Mfanyabiashara ajiua kwa risasi, mwingine achinjwa

Watu wawili wamefariki dunia katika matukio mawili tofauti yaliyotokea mkoani Singida mwishoni mwa wiki likiwemo la mfanyabiashara kujipiga risasi kichwani na mwingine huchinjwa shingo, kutolewa koromeo na ulimi.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Geofrey Kamwela alisema katika tukio la kwanza, mfanyabiashara Mashaka Omari (30) alikutwa chumbani kwake Mtaa wa Ipembe akiwa amekufa baada ya kujipiga risasi kichwani.
Alisema mfanyabiashara huyo alijiua kwa kutumia bastola yake yenye namba TZ CA 895101 ambapo polisi walikuta ganda moja la risasi iliyotumika lakini magazini ilikuwa na risasi 11," alisema Kamanda Kamwela.
Uchunguzi wa awali unaonesha marehemu alikuwa na mgogoro kati yake na mtu mwingine ambaye hakutajwa kwa ajili ya masuala ya kiusalama hivyo kusababisha ajiue.
"Marehemu aliacha ujumbe huo wa maandishi kwenye gari lake namba T664 EES aina ya Toyota RAV 4 ambalo alikuwa ameliegesha nje ya ofisi yake," alisema na kuongeza kuwa, uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea.
Katika tukio lingine, mkazi wa Kijiji cha Sambaru, Wilaya ya Ikungi, Tatu Selemani (42), alichinjwa shingo na kitu chenye ncha kali na watu wasiofahamika saa 1:30 asubuhi.
Kamanda Kamwela alieleza licha ya kuchinjwa shingo pia marehemu alitolewa koromeo, ulimi, kuchunwa ngozi usoni na kutolewa sikio la kushoto ambapo mwili wake ulikutwa umbali wa mita 80 kutoka nyumbani kwake.
Alisema katika tukio hilo, mtu mmoja Amosi Shenan maarufu kwa jina la 'Babu', mkazi wa kijiji hicho ambaye ni mume wa marehemu, amekamatwa kwa mahojiano zaidi na uchunguzi bado unaendelea

Chanzo;Majira

Padri anayedaiwa kutelekeza mtoto kuburuzwa kortini tena leo

Mahakama ya Mwanzo Utemini iliyopi mjini hapa Mkoa wa Singida, leo inatarajia kuendelea kusikiliza kesi inayomkabili Padri  wa Kanisa Katoliki mjini hapa,  Deogratius Makuri ya kumtelekeza bila  kumhudumia mtoto wake wa kike aliyedaiwa kuzaa na muumini wake.
 Kesi hiyo ilisikilizwa wiki iliyopita na kuahirishwa baada ya kudaiwa mahakamani hapo kuwa padri huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi wa muda mrefu na Maria Boniphance (26) aliyekuwa mhudumu wa kanisa hilo Parokia ya Singida mjini.

 Ilidaiwa mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Ferdnand Njau kuwa wakati wote huo wa mahusiano ya kimapenzi, ndipo mshitakiwa alimpa ujauzito na kuzaa naye mtoto wa kike.

Mlalamikaji (Maria) alidai mahakamani hapo kuwa   baada ya ujauzito huo, aliamua kulifikisha suala hilo kwa wazazi wake ambao walimwendea padri huyo na kukubali kuhusika na mimba hiyo.

Alidai kuwa padri huyo aliahidi kwa maandishi kuwa atamtunza mtoto wake (jina tunalo) hadi hapo atakapokuwa na uwezo wa kujitegemea, kinyume chake ahadi hiyo alitekeleza kwa miezi michache na akasitisha matunzo.

"Pamoja na kuchukua hatua mbalimbali ikiwamo kufikisha suala hilo ofisi ya ustawi wa jamii... aliahidi kupitia hati ya mkataba kuwa atakuwa anatoa kila mwezi Sh. 80,000 na akishindwa afikishwe mahakamani, ndiyo mimi nimeamua kumshitaki, ”alidai mlalamikaji huyo.

Ilidaiwa kuwa pamoja na ahadi hiyo padri Makuri alianza kutoa madai mbalimbali kwamba mtoto huyo siyo wake wa kuzaa, na hapo ndipo aliamua kusitisha matunzo kama alivyoahidi.  .
 
CHANZO: NIPASHE

Ikungi kutumia bil. 25/-

HALMASHAURI ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, inatarajia kutumia shilingi bilioni 25.696 katika mwaka wa fedha 2014/2015 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shughuli za maendeleo.
Akisoma taarifa ya bajeti kwenye kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo jana, Makamu Mwenyekiti Ally Nkangaa, alisema katika kipindi hicho kiasi cha sh bilioni 15.426 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wake.
Hata hivyo alisema katika bajeti iliyopita halmashauri iliomba kuidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 16.953 ambapo hadi kufikia mwezi Desemba mwaka huu, jumla ya shilingi milioni 512.322 zilikuwa zimetumika kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Nkhangaa alisema katika utekelezaji wa bajeti, zipo changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na baadhi ya vijiji na kata kutochangia nguvu kazi na fedha.
Chanzo;Tanzania Dama

Mvua kubwa zaleta madhara Singida, watu watano wahofiwa kufa maji


DSC049001
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida, SACP Geofrey Kamwela, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na tukio la maafa ya mvua kubwa iliyosababisha vifo.
Na Nathaniel Limu, Singida
MVUA kubwa zilizoanza kunyesha mkoani Singida zimeanza kuleta maafa baada ya watu watano kuhofiwa kufa maji kutokana na gari waliolokuwa wakisafiria kusombwa na maji ya mto.
 Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Singida, SACP Geofrey Kamwela amesema tukio hilo limetokea Desemba saba mwaka huu saa 3:30 asubuhi huko katika mto wa Nzalala kijiji cha Kisimba tarafa ya Kisiriri wilayani Iramba.
Amesema siku ya tukio, abiria 16 waliokuwa wakitoka kijiji cha Doromoni kwa kutumia Landrover 110 TDI lenye namba za usajili T.499 ATR, lilisombwa na maji ya mto wakati dereva wake akijaribu kuvuka mto Nzalala.
 Akifafanua, amesema walimpofika kwenye mto huo abiria hao walimwomba dereva huyo asubiri maji ya mto yapungue ili waweze kuvuka lakini dereva huyo alikataa kwa madai maji ni machache.
 “Wakati gari hilo lilipofika katikati ya mto, lilizimika ghafla na wakati huo huo maji ya mto yaliongezeka na kulifunika gari.  Dereva na kondakta waliweza kufanikiwa kutoka na kukimbilia kusikojulikana”
 Aidha, amesema abiria 11 waliweza kuokolewa na wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Iramba na watano hadi sasa haijulikani iwapo wamekufa ndani ya landrover au wamesomba na maji na kupelekwa kusikojulikana.
 Katika hatua nyingine, Kamanda Kamwela, ametoa wito kwa madereva wa vyomba vya moto, baiskeli na watembea kwa miguu kuchukua tahadhari wakati wa kuvuka mito au mabonde kipindi hiki cha mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
 Alitumia fursa hiyo kushauri mamlaka zinazohusika kutengeneza madaraja kwenye mito au mabonde badala ya kuweka zege ambalo husaidia tu katika kipindi cha kiangazi.
 “Aidha nashauri abiria nao wasikubali kujazwa kwenye vyombo vya usafiri tofauti na uwezo hali wa gari” amesema.
Na Mo Blog

MAJAMBAZI WAWILI WAUAWA MKOANI SINGIDA.

TUNAOMBA RADHI KWA HII PICHA


Kamanda wa polisi mkoa wa Singida,SACP Geofrey Kamwela,akionyesha bunduki ya kijeshi aina ya SMG no.34555  iliyokuwa ikitumiwa na watu wawili wanaodhaniwa kuwa majamabazi katika kijiji cha Manga manispaa ya Singida.

WATU wawili wakazi wa manispaa ya Singida ambao majina yao bado hayajajulikana,wakiwa kwenye Jokofu la kuhifadhia maiti baada ya kuuawa wakati wa majibishano ya risasi na polisi.


JESHI  la Polisi mkoani Singida limewauwa watu wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakati wa kurushiana rasasi.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Singida, SACP, Geofrey Kamwela amesema tukio hilo limetokea desemba tisa mwaka huu saa 12:00 jioni, huko katika kijiji cha Manga nje kidogo ya mji wa Singida.
Amesema watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wakiwa na bunduki moja ya kijeshi aina ya SMG, walifika kijijini hapo kwa lengo la kufanya uhalifu.
Kamanda Kamwela, amesema watu hao ambao miili yao imehifadhi kwenye chumba cha mochwari katika hospitali ya mkoa, majina na makazi yao bado hayajajulikana.
Akifafanua, amesema taarifa za siri kutoka kwa raia wema zilifikia jeshi la polisi na ndipo askari polisi walipofika kwenye eneo la tukio.
“Baada ya polisi kufika kijijini hapo watu hao walistuka kuwa wanafuatilwa na askari polisi na hivyo kuanza kukimbia kuelekea kijiji cha Uhamaka kwa kutumia pikipiki yenye namba za usajili T. 634 BTW aina ya Sanlag yenye rangi nyeusi”,amesema Kamwela.
Amesema walipoona Polisi wanawakaribia waliamua kutelekeza pikipiki yao hiyo na kuanza kukimbilia porini kwa miguu.
“Hali ilipokuwa ngumu zaidi, walianza kuwarushia polisi risasi, hivyo polisi nao ikwabidi kujibu mapigo.  Katika majibizao hayo ya risasi, majambazi mawili yaliweza kujeruhiwa huku mmoja akifanikiwa kutoroka”
Amesema majambazi hayo yaliyojeruhiwa yalifariki dunia wakati yanakimbizwa katika hospitali ya mkoa kwa matibabu,lakini yakafia njiani.
Amesema katika eneo la tukio, ilipatikana
bunduki moja aina ya SMG yenye namba 34555 ikiwa na risasi saba kwenye magazine.  Pia pikipiki iliyokuwa iantumiwa na majambazi hayo, iliwezea kupatikana.
Kamwela alitoa wito kwamba wananchi waendelee na moyo huo huo wa kuwafichua watu wanaowatilia shaka ili waweze kudhibitiwa mapema kabla ya kufanya uhalifu.
Kwa hisani ya Mtandao wa Singida Yetu

WATANO WAFA MAJI NA WENGINE 11 WANUSURIKA

WATU watano wanahofiwa kufa maji na wengine 11 wamenusurika, baada ya gari waliyokuwa wakisafiria kusombwa na maji ya mto kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani mkoani Singida.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida Kamishina msaidizi mwandamizi Geofrey Kamwela, tukio hilo limetokea jana majira ya saa 3: 30 asubuhi katika Kijiji cha Kisimba Wilayani Iramba.
Amesema watu hao waliokuwa wakisafiri kwa gari yenye namba za usajili T.499 ATR aina ya Land rover 110 TDI, walikuwa wakijaribu kuvuka mto Nzalala kutoka eneo Doromoni kwenda Kiomboi Mjini.
Kamanda Kamwela amesema wakati dereva ambaye hajatambuliwa jina wala makazi akijaribu kuvusha, gari hiyo ilizimika katikati ya mto kabla ya kosombwa na maji ikiwa na abiria 16 ndani.
Amesema abiria 11 kati yao wameokolewa na kupelekwa hospitali ya Wilaya ya Iramba kwa matibabu, wakati juhudi za kufukua gari hiyo iliyofukiwa kwa mchanga mita chache kutoka eneo la tukio na kutafuta watu wengine watano ambao hawajulikani walipo zinaendelea kufanywa.
Dereva wa gari hiyo na kondakta wake wanasadikiwa kutoweka baada ya tukio hilo na polisi wanaendelea kuwasaka.

Ajali yaua watano

Singida.Abiria watano wamekufa baada ya gari aina ya Landrover 110 waliyokuwa wanasafiria kusombwa na maji katika Kijiji cha Doromoni Wilaya ya Iramba.
Katika ajali hiyo iliyotolea jana, watu wengine 11 walinusurika baada ya kuruka na kuogelea mara baada ya gari hiyo kupinduka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
Kamwela alisema ajali hiyo ilitokea majira ya asubuhi wakati gari hilo likiwa linabeba abiria 16 kutoka Kijiji cha Doromoni wilayani Iramba kuelekea Kiomboi mjini.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni kujaa kwa maji katika Mto Nzalala kiasi cha kulifunika daraja.
Kamwela alisema wakati dereva alipojaribu kuvuka, gari hiyo ilizidiwa nguvu na maji, hivyo kuisomba.
Baadhi ya abiria walionusurika kwenye ajali hiyo walisema kwamba walipofika kwenye daraja hilo walimwambia dereva asivuke, bali asubiri maji yapungue.
Walidai dereva alikaidi agizo hilo na kuamua kuvuka na alipofika katikati alionekana kubabaika na maji kabla ya maji kuizidi nguvu gari.
Habari ambazo pia hazijathibitishwa zilidai kuwa dereva na kondakta wa gari hilo waliruka na kukimbia eneo la ajali.
Chanzo;Mwananchi

Polisi yaua majambazi wawili

JESHI la Polisi mkoani Singida limewaua kwa kuwapiga risasi majambazi wawili waliokuwa wakijiandaa kufanya uhalifu katika Kijiji cha Manga nje kidogo ya mji wa Singida.
Kamanda wa Polisi mkoani Singida, Godfrey Kamwela alisema tukio hilo limetokea juzi, saa 12:00 jioni baada ya polisi kupata taarifa za siri kutoka kwa raia wema.
Kamwela alisema majambazi hayo yalikuwa na bunduki moja aina ya SMG yenye namba 34555 ikiwa na risasi saba kwenye magazine, huku wakitumia pikipiki T 634 BTW Sanlg.
Aidha, Kamanda Kamwela alisema askari polisi walifika katika eneo hilo, na watu hao walistuka kwa kuwa wanafuatiliwa na askari na hivyo kuanza kukimbia kuelekea Kijiji cha Uhamaka kwa kutumia pikipiki hiyo.
Hata hivyo, alisema walipoona polisi wanawakaribia waliitelekeza pikipiki hiyo na kuanza kukimbia porini kwa miguu, lakini hali ilipokuwa ngumu zaidi walianza kuwarushia polisi risasi, hivyo polisi nao walilazimika kujibu.
“Majibizano hayo ya risasi yalipelekea majambazi wawili kujeruhiwa huku mmoja akifanikiwa kukimbia. Majeruhi hao walifariki dunia wakati wakikimbizwa hospitali ya mkoa kwa matibabu. Maiti zimehifadhiwa hospitalini hapo kwa ajili ya kutambuliwa na ndugu zao,” alisema Kamwela.
Alisema kwenye eneo la tukio ilipatikana bunduki moja aina ya SMG ikiwa na risasi saba na pikipiki iliyokuwa wakiitumia kukimbia. Polisi wanaendelea na uchunguzi   ili kubaini kama kuna mtandao wa majambazi pamoja na kumsaka mtuhumiwa aliyekimbia.
Wakati huohuo, polisi mkoani hapa inawashikilia watu wanne akiwemo mhudumu wa nyumba ya kulala wageni ya Lake Hill Singida Motel kuhusiana na tukio la ujambazi lililotokea kwenye hoteli hiyo.
Kamanda Kamwela alisema wizi huo ulitokea juzi, saa 9:30 usiku, ambapo watu ambao idadi bado haijajulikana wakiwa na bunduki walivamia hoteli hiyo na kuwapora wapangaji vitu mbalimbali.
Alisema watu hao walipofika katika hoteli hiyo walifyatua risasi hewani kwa lengo la kuwatisha wapangaji na walinzi na kufanikiwa kuwafunga kamba walinzi wote watatu na kuingia katika vyumba viwili na kuwanyang’anya wapangaji mali pamoja na fedha.
Aliwataja wanaoshikiliwa kwa tuhuma hizo ni walinzi hao wa kampuni binafsi ya ulinzi ya Mass Security ya mjini Singida ambao ni Juma Mwangwi (35), Zakaria Pastory (23) na Donald Samson (19) na Mhudumu wa hoteli hiyo, Alistides Salvatory  (24).
Kamanda Kamwela alitaja vitu vilivyoporwa kuwa ni kompyuta mpakato moja, simu tatu za mkononi zenye thamani ya sh milioni moja, saa mbili za mkononi moja yenye thamani ya dola 500 za Marekani  pamoja na fedha taslimu sh 800,000 na dola 500
Chanzo;Tanzania Daima

Ofisi ya mtendaji Kondoa yafungwa

OFISI ya mtendaji wa kijiji cha Salanka, kata ya Salanka, wilayani Kondoa, imefungwa kwa kukosa mtendaji wa kijiji kwa muda wa mwaka moja sasa.
Hali hiyo imeelezwa kuchangia wananchi kukosa huduma hivyo na kulazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo kwenye ofisi ya kata.
Mtendaji wa kijiji hicho alisimamishwa na mkutano wa kijiji kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za kijiji.
Akizungumza kwenye mkutano wa kijiji, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Khamis Majaliwa, alisema wamekuwa wakifuatilia suala hilo kwa muda sasa huku Ofisi ya Mkaguzi wa Hesabu za Ndani wa halmashauri hiyo akifika mara moja na hadi sasa hajafika kijijini hapo kwa madai ya kukosa usafiri.
Katika mkutano huo, wanakijiji hao waliazimia kwenda kuonana na Waziri Mkuu kutatua tatizo hilo lililodumu kwa muda wa mwaka sasa licha ya viongozi mbalimbali kuulizwa na kukosa majibu.
Alipoulizwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Omar Kwang’, alisema kwa wakati huo alikuwa yuko nje ya ofisi akiwa likizo na kumtaka mwandishi kusuburi hadi atakaporudi ofisini ndipo atatoa majibu.
Chanzo;Tanzania Daima

MSIMAMO WA CHADEMA MKOA WA SINGIDA DHIDI YA MAAMUZI YA KAMATI KUU - TAARIFA KWA UMMA



                     
WILFRED NOEL KITUNDU
MWENYEKITI CHADEMA MKOA SINGIDA
S.L.P 260
3.12.2013
KATIBU WA CHADEMA MKOA
S.L.P 260
SINGIDA
YAH: - KUJIUZURU UENYEKITI MKOA SINGIDA
Somo hapo lahusika,
Ninapenda kukuarifu kuwa nimeamua kujiuuzuru nafasi yangu ya uenyekiti wa mkoa ambayo nimekuwa nikiitumikia kwa kipindi kirefu sasa kama kielelezo cha kuamini na kudai demokrasia ya kweli ndani ya chama.

Ikumbukwe kwamba mimi ndio mwanachama wa kwanza kujiunga na CHADEMA mkoa wa SINGIDA na ni mwanachama wa 300 kitaifa, hiyo ni heshima kubwa sana kwangu na sipo tayari kuipoteza kwa kukubali kuwa sehemu ya udharirishaji huu wa demokrasia uliopitiliza

Maamuzi na vitendo vinavyoendelea ndani ya chama chetu kwa sasa ni ubakaji na udharirishaji wa demokrasia ya kweli tunayoihubiri mbele ya umma.

Kwa barua hii basi, nimeonelea bora upate ufahamu huo kuwa si vema mimi kuendelea kupingana na dhamira yangu inayonituma kuwa mwanademokrasia wa kweli.

Kwa kipindi hiki kifupi mnaweza mkaendelea kuitumia anuani yangu ya posta mpaka hapo mtakapopata anuani yenu tayari.

Ninatanguliza shukrani zangu za dhati kwa wanachadema wote wanaopinga upuuzi huu uliofanywa na kamati kuu ya chama.

Kusimamia haki, katiba na misingi ya chama ni wajibu wangu, hivyo kwa namna yoyote ile sitaweza kuwa tayari kufumba macho pindi ujinga wa namna hii unapoendelea kutekelezwa kwa uwoga wa uchaguzi.


Nakutakia kila la heri kwenye majukumu yako.

………………………………………………….
Wilfred N. Kitundu

MWENYEKITI CHADEMA
MKOA SINGIDA
S.L.P 260
3.12.2013




Wajasiriamali waelezwa umuhimu wa soko la hisa

MKUU wa Mkoa wa Singida, Dk. Parseko KoneMKUU wa Mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone, ameelezea umuhimu wa soko la hisa katika upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu na uwekezaji kuwa haviwezi kuletwa na masoko ya mitaji pekee.
Kwa mujibu wa mkuu huyo, dhima ya kupata rasilimali na kuzitumia kikamilifu kwenye miradi yenye tija, husababisha ukuaji wa uchumi na kuongeza utajiri.
Dk. Kone amebainisha hayo juzi mjini Singida wakati akifungua semina ya siku mbili kwa wafanyabiashara na wajasiriamali juu ya soko la kukuza ujasiriamali (EGM) iliyofanyika kwenye ukumbi wa Aque Vitae.
Alisema ni muhimu ieleweke wazi kwamba kuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya mafanikio ya masoko ya mitaji na uchumi wa nchi na kusisitiza kwamba moja ya sababu ni serikali kuanzisha na kusaidia maendeleo ya Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Aidha, alibanisha kwamba kampeni hiyo imekuja wakati muafaka ambao serikali imepania kujenga sekta binafsi imara itakayokuwa injini ya uchumi wa taifa.
“Napenda kuchukua fursa hii kuwahakikishia kwamba serikali inatambua mchango wa wadau mbalimbali katika maendeleo ya masoko ya hisa hapa nchini, mwamko kama huu unalenga kujenga uelewa kwa sekta binafsi na umma juu ya fursa zipatikanazo na soko la hisa zinaungwa mkono na serikali.
“Pia nitumie fursa hii kuwataka wadau na wahusika wote kwa ukamilifu wenu kutumia tukio hili ili kutumia fursa zipatikanazo kwenye soko la hisa,” alisema Dk. Kone.
Hata hivyo Dk. Kone alisema tafiti nyingi zimeonyesha kwamba upatikanaji wa mitaji ya wajasiriamali wadogo na wa kati ni changamoto kwa maendeleo ya kukua kwa shughuli za ujasiriamali na sekta hiyo kwa ujumla.
Awali Meneja Uhusiano wa kitaasisi kutoka DSE, Mary Mniwasa, alimweleza mkuu wa mkoa kuwa lengo la semina hiyo ni kampeni ya umma ya kupunguza umaskini hapa nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Singida, Francis Mashuda, alisema wafanyabiashara wanakumbana na changamoto kubwa ya ukosefu wa mitaji.
Semina hiyo ilitarajiwa kuhudhuriwa na wafanyabiashara wa kada mbalimbali na wajasiriamali wasiopungua 65, imefadhiliwa na DSE chini ya uratibu wa TCCIA Mkoa wa Singida.
Chanzo;Tanzania Daimma

Singida watakiwa kuchangamkia Soko la Hisa

 WAJASIRIAMALI na wafanyabiashara mkoani Singida wametakiwa kuchangamkia fursa zilizopo Soko la Hisa la Dar es Salaam ili kuboresha na kuendeleza biashara zao.
Mwito huo ulitolewa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone wakati akifungua semina ya siku mbili juu ya Soko la kukuza ujasiriamali iliyofanyika ukumbi wa Aqua Vitae mjini hapa.
Dk Kone alisema kuwa Soko la Hisa la Dar es Salaam kupitia kitengo chake kipya kijulikanacho kama “Soko la Kukuza Ujasiriamali”, ni suluhisho la upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali kote nchini.
Alisema kuwa soko hilo litatoa suluhisho kwa changamoto zinazowakabili wajasiriamali katika upatikanaji wa uhakika wa mitaji ya muda mrefu kwa ajili ya kuendeleza biashara zao, jambo ambalo limekuwa likiwasumbua wajasiriamali na wafanyabiashara.
“Kwa hiyo basi, soko la kukuza ujasiriamali litasaidia kuleta msukumo wa utekelezaji sera mbalimbali za serikali zinazolenga kuondoa changamoto hizo na kuleta urahisi wa upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya kukuza biashara zao,” Dk Kone alisema.
Aidha, alieleza kuwa soko hilo linatarajiwa kulichangamsha soko kwa ujumla kupitia ongezeko la utoaji na uorodheshaji wa hisa, kupanua wigo na fursa za kuwekeza mitaji na kuongeza ari ya wananchi kujiwekea akiba.
Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa huo, baadhi ya faida ziletwazo na soko hilo ni kupunguziwa kodi katika gawio, kusamehewa kodi kwenye ongezeko la thamani ya mtaji na ushuru wa stempu na punguzo kodi ya makampuni.
Chanzo;Habari Leo

Wavamia nyumba, wazichoma moto

MWENYEKITI wa Kijiji cha Makunda, Kata ya Kyengege, wilayani Iramba kwa kushirikiana na watu wengine zaidi ya 50 wamevamia na kuchoma moto nyumba mbili za wakulima wakipinga kuwa si wazaliwa wa eneo hilo na kujipatia ardhi zaidi ya ekari 285.
Habari za uhakika kutoka katika eneo la tukio hilo zinaeleza tukio hilo limetokea juzi, saa 8:00 mchana katika mashamba ya kilimo Kijiji cha Makunda.
Kwa mujibu wa habari hizo, siku ya tukio watuhumiwa wakiwa na silaha za jadi walivamia makazi ya mkulima mwezao, Esau Talanzia (47) na kuchoma moto nyumba yake.
Pia walichoma magunia sita ya mahindi, magunia mawili ya alizeti godoro moja, fedha taslimu sh 450,000 na vitu vingine vilivyokuwemo, vyote vikiwa na thamani ya sh milioni 1.8.
Pia katika tukio hilo nyumba moja ya Matayo Kizaberga, mkulima na mkazi wa Makunda-Mbugani ilichomwa moto na vitu vyote vilivyokuwemo kuteketea.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba watu 25 akiwamo mwenyekiti wa kijiji wanashikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo.
Kamanda Kamwela alisema chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa mashamba ambapo wanakijiji cha Makunda wanapinga waathirika hao kumiliki ekari 284 wakati si wazawa wa eneo hilo.
Alisema watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Chanzo;Tanzania Daima

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu watakiwa kufika kijiji cha Kazamoyo


unnamed
Baadhi ya wananchi wakiwa wamehamishia makazi yao chini ya mti uliopo kwenye korongo kijiji cha Handa mpakani mwa Wilaya ya Chemba na Singida Vijijini mara baada ya nyumba zao kuchomwa moto na askari polisi na wale wa kikosi cha kupambana na ujangili kwa madai ya kuvamia hifadhi ya msitu wa mgori (PICHA NA HILLARY SHOO).
watoo

 Huyu ni mmoja wa watoto walionashwa na kamera yetu akiwa amelala hoi kwa kukosa chakula na huduma zingine, baada ya nyumba zao kuchomwa moto wakati wa operesheni ya kuwahamisha katika kitongoji cha Kazamoyo kwa madai ya kuvamia hifadhi, hata hivyo wananchi hao wameisha katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka nane toka mwaka 2005 , lakini sheria ya kuingiza eneo hilo kwenye msitu wa hifadhi ya mgori ilifanyika mwaka 2007, (PICHA NA HILLARY SHOO).
.Unyanyasaji dhidi ya wananchi wakithiri wilayani Singida
Na Hillary Shoo, Singida
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wametakiwa kufika katika kitongoji cha Kazamoyo kijiji cha Nguamuhanga tarafa ya Mgori Wilayani Singida vijijini na kujionea unyanyasaji dhidi ya wananchi wakati wa zoezi la kuwaondoa katika hifadhi ya msitu wa mgori.
Hayo yamesemwa juzi katika kitongoji hicho na baadhi ya wananchi walioamua kuhamia kwenye korongo na kuishi chini ya miti kama digidigi kunusuru maisha yao kutokana na vipigo kutoka kwa wa kikosi cha kupambana na ujangili Wilaya ya Singida na askari polisi.
Wamesema ni vyema kituo hicho wakafika mapema ili kuona jinsi ambavyo binadamu wanavyoishi maisha ya shida ta taabu kwenye eneo hilo kufuatia amri ya mkuu wa Wilaya ya kuhamisha kwa muda mfupi.
Wamesema eneo hilo wameishi zaidi ya miaka nane na kujenga makazi bora bila matatizo yoyote, lakini jambo la ajabu ni baada ya Wilaya ya Chemba na Sngida kuwekeana mipaka na kuonekana kuwa wako Singida.
“Wakati tuko kijiji cha Handa Wilaya ya Chemba, tuliishi bila matatizo lakini baada ya kuhamia singida ndipo mambo yalianza kubadilika na kuambiwa kuwa tuko eneo la hifadhi, hii ni ajabu sana , Wilaya moja tuliishi vizuri hii nyingine haitutaki sasa tuende wapi.” Alihoji mmoja wa kina mama.
Licha ya kukosa huduma muhimu kama vile maji, mahema, vyoo baadhi ya kina mama na watoto walionekana wakiwa katika huzuni klubwa huku wengine wakiangua vilio baada ya kuwaona waandishi wa habari wakidhani kuwa ni askari.
Hata hivyo eneo hilo lina mbu wengi, jua kali na mbaya zaidi hivi sasa ni msimu wa mvua katika maeneo hayo, je swali la kujiuliza wataishije hapo wananchi hao zaidi ya 1,000 ambao nyumba zao zimechomwa moto.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Singida Qeen Mlozi amesema zoezi hilo linaendelea sanjari na kuhakikisha wanaondoka kwenye korongo hilo walimojificha.
Hivi karibuni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu alitembelea eneo hilo la kusitisha zoezi la kuwahamisha mpaka pale kamati ya kudumu ya huduma za kijamii ya baraza la madiwani watakapokutana kutoa maamuzi sahihi juu ya wananchi hao.
Hata hivyo agizo hilo la Naibu Waziri limepingwa vikali sana na mkuu wa Wilaya ya Singida Mwalimu Qeen Mlozi kwamba Nyalandu hana mamlaka kisheria ya kusitisha zoezi hilo, na kwamba anayeweza kumwamuru kusitisha zoezi ni Mkuu wa Mkoa pekee na si vinginevyo.
Na Mo Blog



SINGIDA SASA YAJA NA MKAKATI WA KUIBUKA KIRIADHA



                             Picha zote kutoka maktaba ya Singida Yetu Blog

SINGIDA ni moja kati ya mikoa ambayo ilikuwa inafanya vizuri katika mchezo wa riadha miaka ya 1980 na kutoa wanariadha mahiri ambao waliiwakilisha Tanzania katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Mkoa huo ni wenye mandhari nzuri yenye mawe mawe pamoja na mto upande wa kushoto na kulia hususan pale unapofika mkoani hapo.
Hakika mkoa huu ni wenye vitu vingi, lakini kikubwa zaidi ni wakimbiaji wa riadha hususan maeneo ya Singida Vijijini ambako kama wakimbiaji hao wataweza kupewa vifaa maalumu kwa ajili ya kukimbia na wadau wa riadha wakajitokeza na kuchangia zaidi katika riadha, Tanzania itakuwa na medali nyingi na kupata heshima katika nchi mbalimbali duniani.
Nasema hivyo kwa sababu hivi karibuni Mbunge wa Singida Vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu aliandaa mashindano ya riadha hususan vijijini kwa ajili ya kuibua vipaji kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Shrika la African Wildlife Trust (AWT), Pratic Patel.

Mbio hizo zilizojulikana kwa jina la Singida Marathon za kilometa 21, zilianza rasmi Novemba 9, mwaka huu kwa kushirikisha wakimbiaji zaidi ya 400 kutoka Singida Mjini na Singida Vijijini na zilianzia Kijiji cha Mitula, Kata ya Kinyagigi na kuishia Viwanja vya Shule ya Msingu Ntunduu (W) Singida Vijijini.
Mbio hizo zilikuwa za kilometa 21 ambazo ni nusu marathoni na kilometa 5 na mwisho kabisa ni kilometa 2.5 ambazo ziliwashirikisha watoto wa kiume na wa kike. Wakimbiaji walikuwa wamejiandaa wenyewe na walijiandikisha, lakini baadhi yao pamoja na kukabiliwa na ukosefu wa viatu, lakini waliweza kumudu hali hiyo kutokana na mazingira waliyokua nayo na kuonesha vipaji vyao vilivyowashangaza wengi.

Inawezekana kukimbia bila viatu ni jambo lisiloruhusiwa, lakini kutokana na mazingira yenyewe ya vijijini hali hiyo haikuwa kikwazo kwa wakimbiaji hao kukimbia bila viatu ila walionesha kuwa wana moyo na nia ya dhati kuonesha vipaji vyao hakika ilikuwa faraja kubwa kwao kwani mwisho wa siku waliweza kuibuka washindi na wengine wakapata kifuta jasho.

Washindi hao ni Paulo Itambi ambaye aliibuka mshindi wa kwanza kwa upande wa wanaume ambaye alipewa zawadi ya Sh 300,000, Emmanuel Samson wa pili (Sh 200,000) na Samwel Ikungi wa tatu (Sh 100,000). Kwa upande wa wanawake, mshindi wa kwanza Fabiola William (Sh 300,000), Zakia Abdallah (Sh 200,000) na Winfrida Hassani (Sh 100,000).
Mbio za kilometa tano, washindi ni Gabriel Garado (Sh 200,000), Deo Lazaro (Sh 100,000) na Jonas John (Sh 50,000) huku wanawake ni Neema Kisuda (Sh 200,000), Pascalina Silvesta (Sh 100,000) na Christina Yuda (Sh 50,000) ambao washindi wa kilometa 2.5 wakiwa ni Julita Antony (Sh 100,000), Editha Gabriel (Sh 50,000) na Magreth Bernado (Sh 25,000).
Wanaume walikuwa ni Petro Pascal mshindi wa kwanza na kupewa Sh 100,000, Baraka Sebastian (Sh 50,000), Haji Swalehe (Sh 25,000) huku washindi wengine 400 kila mmoja akipewa Sh 10,000. Baada ya washindi hao kukabidhiwa zawadi zao, Patel ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Naibu Waziri Nyalandu, alikabidhi pia medali mbalimbali kwa washindi hao.

Aidha, alitoa changamoto kwa
wananchi hao kuacha tabia ya kuua tembo, bali wanastahili kulindwa na kuhifadhiwa ili kukuza uchumi na kufungua milango ya ajira.
Hata hivyo, baadhi ya washindi walimshukuru Nyalandu kwa kuamua kuanzisha mashindano hayo maeneo ya vijijini ili kuibua vipaji na kutoa rai kwa wadau wa riadha mkoani humo pamoja na sehemu mbalimbali kuanzisha klabu za michezo ya riadha ili kuendeleza vipaji na kuibuavipaji vipya.

Fabiola ambaye ni mkimbiaji mashuhuri wa riadha na aliyeiletea sifa Tanzania, alisema awali alikuwa akikimbia mkoani Kilimanjaro, lakini hivi sasa yupo Singida ambako alihamia Singida Vijijini kwenye Jimbo la Nyalandu, ndio kwao alipozaliwa na anaona fahari kubwa kuona wilaya hiyo ina wakimbiaji wengi na ni wazuri, lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa kwa ajili ya kufanyia mazoezi.

Fabiola na wadau wengine wamemwomba Naibu Waziri pamoja na wadau wengine kushirikiana kwa pamoja ili kuanzisha klabu za michezo ya riadha ili kuibua vipaji vya wakimbiaji waliopo maeneo ya vijijini.

Alisema mkoa huo una wanamichezo wengi, lakini hakuna klabu za michezo hali inayosababisha baadhi ya wanariadha kufanya mazoezi bila ya kuwa na vifaa maalumu, lakini walimpongeza Nyalandu kwa kuanzisha mashindano hayo maeneo ya vijijini ili kuibua wanamichezo wengi watakaoweza kuutangaza mkoa huo pamoja na Tanzania kwa ujumla pale yanapotokea mashindano ya riadha ya ndani na nje ya nchi.
KWA HISANI YA SINGIDA YETU BLOG


Kung’olewa kwa Zitto, Mkumbo: Chadema mikoani watofautiana

Wanachama wa Chadema mikoa mbalimbali nchini pamoja na wananchi wametoa maoni tofauti kuhusu uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho wa juzi kuwavua uongozi viongozi wake watatu; Naibu Katibu Mkuu wake Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo na mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Singida
Kutoka mkoani Singida, uongozi wa chama hicho  jana ulifanya kikao cha faragha kujadili uamuzi wa chama hicho, huku baadhi ya wananchi wakiuelezea uamuzi  huo kuwa umetokana na pupa na kushindwa kuvumiliana, wengine wakitishia kujitoa katika chama hicho.
Kwa zaidi za saa 5 uongozi huo ulikuwa ukijadili hatua hiyo huku ukiahidi kutoa taarifa yake baada ya kikao hicho kilichokuwa kikiendelea hadi baada ya saa 7 mchana.
Habari zaidi kutoka Wilaya ya Iramba mkoani humo zinasema kuwa wanachama wa Chadema wilayani humo wametishia kurudisha kadi za chama hicho kilichokuwa kimeanza kujizolea umaarufu wakisema watafanya hivyo ikiwa Chadema ‘watalitosa jembe’ lao.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili walisema kuwa hatua hiyo inaweza kuipunguzia umaarufu Chadema na kwamba ustawi wa vyama vingi vya siasa unaponzwa na pupa, jazba hata kukosa uvumilivu.
“Kikundi hiki cha viongozi kinasababisha Chadema kumeguka kama tulivyosikia juzi. Kwa maoni yangu kabla hakijawavua uongozi Zitto, Dk Mkumbo na Mwigamba, kilikuwa kinashabikiwa na asilimia 90, hapa Singida, lakini baada ya tukio la juzi la kuwavua uongozi baadhi ya viongozi, nina hakika kinashabikiwa na asilimia 30 ya wananchi,” alisema Juma Mdida.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TLP Wilaya ya Singida, Athumani Nkii, alisema kuwa ustawi  wa vyama vingi vya siasa unaponzwa na vitendo vya pupa, jazba na ubinafsi wa baadhi ya viongozi wake baada ya majina yao kupata umaarufu,wakisahau kuwa umaarufu huo unachangiwa na chama husika.
“Kwa upande wa Kabwe Zitto, nadhani safari zake za nje ya nchi na suala la mapesa ya Uswisi, zitakuwa hazina baraka za Chadema. Kuhusu Dk Kitila Mkumbo, sina kabisa fununu ya madhambi yake,”alisema.
Rukwa
Barua ya kujiuzulu nafasi ya Makamu Mwenyekiti Chadema Tanzania Bara, Said Amour Arfi ambaye pia ni Mbunge wa Mpanda imesambazwa  kwa wapiga kura wake na wananchi wa jimbo hilo ili  wafahamu sababu za msingi za yeye kujiondoa katika nafasi yake.
Katibu wa mbunge huyo, Joseph Mona, alipata taarifa za uamuzi huo wa ghafla, aliosema kuwa ni sahihi.
Chanzo;Mwananchi


KATA YA MTAMAA MANISPAA YA SINGIDA YAPATA NEEMA YA UMEME.


Mjumbe wa halmashauri kuu ya taifa CCM Bw. Hassan Mazala 
(Picha Kutoka Maktaba Yetu)

Kata ya mtamaa manispaa ya Singida inatarajiwa kuunganishiwa nishati ya umeme wa grid wa taifa kupitia mradi wa umeme vijijini REA ili kukabiliana na umasikini wa kipato kwa wananchi wa kata hiyo.
Mjumbe wa halmashauri kuu ya taifa CCM Bw. Hassan Mazala wakati akizungumza na wananchama wa CCM katika kata hiyo ambapo amesema upembuzi yakinifu juu ya mradi huo unatarajiwa kuanza mwezi huu.
Amesema kuwa endapo umeme ukiunganishwa katika kata hiyo kutasaidia wananchi kujishughulisha na shughuli za kiuchumi ambazo zinategemea nishati hiyo na hatimaye kuondokana na umasikini wa kipato unaowakabili wakazi wa kata hiyo
Aidha Bw Mazala ametoa wito kwa wananchi wa kata hiyo kuwa tayari kuonyesha nia ya kuhitaji huduma hiyo kwa kujiandikisha hali ambayo itaongeza juhudi za mradi huo wa REA kwenda kasi kutokana na mahitaji ya idadi kubwa ya watu.
Na Singida yetu Blog

SEMA yagharamia ujenzi wa Vyoo katika shule tano za Manispaa ya Singida.


Meneja wa shrika la SEMA, Ivo Manyanku,(wa kwanza kulia) akitoa taarifa yake ya ujenzi wa vyoo bora katika shule tano za msingi manispaa ya Singida kwa Naibu Waziri TAMISEMI (Elimu), Mh. Kassim Majaliwa (mwenye miwani).Vyoo hivyo vimegharimu zaidi ya shilingi 155 milioni.
Naibu Waziri TAMISEMI (Elimu) Mh. Kassim Majaliwa (aliyeipa kisongo kamera) akizindua rasmi ujenzi wa vyoo bora katika shule ya msingi Unyankindi.Vyoo hivyo bora vimejengwa kwa gharama ya shilingi 155 milioni na shirika la SEMA.Kushoto ni meneja wa SEMA. Ivo Manyanku.
Naibu Waziri wa TAMISEMI (Elimu),Kassim Majaliwa akikata utepe kuashiria ufunguzi wa matumizi ya vyoo bora vya shule ya msingi Unyankindi mjini Singida.Vyoo hivyo vimejengwa na shirika la SEMA kwa gharama ya shilingi 155 milioni.
Moja ya vyoo bora vya shule ya msingi Unyankindi manispaa ya Singida vilivyojengwa na shirika la SEMA la mkoa wa Singida.

Shirika lisilo la kiserikali la Sustainable Environment Management Action (SEMA) la mkoani Singida limetumia zaidi ya shilingi 155 milioni kugharamia ujenzi wa vyoo bora katika shule tano za manispaa ya Singida.

 Shule zilizonufaika na mradi huo ni,Unyankindi,Singidani,Manguamitogho,Mtamaa na Mtisi.

 Hayo yamesemwa juzi na Meneja wa SEMA, Ivo Manyanku wakati akizungumza kwenye hafla iliyofana ya uzinduzi wa vyoo hivyo uliofanyika katika shule ya msingi Unyankindi Singida mjini.

 Amesema fedha hizo zilizotumika katika ujenzi huo zimetolewa ufadhili na shirika la WaterAid Tanzania kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji na usafi shuleni katika halmashauri ya manispaa ya Singida.

 “Vyoo hivi vina matundu 48 ambayo yana uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,903 kati yao wavulana ni 1,446 na wasichana ni 1,457.Idadi hiyo inajumuisha na walemavu 38 ambao 25 ni wavulana na 13 ni wasichana”,amesema Meneja huyo.

 Kwa upande wake mgeni rasmi katika uzinduzi huo,naibu waziri TAMISEMI (elimu),Kassimu Majaliwa,alitumia fursa hiyo kulipongeza shirika la SEMA kwa ujezi bora wa vyoo hivyo ambavyo vimekidhi vigezo vyote vinavyohitajika.

 Amesema serikali na wadau wengine wa maendeleo hawana budi kuliunga mkono shirika la SEMA kwa madai linatelekeza miradi yake kulingana na thamani ya fedha zilizotumika.

 “SEMA binafsi nawapongezeni sana ujenzi huu mtakuwa mmeisaidia serikali katika kupunguza
kero mbalimbali zinazoikabili sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu.Vyoo hivi ni bora mno na vitakuwa vimepunguza kwa kiwango kikubwa uhaba wa vyoo katika shule zetu za msingi”,amesema Majaliwa.

 Wakati huo huo, Naibu Waziri huyo ameuomba uongozi wa halmashauri ya manispaa ya Singida kusimamia matumizi ya vyoo hivyo ili viweze kutumika kwa muda mrefu zaidi.

Chanzo: Singida yetu 
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa