KATIBU MKUU WA CCM KOMREDI KINANA AWAASA WANA CCM KUMUUNGA MKONO MWENYEKITI WAO,RAIS DKT MAGUFULI KATIKA VITA YA KUPAMBANA NA RUSHWA PAMOJA UFISADI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 Katibu MKuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana akisalimiana na Mjumbe wa kamati kuu ya siasa ya Mkoa,Mkuu wa Mkoa wa Singida,Dkt Rehema Nchimbi jana mara baada ya kuwasili katika Kata ya Ilongero,Singida vijijini katika jimbo la Singida la Kaskazini,ambapo Chama cha Mapinduzi jana kilikuwa kinapiga kura za maoni kumchagu Mbunge atakaekiwakilisha chama hicho katika uchaguzi Mdogo wa Ubunge unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni,kufuatia jimbo hilo kuachwa wazi na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo Mh.Lazaro Nyalandu aliyehamia CHADEMA.
 Wajumbe wa Halmashauri kuu ya Wilaya ya Singida Vijijini wakishangilia jambo,wakati Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahamani Kinana alipokuwa akizungumza nao kabla ya kupiga kura ya kumchagua atakaewawakilisha katika nafasi ya Ubunge,na hatimaye kugombea katika uchaguzi mdogo wa Ubunge unaotarajiwa kufanyika jimboni humo hivi karibuni.
Mjumbe wa kamati kuu ya siasa ya Mkoa,Mkuu wa Mkoa wa Singida,Dkt Rehema Nchimbi akizungumza mapema jana kwenye mkutano wa Halmashauri kuu ya Wilaya uliokuwa ukifanyika jana katika kata ya Ilongero,Singida vijijini katika jimbo la Singida la Kaskazini,ambapo Chama cha Mapinduzi kinamtafuta Mbunge atakaekiwakilisha chama hicho katika uchaguzi Mdogo wa Ubunge unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni,kufuatia jimbo hilo kuachwa wazi na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo Mh.Lazaro Nyalandu aliyehamia CHADEMA. 
 Katibu MKuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana akizungumza mapema jana kwenye mkutano wa Halmashauri kuu ya Wilaya uliokuwa ukifanyika jana katika kata ya Ilongero,Singida vijijini katika jimbo la Singida Kaskazini,ambapo Chama cha Mapinduzi kilikuwa kikipiga kura kutafuta Mbunge atakaekiwakilisha chama hicho katika uchaguzi Mdogo wa Ubunge unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni,kufuatia jimbo hilo kuachwa wazi na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo Mh.Lazaro Nyalandu aliyehamia CHADEMA.Ndugu Kinana aliwaasa Wajumbe hao kumchagua mtua anaefaa na atakawasaidia na kuwasemea matatizo yao,na atakae kuwa tayari kuwaletea maendeleo.
Wajumbe wakimsikiliza Ndugu Kinana kwa umakini kwenye mkutano huo.
Baadhi ya Wananchi waliovutiwa na hotuba ya Katibu Mkuu Ndugu Kinana,ilibidi wasogee zaidi na kuendelea kusikiliza

Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Singida Ndugu Juma Kilimba akimkaribisha Mgeni rasmi,Katiibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana aliyepita kuwasalimia na kuona wamejiandaaje na uchaguzi wao wa kura za maoni kwa ajili ya kumchagu Mtu atakaewawakilisha katika uchaguzi Mdogo wa Ubunge unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni,kufuatia jimbo hilo kuachwa wazi na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo Mh.Lazaro Nyalandu aliyehamia CHADEMA.Ndugu Kinana aliwaasa Wajumbe hao kumchagua mtua anaefaa na atakawasaidia na kuwasemea matatizo yao,na atakae kuwa tayari kuwaletea maendeleo.

STORY: Mohammed Enterprises yashinda tuzo nne za ATE 2017

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
  Kampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL Group) imeshinda tuzo nne za Mwajiri Bora wa Mwaka 2017 (EYA) zinazotolewa na Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE), katika hafla ya iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam. MeTL imeshinda tuzo hizo kupitia kampuni zake tanzu ambazo ni Mo Assurance Limited iliyoshinda kipengele cha Tuzo ya Kampuni Ndogo, 21st Century Holding Limited imeshinda nafasi ya pili ya Tuzo ya Mwajiri Bora wa Ndani na Star Oil Tanzania Limited imeshinda tuzo mbili, Tuzo ya Kampuni ya Kati na nafasi ya tatu ya Tuzo ya Mwajiri Bora wa Ndani. Ushindi huo wa tuzo nne, umeiwezesha MeTL Group kuwa moja ya kampuni nne ambazo zimeshinda tuzo nyingi za ATE 2017, na kuwa kampuni ya kizalendo ambayo imeshinda tuzo nyingi kuliko kampuni zingine ambazo zimeshiriki katika tuzo hizo.
Kutoka kushoto ni Mkuu wa kitengo cha Rasilimali Watu wa kampuni ya Royal Soap, Jackline Mbaga, Mkuu wa kitengo cha Rasilimali Watu wa kampuni ya Star Oil Tanzania Limited , Ester Dotto, Meneja Mkuu wa Mo Assurance Limited, Kura Bonniface, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Mohammed Enterprises, Hassan Dewji, Meneja Mauzo na Mkuu wa kitengo cha Rasilimali Watu wa kampuni ya 21st Century Holding Limited, David Mziray, Ofisa wa kitengo cha Rasilimali Watu wa Mohammed Enterprises, Jessica Julius, Mkuu wa kitengo cha Rasilimali Watu wa kampuni ya 21st Century Textiles, Godfrey Ndimbo na Mkuu wa kitengo cha Rasilimali Watu wa kampuni ya 21st Century Food and Packaging, Anna Zongo wakiwa na tuzo nne ambazo wameshinda kwenye tuzo za ATE 2017.
Akizungumza kuhusu ushindi huo, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa MeTL Group, Hassan Dewji, alisema wamefurahishwa na ushindi huo, lakini pia unaonyesha jinsi gani kampuni inafanya vizuri katika soko la hapa nchini. "Tuna furaha kushiriki kwenye tuzo za ATE 2017 na tuna furaha kushinda tuzo nne, naamini tumekuwa moja ya kampuni tano ambazo zimeshinda tuzo nyingi. Nafikiri sisi ni moja ya kampuni kubwa nchini na tunaendelea kukua na kugusa maisha ya watu wengi kila siku, ushindi kama huu utuwezesha kuongeza juhudi zaidi," alisema Dewji.

NAIBU WAZIRI MADINI ATEMBELEA MACHIMBO YA JASI MKOANI SINGIDA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 




Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo hapo jana alifanya ziara kwenye machimbo ya Jasi (Gypsum) ya Mkoani Singida na kuzungumza na Wafanyabiashara na Wachimbaji wa Madini hayo ambapo aliwahakikishia ushirikiano wa dhati wa kufikia malengo waliyojiwekea.
Alitembelea maeneo ya machimbo ya Madini ya Jasi na Viwanda vidogo vya uongezaji thamani ya madini hayo ikiwemo viwanda vya kusaga madini ya Jasi ambayo unga wake unasafirishwa nje ya Mkoa huo, viwanda vya kutengeneza chaki vilivyopo Itigi na kiwanda cha utengenezaji wa mapambo ya majumbani kilichopo Singida Mjini.
Naibu Waziri Nyongo yupo Mkoani Singida kwenye ziara ya siku Tatu ya kutembelea maeneo mbalimbali ya uchimbaji wa madini Mkoani humo ili kujionea shughuli zinazofanywa kwenye maeneo hayo na kuzungumza na wachimbaji wa madini ili kubaini changamoto zinazowakabili kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wake.
Kwa mujibu wa wachimbaji wa madini hayo, Madini ya Jasi hutumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kutengenezea chaki, hospitalini kwa watu waliovunjika na kutengeneza viungo bandia, kutumika kutengenezea saruji, urembo majumbani, hutumika kama insulation kwenye majengo makubwa kwa kuwa Jasi huzuia moto, kutengenezea midoli na masanamu, kutengeneza meno bandia na pia hutumika kama mbolea
 

TUNAZO RASILIMALI NYINGI LAKINI BADO KUNA HALMASHAURI ZINALALAMIKA HAKUNA MAPATO; DKT NCHIMBI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amezitaka halmashauri za Mkoa wa Singida kuacha kulalamika kukosa mapato bali watumie vizuri rasilimali nyingi zilizopo, ambazo zikitumika vizuri zinaweza kuongeza mapato yao.
Dkt Nchimbi ametoa kauli hiyo mapema leo wakati akifungua mafunzo ya kutambua fursa na vikwazo kwa ajili ya kupanga miradi ya maendelo kwa jamii (O&OD) yaliyoandaliwa na ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kwa watendaji wa halmashauri zote za mkoa wa Singida.
Amesema Mkoa una fursa nyingi katika sekta ya kilimo, utalii, ufugaji, madini na uvuvi ambazo bado hazijatumiwa vizuri na halmashauri katika kukuza uchumi wa viwanda kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa wa Singida.
“Singida ina zalisha Vitunguu vingi na bora nchini, ina zalisha viazi zitani vingi na vyenye ubora, singida pia ni mzalishaji mkubwa wa alizeti na mafuta ya alizeti huku tukiwa na viwanda zaidi a 120 vya kusindika mafuta ya alizeti, katika sekta ya utalii tuna vivuti vngi ikiwemo bwawa la kuongelea ‘swimming pool’ lililojengwa na mjerumani na lipo katikati ya pori lakini vyote hivi hatujavitumia vizuri,” amesisitiza Dkt Nchimbi.
Dkt Nchimbi ameongeza kuwa halmashauri zinapaswa kutotumia mafunzo hayo kulalamika bali mafunzo hayo yawajengee uwezo wa kutambua wapi kuna pengo katika maendeleo ya jamii na kisha kuanisha fursa na mikakati ya kuzitumia fursa hizo kuziba pengo hilo.
Aidha amewataka kutumia fursa ya malengo na mitazamo waliyonayo ambayo inaweza kuleta maendeleo pamoja na kuhakikisha kuwa mafunzo hayo yanawajengea uwezo wa kubaini na kuitumia ajenda ya fursa na vikwazo katika maendeleo kwa ngazi zote.
Dkt Nchimbi amesema matarajio yake ni kuona kila mshiriki wa mafunzo hayo ana mabadiliko ya tabia katika utendaji wake ambapo mabadiliko hayo yanaweza kupimika aidha kwa macho au viashiria vingine.
Ameongeza kuwa matarajio ya mengine ni kuwa na Singida mpya yenye takwimu sahihi za bidhaa zote zinazozalishwa Mkoani Singida ili kuzitumia takwimu hizo katika kupanga mikakati ya maendeleo pamoja na kutangaza fursa zote zilizopo Mkoani hapa.
Dkt Nchimbi ameeleza kuwa mafunzo hayo wamepatiwa ili kutatua changamoto zilizopo na endapo kutaendelea kuwepo kwa changamoto hizo katika sekta mbalimbali ikiwemo za kilimo, afya, maji, elimu, barabara na utawala bora basi tumi nzima ya fursa na vikwazo itakuwa imeshindwa.

DKT NCHIMBI ASHAURI WAHADZABE WAPEWE AJIRA ZA MUDA KUPITIA TASAF.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi ameshauri Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) uanzishe kazi za ajira za muda, kwa walengwa wa Mpango huo kutoka jamii ya Wahadzabe waliopo Wilayani Mkalama ili uwasaidie kuinua uchumi wao.
Dkt Nchimbi ametoa ushauri huo mara baada ya kutembela kijiji cha Singa Wilayani Mkalama na kuona bwawa litakalotumika kuhifandhi maji ya mvua kwa ajili ya shughuli mbalimbali lililojengwa na walengwa wa Tasaf Kijijini hapo kisha kutembelea kijiji cha Munguli Kata ya Mwangeza Wilayani  humo aliposhuhudia malipo ya walengwa wa kihadzabe wa Mpango wa Tasaf.
Ameeleza kuwa jamii ya wahadzabe hawana mradi unaohusisha kazi za ajira za muda ambazo zimekuwa zikisaidia katika kuongeza kipato, kuwafundisha thamani ya kazi pamoja na kutekeleza miradi ambayo imekuwa ikisaidia jamii nzima kama vile mabwawa na  barabara.
“Nashauri TASAF kabla ya msimu huu wa mvua kuisha muwaletee na hawa wahadzabe mradi wa ajira za muda kama ambavyo walengwa wa vijiji vingine wamekuwa wakifanya kazi hizo na zimekuwa zikichangia maendeleo kwa vijiji vyao”, ameeleza na kuongeza kuwa,
“Miradi ya ajira za muda zitawafundisha Wahadzabe kujituma kufanya kazi ambazo zinachangia maendeleo ya jamii huku kazi hizi zikiwa kama darasa la wao kujifunza kwa vitendo kuwa kama anaweza kwa mfano kushiriki kujenga bwawa basi anaweza kufanya jambo kubwa katika familia au maisha yake”, amesisitiza Dkt Nchimbi.
Aidha ametoa tahadhari kwa walengwa hao wa kihadzabe kuwa wasitumie pesa wanayopewa kwa kunywa pombe badala yake pesa hiyo itumike sawasawa na maelekezo ya mpango huo na hatua zichukuliwe kwa wale watakaokaidi.
Kwa upande wake Afisa Ufuatiliaji Kutoka Tasaf Makao Makuu Anna Njau ambaye aliambatana na Mkuu wa Mkoa Dkt Nchimbi katika ziara yake ameeleza kuwa ushauri huo ni mzuri na una lengo la kuwasaidia wananchi kama ambavyo Tasaf imekuwa na lengo la kuinua jamii hasa kaya masikini hivyo wazo hilo ataliwasilisha makao makuu kwa ajili ya utekelezaji.
Baadhi ya wahadzabe waliofika kupokea fedha za Mpango wa Tasaf wameeleza kuwa fedha hizo zimewasaidia kuwainua kiuchumi kwa kuhakikisha wana chakula cha kutosha, watoto wameenda shule, watoto wadogo wamepelekwa kliniki huku wakijiendeleza zaidi kiuchumi kwa ufugaji mdogo wa kuku na mbuzi pamoja na kuboresha makazi yao.
Jamii ya Wahadzabe waliopo Kijiji cha Munguli na hasa kitongoji cha Kipamba Wilayani Mkalama wamekuwa wakiishi kwa kutegemea uwindaji wa wanyama pori, kula asali, ubuyu, matunda na mizizi mbalimbali ambapo juhudi za Serikali kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (Tasaf) umesaidia jamii hiyo kuanza kupeleka watoto shule, kuanzisha shughuli za uzalishaji mali kama vile kilimo na ufugaji.

ILI KUPUNGUZA AJALI BARABARANI; MADEREVA WAHIMIZWA KUJIUNGA NA CHUO KIKUU HURIA SINGIDA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 



Madereva wa vyomo vya moto hasa bajaji na bodaboda wamewahimizwa kujiunga na chuo kikuu huria ili waweze kujiendeleza kielimu na kuboresha huduma zao, ambapo kwa kufanya hivyo watasaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa ajali za barabarani. 

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi ametoa wito huo juzi wakati akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani yaliyofanyika kwenye kituo cha zamani cha mabasi cha Mjini Singida. 

Amesema masomo ya chuo kikuu huria humwezesha mtu kujiendelea kwa kupata elimu bora bila kuathiri shughuli zake za kila siku hasa za kujipatia kipato. 

“Dereva wa bodaboda, bajaji au mkazi yeyote mkoani kwetu, tusiridhike na elimu tuliyonayo, kumbukeni elimu haina mwisho. Hivyo tutumie chuo chetu hiki cha huria kujiendeleza kielimu. Tukiwa na wasomi wengi mkoa wetu kwa vyovyote   lengo la kuwa na uchumi wa kati na chini ya viwanda utalifikia kwa haraka”, amesema.

Dkt Nchimbi amwataka madereva wa vyombo vya moto kutii na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali na sio tu kuendeshwa na kamera za barabarani.

“Baadhi  ya madereva wa vyombo vya moto, hawaheshimu kabisa sheria za usalama barabarani, wanaendeshwa na  kamera. Siku moja yupo dereva mmoja wa bodaboda alikuwa mbele yangu, huku akiandika ujumbe kwenye simu yake. Utamaduni huu haufai kwa sababu ni chanzo cha ajali”,amesema Dkt.Nchimbi. 

Aidha amemtaka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP Debora Magiligimba kusimamia zoezi la madereva wa bajaji na bodaboda kujiunga na Chuo kikuu Huria. 

“Hebu angalia uwezekano wa kuanzisha mfuko maalumu kwa ajili ya madereva hawa kujiendeleza kielimu. Tunataka ifike siku tuwe na madereva hawa wana diploma au digrii, kwa hili nina imani na wewe utaweza kuwasaidia vizuri”, amesema.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amesema atagharamia safari ya viongozi wa madhehebu ya dini kwa kutoa kiasi cha shilingi laki tano, kwenda kufanya sala maalum kwenye maeneo yaliyokidhiri  kwa vitendo vya ajali. 

“Karibu kila wilaya ina eneo ambalo ajali haziishi kutokea mara kwa mara. Nina imani Mungu hajanipa mkoa wenye maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajali. Nimekubaliana na viongozi  wangu wa madhehebu ya dini wataenda katika maeneo hayo, na kuomba Mungu atuondolee balaa la ajali za barabarani kwenye maeneo hayo” amesema. 

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP Debora Magiligimba amewaagiza viongozi wa madereva wa bodaboda na bajaji, kusimamia vema madereva hao ili wapunguze ajali za barabarani. 

Mmoja kati ya wakazi wa Manispaa ya Singida, Njolo Kidimanda, amesema kuwa kuna haja  serikali kuongeza kiwango cha faini kwa madai kiwango kilichopo, hakiwaogopeshi kabisa  baadhi ya madereva.
Aidha, Kidimanda ameshauri madereva kuwa mstari wa mbele katika kuchangia damu salama, ili kusaidia majeruhi wa ajali barabarani wenye hitaji la damu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, jumla ya watu 68 wamefariki kutokana na ajali za barabarani kati ya Januari hadi Oktoba mwaka huu. Idadi hiyo imeonyesha kupungua kwa vifo vitokanavyo na ajali za  barabarani kwa kuwa katika kipindi hicho hicho mwaka jana, watu 152 walifariki.

WAZIRI MKUU MAJALIWA AHIMIZA MFUMO WA ELIMU YA JUU UANDAE RASILIMALI WATU ILI KUFIKIA TAIFA LA UCHUMI WA KATI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 



Picha/habari na Nathanieli Limu-Singida
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassimu Majaliwa Kassim amesema kuna haja ya kuangalia upya mfumo wa elimu ya juu nchini ili kuuboresha uweze kusaidia kutayarisha haraka rasilimali watu walioelimika  zaidi, watakaoliwezesha  taifa kuwa na maendeleo na kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema huyo jana wakati akizungumza kwenye kilele cha mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu huria cha Tanzania yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kanisa Katoliki mjini Singida. 
“Kwa kuzingatia malengo ya dira ya taifa ya maendeleo na mwelekeo wa serikali ya awamu ya tano, napenda nisisitize kuwa dira ya utendaji wenu ijikite katika maeneo yaliyoainishwa chini ya mwamvuli wa kauli mbiu ya chuo-elimu bora na nafuu kwa wote”, amesema. 
Amesisitiza kwa kusema kwa uchumi wa kati na wa viwanda, hauwezi kufikiwa au kuwa endelevu pasipo kuwa na kiwango cha udahili katika elimu ya juu cha angalau asilimia 23. 
“Hivi sasa kiwango cha Tanzania cha udahili katika elimu ya juu ni aslimia nne (4). Kiwango hiki ni kidogo hata kuliko nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambao licha ya hali ya vita nchini mwao kwa muda mrefu,wamefikia asilimia saba (7)”,amefafanua.
Waziri Mkuu Majaliwa amefafanua zaidi kwa kusema kuwa takwimu zinaonyesha kwamba karibu nchi zote washiriki katika jumuiya ya Afrika mashariki, ukiacha Burundi, zina viwango vya juu zaidi vya udahili katika elimu ya juu ikilinganishwa na kiwango cha Tanzania. 
Amesema kwa mujibu wa sera ya elimu ya mwaka 2014 mfumo wa elimu na mafunzo umetawaliwa na muundo wa kitaaluma wenye dhana ya kuchuja wahitimu kwa kila ngazi ili kupata wachache wenye uwezo mkubwa katika taaluma.
“Hali hii inatokana na nafasi za elimu na mafunzo ngazi za juu kuwa chache kadri wanafunzi wanavyohitimu kuanzia ngazi ya elimu ya msingi na kuendelea. Kwa uhaba wa nafasi za elimu ya juu na ufinyu wa bajeti ndio unaosababisha kutumia muundo wa kuchuja badala ule wa kutoa fursa kulingana na uwezo, vipaji na vipawa”, amesema na kuongeza;
“Huu ndio mfumo ambao unahitaji kuhuishwa na mfumo wa elimu huria na masafa kama alivyoeleza Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia Profesa Joyce Ndalichako kwamba mazingira, vigezo na masharti ya mchakato huu vimeainishwa katika sera ya elimu na mafunzo 2014’. 
Wakati huo huo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali inaunga mkono azma ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya kuanzisha dawati maalum kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa elimu huria na masafa.
“Kupitia hafla hii, ninaagiza dawati kama hili lianzishwe pia katika Tume ya vyuo vikuu (TCU) na Baraza la elimu ya ufundi (NACTE), kwa lengo la kuhakikisha kuwa taratibu zao za ithibati zinazingatia na kukidhi matakwa ya viwango vya mfumo wa elimu huria na masafa”, amesema.
Katika Mahafali hayo Mkuu wa Chuo Kikuu Huria na Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Peter Pinda amemtunuku shahada ya heshima ya uzamivu Balozi Nicolous Kuhanga ambaye mchango wake umetajwa kuwa mkubwa hasa wakati wa kuanzishwa kwa chuo hicho.
Zaidi ya wahitimu 2200 wamehitimu katika Chuo Kikuu hicho na kutunikiwa shahada mbalimbali ambapo mke wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Mama Mary Majaliwa, amekuwa miongoni mwa wahitimu akitunukiwa shahada ya uzamili katika Elimu ya Utawala, Mipango na Sera.

NAIBU WAZIRI TAMISEMI AZIAGIZA HALMASHAURI KUTUMIA ‘MAFUNDI WAZAWA’ KATIKA MIRADI MIDOGO; AFURAHISHWA NA MIRADI YA WILAYANI MKALAMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Joseph Kakunda akipima kiasi cha saruji kilichowekwa kwenye mchanga katika ujenzi shule ya Sekondari Iguguni Wilayani Mkalama katika ziara yake ya Siku moja kufuatilia utoaji huduma mbalimbali kwa jamii.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Joseph Kakunda akisisitiza jambo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhandisi Jakson Masaka (kulia kwake) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga (kushoto kwake).
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Joseph Kakunda akisalimiana na mwenyeji wake Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhandisi Jaksoni Masaka mara baada ya kuwasili wilayani humo kwa ajili ya Ziara ya ufuatiliaji wa miradi ya elimu na maji.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Joseph Kakunda akisalimiana na Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkalama Elizabeth Rwegasira mara baada ya kuwasili wilayani humo kwa ajili ya Ziara ya ufuatiliaji wa miradi ya elimu na maji.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Joseph Kakunda ameziagiza halmashauri zote nchini kutumia mafundi wa kawaida wazawa waliopo katika maeneo yao katika miradi yote midogo kupitia utaratibu unaojulika kama ‘force account’. Naibu Waziri Kakunda ametoa agizo hilo jana mara baada ya kufanya ziara Wilayani Mkalama kufuatilia utoaji wa huduma mbalimbali kwa jamii huku akijikita zaidi katika sekta ya Maji na Elimu, ambapo ametembelea mradi wa maji Iguguno na Shule ya Sekondari Iguguno.

“Matumizi ya Wakandarasi yabaki katika miradi mikubwa tu lakini miradi yote midogo tuwatumie mafundi waliopo katika maeneo yetu, mafundi hawa wazawa wanatekeleza kazi kwa ubora kama huu ambao nimeuona leo na kwa gharama ambazo ni nzuri,” amesisitiza mara baada ya kutoa agizo hilo. Ameeleza kuwa gharama na ubora wa mradi wa Shule ya Sekondari ya Iguguno ambao unajumuisha ujenzi na ukarabati wa madarasa 8, mabweni mawili, vyoo vyenye matundu 11, bwalo la chakula na maabara ambapo vyote hivyo vimegharimu milioni 416, unatosha kudhirihisha kuwa mafundi wa kawaida wazawa wanaweza kufanya kazi nzuri.

“Huu mradi endapo tungetumia utaratibu wa wakandarasi na wazabuni hiyo gharama ya milioni 416 ingekuwa kama robo ya gharama, nasisitiza wakandarasi na wazabuni watumike katika miradi mikubwa tu”, Naibu Waziri Kakunda amesisitiza.

Ameongeza kwa kuipongeza halmashauri hiyo kwa kutekeleza mradi mkubwa wa maji ambao umewezesha usambazaji wa maji katika kata yote ya Iguguno na kuwasaidia wananchi wasihangaike kupata maji. Aidha Naibu Waziri Kakunda ameonekana kutofurahishwa na taarifa kuhusu wanafunzi 12 waliokatishwa masomo tangu mwezi Januari Mwaka huu kutokana na sababu ya kupewa ujauzito, ambapo ametoa rai kwa wazazi na walezi wote nchini kuwa mstari wa mbele kukomesha tatizo hilo.

Ameeleza kuwa wazazi wengi wamekuwa wakifanya makubaliano ambapo mwanafunzi aliyepewa ujauzito anamkana mhalifu aliyempa ujauzito ili kumuepusha na kifungo cha miaka 30 jela, jambo linalofanya kesi nyingi kukosa ushahidi huku tatizo la mimba kwa wanafunzi likiendelea kuwepo.

Naibu Waziri Kakunda amesema ili kukomesha hilo serikali kupitia Wizara yake ina dhamira ya kupeleka hati ya dharula bungeni ili itungwe sheria itakayofuta dhamana ya mtuhumiwa atakayempa ujauzito mwanafunzi huku uchunguzi wa Vinasaba (DNA) utatakiwa kufanyika ili kuthibisha kama mtuhumiwa ndiye baba wa mtoto ama la.

Awali, Mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe. Alan Kiula amewasilisha changamoto mbalimbali za Wilaya hiyo kwa Naibu Waziri Kakunda kwa kumueleza changamoto kubwa ni kutokuwa na hospitali ya Wilaya.

Mhe. Kiula ameongeza kuwa upungufu wa watumishi katika Wilaya hiyo hasa wa Sekta ya Elimu na Afya umekuwa ukikwamisha baadhi ya shughuli kufanyika kwa kasi inayotakiwa.

Aidha amemshukuru Naibu Waziri Kakunda kwa ahadi yake ya kuitazama Wilaya hiyo kwa jicho la pekee katika mgao ujao wa watumishi kwa Mwezi Disemba na Januari huku akimuhakikishia kuwa Halmashauri itafanya kwa haraka taratibu za awali za upatikanaji wa eneo kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya.

BWANA HARUSI AFARIKI, MKEWE AJERUHIWA AJALINI WAKITOKA KUFUNGA NDOA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Imeandikwa na Abby Nkungu, Singida.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Debora Magiligimba
WATU 12 wamekufa na wengine 22 kujeruhiwa katika ajali iliyotokea kijiji cha Ighuka wilayani Ikungi kwenye Barabara Kuu ya Singida – Manyoni baada ya Toyota Hiace walimokuwa wakisafiria kutoka kumchukua bibi harusi kugongana uso kwa uso na Toyota Noah iliyokuwa imepakia watu kutoka msibani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Debora Magiligimba alisema kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa mbili usiku kwa kulihusisha gari lenye namba za usajili T 581 BBV iliyokuwa ikitokea Singida kwenda Manyoni na T 423 CFF iliyokuwa ikitokea Manyoni kwenda Singida.
Alisema kuwa ingawa uchunguzi wa kina juu ya chanzo cha ajali hiyo bado unaendelea, taarifa za awali zinaonesha kuwa sababu kuu ni mwendo kasi na uzembe wa madereva.
“Baadhi ya majeruhi walituambia dereva wa Toyota Hiace aliyekuwa anatoka Singida mjini alihama kutoka upande wake na kwenda upande wa pili wa barabara ambako aligongana uso kwa uso na Noah iliyokuwa imebeba watu waliokuwa wakitoka msibani na kusababisha vifo vya abiria 10 hapo hapo na majeruhi 24,” alisema.
Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa mkoa wa Singida, Dk Ng’hungu Kusenza alisema kuwa majeruhi wawili waliofikishwa Hospitali ya Misheni Puma kwa ajili ya matibabu pia walikufa hivyo kufanya idadi ya watu waliokufa kuwa 12.
Aliwataja waliokufa ambao miili yao imehifadhiwa Hospitali ya mkoa kuwa ni John Duma, Jasson Nsunza, Abubakar Omari, Mary Kinku, Mwanaidi Juma na Husna Juma, Wengine ambao miili yao imehifadhiwa Hospitali ya Misheni Puma wilayani Ikungi ni Ezekiel Joseph, Mussa Daniel, Namtaki Daniel, Hamis Omari, Jumanne Mganga na Wansola Shalua. Habari ambazo hazijathibitishwa zinadai kuwa Bwanaharusi na madereva wa magari yote mawili ni miongoni mwa watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo.
CHANZO HABARI LEO 

MIZAHA KATIKA MIRADI YA MAJI HAITAVUMILIWA MKOANI SINGIDA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Ofisi ya Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Singida imedhamiria kusimamia uboreshaji wa huduma za maji mkoani hapa huku mizaha itakayofanywa na mtu yeyote katika miradi ya maji, kutovumiliwa.

Kaimu Katibu Tawala Sehemu ya Maji Mkoa wa Singida Mhandisi Lyidia Joseph amebainisha hayo leo wakati wa kikao maalumu na Timu ya usimamizi wa sekta ya maji ya halmashauri ya Wilaya  ya Manyoni, kwa ajili ya kufuatilia usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maji.

Mhandisi Lydia amewaeleza wataalamu hao kuwa uongozi wa mkoa hautavumilia endapo kuna mtumishi yeyote atafanya mzaha katika kusimamia miradi ya maji kwakuwa mkoa umekuwa ukitoa ushirikiano wa kutosha hivyo hakuna sababu ya kushindwa kufanya vizuri.

“Sisi katika ngazi ya mkoa hatutavumilia mzaha katika masuala ya maji, tupo tayari kutoa ushirikiano popote mnapoona mnakwama ili tu tufikie malengo yetu ya kutoa huduma bora za maji kwa wananchi, hali ilivyo sasa hairidhishi kabisa, tufanye kazi kwa kasi zaidi”, ameongeza Mhandisi Lydia.

Amesema, halmashauri hiyo inapaswa kuhakikisha inatekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi la kuongeza asilimia ya upatikanaji wa maji katika halmashauri hiyo kutoka 45 hadi 72 ifikapo mwezi Juni, 2018 pamoja na kuandaa takwimu sahihi za upatikanaji wa maji ifikapo Disemba mwaka huu.

Mhandisi Lydia amefafanua kuwa halmashauri hiyo itaweza kuongeza asilimia ya upatikanaji maji na kufikia lengo la asilimia 72 endapo watendaji wote hasa wajumbe wa timu ya usimamizi wa sekkta ya maji, watashirikiana kusimamia ujenzi wa miradi mitano pamoja na ukarabati wa miradi minne iliyopo kwenye bajeti.

“Kila Mjumbe hapa ana kazi ya kufanya katika miradi hii ya Makanda, Nyaranga, Kikombo, Makutopola na Kicheho inayojengwa pamoja na ile ya Sanza, Mkwese, Londoni na Sorya inayokarabatiwa, Kitengo cha ugavi kisimamie taratibu za manunuzi zinafuatwa pamoja na kuhakiki ubora wa mkandarasi, mwanasheria aelekeze taratibu za kisheria, Maendeleo ya jamii ahakikishe wananchi wanaujua mradi vizuri, kila mmoja akitekeleza jukumu lake ipasavyo tutafikia lengo”, ameeleza na kuongeza kuwa,

“Idara ya maji msifanye siri miradi ya maji na kujifungia wenyewe hakikisheni timu hii ya usimamizi wa sekta yenu inafahamu vizuri miradi yote ya maji pamoja na kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo, mkifanya hivyo mtaenda kwa kasi na kazi itafanyika kwa ufanisi, sio kila kitu mfanye wenyewe tu”, ameongeza Mhandisi Lydia.

Aidha Mhandisi Lydia amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Charles Fussi kwa kujitoa kwake katika kusimamia na kutoa fedha za kusaidia miradi ya maji akitoa mfano wa kiasi cha milioni 16 zilizotolewa na mkurugenzi huyo kutoka katika makusanyo ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji.

Naye Mhandisi wa Maji kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Athanas Nziku ameieleza timu hiyo kuwa usimamizi wa jumuiya za watumia maji ni jambo muhimu kwakuwa takwimu zimeonyesha jumuiya hizo zimekuwa zikikusanya pesa nyingi sambamba na matumizi makubwa ya fedha wanazokusanya.

Mhandisi Nziku amewafafanulia kuwa jumuiya hizo za watumia maji zinapokusanya fedha nyingi sambamba na kutumia fedha nyingi ni moja ya kiashiria kuwa miradi hiyo ya maji inaweza kufa hivyo wazitembelee na kuona tatizo liko wapi endapo liko ndani ya uwezo wa halmashauri liweze kutatuliwa mapema.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mkwese na Mwenyekiti wa huduma za Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Robert Kenze amesema, halmashauri hiyo imedhamiria kuboresha huduma za maji ambapo ajenda ya maji imewekwa kipaumbele katika vikao vyote muhimu.

Kenze amesema wakuu wa Idara wa halmashauri hiyo watashirikiana na Idara ya maji wilayani humo huku wanasiasa wakiwa tayari kutoa elimu na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa