida wakati akifungua semina ya siku mbili kwa wafanyabiashara na wajasiriamali juu ya soko la kukuza ujasiriamali (EGM) iliyofanyika kwenye ukumbi wa Aque Vitae.
Alisema ni muhimu ieleweke wazi kwamba kuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya mafanikio ya masoko ya mitaji na uchumi wa nchi na kusisitiza kwamba moja ya sababu ni serikali kuanzisha na kusaidia maendeleo ya Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Aidha, alibanisha kwamba kampeni hiyo imekuja wakati muafaka ambao serikali imepania kujenga sekta binafsi imara itakayokuwa injini ya uchumi wa taifa.
“Napenda kuchukua fursa hii kuwahakikishia kwamba serikali inatambua mchango wa wadau mbalimbali katika maendeleo ya masoko ya hisa hapa nchini, mwamko kama huu unalenga kujenga uelewa kwa sekta binafsi na umma juu ya fursa zipatikanazo na soko la hisa zinaungwa mkono na serikali.
“Pia nitumie fursa hii kuwataka wadau na wahusika wote kwa ukamilifu wenu kutumia tukio hili ili kutumia fursa zipatikanazo kwenye soko la hisa,” alisema Dk. Kone.
Hata hivyo Dk. Kone alisema tafiti nyingi zimeonyesha kwamba upatikanaji wa mitaji ya wajasiriamali wadogo na wa kati ni changamoto kwa maendeleo ya kukua kwa shughuli za ujasiriamali na sekta hiyo kwa ujumla.
Awali Meneja Uhusiano wa kitaasisi kutoka DSE, Mary Mniwasa, alimweleza mkuu wa mkoa kuwa lengo la semina hiyo ni kampeni ya umma ya kupunguza umaskini hapa nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Singida, Francis Mashuda, alisema wafanyabiashara wanakumbana na changamoto kubwa ya ukosefu wa mitaji.
Semina hiyo ilitarajiwa kuhudhuriwa na wafanyabiashara wa kada mbalimbali na wajasiriamali wasiopungua 65, imefadhiliwa na DSE chini ya uratibu wa TCCIA Mkoa wa Singida.
Chanzo;Tanzania Daimma
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa