Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi (katikati) akimkabidhi
mmoja kati ya wa wakulima wa Pamba wa kijiji cha Kinyangiri Wilayani
Mkalama kilo kumi za mbegu za zao la pamba zilizotolewa bure na Serikali
kwa wakulima hao. Kushoto kwa Mkuu wa Mkoa ni Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Bodi ya Pamba nchini, Marco Mtunga.
Mkulima wa Pamba Bi Johari kutoka kijiji cha Kinyagiri Wilayani
Mkalama akibeba mbegu za Pamba kilo kumi alizokabidhiwa na Mkuu wa Mkoa
wa Singida Dkt Rehema Nchimbi, mbegu hizo zimetolewa bure kwa wakulima
wa Pamba Mkoa wa Singida.
Mama Devid Mkulima wa Pamba wa Kijiji cha Kinyangiri Wilayani Mkalama
akijifunza kwa vitendo namna ya kuandaa kamba inayotumika kuonyesha
vipimo vya upana na urefu katika kupanda pamba badala ya kilimo cha
mazoea cha kumwaga mbegu bila kufuata kipimo chochote.
Wakulima wa Pamba wa Kijiji cha Lyelembo Wilayani Mkalama
wakiwasikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi na Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Bodi ya Pamba nchini Marco Mtunga (hawapo pichani)
kabla ya kupewa mbegu za pamba zilizotolewz bure.
Wakulima wa pamba wa kijiji cha Kinyangiri Wilayani Mkalama
wakimfuatilia kwa makini mtaalam kutoka Bodi ya Pamba Nchini
akiwaelekeza namna ya kupuliza dawa ya kuuwa wadudu waharibifu wa pamba,
viuatilifu hivyo vitatolewa bure na serikali kwa wakulima wote wa pamba
Mkoani Singida.
Serikali
imeahidi kutoa bure pembejeo za kilimo kwa wakulima mbali mbali wa zao
la pamba mkoani Singida kuanzia msimu huu wa kilimo ikiwa ni moja ya
juhudi za kuhamasisha na kufufua kilimo hicho mkoani hapa.
Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Bodi ya Pamba nchini, Marco Mtunga ameeleza hayo
juzi katika vijiji vya Kinyangiri na Lyelembo wilayani Mkalama katika
siku ya kwanza ya ziara yake ya siku mbili kuhimiza Kilimo cha pamba
mkoani Singida.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi huyo, Kampuni ya Biosustain iliyopo mjini hapa
imepewa jukumu la kuleta na kusambaza mbegu na madawa yote yahusuyo
kilimo cha pamba bure na kwamba gharama ya pembejeo hizo italipwa na
Serikali.
Kutokana
na hilo, Mkurugenzi huyo amewataka Wakulima kutumia vyema fursa hiyo
kwa kulima mashamba makubwa zaidi lakini pia kwa kuzingatia tija na
ubora wa pamba.
Amesema
kuwa Wakulima wataweza kufanya hivyo tu iwapo pia watawatumia
kikamilifu wataalamu wao wa kilimo na kufuata Kanuni na Taratibu za
kilimo bora.
“Mmepewa
upendeleo maalum, kazi yenu sasa ni kulima tu, malipo ya mbegu na
viuatilifu vyote italipwa na Serikali. Hapa hakuna kisingizio cha
kushindwa kulima”, amesema Mtunga na kuongeza;
“Pandeni
vizuri ili wakati mnatumia dawa, kiwango kikubwa cha dawa kisipotee
bure maana kama hukupanda kwa mstari lazima kutakuwa na ugumu wa
kupulizia mimea yako. Jengeni utamaduni wa kuwatumia wataalamu wa kilimo
kama ilivyo kwa wafugaji mifugo yao inapopatwa na maradhi”.
Aidha,
amewataka wakulima wa zao hilo kuhakikisha wanang'oa masalia yote ya
misitu ya pamba na kuichoma moto kwa kuwa, kwa kuacha kufanya hivyo
wanaruhusu wadudu waliomo kwenye masalia kuendelea kunenepeana na hivyo
kuhatarisha mazao mapya yanayopandwa.
Mkurugenzi
huyo amewasihi wakulima kuacha kuchanganya kilimo cha pamba na mazao
mengine akisema kuwa tafiti zinaonesha pamba iliyochanganywa na mazao
mengine hutoa vitumba vitatu tu ikilinganishwa na vitumba 10 kwa kilimo
cha pamba iliyolimwa peke yake.
Wakulima
wa zao hilo wamemueleza Mkurugenzi huyo kuwa, moja ya sababu za kushuka
kwa uzalishaji pamba kwenye maeneo yao ni pamoja na bei kuwa ndogo kwa
kisingizio cha Soko la Kimatafa kushuka na kuchezewa mizani wanazotumia
kupima mazao yao, hali inayowapunja kimapato.
Hata
hivyo, wamejibiwa kuwa suluhisho la kuchezewa mizani lipo mikononi mwao
ili mradi tu wajenge tabia ya kuhoji mara moja wanapoona mambo yanaenda
isivyo badala ya kusubiri hadi siku ya vikao.
Wakati
huohuo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amewataka watendaji
wote wa serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Singida kulima
ekari moja ya pamba kila mmoja ili kuamsha hamasa kwa wananchi wengine.
Dkt
Nchimbi ameongeza kwa kuwataka watendaji hao kuliweka zao la pamba kama
ajenga katika vikao vyao, huku akiwataka viongozi wa dini na vikundi vya
kwaya kuonyesha mfano kwa kulima vizuri pamba.
Ameongeza
kuwa vijana wanaocheza vijiweni ‘pooltable’ waache mara moja na
kujikita katika kilimo cha pamba kwa kuwa ni chanzo kikubwa na cha
uhakika cha kujipatia fedha na hivyo kuchangia kukuza uchumi.
Aidha
amewataka wakulima wa pamba kuwasikiliza wataalamu na sio kupanda kwa
mazoea huku akishauri kuwa mikutano yote inayohusu kilimo cha pamba
ifanyike katika mashamba ya wakulima.
Dkt Nchimbi ameeleza kuwa kauli mbiu mpya ya kilimo cha pamba kwa Mkoa wa Singida ni, ‘Singida Mpya, kwa Pamba yenye Tija’.
0 comments:
Post a Comment