Home » » WAZAZI SINGIDA WASHINDWA KULIPA ADA ZA SHULE

WAZAZI SINGIDA WASHINDWA KULIPA ADA ZA SHULE

Na Nathaniel Limu, Singida
BAADHI ya wazazi wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Singida iliyopo Manispaa ya Singida, hawalipi ada kwa wakati na kitendo hicho kinachangia tatizo la utoro shuleni hapo.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa juzi na Mkuu wa Shule hiyo, Francis Ibabila, wakati akisoma risala katika mahafali ya 11 ya wahitimu 56 wa kidato cha nne.

Alisema kitendo cha wazazi hao kutolipa ada kwa muda mwafaka, kinasababisha wanafunzi kuwa nje ya shule kwa muda mrefu na kuwasababishia kutofanya vizuri katika mitihani yao.

Alisema wakati umefika kwa wazazi kujipanga vizuri na kuhakikisha wanalipa ada za watoto wao kwa wakati.

Katika hatua nyingine, alisema wanakabiliwa na tatizo la wanafunzi kutumia vileo, kuvaa mavazi ambayo si sare ya shule, kulegeza suruali na matumizi ya simu za mkononi.

“Hayo yote yanachangiwa na wazazi wenyewe kwa kuwa watoto hawa wanatoka nyumbani mwao kila siku kuja shuleni. Matatizo hayo yamesababisha baadhi ya wanafunzi kusimamisha masomo yao na wengine kufukuzwa kabisa,” alisema Mwalimu Ibabila.

Hata hivyo, alisema endapo wazazi watakuwa tayari kushirikiana kwa karibu na walimu, matatizo hayo yote yanaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Alisema pamoja na matatizo hayo, shule hiyo imeweza kupata mafanikio makubwa ikiwamo kukamilisha majengo ya utawala, vyumba vya madarasa vya kutosha, mabweni mawili, majiko mawili, stoo, maabara na nyumba sita za kuishi wafanyakazi.

“Tumejenga ukuta kwa ajili ya usalama wa wanafunzi na kudhibiti nidhamu ya wanafunzi kwa ujumla. Vile vile tumenunua gari ambalo linasaidia kurahisisha shughuli mbalimbali za shule,” alisema Mwalimu Ibabila.

Alisema mwaka jana, wanafunzi 49 ambapo kati yao 43 walifaulu na sita walishindwa na shule hiyo ilishika nafasi ya sita kati ya shule 84 za Mkoa wa Singida na ilishika nafasi ya 579 kati ya shule 3,108 kitaifa.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa