MKAZI WA SINGIDA AKUTWA AMEJINYONGA KWA KUTUMIA WAYA.



Kijana wa kiume anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 28 na 33 mfanyabiashara za machinga mjini Singida,Bakari Kavite,mwili wake umeokotwa leo (31/10/2012) saa moja na nusu  akiwa amejinyonga kwenye nyumba ya sinema ya Furaha jirani na hotel yenye hadhi ya kitalii ya Stanely motel.Amejinyonga hadi kufa kwa kutumia waya.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida,Linus Sinzumwa,ameahidi kutoa taarifa baadaye kuhusiana na tukio hilo.(Picha zote na Nathaniel Limu).
Askari na Wakazi wa Singida wakibeba mwili wa Marehemu kuupeleka Hospital kwa ajili ya uchunguzi.
Wananchi wakiwa wamekusanyika eneo la tukio.
Mo Blog

MKULIMA WA SINGIDA KIZIMBANI KWA TUHUMA KUMNAJISI MWANAE WA DARASA LA PILI.



Na Nathaniel Limu.
Kijana mmoja mkulima wa kijiji cha Ughandi ‘B’ tarafa ya Mtinko jimbo la Singida kaskazini, amepandishwa kizimbani akituhumiwa kumwingilia kimwili mtoto wake wa kike anayesoma darasa la pili.
Kijana huyo ni Juma Abrahaman na umri wake ni miaka thelathini (30).
Mwendesha mashitaka Geofrey Luhanga amedai mbele ya hakimu wa mahakama ya wilaya ya Singida Flora Ndale, kuwa mnano Septemba 9 mwaka huu majira ya jioni, mshitakiwa Juma kwa makusudi, alimwingilia kimwili mtoto wake wa kike kitendo anachojua wazi kuwa ni kinyume na sheria.
Akifafanua amedai kuwa mshitakiwa alimwita mtoto wake (jina tunalo) chumbani kwake na kisha kumfanyia kitendo hicho cha kinyama.
Wakati mshitakiwa akifanya kitendo hicho mke wake alikuwa jirani akiendelea na shughuli zake za nyumbani.
Mshitakiwa amekana shitaka na yupo ndani hadi oktoba 31 mwaka huu kesi yake itakapotajwa tena.
Mshitakiwa alishindwa kupata mtu wa kumdhamini na hivyo kulazimika kwenda mahabusu gerezani.

SIRUNGONET YAANZA KUENDESHA MIDAHALO



na Jumbe Ismaily, Singida
MTANDAO wa asasi za kiraia wilaya ya Singida vijijini (SIRUNGONET) umetangaza kuanza kuendesha midahalo ya mikakati ya kupunguza umaskini na kuongeza kipato kwa jamii kwenye jimbo la Singida Kaskazini, Singida Magharibi na Singida Mashariki.
Mratibu wa Sirungonet wilayani hapa, Sombi Sombi, alisema jana kuwa leo wataanza mdahalo katika kijiji cha Itaja, tarafa ya Mgori.
Alisema Oktoba 23, wataendesha mdahalao kijiji cha Puma, kilichoko jimbo la Singida Magharibi kuanzia saa tatu asubuhi ambapo wananchi watapata fursa ya kutoa maoni yao wakati saa sita mchana wananchi wa kijiji cha Dung’unyi katika jimbo la Singida Magharibi watapa nafasi ya kutoa maoni yao pia.
Aidha, mratibu huyo alisema lengo la midahalo hiyo ni kuimarisha mahusiano kati ya wananchi na wabunge au wawakilishi wao.
“Midahalo hii inalenga kutoa fursa ya majadiliano kati ya wabunge, madiwani na watendaji wa serikali ili kuimarisha ari ya ushiriki na ushirikishwaji wa wananchi katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima

MWENDO KASI WASABABISHA KIFO CHA MCHUNGAJI JACKSON HUSENA KATIKA AJALI YA BARABARANI MKOANI SINGIDA.



Kamanda wa polisi mkoa wa Singida Linus Sinzumwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) ya ajali iliyoua  mchungaji wa kanisa la Pentekoste.
(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Mtu mmoja amekufa papo hapo na wengine wanne kujeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao baada ya gari waliyokuwa wakisafiria kuacha njia kisha kupinduka mkoani Singida.
Kamanda wa polisi mkoa wa Singida Kamishina msaidizi Linus Sinzumwa, amesema ajali hiyo imetokea majira ya saa tano usiku katika eneo la mzunguko mjini Manyoni barabara kuu ya Dodoma-Mwanza.
Amesema wakati wa tukio hilo  wachungaji wa kanisa la Pentekosti walikuwa wakisafiri kwa gari ndogo aina ya Land Cruiser yenye namba za usajili T.531 EAT wakitokea Mwanza kwenye mkutano wa injili, kurejea Dodoma.
Hata hivyo, amesema kutokana na kile kinachosadikiwa kuwa mwendo kasi baada ya kufika eneo la mzunguko Manyoni,  dereva wa gari hiyo alishindwa kuilmudu kabla ya kuacha njia na kupunduka.
Kamanda Sinzumwa amesema hali hiyo ilisababisha kifo cha mchungaji Jackson Husena (58) papo hapo huku wachungaji wengine Jonas Chungu, Pasian Chiwanda na Stephano Ulaya, wakijeruhiwa.

MFUKO WA BIMA SINGIDA WAWATAKA MADIWANI KUHAMASISHA WANANCHI KUHUSU FAIDA ZA MFUKO HUO.

Maafisa wa mfuko wa taifa wa biwa ya afya (NHIF) wakiwa ofisini kwao katika majengo ya chuo cha VETA  mjini Singida,Kulia ni afisa msimamizi wa ofisi ya mkoa wa Singida na kushoto ni afisa matekelezo Isaya Sheikifu.(Picha na Nathaniel Limu).
Nathaniel Limu.
Madiwani wa halmashauri ya wilaya na manispaa ya Singida, wamehimizwa kuongeza kasi ya kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF), ili waweze kujijengea mazingira mazuri ya kupata tiba hasa kipindi hali zao kiuchumi zinapokuwa sio nzuri.
Wito huo umetolewa na Afisa Matekelezo wa mfuko wa taifa wa bima ya afya (NHIF) mkoani Singida Isaya Sheikifu wakati akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani  halmashauri ya wilaya ya Singida.
Amesema kutokana na kweli kwamba wananchi wengi hawawezi kuwa na fedha za matumizi mbali mbali yakiwemo ya matibabu wakati wote, njia pekee ya kuwa na uhakika wa matibabu ni pindi akiujua na mfuko wa afya ya jamii.
Sheikifu amesema ili kaya iweze kujiunga na mfuko huo, inapaswa kulipa shilingi 5,000 tu, halafu baba, mke na watoto wanne walio chini ya umri wa miaka 18, wote watatibiwa mwaka mzima bila kutoa gharama nyingine tena.
Katika hatua nyingine, Afisa huyo pia amewahamasisha madiwani kujiunga na mfuko wa taifa wa bima ya afya (NHIF), ili pamoja na mambo mengine, waweze kupata fursa ya kutibiwa hata wanapokuwa nje ya mkoa.

WANANCHI SINGIDA KUANZA KUTOA MAONI JUU YA KATIBA KUANZIA OKTOBA 17-27, 2012.



Mkuu wa wilaya ya Singida mwalimu Queen Mlozi akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) juu ya ujio wa tume ya kukusanya maoni ya Katiba kwenye wilaya hiyo.
(Picha na Nathaniel Limu).
Na  Nathaniel Limu.
Tume ya mabadiliko ya katiba, inatarajia kuanza kukusanya maoni ya wananchi wa wilaya ya Singida kuanzia oktoba 17 hadi 27 mwaka huu.
Akitoa taarifa ya ujio wa tume hiyo wilayani humo kwa waandishi wa habari hiyo Mkuu wa wilaya ya Singida Mwalimu Queen Mlozi  amesema  wilaya hiyo yenye halmashauri mbili, tume hiyo itaanza kukusanya maoni kwenye kata kumi za halmashauri ya manispaa ya Singida kuanzia Oktoba 17 hadi 21 mwaka huu.
Amezitaja kata hizo za manispaa kuwa ni wankoko,Unyambwa,Mandewa,Mtipa,Kisaki,Mungumaji,Majengo,Unyambwa,Mughanga na Mtamaa.
Aidha, mkuu wa wilaya amesema kwa upande wa halmashauri ya wilaya ya Singida vijijini, tume hiyo itaanza kukusanya maoni kuanzia oktoba 22 hadi 27 mwaka huu.
Mlozi ametaja kata zilizochaguliwa kutembelewa na tume hiyo kuwa ni Msisi,Kinyeto,Mtinko,Maghojoa,Mgori,Ngimu,Merya,Ilongero,Maghojoa,Mgori,Ngimu,Merya,Ilongero, Ughandi na Ngamu.
Amesema kila siku tume hiyo itakapo tembelea kata mbili ambapo kata ya kwanza wananchi watatoa maoni yao kuanzia saa tatu asubuhi na kata ya pili shughuli itaanza saa nane mchana.
Alitumia fursa hiyo kutoa wito kwamba wananchi wajitokeze kwa wingi kutoa maoni yao wakati watakapokuwa wanapewa muda wa dakika tano na endapo itashindikana kutumia njia hiyo,basi watumie njia ya kuandika maoni yao kwa maandishi.
Pia amewaonya kwamba wasishawishiwe na mtu au kiongozi katika kutoa maoni yao.

MKAZI WA SINGIDA AJIUA BAADA YA KUMKATAKATA VISU MPENZI WAKE AKIFIKIRI AMEMUUA KUFUATIA KUSHINDWA KULIPA MAHARI.


Mhudumu wa chuo cha VETA mjini Singida Maria Chilinde akiwa wodini katika hospitali ya mkoa akipatiwa matibabu ya majeraha baada ya kukatwa katwa visu na mchumba wake.(Picha na Nathaniel Limu).
Na. Nathaniel Limu
Kijana mmoja mkazi  wa mkoa wa Dodoma  aliyetambulika kwa jina moja  la Oscar  anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 24,  amejiuwa kwa kutumia pazia la dirisha.
Oscar amejiuwa oktoba 13 mwaka huu usiku wa kuamkia leo muda mfupi  baada ya  kumkatakata vibaya  mchumba wake Maria  Chilinde (25).Maria ni mhudumu wa chuo cha VETA  Mjini  Singida, na amepata dhahama hiyo kwenye nyumba anayoishi ya VETA.
Maria ambaye amepoteza   damu nyingi  zilizosababishwa na majeraha ,  amelazwa wodi namba mbili,   katika Hospitali ya Mkoa  iliopo mjini Singida.
 Kwa mujibu wa  muuguzi wa wodi hiyo ambaye  ameomba jina lake  lisitajwe  kwa madai kwamba  sio msemaji wa hospitali hiyo,  alisema hali ya Maria  inaridhisha na akadai  akimaliza chupa ya damu aliyotundikiwa, anaweza kuanza kuongea.
Akifafanua zaidi,alisema Maria ana majeraha makubwa Kichwani,mkononi, na sehemu za mbavu.
 Habari za uhakika kutoka eneo la tukio  zinadai kuwa Oscar (marehemu), ana kawaida ya kumtembelea  Maria mara kwa mara. Wakati mwingine alikuwa akimaliza mwezi  akiwa na mchumba wake.
Hata hivyo inadaiwa kuwa kuna kipindi wazazi wa Maria walikuwa wanadai walipwe mahari ya shilingi milioni mbili na Oscar,ili aweze kuruhusiwa kumwoa Maria.
Habari zaidi zinadai kuwa  baada ya kijana  Oscar alishindwa kutoa mahari  hiyo ya shilingi milioni mbili  kitendo kilichopelekea wazazi waanze kukataa binti yao kuolewa na Ocsar.
Habari hizo  zinadai kuwa  kitendo hicho  kilichasababisha  kijana huyo atake  kumuuwa mchumba wake na  kisha yeye naye ajiuwe.
Oscar baada ya kumcharanga mchumba wake Maria  kwa kisu na kusababisha azirai,  alihisi Maria ameishafariki dunia.
Baada ya  Oscar kuhisi  Maria amefariki dunia alichukua kipande cha pazia akapanda juu ya stuli  kisha kufunga pazia kwenye kenchi.  Zoezi hilo lilipomalizika la kujitundika alisukuma stuli pembeni  kuanza kuning’inia na kupelekea kupoteza maisha yake.
Kamanda wa polisi mkoa wa Singida,Linus Sinzumwa amekiri kutokea kwa tukio hilo na amedai upelelezi zaidi unaendelea.

WAZIRI MAGUFULI APONGEZA WAANDISHI KWA KUCHANGIA KUKARABATIWA KWA KIPANDE CHA BARABARA IRAMBA.


Waziri wa ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli akikagua kipande cha barabara (kilometa 33) zinazorudiwa kujengwa kwa kiwango cha lami na kampuni ya CHICO ambayo inadaiwa awali kuijenga chini ya kiwango. Kampuni ya CHICO inajenga kipande hicho kwa gharama zake pamoja na mkandarasi mshauri. Gharama ya ujenzi wa kipande hicho kinachoanzia katika kijiji cha Misigiri hadi Shelui ni zaidi ya shilingi bilioni 80.
Meneja wa TANROADS mkoa wa Singid Mhandisi Yustaki Kangole akitoa taarifa yake ya ujenzi wa kipande cha barabara kinachoanzia kijiji cha Misigiri hadi Shelui kilometa 33. Kipande hicho kinarudiwa kujengwa na kampuni ya kichina CHICO baada ya awali kukijenga chini ya kiwango.
Waziri wa ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli (wa kwanza kushoto) akiwa na mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone (katikati) na Mkuu wa wilaya ya Iramba Yahaya Nawanda (wa kwanza kulia). Muda mfupi kabla ya waziri Magufuli kuzungumza na wafanyakazi wa kampuni ya CHICO.  
Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wafanyakazi (hawapo kwenye picha) wa kampuni ya CHICHO inayorudia kujenga kipande cha kilometa 33 kinachoanzia kijiji cha Misigiri hadi Shelui wilayani Iramba.
Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza waandishi wa habari kwa juhudi zao za kutangaza/kuandika bila kuchoka habari za ubovu wa kipnade cha barabara kuu cha mlima  Sekenke wilayani Iramba.
Amesema juhudi hizo za kuanika hadharani ubovu wa kipande hicho na madhara yake, zimechochea serikali kulazimisha kampuni ya CHICO, kurudia kwa gharama zake kukijenga upya kipande hicho chenye urefu wa kilomita 33.3.
Dkt. Magufuli ametoa pongezi hizo wakati akizungumza kwenye kikao cha pamoja cha wafanyakazi wa kampuni ya CHICO na viongozi mbali mbali wa seriklai mkoa wa Singida.
Amesema kazi ya kulazimisha kampuni ya CHICO kurudia kukijenga kipande hicho, haikuwa rahisi kwa madai kwamba ilikwisha kabidhi barabara hiyo baada ya kipindi kilichowekwa kisheria cha uangalizi wa ubora wa barabara (defect liability period) kukamilika Januari mwaka 2009.
Magufuli amesema pamoja na kukabidhi barabara hiyo, haikuchukua miezi miwili kipande hicho cha barabara kilibainika kujengwa chini ya kiwango, baada ya kuanza kuharibika kwa kasi.
Akifafanua zaidi, Waziri huyo amesema uharibifu huo ulipigiwa kelele sana na watu mbali mbali, wakiwemo waandishi wa habari.
Kwa upande wa Makandarasi na makandarasi washauri kujenga barabara chini ya kiwango, amesema serikali haitawavumilia makandarasi wa aina hiyo, itawanyang’anya kazi waliyopewa.
Aidha, Magufuli alisema wakurugenzi watendaji wa halmashauri watakaotumia vibaya fedha za mfuko wa barabara, nao watajibishwa.
Katika hatua nyingine, waziri Magufuli ameipa kampuni ya CHICO miezi mitatu kuhakikisha imemaliza ujenzi huo wa kilomita 33.3, vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya kampuni hiyo.
Kwa upande wake meneja wa site wa CHICO Stone Chene, amesema kazi hiyo itawagharimu CHICO zaidi ya dola za kimarekani milioni tano. 

TANROADS SINGIDA YALAMBA SH BILIONI 4



Na Nathaniel Limu, Singida
WAKALA wa Barabara (TANROAD) mkoani Singida, umetumia zaidi ya Sh bilioni 4.4, kugharamia matengenezo ya barabara kwa kiwango cha udongo na chagarawe.

Hayo yalisemwa juzi na Meneja wa TANROADS mkoani hapa, Mhandisi Yustaki Kagole, wakati akitoa taarifa yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Paseko Kone.

Kagole alisema, matengenezo hayo yalifanyika katika kipindi cha mwaka 2011/2012, ambapo matengenezo ya kawaida ya kilomita 637, yamegharimu zaidi ya Sh milioni 897.

"Matengenezo ya vipindi maalumu ya kiliomita 102, yamegharimu zaidi ya Sh bilioni 1.8 na matengenezo ya sehemu korofi yenye urefu wa kilomita 48.2, nayo yamegharimu zaidi ya Sh milioni 640.6,” alisema.

Alisema mategenezo madogo kwa ajili ya kulinda na kutunza madaraja tisa, yamegharimu Sh milioni 23.1, wakati matengenezo makubwa ya madaraja na ujenzi wa makalavati manne, yamegharimu zaidi ya Sh milioni 351.3.

“Miradi midogo ya maendeleo ya barabara za mkoa zenye urefu wa kilomita 51, umegharimu zaidi ya Sh milioni 714.3,” alisema.

Alisema lengo lao ni kuhakikisha kuwa, barabara zote zinapitika kwa urahisi wakati wote wa mwaka kwa ajili ya kutia chachu maendeleo ya wananchi.

TANROADS mkoa wa Singida, unahudumia zaidi jumla ya kilomita 1,689.5, ambapo kati ya hizo, barabara kuu (truck roads) ni kilomita 674.2 na barabara za mkoa ni kilomita 1,015.3.

Hadi mei mwaka huu, mkoa ulikuwa na barabara za kiwango cha lami zenye urefu wa kilomita 340 kwa barabara kuu.

Chanzo: Mtanzania


‘POLISI OMBENI VIBALI TANROADS’



na Halima Jamal, Manyoni
KUTEUA kwa jeshi a polisi vituo vya vizuizi bila kupata kibali cha Wakala wa Barabarani (TANROADS), kumesababisha uharibifu wa barabara za lami zinazojengwa kwa gharama kubwa.
Hayo yamesemwa jana na Meneja wa TANROADS mkoani Singida, Yustaki Kangole, wakati akitoa taarifa yake kwa mkuu wa mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone, ambaye ameanza ziara ya siku mbili kukagua hali ya barabara.
Alisema Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani, limekuwa na tabia ya kuchagua maeneo yasiyofaa kwa ajili ya kuegesha magari makubwa kwa ukaguzi wao.
Aidha Kangole alisema ni vema jeshi hilo likaishirikisha TANROADS katika kuchagua maeneo ya ukaguzi wa magari ili uharibifu wa barabara hizo zinazojengwa kwa gharama kubwa usiendelee kutokea tena.
Meneja huyo aliyataja maeneo ambayo jeshi la polisi linayatumia bila ya ridhaa ya TANROADS kuwa ni Mzani wa Njuki, eneo la Ikungi, Manyoni na Misuna.
“Tunashauri uongozi wa mkoa, utoe maelekezo kwa polisi kuomba vibali TANROADS ili upewe maeneo ya vizuizi kwa kushauriana na TANROADS. Yapo maeneo maalumu katika barabara za lami ambayo magari mazito yanaruhusiwa kusimama bila kuleta madhara,” alisema Kangole.
Aidha Kangole alisema kuna tatizo jingine sugu la watumiaji barabara hasa madereva wa malori makubwa kutengenezea magari yao juu ya tabaka la lami na hivyo kuharibu barabara kwa jeki, mawe na mafuta ya magari.
“Pamoja na TANROADS kuanzisha kitengo cha elimu kwa umma, bado tatizo hili limeshamiri sana katika maeneo ya Mlima Saranda, Ikungi, Iguguno, Ulemo, Misigiri na Shelui. Tunadhani nguvu ya dola inahitajika katika hili,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima

Magufuli Ateta Na Makandarasi


 Akizungumza na uongozi wa kampuni ya CHICO (hawapo pichani), Magufuli aliwataka kutekeleza mradi huo kwa kuzingatia makubaliano
 John Magufuli akizungumza na wafanyakazi wa kampuni ya CHICO
 Magufuli akikagua barabara inayokarabatiwa na kampuni ya CHICO kutoka nchini China baada ya kujenga chini ya kiwango mwaka 2008
 Meneja TANROADS mkoa Singida Yustak Kangole akitoa taarifa ya marudio ya ujenzi wa barabara Sekenke-Shelui, km 33.3, kwa waziri
Singida.
Oktoba09,2012.
Makandarasi.....
WIZARA ya Ujenzi imewakumbusha Wakandarasi nchini kujenga barabara zinazolingana na thamani ya fedha, iliyopo kwenye mikataba yao.
Agizo hilo limetolewa leo mkoani Singida na Waziri John Magufuli, wakati anakagua marudio ya ujenzi wa barabara, eneo la mlima Sekenke-Shelui, yenye urefu wa kilomita 33.3.
Amesema serikali imetumia zaidi ya Sh.Bilioni 35, kugharamia ujenzi huo, lakini mkandarasi China Henan International Cooparation Group Co Ltd(CHICO), ilijenga chini ya kiwango.
Aidha ameuagiza uongozi wa kampuni hiyo kuwapatia wafanyakazi wake vifaa vya kufanyia kazi, hasa viatu na gloves kwa ajili ya kuvaa mikononi.
Hata hivyo meneja TANROADS Mkoa Singida, Yustak Kangole amesema barabara hiyo baada ya kukamilika Januari, 2008, ilichukua miezi miwili kuanza kubomoka, kutokana na ujenzi hafifu. 
Kwa mujibu wa meneja mradi wa barabara hiyo, mhandisi Stone Chen, marudio ya ujenzi yanaigharimu kampuni zaidi ya S h.Bilioni kumi. 
Na Elisante John 




MH. DIANA CHILOLO AWABWAGA WAPINZANI WAKE NAFASI YA MWENYEKITI WA UMOJA WA WANAWAKE TANZANIA UWT (CCM) MKOA WA SINGIDA.



Mbunge wa viti maalum (CCM) mkoa wa Singida Diana Mkumbo Chilolo akiwashukuru wajumbe wa mkutano mkuu wa UWT mkoa wa Singida kwa kumchagua tena kuwa mwenyekiti wao kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.Chilolo alipata kura 431 dhidi ya kura 451 zlizopigwa.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi wa UWT CCM mkoa wa Singida akitoa maelekezo kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi huo.
Mbunge wa viti maalum mkoa wa Singida Martha Mlata (waliokaa mbele anayesikiliza simu) na baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa UWT mkoa wa Singida.Kulia kwake ni mbunge wa viti maalum mkoa wa Singida Diana Chilolo.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa UWT mkoa wa Singida.Uchaguzi huo umefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA mjini Singida.(Picha zote na Nathaniel Limu).
Diana Mkumbo Chilolo ametetea kwa kishindo nafasi yake kama Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania UWT (CCM) mkoa wa Singida baada ya kupata kura 431 dhidi ya 451 zilizopigwa.
Kwa ushindi huo, Chilolo ambaye pia ni mbunge wa viti maalum mkoani Singida amewaacha kwa mbali wapinzani wake Pendo Kone aliyepata kura 11 na mwalimu Sundi Samike aliyeambulia kura nane.
Msimamizi wa mkutano huo mkuu wa uchaguzi Dkt. Parseko Kone amemtangaza mkuu wa wilaya ya Manyoni Fatuma Towfiq kuwa amaechaguliwa katika nafasi ya mjumbe wa baraza kuu taifa UWT.
Amesema mfanyakazi wa TANROADS mkaoni Singida Sara Mkumbo, amememgaragara vibaya mpinzani wake Mwajuma Shaa kwa kura 247 dhidi ya kura 153.
Dkt. Kone ambaye ni mkuu wa mkoa wa Singida amewataja washindi wa baraza la UWT kutoka wilaya ya Singida vijijini kuwa ni Halima Kundya na Debora Andrew.
Amesema kutoka wilaya ya Ikungi ni Mariamu Limu na Tatu Dahani, wilaya ya Iramb ni Monica Samwel na Elimaba Lula, wilaya ya Mkalama ni Mariamu Kahola na Helena Kitila, Manispaa Singida ni Aisha Matembe na Sara Mkumbo wakati wilaya ya Manyoni ni Magreth Mlewa na Rehema Chizumwa.
Aidha Dkt. Kone amesema Hadija Nyuha ameshinda nafasi ya uwakilishi wa jumuiya ya wazazi kwenye mkutano mkuu wa UWT, wakati Mwakilishi wa UVCCM ni Janet Mughwai.
Jane Kishari amechaguliwa kuwa mjumbe kwenye mkutano mkuu wa CCM mkoa.

HANJE BANARBAS AUKWAA TENA UENYEKITI WA CCM SINGIDA VIJIJINI KWA MIAKA MITANO IJAYO.


Mgombea nafasi ya uenyekiti wa CCM wilaya ya Singida vijijini Hanje Narumba Barnabas akijinadi kuomba kura kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi CCM (hawapo pichani) huku akiwa amebeba biblia mkononi.Hanje alitetea nafasi yake hiyo baada kupata kura 607.
Mwenyekiti mteule wa CCM wilaya ya Singida vijijini Hanje Narumba Barnabas akiwa haamini kama kweli katetea nafasi yake kutokana na upinzani mkali kwenye uchaguzi huo.
Baadhi ya wajumbe 1,200 waliohudhuria mkutano mkuu wa uchaguzi wa CCM wilaya ya Singida vjijini.(Picha na  Nathaniel Limu).
Mkutano mkuu wa uchaguzi CCM wilaya ya Singida vijijini umemchagua tena Hanje Narumba Banarbas, kuwa mwenyekiti wake kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Hanje ametetea kiti chake hicho baada ya kupata kura 607 na kufuatiwa kwa mbali na mpinzani wake wa karibu Mwiru Juma aliyepata kura 480.
Waombaji wengine wa nafasi hiyo ya mwenyekiti  wa wilaya, ni Ngala aliyepata  kura 56 na Sima Luther aliambulia kura 51.
Naibu Waziri wa Mali Asili na Utalii Lazaro Samweli Nyaland alishinda kwa kishindo nafasi ya mjumbe wa halmashauri ya taifa (NEC), baada ya kupata kura 897 kati ya kura 1,157 zilizopigwa.
 Mh. Nyalandu ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Singida Kaskazini, alifuatiwa kwa mbali na Dafi Bulali aliyepata kura 131,huku Manase Saba Saba (102) na Juma kura 27 tu.
Msimamizi wa uchaguzi huo Mosses Matonya, aliwatangaza washindi wa tano wa mkutano mkuu taifa na kura zao kwenye mabano, kuwa Monko (819) na mkuu wa wilaya ya Singida, mwalimu Queen Mlozi (731).
Aliwataja wengine kuwa ni Amani Nyekele (572), Rehema Majii (554) na Aziza Kiduda (455).
Nafasi hiyo ya wajumbe watano ilikuwa inawaniwa na wajumbe 12.
Matonya ambaye ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Manyoni, aliwataja washindi wa nafasi za ujumbe wa halmashauri kuu wilaya kundi la vijana, kuwa ni Manase Sabasaba (705), Jumanne Salum (716), Daud Elias (665) na Hilda Lazaro (666).
Alisema nafasi ya wajumbe wa halmashauri wilaya kupitia kundi la wanawake, zimechukuliwa na Amina Mweri aliyepata kura 1,468, Hilda Lazaro (672), Neema Matiti (696) na Zuena Mohammede (621).
Matonya alisema nafasi za wajumbe wa halmashauri kuu kundi la wazazi, zimechukuliwa na Justin Monko aliyepata kura 646, Edward Yaredi (374), Ilanda (353) na Ramadhani Mangu (292).
Awali mwenyeikiti wa CCM anayemaliza muda wake Joramu Allute, waliwataka wajumbe kuchagua viongozi wenye makazi yao mkoani Singida na si vingionevyo, kwa madai kuwa viongozi hao watawatumikia wananchi kwa muda mwingi zaidi.
Allute anatetea nafasi yake hiyo.
Pia mgombea mwingine wa nafasi ya mwenyekiti CCM mkoa Amani Rai alisema kuwa nyakati za kuongozwa na wazee zimepita na sasa ni nyakati za vijana kuongoza kwa madai wana uwezo wa kukabiliana na upinzani.

GHARAMA ZA MRADI WA UMEME ZAFIKIA MIL. 101/-



na Jumbe Ismaily, Singida
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida, limesema gharama za mradi wa umeme kutoka Mtinko hadi Ikhanoda zimepanda kutoka sh milioni 23 mwaka 2004 hadi kufikia sh milioni 101 mwaka huu.
Meneja wa TANESCO Mkoa wa Singida, Maclean Mbonile, alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mwishoni mwa wiki iliyopita.
Alisema mradi huo ulioanza mwaka 2003 ulitarajiwa kukamilika mwaka 2004, lakini haukuweza kukamilika kutokana na sababu mbalimbali za kiufundi.
Alizitaja sababu zilizokwamisha mradi huo kuwa ni vifaa vyote vya mradi kupelekwa kwenye miradi mingine, licha ya taarifa zake kuonyesha kuwa vimepelekwa kwenye mradi huo.
Aidha, alisisitiza kutokana na mradi huo kukaa muda mrefu bila kukamilika, watendaji wa shirika hilo wamekuwa wakiingiwa ugumu kuuombea fedha na hivyo wananchi kuendelea kukosa huduma hiyo.
Alifafanua baada ya mashauriano ya muda mrefu uongozi wa TANESCO Mkoa wa Singida walilazimika kutoa ufafanuzi juu ya hilo na kufanikiwa kutengewa sh milioni 101 kwa ajili ya kuukamilisha mradi huo unaofadhiliwa na shirika hilo.
“Kwa kweli mradi huu umetusumbua sana namna ya kuukamilisha, kwani kila unapoomba fedha hatukufanikiwa kupata kutokana na taarifa zilizoandikwa kuwa mradi umekamilika na wananchi wameanza kupata huduma,” alisisitiza Mbonile.
Akizungumzia kupatikana kwa fedha za mradi huo, Diwani wa Ikhanoda, Hinga Mnyawi, alisema hali hiyo inaleta faraja kwa wananchi wa kata hiyo, kwani wamekuwa na hamu ya kupata huduma hiyo kwa muda mrefu.
Chanzo: Tanzania Daima
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa