MKUU
wa Mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone, ameelezea umuhimu wa soko la hisa
katika upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu na uwekezaji kuwa haviwezi
kuletwa na masoko ya mitaji pekee.
Kwa mujibu wa mkuu huyo, dhima ya kupata rasilimali na kuzitumia
kikamilifu kwenye miradi yenye tija, husababisha ukuaji wa uchumi na
kuongeza utajiri.
Dk. Kone amebainisha hayo juzi mjini Singida wakati akifungua semina
ya siku mbili kwa wafanyabiashara na wajasiriamali juu ya soko la kukuza
ujasiriamali (EGM) iliyofanyika kwenye ukumbi wa Aque Vitae.
Alisema ni muhimu ieleweke wazi kwamba kuna uhusiano wa moja kwa moja
baina ya mafanikio ya masoko ya mitaji na uchumi wa nchi na kusisitiza
kwamba moja ya sababu ni serikali kuanzisha na kusaidia maendeleo ya
Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Aidha, alibanisha kwamba kampeni hiyo imekuja wakati muafaka ambao
serikali imepania kujenga sekta binafsi imara itakayokuwa injini ya
uchumi wa taifa.
“Napenda kuchukua fursa hii kuwahakikishia kwamba serikali inatambua
mchango wa wadau mbalimbali katika maendeleo ya masoko ya hisa hapa
nchini, mwamko kama huu unalenga kujenga uelewa kwa sekta binafsi na
umma juu ya fursa zipatikanazo na soko la hisa zinaungwa mkono na
serikali.
“Pia nitumie fursa hii kuwataka wadau na wahusika wote kwa ukamilifu
wenu kutumia tukio hili ili kutumia fursa zipatikanazo kwenye soko la
hisa,” alisema Dk. Kone.
Hata hivyo Dk. Kone alisema tafiti nyingi zimeonyesha kwamba
upatikanaji wa mitaji ya wajasiriamali wadogo na wa kati ni changamoto
kwa maendeleo ya kukua kwa shughuli za ujasiriamali na sekta hiyo kwa
ujumla.
Awali Meneja Uhusiano wa kitaasisi kutoka DSE, Mary Mniwasa,
alimweleza mkuu wa mkoa kuwa lengo la semina hiyo ni kampeni ya umma ya
kupunguza umaskini hapa nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Singida, Francis
Mashuda, alisema wafanyabiashara wanakumbana na changamoto kubwa ya
ukosefu wa mitaji.
Semina hiyo ilitarajiwa kuhudhuriwa na wafanyabiashara wa kada
mbalimbali na wajasiriamali wasiopungua 65, imefadhiliwa na DSE chini ya
uratibu wa TCCIA Mkoa wa Singida.
Chanzo;Tanzania Daimma
0 comments:
Post a Comment