WATU SITA WASHIKILIWA NA POLISI MKOANI SINGIDA KWA KUKUTWA POMBE BANDIA AINA YA VIROBA VYA JOGOO NA KONYAGI.




Kamanda wa polisi mkoa wa Singida ACP Linus Sinzumwa.
Na Nathaniel Limu. 
Jumla ya watu sita wakiwemo wakazi wawili wa jijini Dar-es-salaam, wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Singida kwa tuhuma ya kupatikana na kiasi kikubwa cha pombe kali aina ya viroba vya jogoo/konyagi inayosadikika kuwa ni bandia.
Watuhumiwa hao ni Hagai Mwalumile (38), Yusuph George (28), Geofrey Mushi (45) na mmoja mwenye umri wa miaka 17 ambaye bado hajatambuliwa jina lake.
Watuhumiwa hao wote ni wakazi wa Mitunduruni mjini Singida.
Watuhumiwa ambao ni wakazi wa jijini Dar-es-salaam ni Mohammed Rashid (42) na Richard Leonard (32).
Kamanda wa polisi mkoa wa Singida ACP Linus Sinzumwa, amesema watuhumiwa hao kwa pamoja wamekamatwa Septemba 22 mwaka huu eneo la Unyankindi kata ya Mitunduruni mjini Singida, kwenye nyumba ya mtuhumiwa Godfrey Mushi.
Kamanda Sinzumwa amesema nyumba ya mtuhumiwa Godfrey Mushi, inasadikika kuwa iligeuzwa na kuwa kiwanda maalum kwa ajili ya kutengeneza pombe kwa njia ya kienyeji.
Amesema kuwa ndani ya nyumba hiyo, kumesimikwa mtambo wa kutengeneza kienyeji viroba vya pombe aina ya jogoo na konyagi bandia, ambayo ni hatari kwa maisha ya binadamu.
Kamanda huyo ametaja bidaa iliyokamatwa kuwa ni katoni 49 za viroba, katoni 6 za konyagi kila moja ikiwa na pakiti na majiko ya manne ya mchina 4.
Ametaja bidhaa zingine kuwa ni sprit lita tatu na nusu, vyuma vya ku-sealed 11, soletape 4, marker  pen 6, mkasi moja, outer tupu za konyagi 1,561, outer tupu za viroba 235, katoni tupu za konyagi 12 na pamba bunda tatu.
Kamanda huyo amesema kuwa watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wo wote upelelezi utakapokamilika. 

DC AHIMIZA UJENZI WA MAABARA

Na Nathaniel Limu, Singida

SERIKALI ya Wilaya ya Singida, imewaagiza wakazi wa Manispaa ya Singida, kuunganisha nguvu zao pamoja kuchangia ujenzi wa maabara katika shule zote za sekondari za kata.

Kasi na nguvu zilizotumika kujenga shule za sekondari za kata, ziongezeke zaidi ili ifikapo Oktoba 20, mwaka huu, majengo ya maabara yawe yamefikia hatua nzuri ya kupauliwa.

Agizo hilo, limetolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Queen Mlozi, wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Utemini.

Alisema, suala la ujenzi wa maabara ni muhimu, wakati huu wa dunia ya sayansi na teknolojia.

Alisema wazazi na walezi, lazima watambue hilo, ili waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa maabara mahali watoto wao, watajifunza kwa vitendo masuala ya sayansi.

“Tuanze na majengo kwanza, mambo mengine kama ya vifaa na huduma ya umeme, hayo yatafuata baadaye,” alisema mkuu huyo wa wilaya.

Alisema jengo la maabara, likiwepo ni rahisi mno kupatiwa vifaa au msaada wa kuunganishiwa umeme.

Alisema kata zitakazowahi kuanza ujenzi wa maabara na kufikia hatua nzuri ya kupaua kabla ya Oktoba 20, mwaka huu, ataziunga mkono kwa kuzisaidia fedha.

“Kwa hapa kwenu Utemini, nyie andaeni tu siku ya kufanya harambee ya kuchangia ujenzi wa maabara, mimi nawaahidi nitakuja pamoja na wadau wa maendeleo, ili kwa pamoja tuje tuwaunge mkono,” alisema Mlozi.

Kuhusu ombi la kuipatia shule hiyo umeme na barabara bora, aliahidi kulifanyia kazi mapema iwezekanavyo.

DC Mlozi, yupo kwenye ziara ya kujitambulisha kwa wakazi wa Manispaa ya Singida, kuhimiza ujenzi wa maabara na ujenzi wa vyumba vya madarasa, kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza mwakani.

Halmashauri ya Manispaa ya Singida, ina jumla ya shule za sekondari 17, zikiwemo za Serikali na tatu za madhehebu ya dini na watu binafsi. Kati ya shule hizo, tatu tu ndizo zenye maabara.
Chanzo: Mtanzania

SINGIDA KUENDESHA ZOEZI LA KUBAINI WANAONG’OA ALAMA ZA BARABARANI



Na Nathaniel Limu
MKOA wa Singida unakusudia kuendesha zoezi maalumu la ukaguzi wa magari na pikipiki, ili kuwabaini watu wanaong’oa alama za usalama barabarani na kuzifunga kwenye vyombo vyao.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Singida, Queen Mlozi, katika hotuba yake ya kuhadhimisha kilele cha wiki ya nenda kwa usalama barabarani, iliyofanyika kwenye uwanja wa Namfua mkoani hapa.

Alisema pamoja na uzembe wa madereva, mwendo kasi, ulevi na elimu duni ya usalama barabarani, sababu nyingine ya ajali nyingi kutokea ni kutokuwepo kwa alama muhimu za usalama barabarani.

DC Mlozi, alisema uchunguzi unaonesha wazi kuwa, nyingi ya alama hizo ikiwemo viakisi mwanga hung’olewa na kufungwa kwenye magari na pikipiki za watu binafsi.

"Tabia hii hatutaivumilia hata kidogo, tumeandaa mkakati wa kuhakikisha wizi wa aina hiyo unakoma kabisa, ili kupunguza matukio ya ajali ambayo yanagharimu maisha ya Watanzania na mali zao," alisema.

Takwimu zinaonesha kuwa, katika kipindi cha Januari hadi Agosti mwaka huu, jumla ya watu 83 wamekufa na wengine 192 kujeruhiwa kutokana na ajali 158 mkoani Singida.
Chanzo: Mtanzania

WAZAZI WAKERWA NA ‘VI-MINI’ VYA WANAVYUO SINGIDA, WASHITAKI KWA DC

Mwandishi wetu, Singida Yetu
WAZAZI katika halmashauri ya Manispaa ya Singida wamelalamikia mavazi yanayovaliwa na wanafunzi wa vyuo vya uhazili na uhasibu  vilivyopo katika  mji wa Singida kwa madai  kuwa  yanachangia kuharibu  na kuleta  mmomonyoko wa maadili  kwa  watoto.

Wakizungumza kwenye viwanja vya shule ya Sekondari ya Utemini katika kikao  chao na mkuu wa  wilaya ya  Singida  bibi Queen Mlozi,  wazazi hao wamesema mavazi  ya wanachuo hao yamekuwa kero  na kusababisha  mmomonyoko wa maadili kwa jamii.

Wamedai kuwa  baadhi  ya wanafunzi  wa  kike katika  vyuo  hivyo wanavaa nguo  fupi   sana  kinyume na maadili ya kitanzania   ambazo zinaweza  kuwa kuchochea vitendo vya ngono.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Singida  bibi Mlozi  amesema ingawa hata yeye ameliona tatizo lakini ni  vyema ikaeleweka kuwa  hizo ni athari za utatandawazi na ni  vigumu kuzizuia.

Hata  hivyo  mkuu huyo  wa wilaya ya Singida ameahidi kukutana na walimu na  wanafunzi wa vyuo hivyo ili  kuzungumzia tatizo hilo  na kujaribu kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.
Blogzamikoa 

AFUNGWA MIAKA 60 JELA KWA KOSA LA UNYANG’ANYI NA KUBAKA

Mwandishi wetu, Singida Yetu
MAHAKAMA ya hakimu mkazi mjini Singida imemhukumu mwanaume mmoja   kifungo cha miaka 60 jela baada ya kumtiwa hatiani kwa makosa ya unyang’anyi na kubaka.
Aliyekumbwa na adhabu hiyo ametajwa kuwa Omari Msawila (50) mkazi wa eneo la Minga  katika Manispaa ya Singida.

Mapema mwendesha mashitaka Geofry Luhanga alidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo siku ya disemba 30 mwaka jana majira ya saa 6.15 usiku huko maeneo ya Karakana Singida mjini
Mbele ya hakimu Chiganga Tengwa   wa mahakama hiyo ilidaiwa kuwa mshitakiwa akiwa na wenzake ambao hadi sasa hawajakamatwa walivunja nyumba ya mtu mmoja kisha kuingia ndani.
Ililelezwa kuwa   mshitakiwa na wenzake walinyang’anya shilingi 90,000 taslimu pamoja na mali mbalimbali ikiwemo madebe matatu ya mahindi kisha kumbaka mke wa mlalamikaji kabla ya kutoweka.
 Akitoa hukumu hiyo, hakimu Tengwa amesema kutokana na kuridhishwa  bila kuacha shaka lolote na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka, mshitakiwa atatumikia  kifungo cha miaka 30 jela kwa unyang’anyi na miaka mingine kama hiyo kwa kosa la kubaka.
Blogzamikoa

SERIKALI YA SINGIDA YAZITAKA MANISPAA KUCHANGIA UJENZI WA MAABARA ZA SHULE ZA KATA.




Mkuu wa wilaya ya Singida Mwalimu Queen Mlozi, akizungumza na wananchi wa kata ya Utemini manispaa ya Singida akihamasisha ujenzi wa maabara katika shule za sekondari za kata na kujitambulisha.


Diwani wa kata ya Utemini CCM jimbo la Singida mjini Baltazar Kimario, akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya sekondari kata ta Utemini. Mkutano huo ulitumika kwa Mkuu wa Wilaya Mlozi kuhamasisha ujenzi wa maabara.
 
Baadhi wa wakazi wa Utemini mjini Singida waliohudhuria mkutano wa hadhara ulioitishwa kwa ajili ya mkuu wa wilaya ya Singida Queen Mlozi, kuhimiza ujenzi wa maabara.
Mkuu wa wilaya ya Singida,mwalimu Queen Mlozi (wa kwanza kushoto) akishiriki kutoa burudani na kikundi cha uhamasishaji cha nyota njema cha Utemini, kwenye mkutano wa hadhara.(Picha na Nathaniel Limu).
 Serikali  ya wilaya ya Singida imewaagiza  wakazi wa manispaa ya Singida, kuunganisha nguvu zao pamoja kuchangia ujenzi wa maabara katika shule zote za sekondari za kata.
Kasi na nguvu zilizotumika kujenga shule za sekondari za kata, zimetakiwa ziongezeke zaidi ili ifikapo oktoba 20 mwaka huu, majengo ya maabara yawe yamefikia  katika hatua nzuri ya kupauliwa.
Agizo hilo limetolewa na mkuu wa wilaya ya Singida Mwalimu Queen Mlozi, wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Utemini jimbo la Singida mjini.
Amesema suala la ujenzi wa maabara ni muhimu mno katika wakati huu wa dunia ya sayansi na teknolojia.
Mlozi amesema wazazi na walezi ni lazima watambue hilo, ili waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa maabara mahali watoto wao, watajifunza kwa vitendo masuala ya sayansi. 
Mo Blog

MBALI NA KASORO NDOGO MTIHANI WA DARASA LA SABA SINGIDA WAANZA VYEMA.



Na.Nathaniel Limu-Singida.
Mtihani  wa kumaliza elimu ya msingi unaohusisha wanafunzi 27,749 wa darasa la  saba mkoani Singida umeanza kwa amani na utulivu licha ya  kujitokeza kwa kasoro ndogondogo.
Miongoni mwa kasoro hizo ni pamoja na  utoro, baadhi ya wanafunzi kutojua  kusoma na kuandika na walimu na wasimamizi kulalamikia mfumo wa maswali ya kuchagua na kuweka vivuli.
Katika  shule ya msingi  Mtisi  iliyopo umbali wa zaidi ya kilomita 24 kusini magharibi mwa mji wa Singida, wasimamizi  wa mtihani huo wamesema kati ya 34 watahiniwa nane (8) hawakufanya mtihani kutokana na utoro na wengine sita wameshindwa kusoma wala kuandika.
Hata  hivyo afisa elimu mkoa wa Singida  Yusuf  Kipengele, amesema mbali ya kasoro hizo  hakuna dosari nyingine kubwa iliyojitokeza na kuathiri ufanyaji huo wa mtihani ulioanza leo.
Kipengele ametoa wito kwa wasimamizi  wa mtihani  huo kuwa waadilifu na kutojihusisha na udanganyifu vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria pindi watakapobainika. 

WAHAMIAJI HARAMU WATANO KUTOKA ETHIOPIA WANASWA NA POLISI MKOANI SINGIDA.



Kamanda wa polisi mkoa wa Singida ACP Linus Sinzumwa akitoa taarifa ya wahamiaji haramu kutoka Ethiopia kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha).Picha na Nathaniel Limu.
Jeshi la polisi mkoa wa Singida linawashikilia rai watano wa nchini Ethiopia kwa tuhuma ya kuingia na kuishi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila ya kuwa na kibali.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa polisi mkoa wa Singida ACP Linus Sinzumwa, ameisema wahamiaji hao haramu, wamekamatwa septemba 18 mwaka huu saa kumi jioni wakiwa ndani ya nyumba ya kulala wageni ya Singida Modern iliyopo Kibaoini.
Sinzumwa amesema kuwa rai hao ambao bado haijajulikana wameingia wapi na walikuwa wakielekea nchi gani, wamekamatwa baada ya raia wema kutoa taarifa polisi.
Kamanda Sinzumwa amesema kuwa hivi sasa vijana hao kutoka Ethiopia, wanaendelea kuhojiwa na maafisa wa uhamiaji na mara mahojiano hayo yatakapomalizika, watuhumiwa watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayowakabili.  
Mo Blog 

SACCOS 7 MKOANI SINGIDA ZAFANIKIWA KUPATA MIKOPO YENYE THAMANI YA SHILINGI BILIONI 1.4 KUTOKA CRDB.


Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi vyeti kwa viongozi wa SACCOS saba za mikoa ya Singida na Manyara. Vyeti hivyo vimetolewa na mfuko wa uwezeshaji (Wananchi Empowement Fund) baada ya SACCOS hizo kufanikiwa mikopo ya thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.4.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt.Parseko Kone akikabidhi cheti kwa viongozi wa SACCOS ya Jipe Moyo ya kata ya Kinyangiri wilayani Mkalama.
Katibu Mtendaji wa baraza la taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi Dk. Anacleti Kashuliza akitoa taarifa yake kwenye hafla ya kukabidhi vyeti kwa SACCOS saba za mkoa wa Singida na Manyara. Wa kwanza kushoto ni mkuu wa mkoa wa Singida na wa kwanza kulia ni mkuu wa wilaya ya Singida Queen Mlozi. 
Meneja mikopo wa CRDB tawi la mkoa wa Singida Mbwana Hemed akitoa salamu zake kwenye hafla ya kukabidhi vyeti kwa SACCOAS saba za mkoa wa Singida na Manyara.
Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria hafla ya kukabidhi vyeti kwa SACCOS za mkoa wa Singida na Manayara. Wa kwanza kushoto ni Halima Jamal wa gazeti la Tanzania Daima akifuatiwa na Abbya Nkungu wa Habari Leo na Daily News pia ni Katibu wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Singida. Wa kwanza kulia ni Elisante John wa Radio Cluods na Nipashe na wa pili kulia ni Awilla Sila wa Mwananchi na The Citizen.
Baadhi ya viongozi wa SACCOS za mkoa wa Manyara na Singida, wakipata ‘msosi’ muda mfupi baada ya kukabidhiwa vyeti na mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone.(Picha na Nathaniel Limu).
Na. Nathaniel Limu
Benki ya CRDB tawi la mkoa wa Singida imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi biloni 1.4 kwa SACCOS saba za mkoa wa Singida na Manyara.
Akizungumza kwenye hafla ya utoaji wa vyeti kwa SACCOS za mikoa ya Manyara na Singida zilizopta mikopo kutoka mfuko wa uwezeshaji (Mwananchi Empowerment Fund), Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone amesema SACCOS nne za mkoa wa Singida, zimekopeshwa zaidi ya shilingi milioni 255.5 sawa na aslimia 3.32 ya fedha hizo, wakati SACCOS tatu za mkoa wa Manyara zenyewe zimekopeshwa zaidi ya shilingi bilioni 1.2.
Kuhusu marejesho, Dkt. Kone amesema hadi kufikia Julai 31 mwaka huu, kiwango cha urejeshaji kilifikia aslimia 94.4.Kwa upande wa mkoa wa Singida pekee, kilifikia asilimia 91.7.
 Amesema hata hivyo ipo tatizo la urejeshaji kwa SACCOS ya Kumekucha ya Itigi Manyoni ambayo ilikopeshwa jumla ya shilingi 84,472,000.
Fedha hizo  zilipaswa ziwe zimerejeshwa kabla ya Agosti 31 mwaka huu, lakini hadi  sasa SACCOS hii inadaiwa shilingi 21,168,000 ambazo ni asilimia 25 ya mikopo iliyotolewa kwa mkoa wa Singida.
Dkt .Kone amesema mbaya zaidi ni kwamba wengi wa viongozi  wa SACCOS hiyo ni miongoni mwa wadaiwa sugu wa mikopo hiyo.
SACCOS za Lusilille  na Tumaini za Manyoni na Jipe moyo ya Iramba zilishamaliza kurejesha mikopo yao.
Kwa upande wao viongozi wa SACCOS hizo wameomba muda wa kurejesha mikopo uongezwe zaidi ili waweze kupata muda wa kutosha kupata faida ya itakayotosheleza  kulipa mikopo na kubakiwa na akiba ya kukidhi mahitaji.
MO BLOG
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa