Abiria wapatao 15 walijeruhiwa kutokana na taharuki iliyotokea baada ya kichwa cha treni kimoja kati ya viwili vilivyokuwa vinapandisha treni ya abiria kushika moto kati ya maeneo ya Stesheni za Saranda na Manyoni jana Septemba 8, 2012 majira ya saa moja jioni. Taharuki hiyo ilisababisha abiria kuanza kuruka nje pamoja na kukanyagana.
Majeruhi wanane waliruka kutoka behewa lililokuwa karibu na vichwa vya treni wakati wengine saba walitoka katika mabehewa mengine 14.
Hali hiyo iliweza kudhibitiwa pale Dereva na wasaidizi wake walipofanikiwa kusimamisha treni na kutenganisha vichwa hivyo na mabehewa ya abiria ambapo kichwa kilichokuwa kimeshika moto kilikokotwa hadi stesheni ya Manyoni mnamo saa 01:15 usiku. Baada kufanikiwa kukizima kichwa kilichokuwa kinawaka saa 1:45 usiku kichwa kizima cha treni kilirejea eneo la tukio na kuyavuta mabehewa ya abiria na kuwasili Stesheni ya Manyoni saa 3:15 ambako uhakiki wa abiria waliojeruhiwa ulifanyika.
Abiria 15 waliojeruhiwa walikimbizwa hospitali ya Manyoni ambako baada ya uchunguzi abiria wawili walikutwa na majeraha makubwa. Majeruhi hao wametambuliwa kwa majina kuwa Bwana Batholomew Raphael aliyevunjika mkono wa kushoto na Bibi Sikujua Mtonzi aliyevunjika mguu wa kulia. Majeruhi hawa wamehamishiwa hospitali kuu ya Mkoa wa Dodoma. Wengine 13 walitibiwa na kuruhusiwa kuendelea na safari .
Treni iliondoka Manyoni Tabora saa 7: na dakika 40 usiku na iliwasili Stesheni ya Tabora saa 3 na dakika 30 leo asubuhi hii na imeondoka saa 5 na dakika 30 asubuhi kuelekea Kigoma ambapo inatarajiwa kuwasili usiku wa manane leo.
Imetolewa na Afisi ya Uhusiano kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TRL Mhandisi Kipallo Aman KIsamfu!
Imetumwa katika Blogu ya Jamii
Na Midladjy Maez
(Meneja Uhusiano TRL)
Dar es Salaam,
Septemba 09, 2012
0 comments:
Post a Comment