Home » » Padri anayedaiwa kutelekeza mtoto kuburuzwa kortini tena leo

Padri anayedaiwa kutelekeza mtoto kuburuzwa kortini tena leo

Mahakama ya Mwanzo Utemini iliyopi mjini hapa Mkoa wa Singida, leo inatarajia kuendelea kusikiliza kesi inayomkabili Padri  wa Kanisa Katoliki mjini hapa,  Deogratius Makuri ya kumtelekeza bila  kumhudumia mtoto wake wa kike aliyedaiwa kuzaa na muumini wake.
 Kesi hiyo ilisikilizwa wiki iliyopita na kuahirishwa baada ya kudaiwa mahakamani hapo kuwa padri huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi wa muda mrefu na Maria Boniphance (26) aliyekuwa mhudumu wa kanisa hilo Parokia ya Singida mjini.

 Ilidaiwa mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Ferdnand Njau kuwa wakati wote huo wa mahusiano ya kimapenzi, ndipo mshitakiwa alimpa ujauzito na kuzaa naye mtoto wa kike.

Mlalamikaji (Maria) alidai mahakamani hapo kuwa   baada ya ujauzito huo, aliamua kulifikisha suala hilo kwa wazazi wake ambao walimwendea padri huyo na kukubali kuhusika na mimba hiyo.

Alidai kuwa padri huyo aliahidi kwa maandishi kuwa atamtunza mtoto wake (jina tunalo) hadi hapo atakapokuwa na uwezo wa kujitegemea, kinyume chake ahadi hiyo alitekeleza kwa miezi michache na akasitisha matunzo.

"Pamoja na kuchukua hatua mbalimbali ikiwamo kufikisha suala hilo ofisi ya ustawi wa jamii... aliahidi kupitia hati ya mkataba kuwa atakuwa anatoa kila mwezi Sh. 80,000 na akishindwa afikishwe mahakamani, ndiyo mimi nimeamua kumshitaki, ”alidai mlalamikaji huyo.

Ilidaiwa kuwa pamoja na ahadi hiyo padri Makuri alianza kutoa madai mbalimbali kwamba mtoto huyo siyo wake wa kuzaa, na hapo ndipo aliamua kusitisha matunzo kama alivyoahidi.  .
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa