IGP SIRRO AMALIZA ZIARA YAKE MIKOA YA KANDA YA ZIWA KWA KISHINDO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro, akizungumza na baadhi wa  Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoa wa Singida, wakati alipofika katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa huo kwa lengo la kujitambulisha na kuzungumza na askari na maofisa wa Jeshi hilo pamoja na kujua changamoto wanazokutananazo wakitekeleza majukumu yao. Picha na Jeshi la Polisi. 

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro, akizungumza na askari na maofisa wa Jeshi hilo na kuwataka wafanyekazi kwa kutenda haki na kusimamia misingi ya sheria na taratibu, IGP Sirro yupo mkoani Singida kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kujitambulisha na kuzungumza na askari na kujua changamoto wanazokutananazo wakitekeleza majukumu yao. Picha na Jeshi la Polisi. 
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro, akizungumza na kikosi cha Polisi wanawake baada ya kukagua gwaride la heshima lililoandaliwa kwa ajili yake alipowasili mkoani Singida, kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kujitambulisha na kuzungumza na askari na kujua changamoto wanazokutananazo wakitekeleza majukumu yao. Picha na Jeshi la Polisi. 


Na Jeshi la Polisi Nchini

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro, amemaliza ziara yake katika mikoa ya kanda ya ziwa pamoja na mkoa wa Singida, huku akiacha morali kwa watendaji wa Jeshi hilo hatua ambayo italiwezesha ieshi hilo kufanyakazi zake kwa weledi katika kukabiliana na matishio ya uhalifu na wahalifu.

IGP Sirro, amefanya ziara hiyo ikiwa ni mkakati wake aliojiwekea tangu alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Jeshi hilo kwa lengo la kujitambulisha na kuzungumza na askari na maofisa ili kujua namna wanavyotekeleza majukumu yao ya kazi za Polisi.

Katika mazungumzo yake IGP Sirro, amewataka askari na maofisa kutimiza wajibu wao kwa kutenda haki na bila uwoga wala kumuonea mtu muhali jambo ambalo litarahisisha upatikanaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu katika jamii.

Hata hivyo, katika mabaraza ya kuzungumza na askari na maofisa baadhi ya hoja kadhaa ziliibuliwa kwa baadhi ya askari waliopata nafasi ya kutoa mawazo yao, ambapo IGP Sirro aliahidi kuzishughulikia mapema ili kuzidisha morari katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Aidha, katika ziara yake IGP Sirro, alipata fursa ya kukutanana Wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama ya mkoa huku masuala kadhaa ya kiusalama na mbinu na mikakati ikijadiliwa katika kamati hizo na kuahidi kutoa ushirikiano utakaowezesha kukabiliana na matishio mbalimbali ya kiuhalifu.

IGP SIRRO ALIPONGEZA JESHI LA POLISI MKOA WA SINGIDA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

1
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akipiga saluti wakati wa paredi ya polisi iliyoandaliwa lililoandaliwa  kwa ajili yake kulikagua mapema leo kwenye viwanja vya kambi ya  FFU mjini hapa.

2
Mkuu wa Jeshi la Polisi  nchini IGP Simon Sirro akikagua baadhi ya askari wa jeshi la polisi  mjini  Singida leo piga saluti wakati wa paredi ya polisi iliyoandaliwa lililoandaliwa  kwa ajili yake kulikagua.
3
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada kukagua askari polisi waliokuwa kwenye  paredi kwenye viwanja vya kambi ya  FFU mjini hapa.
………………………….
Picha/Habari na Gasper Andrew.
Mkuu wa Jeshi la polisi nchini (IGP), Simon Sirro amelipongeza jeshi la polisi Mkoani Singida kwa juhudi zake za kupunguza matukio ya uhalifu yakiwemo ya utekeji wa magari kwa kiwango kikumbwa.
IGP  Siro ametoa pongezi hizo  leo asubuhi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari  kweye viwanja vya kambi  ya kikosi  cha kuzuia fujo (FFU) mjini  hapa.
Amesema matukio ya uhalifu mbalimbali mkoani Singida yamekupungua kwa kiwango kikubwa kwa  sasa, ikilinganishwa na miaka ya  nyuma.
“Hatua hii  inachangia  uwepo  wa amani  na utulivu kwa  wananchi  wa  mkoa wa Singida hivyo  kutoa fursa   kuweza  kujiletea maendeleo yao ya mkoa na  taifa   kwa ujumla” amesema.
IGP Siro  amesema  mafanikio  hayo yamechangiwa   na wananchi kwa kiwanngo  kikubwa  kwa kutoa ushuirikiano  kwa jeshi la polisi. 
Akifafanua amesema wananchi wamekuwa wakitoa  taarifa sahihi na kwa  wakati kwa jeshi la polisi  pindi wanapobaini  dalili  ama  matukio ya kihalifu.
“Kwa sasa kwa kweli  wananchi hata ninyi waandishi  wa habari mnatupa  ushirikiano  mzuri sana. Ushirikiano huu unachangia  kazi zetu kuwa nyepesi  na za mafanikio makubwa. Sasa  hivi  kule Kibiti mkoani Pwani, wananchi wanatusaidia mno taarifa  zinazohusu  mauaji ya watu  wasiokuwa  na hatia”, amefafanua zaidi.
IGP Siro amesema kwa sasa Tanzania inaonewa wivu na nchi jirani kwa namna tulivyo dhibiti matukio ya kihalifu na kupelekea nchi kuendelea kudumisha amani na utulivu.
Wakati huo huo, Mkuu huyo  wa jeshi la polisi ametumia fursa hiyo  kuwaomba wananchi  waendelee  kushirikiana na jeshi hilo, kufichua  baadhi ya watu wanaojihusisha na matukio mbalimbali   ya kihalifu ili waweze kuchukulia  hatua stahiki.

RAIS DKT. MAGUFULI AFUNGUA BARABARA YA ITIGI-MANYONI-CHAYA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akikaribishwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi alipowasili Mkoani Singida eneo la Itigi ili kufungua Barabara ya Itigi -Manyoni -Chaya yenye urefu wa kilometa 89.5 iliyojengwa na Serikali kwa asilimia mia moja. Mheshimiwa Rais alikuwa akitokea kwenye ziara ya siku tatu Mkoni Tabora kupitia Singida akiwa njiani kuelekea  Dodoma  Julai 25,2017.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli (wa pili kushoto) na viongozi wengine wa mkoa wa Singida wakiondoa kitambaa kuashiria kufunguliwa rasmi kwa  barabara ya Itigi -Manyoni -Chaya yenye urefu wa kilometa 89.5 iliyojengwa kwa fedha za Serikali kwa  asilimia mia moja.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Viongozi wengine wa Mkoa wa Singida na Tabora Wakikata Utepe kama ishara ya kufunguliwa Rasmi kwa  Barabara ya Itigi -Manyoni -Chaya yenye urefu wa kilometa 89.5 iliyojengwa kwa fedha za Serikali kwa  asilimia mia moja.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kulia akiteta jambo na Mwakilishi wa Kampuni ya PowerChina International Group Limited nchini Bw. Wang Chao wakati wa Ufunguzi wa  Barabara ya Itigi -Manyoni -Chaya yenye urefu wa kilometa 89.5 iliyojengwa kwa fedha za Serikali kwa  asilimia mia moja.
  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwashukuru na kuwasalimia kwa kupunga mikono kwa wananchi wa Itigi na Manyoni walioshiriki na Kushuhudia Ufunguzi wa  Barabara ya Itigi -Manyoni -Chaya yenye urefu wa kilometa 89.5 iliyojengwa kwa fedha za Serikali kwa  asilimia mia moja.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwaaga wananchi wa Itigi na Manyoni walioshuhudia Ufunguzi wa  Barabara ya Itigi -Manyoni -Chaya 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwahutubia Wananchi Kijiji Cha Tula Uyui Mkoani Tabora waliojitokeza Barabarani Kumsalimia akiwa njiani kuelekea Mkoani Dodoma akitokea kwenye ziara ya siku tatu Mkoni Tabora Julai 25,2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisisitiza jambo akiwa njiani katika moja ya mikutano ya barabarani kwa  waliojitokeza  Kumsalimia akiwa njiani kuelekea Mkoani Dodoma akitokea kwenye ziara ya siku tatu Mkoni Tabora Julai 25,2017.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia wananchi wa Itigi na Manyoni wakati wa Ufunguzi wa  Barabara ya Itigi -Manyoni -Chaya yenye urefu wa kilometa 89.5 iliyojengwa kwa fedha za Serikali kwa  asilimia mia moja.
Wananchi wa Itigi na Manyoni wakimsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwatubia kwenye Ufunguzi wa  Barabara ya Itigi -Manyoni -Chaya yenye urefu wa kilometa 89.5 iliyojengwa kwa fedha za Serikali kwa  asilimia mia moja. 
Picha zote na IKULU


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwapungia mkono wakazi wa Itigi mara baada ya kuzungumza nao na kuzindua barabara Manyoni-Itigi-Chaya, ambapo pamoja na mambo mengine ameagiza ujenzi wa barabara ya Chaya-Nyaua yenye kilomita 85 na ujenzi uanze ndani ya siku 45 ili barabara hiyo ikamilike kwa kiwango cha lami.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na umati wa wakazi wa Itigi waliojitokeza kumlaki na kushuhudia uzinduzi wa barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya, Rais Magufuli amewataka wana Itigi kutumia fursa ya kuwa jirani na Makao makuu ya nchi kwa kufanya kazi kwa bidii na kuzalisha bidhaa ambazo zitauzwa huko Dodoma.
 Umati wa wakazi wa Itigi waliojitokeza kumlaki Rais Magufuli na kushuhudia uzinduzi wa barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya, wakazi hao wamempongeza na kumshukuru Rais Magufuli kwa kuwajengea barabara hiyo ambayo ni muhimu kwa kuwaunganisha na mikoa ya Tabora na Kigoma.
 Sehemu ya barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya ambayo imezinduliwa leo na Rais Magufuli, Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 89.3 kwa kiwango cha lami imefungua fursa ya usafirishaji kwa urahisi kutoka kanda ya Kati yaani Singida na Dodoma Kuelekea mikoa ya Tabora na Kigoma hadi nchi za jirani za Burundi na Kongo.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Makame Mbarawa akimkaribisha Rais Magufuli azungumze na wananchi wa Itigi, ambapo amesema barabara ya Manyoni Itigi Chaya imegharimu shilingi bilioni 114.692 na kiunganishi cha Mikoa ya Singida, Tabora na Kigoma kuelekea Makao makuu ya Nchi yaani Dodoma.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiambatana na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi kwenye eneo la mkutano wa hadhara mara baada ya kuwasili eneo la Njiapanda Itigi, alipozungumza na wananchi wa eneo hilo na kuzindua barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya.
 Umati wa wakazi wa Itigi waliojitokeza kumlaki Rais Magufuli na kushuhudia uzinduzi wa barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya, wakazi hao wamempongeza na kumshukuru Rais Magufuli kwa kuwajengea barabara hiyo ambayo ni muhimu kwa kuwaunganisha na mikoa ya Tabora na Kigoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amkimsikiliza kwa makini Mhandisi wa TANROADS mkoa wa Singida Leonard Kapongo mapema leo. Katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Itigi, Rais Magufuli amemuagiza Meneja huyo na Wizara ya ujenzi kupitia upya gharama za ujenzi wa barabara ya Mkiwa-Itigi itakayoelekea Makongorosi yenye urefu wa kilomita 57 ambapo gharama za ujenzi wa barabara hiyo ni bilioni 104

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO AZINDUA BODI MPYA YA USHAURI YA WIZARA - TAASISI YA UHASIBU TANZANIA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akizungumza muda mfupi kabla hajazindua Bodi mpya ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA). Uzinduzi huo umefanyika hivi karibuni katika kampasi ya TIA tawi la Singida mjini.
 Mwenyekiti wa Bodi mpya ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Said Chiguma akizungumza kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa Bodi mpya ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA). Uzinduzi huo umefanyika hivi karibuni katika kampasi ya TIA tawi la Singida mjini.
 Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Joseph Kihanda, akitoa nasaha zake kwenye hafla ya uzinduzi wa Bodi mpya ya Ushauri ya Taasisi hiyo. Uzinduzi huo umefanyika hivi karibuni katika kampasi ya TIA tawi la Singida mjini.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa  Bodi mpya ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA). Uzinduzi huo umefanyika hivi karibuni katika kampasi ya TIA Singida mjini. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Bodi mpya ya Ushauri TIA Said Chiguma na Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA Joseph Kihanda na kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhe. Elias Tarimo na Mjumbe wa Bodi Dkt. Leonada.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango  Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amezindua Bodi mpya ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kwa lengo la kuimarisha ufanisi wa Taasisi  na uangalizi wa karibu.

Akizungumza hivi karibuni wakati wa uzinduzi huo uliofanyika  Taasisi ya Uhasibu Tanzania kampasi ya Singida  Dkt. Kijaji amesema Bodi hiyo itamsaidia Waziri wa Fedha na Mipango kupata ushauri wa kitaalam  na hatimaye kutoa maamuzi  yenye tija kwa Taasisi na Taifa kwa ujumla.

 "Bodi hii ya Ushauri inategemewa kutoa mchango  wa mawazo na  kitaalam yanayohusu uendeshaji  na uboreshaji wa  Taasisi yetu ya TIA ili kuendana na mabadiliko yanayoendelea duniani katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kiteknolojia, kisiasa na kijamii", amesema Dkt. Kijaji.

Dkt. Kijaji ameongeza kuwa Bodi hiyo ina wajibu wa kujua ubora wa wanafunzi wanaohitimu katika chuo hicho ikiwa ni pamoja na ubora wa vyeti vyao kuendana na uwezo wao wa kufanya kazi katika fani walizosomea na kukabiliana na changamoto kwenye maeneo ya kazi.

Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania Said Chiguma amesema Taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto ya uchache wa miundombinu kama vile kumbi za mihadhala, madarasa, maktaba na maabara za kompyuta ambavyo ni nyenzo muhimu katika utoaji wa elimu iliyo bora.

Chiguma amesema ili kupunguza changamoto hizo, Taasisi inajitahidi kutenga fedha inazozikusanya ili kukarabati na kujenga majengo mbalimbali kwa ajili ya kuboresha elimu na kuongeza uwezo wa kudahili wanafunzi wengi zaidi.

Taasisi ya Uhasibu Tanzania ni chuo cha Serikali ambacho kinatoa mafunzo katika fani za Uhasibu, Ununuzi na Ugavi, Usimamizi wa Biashara, Uongozi wa Rasilimali Watu, Masoko na Uhusiano wa Umma pamoja na Uhasibu wa Fedha za Umma kuanzia ngazi ya Astashahada (Certificate), Stashada (Diploma)  na Shahada (Degree).

ONYO KALI KWA WAUZA PEMBEJEO FEKI, HATUA KALI ZITACHUKULIWA KWA WATAKAOBAINIKA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

 
 Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Singida Beatus Chowaji akisoma bango mara baaa ya kuzindua mradi wa Faida Mali unaoshirikiana na shirika la AMDT katika kuwasaidia wakulima wa Alizeti Singida.

Mkurugenzi wa Shirika la AMDT Michael Kayombo akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa Faida Mali wenye lengo la kuwasaidia wakulima wa Alizeti Singida kulima kibiashara.
 
 Baadhi ya wadau waliohudhuruia uzinduzi wa mradi wa Faida Mali wenye lengo la kuwasaidia wakulima wa Alizeti Singida kulima kibiashara.

 
 Mkurugenzi wa mradi wa Faida Mali mkoa wa Singida Tom Silayo akisoma taarifa ya mradi huo kwa wajumbe waliohudhuria uzinduzi wa mradi utakaowasaidia wakulima kulima alizeti kibiashara.

 
 Mtendaji Mkuu wa Chama cha wasindikaji wa Mbegu za alizeti Tanzania Daud Musa Mwasantaja akiwahakikishia wakulima wa alizeti upatikanaji wa soko katika uzinduzi wa Mradi wa Faida Mali.



Wauzaji wa pembejeo ambao sio waaminifu wamepewa onyo kali na endapo atabainika yeyote anayewalaghai wakulima na kuwauzia pembejeo ambazo sio hali hatua kali dhidi yake zitachukuliwa.

Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Singida Beatus Chowaji ametoa onyo hilo wakati akizindua mradi wa Faida Mali unaoshirikiana na shirika la AMDT katika kuwasaidia wakulima wa alizeti Mkoani Singida ili kulima zao hilo kibiashara zaidi.

Chowaji amesema kumekuwepo na malalamiko kwa baadhi ya wakulima ambao hukumbana na wauzaji wa pembejeo ambao sio waaminifu na kuwalaghai kwakuwa wakulima hao hawana elimu na uelewa hasa wa viuatilifu au mbegu ambazo ni halisi.

Ameongeza kuwa mkono wa serikali ni merfu na utawabaini popote walipo hivyo waache mara moja kwani kwa kufanya hivyo wanakirudisha nyuma kilimo cha alizeti ambacho ni tegemeo kwa ajili ya uchumi wa viwanda Mkoani Singida.

“Singida tuna Viwanda vya kuamua mafuta ya alizeti vikubwa viwili, vya kati vitatu na vidogo 115 na kufanya jumla ya viwanda vya alizeti kuwa 120, vyote hivyo vinategemea alizeti ya mkulima, lakini pia mkulima anakuwa na matarajioa makubwa, hao wauzaji pembejeo wasio waaminifu hatutawavumilia, tena waache mara moja”, amesisitiza Chowaji.

Aidha amelipongeza shirika la AMDT kupitia mradi wa Faida mali kwa kuuchagua Mkoa wa Singida ili kuboresha kilimo cha alizeti hasa kwa ajili ya mkulima mdogo.

Chowaji amesema viwanda vya alizeti Mkoani Singida hufanya kazi kwa miezi minane kwa mwaka badala ya mwaka mzima kutokana na kuwa alizeti inayozalisha bado haitosheleshi viwanda hivyo kufanya kazi mwaka mzima.

Amesema matumaini makubwa ya serikali mkoani hapa ni kuwa mradi huo utasaidia kuongeza uzalishaji wa zao hilo ili kuifanya Singida ya Viwanda kuwa bora zaidi pamoja na kuliboresha zao lenyewe la alizeti kwa kutumia pembejeo za kisasa zaidi.

Chowaji amewataka wakulima wote wa alizeti kuchangamkia fursa hiyo kwa kujiunga katika vikundi ili waweze kufikiwa kwa urahisi na kunufaika, pia waache kilimo cha mazoea kwakuwa alizeti ni biashara kubwa ambayo itawakomboa kiuchumi na kukupa pato la mkoa wa Singida.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la AMDT Michael Kayombo amesema shirika hilo kupitia Mradi wa Faida mali utahakikisha unasaidia upatikanaji wa mikopo kwa wakulima wadogo wa alizeti Mkoani singida.

Kayombo ameongeza kuwa mradi utaboresha huduma za ugani kwa kutoa taarifa sahihi na mapema juu ya kilimo cha alizeti kwa wakulima na taarifa hizo zitatolewa kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno hivyo kuwafikia mapema.

Amreongeza kuwa watahakikisha wakulima wanapata soko la uhakika la zao hilo ndani na nje ya mkoa wa singida pamoja na kuhakikisha bei ya zao hilo ni yenye kumnufaisha mkulima na sio kumdidimiza zaidi.

Naye Mtendaji Mkuu wa Chama cha wasindikaji wa Mbegu za alizeti Tanzania Daud Musa Mwasantaja amesema viwanda vya alizeti bado vina uhitaji mkubwa wa alizeti kwa kuwa viwanda vyao vimekuwa vikiendeshwa chini ya malengo kutokana na mbegu hizo kuwa chache.

Mwasantaja amesema wana imani kuwa mraadi wa Faida Mali utasaidia kuongeza uzalishaji wa alizeti hivyo kuwasaidia kuongeza pia uzalishaji katika viwanda vyao.

Ameongeza kuwa watatoa ushirikiano wa kutosha na hivyo wakulima wasiwe na wasiwasi walime zao hilo kwa wingi watapata wateja na kwa bei ambayo ni nzuri.

Nao wakulima walioshiriki uzinduzi wa maradi huo wamesema mradi huo umekuja muda muafaka kwakuwa na wao wanatamani kupata faida kutokana na kilimo hicho kwakuwa baadhi bado wanalima kwa mazoea na kwa kutumia mbegu ambazo hazizalishi kwa wingi.

SITAVUMILIA HATI CHAFU KATIKA HALMASHAURI YOYOTE MKOANI KWANGU-DKT NCHIMBI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

 Mkuu wa Mkoa wa Singia Dkt Rehema Nchimbi akizungumza na Meya wa Manispaa ya Singida Gwae Chima Mbua kabla ya kuanza kwa baraza Maalumu la madiwani wa Manispaa ya Singida kujadili hoja za Mkaguzi wa Fedha za Serikali.
 Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida Bravo Kizito Lyampembile akifungua baraza Maalumu la madiwani wa Manispaa ya Singida kujadili hoja za Mkaguzi wa Fedha za Serikali.
 Baadhi ya Viongozi wa Manispaa ya Singida wakifuatilia baraza Maalumu la madiwani wa Manispaa ya Singida kujadili hoja za Mkaguzi wa Fedha za Serikali.
  Madiwani wa manispaa ya Singida wakifuatilia baraza Maalumu la madiwani wa Manispaa ya Singida kujadili hoja za Mkaguzi wa Fedha za Serikali.
Madiwani wa manispaa ya Singida wakiwa wamesimama kuridhia hoja katika baraza Maalumu la madiwani wa Manispaa ya Singida kujadili hoja za Mkaguzi wa Fedha za Serikali.
 
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amesema hatavumilia kuona halmashauri inafanya uzembe na kupata hati chafu ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Fedha za Serikali kwakuwa itamchafua yeye na taswira ya uongozi wote wa Mkoa wa Singida.

Dkt Nchimbi ametoa kauli hiyo mapema jana wakati wa baraza maalumu la madiwani wa Manispaa ya Singida la kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za serikali ambazo amesema hoja nyingi zimetokana na uzembe.

Amesema licha ya kuipongeza Manispaa ya Singida kwa kupata hati safi, uwepo wa hoja umedhihirisha kuwa kuna baadhi ya watendaji wanafanya kazi kwa uzembe na kutofuata taratibu na sheria hivyo wajirekebishe haraka.

Dkt Nchimbi ameongeza kuwa hoja nyingi zinajitokeza kwa kukosa umakini na watendaji kufanya kazi kwa mazoea hali ambayo ikiendelea inaweza kuipelekea manispaa kupata hati isiyoridhisha hivyo kupata hati safi kuwaongezee nguzu ya kuboresha utendaji kazi wao.

Aidha amewashauri wakuu wa idara na watumishi wengine kuitendea haki manispaa yao kwa kuchapa kazi kuwa wadilifu na kufuata sheria kwani wakifanya hivyo wataepuka hoja zisizo za lazima na kuharakisha maendeleo.

Dkt Nchimbi amewasisitizia matumizi ya muda kuwa yenye tija ambapo amelaani kitendo cha kutumia muda mwingi kwenye vikao ambavyo havina tija bali watumie muda kidogo kwenye vikao na muda mwingi kutatua kero za wananchi, huku akiahidi kufuatilia matumizi ya muda unaotumika kwenye vikao.

Ameongeza kuwa watendaji wote wanapaswa kubadilika na kuendana na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Hapa kazi tu ili waweze kupunguza hoja na kufuta zile zisizo za lazima.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt Angelina Lutambi amewaasa watendaji kuitumia vema dhamana ya utumishi wa umma kwa kuhakikisha wanaleta mabadiliko ya kimaendeleo.

Dkt Lutambi ameongeza kuwa watumishi wa umma wanapaswa kufahamu kuwa jutendaji wao ukilega lega athari yake inamkumba mwananchi kwakuwa atachelewa kupata maendeleo, hivyo bidii katika utumishi umma ni muhimu.

Amewasisitizia kuwa mikakati na malengo ya maendeleo ya kimkoa na kitaifa haitaweza kufikia endapo watendaji hawatakuwa waadilifu na wakiendekeza uzembe hivyo wajitume kwa bidii kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.

Naye Diwani Viti maalumu Magreth Malecela amemshukuru Mkuu wa Mkoa Dkt Nchimbi kwa kuwapa vyeti ambavyo vilitolewa kwa madiwani wote waliopata mafunzo ya usimamizi wa ruzuku na miradi ya serikali.

Malecela ameongeza kuwa ushirikiano na ushauri wanoaupata kutoka kwa Dkt Nchimbi utaisaidia manispaa kuwa na maendeleo huku akiahidi kwa niaba ya madiwani wenzake kuwa watafuata maelekezo na ushauri kwa manufaa ya manispaa ya Singida.
 

ELIMU SAHIHI ITUMIKE KWANZA KABLA YA MATUMIZI YA SHERIA KWA WAKEKETAJI - WOWAP

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

 Mzee maarufu na mwenyeji wa Msange Bi Greta Musa Nyonyi akichangia hoja katika semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.
 Mratibu wa Mradi wa Kupinga Ukeketaji (WOWAP) Nasra Suleiman akizungumza na washiriki wa semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.
 Afisa Maendeleo ya Jamii kata ya Msange Magni Oisso akichangia hoja katika semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.
 Washiriki wa semina ya kupinga ukeketaji iliyoandaliwa na Mradi wa WOWAP wakifuatilia kwa umakini filamu fupi ya Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.

Mzee wa Kimila Hosea Mnyambi akichangia hoja katika semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.
 
Elimu sahihi juu ya madhara ya ukeketaji ya muda mfupi na mrefu inatakiwa itolewe kwa jamii kabla ya kuwachukulia hatua baadhi yao wanaoendelea kufanya vitendo vya ukeketaji licha ya uwepo wa sheria kali.

Rai hiyo imetolewa mapema leo na Mratibu wa Mradi wa Kupinga Ukeketaji (WOWAP) Nasra Suleiman katika semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida, kwa ushirikiano wa Ofisi ya Ustawi wa Jamii Mkoa wa Singida na mradi huo kwa ufadhili wa shirika la WAAF-Japan.

Mratibu huyo amesema nguvu ya sheria itasaidia kuondoa ukeketaji endapo wananchi wengi watakuwa na uelewa wa kutosha juu ya madhara ya ukeketaji na kuamua kwa hiyari kuachana na mila hiyo.

“Sheria isiwe nguvu pekee ya kupambana na ukeketaji, tukifanya hivyo itafikia kipindi tutakwama kwa kiasi kikubwa kwa kuwa watu wataendelea kukeketa kwa kificho ili wasikamatwe, lakini kila mwana jamii akiwa na elimu ya kutosha ya madhara hayo, nguvu ya sheria itatumika tu kwa wachache watao kaidi”, amesisitiza Nasra.

Ameongeza kuwa Watendaji wa kata na vijiji wana uwezo mkubwa wa kubadilisha mtazamo na mila ya ukeketaji kwa kuelimisha wananchi wao hasa baada ya semina zinazoandaliwa na miradi au mashirika Fulani kwakuwa zinawajengea uwezo ili waweze kutoa elimu sahihi na mbinu za kuelimisha.

Nasra amesisitiza kuwa jukumu la elimu lisiachwe kwa sekta binafsi kama mradi wake wa WOWAP pekee bali liwe jukumu la jamii nzima huku akifafanua kuwa elimu inayotakiwa kutolewa ni ile inayoelezea madhara ya ukeketaji na sio kuwakataza kwa kigezo cha kutii sheria pekee.

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii kata ya Msange Magni Oisso amesema katika kata hiyo ukeketaji umekufanyika kwa siri sana kwa kuogopa mkono wa sheria huku wahanga wakiwa watoto wachanga na wale waliomaliza kliniki.

Oisso amesema kumekuwa na usiri mkubwa huku wakeketaji wakibadili mbinu namna za kujificha wasigundulike kwa jamii ambayo elimu imeanza kuwafikia baadhi yao.

Aidha amependekeza kuwa ili kukomesha ukeketaji moja ya njia ni kutoa elimu katika vituo vya kutolea huduma za uzazi na mtoto ili mtoto aweze kunusurika pia elimu itolewe shuleni kwa ngazi zote kuanzia darasa la awali hadi la saba.

Akichangia mada katika semina hiyo mzee maarufu na mwenyeji wa Msange Bi Greta Musa Nyonyi amesema elimu ni bora zaidi kuliko kuwaogopesha wanajamii kwa kutumia sheria kwakuwa watatafuta namna ya kutekeleza azma yao kwa usiri ili kukwepa mkono wa sheria na sio kuacha.

Greta ameongeza kuwa kwa sasa kutokana na kuwa wakeketaji wamebainika kuwa wanakeketa watoto wachanga na hugundulika wakienda kliniki baadhi yao wanabadili mbinu na kusubiri mtoto amalize kliniki ndipo anakeketwa.

Naye Mzee wa Kimila Hosea Mnyambi amesema yeye amekulia katika familia ya wakeketaji na wamekuwa wakirithishwa mbinu za ukeketaji kizazi hadi kizazi ila kutokana na kuwepo kwa sheria, dini kuhubiri madhara ya ukeketaji, mila hiyo wameiacha.

Amesema wachache wanaoendelea kufanya vitendo hivy o ha wanawake wamekuwa wakifanya kwa usiri mkubwa huku akina baba wakiwa hawana taarifa ya kinachoendelea na endapo mtoto anafariki hudanganywa ugonjwa uliopelekea kifo cha mtoto.

Mzee Mnyambi amesema elimu iendelee kutolewa hasa kwa kutumia vyombo vinavyoaminika mfano vyama vya siasa, dini na vikundi vya kuweka na kukopa pamoja na kuiweka agenda ya ukeketaji kwa vikao vya Kata na vijiji.

Semina ya kupinga ukeketaji Kata ya Msange imefanywa na mradi wa WOWAP kwa ushirikiano wa maafisa ustawi wa jamii mkoa wa Singia kwa watendaji wa kata na vijiji, watoa huduma za afya, polisi, waalimu, wawakilishi wa viongozi wa dini, maafisa ustawi wa jamii na maendeleo ya jamii, wazee maarufu na wa kimila ili wawe mabalozi wa kusambaza elimu hiyo kwa jamii inayo wazunguka.

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa