Home » » KIGOGO CCM ALIA RAFU

KIGOGO CCM ALIA RAFU

Na Elisante John
Kutuhumiana miongoni mwa wagombea wa nafasi za uongozi katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) na jumuiya zake, kumeendelea kukitesa chama hicho.

Tuhuma za rushwa zimeibuka katika kinyang’anyiro cha nafasi ya Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida, baada ya kada mkongwe kulalamika hadharani kwamba anasukiwa mizengwe ili aikose nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa chama hicho.

Kada huyo ni Mbunge wa zamani wa Iramba Magharibi, Mgana Msindai, ambaye amelalamika hadharani wakati akirejesha fomu zake za kugombea nafasi hiyo.

Baada ya kurejesha fomu hizo, Msindai alilalamika kuwa anafanyiwa mizengwe kutokana na kuchafuliwa jina lake, akisingiziwa kwamba anataka kutoa rushwa ili achaguliwe kwa kugharimia mikutano ya chama hicho.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Msindai alisema njama hizo zinaonyesha wazi kuwa zimeandaliwa kwa lengo la kumchafua ili aonekane hafai kuwa kiongozi wa chama chake.
 
Kutokana na hali hiyo, Msindai aliyekuwa mbunge wa Iramba Magharibi 1995-2010, alimtaka Katibu wa CCM Wilaya ya Mkalama, Salum Mpamba, kumuomba radhi, kwa kutangaza kuwa atafadhili mikutano ya chama na jumuiya zake ngazi ya wilaya hiyo.
 
Msindai alidai kuwa Agosti 28, mwaka huu katika kikao cha CCM Wilaya ya Mkalama, katibu huyo aliwatangazia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa wilaya hiyo kuwa yeye (Msindai), atagharimia mikutano yote ya chaguzi za jumuiya ya chama hicho, jambo ambalo alisema siyo kweli na hafahamu chochote juu ya kauli hiyo.
 
Msindai alisema kitendo cha katibu huyo kutoa kauli hiyo ya ahadi kwenye mkutano mkubwa kama huo kwa niaba yake (Msindai) bila kuwasiliana naye, kinalenga kumchafua ili aonekane ni mtoa rushwa, hivyo amemtaka katibu huyo amwombe radhi kwa maandishi.
 
Hata hivyo, NIPASHE ilipowasiliana na Mpamba kutoa ufafanuzi wa madai ya Msindai, alisema kauli yake haikuwa na nia ya kumchafua mgombea huyo, bali yeye (Mpamba) akiwa kiongozi wa chama, alikubaliana na wenzake kuomba msaada kwa wagombea na wana-CCM wengine akiwemo Msindai kwa ajili ya kusaidia kugharimia chaguzi hizo.
 
“Tulikuwa hatujawaandikia barua, lakini tutawaomba wote kuanzia Joramu Allute (Mwenyekiti anayemaliza muda wake) na Msindai bila kujua kuwa na yeye ni miongoni mwa wagombea wa nafasi hiyo ya mwenyekiti wa mkoa,” alisema Mpamba.
 
Msindai ni kati ya wanachama sita waliochukua na kurejesha fomu kuomba kuteuliwa na chama hicho kuwania uenyekiti wa mkoa wa Singida katika uchaguzi  uliopangwa kufanyika mwezi  ujao. Wengine walioomba ni Allute, Amani Rai, Haruna Kabombwe, Hussein Yusufu na Joseph Saenda.
Chanzo: Nipashe

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa