Wanachama wa Chadema mikoa mbalimbali nchini pamoja na wananchi
wametoa maoni tofauti kuhusu uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho wa juzi
kuwavua uongozi viongozi wake watatu; Naibu Katibu Mkuu wake Zitto
Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo na mwenyekiti wa chama
hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Singida
Kutoka mkoani Singida, uongozi wa chama hicho
jana ulifanya kikao cha faragha kujadili uamuzi wa chama hicho, huku
baadhi ya wananchi wakiuelezea uamuzi huo kuwa umetokana na pupa na
kushindwa kuvumiliana, wengine wakitishia kujitoa katika chama hicho.
Kwa zaidi za saa 5 uongozi huo ulikuwa ukijadili
hatua hiyo huku ukiahidi kutoa taarifa yake baada ya kikao hicho
kilichokuwa kikiendelea hadi baada ya saa 7 mchana.
Habari zaidi kutoka Wilaya ya Iramba mkoani humo
zinasema kuwa wanachama wa Chadema wilayani humo wametishia kurudisha
kadi za chama hicho kilichokuwa kimeanza kujizolea umaarufu wakisema
watafanya hivyo ikiwa Chadema ‘watalitosa jembe’ lao.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili
walisema kuwa hatua hiyo inaweza kuipunguzia umaarufu Chadema na kwamba
ustawi wa vyama vingi vya siasa unaponzwa na pupa, jazba hata kukosa
uvumilivu.
“Kikundi hiki cha viongozi kinasababisha Chadema
kumeguka kama tulivyosikia juzi. Kwa maoni yangu kabla hakijawavua
uongozi Zitto, Dk Mkumbo na Mwigamba, kilikuwa kinashabikiwa na asilimia
90, hapa Singida, lakini baada ya tukio la juzi la kuwavua uongozi
baadhi ya viongozi, nina hakika kinashabikiwa na asilimia 30 ya
wananchi,” alisema Juma Mdida.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TLP Wilaya ya
Singida, Athumani Nkii, alisema kuwa ustawi wa vyama vingi vya siasa
unaponzwa na vitendo vya pupa, jazba na ubinafsi wa baadhi ya viongozi
wake baada ya majina yao kupata umaarufu,wakisahau kuwa umaarufu huo
unachangiwa na chama husika.
“Kwa upande wa Kabwe Zitto, nadhani safari zake za
nje ya nchi na suala la mapesa ya Uswisi, zitakuwa hazina baraka za
Chadema. Kuhusu Dk Kitila Mkumbo, sina kabisa fununu ya madhambi
yake,”alisema.
Rukwa
Barua ya kujiuzulu nafasi ya Makamu Mwenyekiti
Chadema Tanzania Bara, Said Amour Arfi ambaye pia ni Mbunge wa Mpanda
imesambazwa kwa wapiga kura wake na wananchi wa jimbo hilo ili
wafahamu sababu za msingi za yeye kujiondoa katika nafasi yake.
Katibu wa mbunge huyo, Joseph Mona, alipata taarifa za uamuzi huo wa ghafla, aliosema kuwa ni sahihi.
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment