Home » » SINGIDA KUENDESHA ZOEZI LA KUBAINI WANAONG’OA ALAMA ZA BARABARANI

SINGIDA KUENDESHA ZOEZI LA KUBAINI WANAONG’OA ALAMA ZA BARABARANI



Na Nathaniel Limu
MKOA wa Singida unakusudia kuendesha zoezi maalumu la ukaguzi wa magari na pikipiki, ili kuwabaini watu wanaong’oa alama za usalama barabarani na kuzifunga kwenye vyombo vyao.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Singida, Queen Mlozi, katika hotuba yake ya kuhadhimisha kilele cha wiki ya nenda kwa usalama barabarani, iliyofanyika kwenye uwanja wa Namfua mkoani hapa.

Alisema pamoja na uzembe wa madereva, mwendo kasi, ulevi na elimu duni ya usalama barabarani, sababu nyingine ya ajali nyingi kutokea ni kutokuwepo kwa alama muhimu za usalama barabarani.

DC Mlozi, alisema uchunguzi unaonesha wazi kuwa, nyingi ya alama hizo ikiwemo viakisi mwanga hung’olewa na kufungwa kwenye magari na pikipiki za watu binafsi.

"Tabia hii hatutaivumilia hata kidogo, tumeandaa mkakati wa kuhakikisha wizi wa aina hiyo unakoma kabisa, ili kupunguza matukio ya ajali ambayo yanagharimu maisha ya Watanzania na mali zao," alisema.

Takwimu zinaonesha kuwa, katika kipindi cha Januari hadi Agosti mwaka huu, jumla ya watu 83 wamekufa na wengine 192 kujeruhiwa kutokana na ajali 158 mkoani Singida.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa