Home » » MAGUFULI AMKAMIA MKANDARASI SEKENKE

MAGUFULI AMKAMIA MKANDARASI SEKENKE

na Mwandishi wetu
WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ameapa kuwa mkandarasi aliyejenga kipande cha barabara kati ya Sekenke hadi Shelui mkoani Singida hatapata kazi yoyote ya ujenzi tena nchini kutokana na kufanya kazi hiyo chini ya kiwango.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 33 iliyoanza kujengwa Februari 11, 2005 na kukabidhiwa kwa serikali Februari 10, 2007, kwa sasa imeharibika ikiwa imechimbika mashimo makubwa katikati hasa eneo hatari la Sekenke lenye milima, miteremko na kona kali, hivyo kutia hofu ya usalama wa abiria na magari.
Akizungumza na gazeti hili juzi kuhusu hali hiyo, Waziri Magufuli alisema tayari ametoa maagizo kwa mkandarasi aliyejenga barabara hiyo kuhakikisha anairudia kwa gharama zake kuanzia mwezi huu.
“Mimi inanisikitisha sana kuona barabara mpya kama hiyo ambayo imejengwa kwa fedha za mkopo inaharibika kiasi hiki. Kweli ni udhaifu wa usimamizi, lakini huyo mkandarasi namwapia kuwa hatapata kazi ya ujenzi tena hapa nchini mimi nikiwa hai,” alisema.
Magufuli alisisitiza kuwa, haileti maana kuona fedha za walipakodi zikitumia kulipia mkopo ambao hawakunufaika nao kwani mradi husika unakuwa umeharibika kwa muda mfupi.
“Hii barabara imejengwa na kampuni ya CHICO kutoka China ambayo ilikuwa chini ya mkandarasi kutoka Uholanzi na fedha hizi tumezikopa ili kujenga hizo barabara, sasa nimemtaka airudie haraka kama nilivyofanya kwa mkadarasi aliyejenga barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam, aliyejenga chini ya kiwango,” alisema Waziri Magufuli.
Alisisitiza kuwa, suala la uhalibifu wa barabara halina itikadi za vyama kwani faida na madhara yake ni kwa watanzania wote, hivyo akawaomba wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika pale wanapobaini hujuma za uharibifu wa miundombinu ya barabara.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa