Ofisi
ya Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Singida imedhamiria kusimamia uboreshaji wa
huduma za maji mkoani hapa huku mizaha itakayofanywa na mtu yeyote
katika miradi ya maji, kutovumiliwa.
Kaimu
Katibu Tawala Sehemu ya Maji Mkoa wa Singida Mhandisi Lyidia Joseph
amebainisha hayo leo wakati wa kikao maalumu na Timu ya usimamizi wa
sekta ya maji ya halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, kwa ajili ya kufuatilia usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maji.
Mhandisi
Lydia amewaeleza wataalamu hao kuwa uongozi wa mkoa hautavumilia endapo
kuna mtumishi yeyote atafanya mzaha katika kusimamia miradi ya maji
kwakuwa mkoa umekuwa ukitoa ushirikiano wa kutosha hivyo hakuna sababu
ya kushindwa kufanya vizuri.
“Sisi
katika ngazi ya mkoa hatutavumilia mzaha katika masuala ya maji, tupo
tayari kutoa ushirikiano popote mnapoona mnakwama ili tu tufikie malengo
yetu ya kutoa huduma bora za maji kwa wananchi, hali ilivyo sasa
hairidhishi kabisa, tufanye kazi kwa kasi zaidi”, ameongeza Mhandisi
Lydia.
Amesema,
halmashauri hiyo inapaswa kuhakikisha inatekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa
wa Singida Dkt Rehema Nchimbi la kuongeza asilimia ya upatikanaji wa
maji katika halmashauri hiyo kutoka 45 hadi 72 ifikapo mwezi Juni, 2018
pamoja na kuandaa takwimu sahihi za upatikanaji wa maji ifikapo Disemba
mwaka huu.
Mhandisi
Lydia amefafanua kuwa halmashauri hiyo itaweza kuongeza asilimia ya
upatikanaji maji na kufikia lengo la asilimia 72 endapo watendaji wote
hasa wajumbe wa timu ya usimamizi wa sekkta ya maji, watashirikiana
kusimamia ujenzi wa miradi mitano pamoja na ukarabati wa miradi minne
iliyopo kwenye bajeti.
“Kila
Mjumbe hapa ana kazi ya kufanya katika miradi hii ya Makanda, Nyaranga,
Kikombo, Makutopola na Kicheho inayojengwa pamoja na ile ya Sanza,
Mkwese, Londoni na Sorya inayokarabatiwa, Kitengo cha ugavi kisimamie
taratibu za manunuzi zinafuatwa pamoja na kuhakiki ubora wa mkandarasi,
mwanasheria aelekeze taratibu za kisheria, Maendeleo ya jamii ahakikishe
wananchi wanaujua mradi vizuri, kila mmoja akitekeleza jukumu lake
ipasavyo tutafikia lengo”, ameeleza na kuongeza kuwa,
“Idara
ya maji msifanye siri miradi ya maji na kujifungia wenyewe hakikisheni
timu hii ya usimamizi wa sekta yenu inafahamu vizuri miradi yote ya maji
pamoja na kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo, mkifanya hivyo mtaenda
kwa kasi na kazi itafanyika kwa ufanisi, sio kila kitu mfanye wenyewe
tu”, ameongeza Mhandisi Lydia.
Aidha
Mhandisi Lydia amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Manyoni Charles Fussi kwa kujitoa kwake katika kusimamia na kutoa fedha
za kusaidia miradi ya maji akitoa mfano wa kiasi cha milioni 16
zilizotolewa na mkurugenzi huyo kutoka katika makusanyo ya ndani kwa
ajili ya ujenzi wa mradi wa maji.
Naye
Mhandisi wa Maji kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Athanas Nziku ameieleza
timu hiyo kuwa usimamizi wa jumuiya za watumia maji ni jambo muhimu
kwakuwa takwimu zimeonyesha jumuiya hizo zimekuwa zikikusanya pesa
nyingi sambamba na matumizi makubwa ya fedha wanazokusanya.
Mhandisi
Nziku amewafafanulia kuwa jumuiya hizo za watumia maji zinapokusanya
fedha nyingi sambamba na kutumia fedha nyingi ni moja ya kiashiria kuwa
miradi hiyo ya maji inaweza kufa hivyo wazitembelee na kuona tatizo liko
wapi endapo liko ndani ya uwezo wa halmashauri liweze kutatuliwa
mapema.
Kwa
upande wake Diwani wa Kata ya Mkwese na Mwenyekiti wa huduma za Jamii
wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Robert Kenze amesema, halmashauri
hiyo imedhamiria kuboresha huduma za maji ambapo ajenda ya maji imewekwa
kipaumbele katika vikao vyote muhimu.
0 comments:
Post a Comment