Serikali
imedhamiria kuwaunganisha wakulima wakubwa wa mazao ya chakula wa kata
tano za Wilaya ya Iramba kwa kujenga daraja na makaravati manne katika
barabara yenye urefu wa kilomita 38.6 yatakayo gharimu shilingi bilioni
4.1.
Akiweka
jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Mto Mtoa na makaravati katika
barabara ya shelui-Mtoa-Urughu Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Amour
Hamad Amour amesema serikali imedhamiria kuwaunganisha wananchi ili
wazalishe mazao, waanzishe viwanda kisha kusafirisha bidhaa.
Amour amesema kwakuwa barabara hiyo inahudumia wananchi wa kata
za Shelui, Mtoa, Mtekente, Urughu na Ndago wananchi wa maeneo hayo
watumie fursa ya kuwa na barabara nzuri kwa kutengeneza viwanda vidogo,
vya kati na vikubwa na kisha kusafirisha bidhaa na sio mazao kama mali
ghafi.
Amesema
kwa kufanya hivyo wakulima wa mazao wataweza kujiongeza kipato chao kwa
kuwa hawatapunjwa kwa kuuzwa mali ghafi ambayo hupelekwa kwenye viwanda
vya nchi nyingine hivyo barabara hiyo iwe hamasa kwao kuzalisha kwa
wingi pamoja na kuanzisha viwanda kwa wingi.
Mradi
huo wa barabara na makaravati unatekelezwa kupitia mpango wa kuondoa
vikwazo kwenye barabara za vijijini, mpango unaofadhiliwa na serikali ya
Tanzania kwa kushirkiana na serikali za Uingereza na Ireland Kaskazini.
Kukamilika
kwa ujenzi wa daraja na makaravati hayo kutawezesha barabara hiyo
kupitika kwa kipindi cha mwaka mzima na hivyo kuwanufaisha wakazi elfu
79 wa kata hizo pamoja na kuwezesha utoaji wa huduma za kijamii katika
eneo hilo lenye shule za msingi 29, shule za sekondari 6, zahanati 7 na
kituo cha afya kimoja.
Wakati
huo huo Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru Amour Hamad Amour amezindua
mradi wa ghala la kuhifadhia chakula katika kijiji cha Nselembwe ambalo
litakuwa likihudumia jamii ya kata za Ulemo,Mgongo, Ntwike, Shelui na
Mtoa.
Akifungua
ghala hilo Amour amesema kauli mbiu ya mwenge wa uhuru mwaka huu ni
shiriki kukuza uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya taifa hivyo ujenzi wa
ghala ili kuhifadhi mazao unasaidia wananchi kutoyauza ovyo mazao na
kuyahifadhi mahali salama kabla ya kuyachakata kuwa bidhaa.
Amesema
mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 350 utaweza kuwasaidia
wananchi kuhifadhi mazao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani na kuwa na
kauli moja juu ya bei ya mazao pia watakua na uhakika wa mazao.
Amour
amewasisitiza wananchi wa kata hizo kuzalisha kwa wingi kwa kuwa sasa
wana uhakika wa sehemu salama ya kutunzia mazao yao ili wasishawishike
kuyauza kwa bei ndogo.
Mwenge
wa Uhuru ukiwa Wilayani Iramba umetembelea miradi yenye thamani ya
shilingi bilioni 4.8 huku ukipitia miradi 6 na kuona shughuli 5 katika
vijiji 10 na tarafa 4 katika umbali wa km 119.1.
0 comments:
Post a Comment