Kamanda wa polisi mkoa wa Singida Linuys Sinzumwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) ya ajali iliyoua vijana wawili ndugu. (Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Vijana wawili wa familia moja wakazi wa kijiji cha Mwankoko manispaa ya Singida wamegongwa na gari aina ya Land Rover na kufariki dunia papo hapo.
Vijana hao ni Seleman Juma (42) na Mohammede Juma (33).
Kamanda wa polisi mkoa wa Singida Linus Sinzumwa amesema vijana hao wamegongwa Agosti 29 mwaka huu katika barabara ya Singida mjini – Kindaa eneo la kijiji cha Mwankoko.
Amesema siku ya tukio, vijana hao wakiwa na baskeli zao wakitokea kitongoji cha Isomia kata ya Mwankoko wakielekea Singida mjini, waligongwa na Land Rover T.501 ASG ambayo iliwafuata hadi nje ya barabara.
Akifafanua, Sinzumwa amesema Land Rover hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na dereva ambaye hadi sasa jina lake halijafahamika, liliacha barabara na kuwafuata vijana hao ambao walikuwa nje ya barabara na kuwagonga na kusababisha vifo vyao papo hapo.
Sinzumwa amesema tayari wameanzisha msako mkali wa kumsaka dereva huyo akamatwe na kisha kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Katika hatua nyingine, Kamanda huyo amesema kuwa jumla ya waumini wa kiislamu wanne, wanashikiliwa kwa tuhuma ya kugoma kushiriki zoezi la sensa.
Amewataja waumini hao kuwa ni Jidawi Ramadhani (31), Hussein Juma (23), Saidi Maulid (19) na Hamisi Shaban (18) wote ni wakazi wa Singida mjini.
Amesema watuhumiwa hao wamekamatwa baada ya kugoma kutoa taarifa zao kwa makarani wa sensa.
Chanzo: Mo blog
0 comments:
Post a Comment