RC ASISITIZA WANANCHI KUSOMEWA MAPATO NA MATUMIZI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

SERIKALI za vijiji mkoani Singida zimetakiwa kuwasomea wananchi wake kwa mujibu wa taratibu taarifa za mapato na matumizi ya makusanyo mbalimbali wanayofanya ili kuondoa malalamiko yoyote yasiyo ya lazima.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone alitoa agizo hilo katika Kata ya Kindai wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya maabara kwenye shule mbalimbali za sekondari zilizopo Manispaa hiyo.
Mkuu huyo wa Mkoa alilazimika kutahadharisha hilo baada ya baadhi ya wananchi kulalamika mbele ya yake kuwa uongozi wa kata hiyo hauna utamaduni wa kuwasomea taarifa za mapato na matumizi kwa mujibu wa taratibu na kuna ubadhirifu mkubwa.
Chanzo;Habari Leo

SIKIKA YAWAGAWA MADIWANI KONDOA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
BAADHI ya madiwani katika Halmashauri ya Wilaya Kondoa, wamejitokeza kupinga uamuzi uliofikiwa na Baraza la Madiwani wa kulifukuza Shirika la Sikika wilayani humo.
Wakizungumza na gazeti hili hivi karibuni, madiwani hao walisema uamuzi huo hauna afya kwa maendeleo ya wilaya hiyo, kwani shirika hilo lilikuwa likisaidia kuonyesha udhaifu uliopo katika idara ya afya.
Kwa mujibu wa madiwani hao, uamuzi wa shirika hilo kufukuzwa ulianza kutengenezewa mazingira kwa madiwani wa CCM kufungwa na msimamo wa kichama juu ya shirika hilo.
Diwani wa Kata ya Kondoa Mjini, Hamza Mafita (CCM), alisema Sikika ni jicho la pili ambalo kama lingetumiwa vizuri lingeweza kuwasaidia madiwani kuona uchafu mahala ambapo wameshindwa kuufikia.
“Kuhusu Sikika mimi nilijua shirika hili litafukuzwa tu kwa sababu ya viongozi wetu kupenda kulinda ufisadi. Katika bajeti ya mwaka 2012/2013 miradi ya afya shughuli namba 12 ilitengewa bajeti ya sh milioni 17 kwa ajili ya kukarabati vizimba vya kuchomea takataka.
“Ilikuwa ni kwa ajili ya vituo vya afya vya Hamai na Mrijo. Kizimba cha Hamai kilijengwa chini ya kiwango thamani yake hata milioni mbili hakifiki, Mrijo kule hicho kizimba chenyewe hakipo,” alisema.
Diwani wa Viti Maalumu, Hija Suru (CCM), alisema uamuzi wa shirika hilo kufukuzwa ulikuwa na msukumo ndani yake wenye sura inayotiliwa shaka dhidi ya madiwani.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Suruke, Jafari Ganga (CUF) alisema uamuzi huo ulifanywa na madiwani wa CCM lakini madiwani wa upinzani walipiga kura ya kukataa shirika hilo kufukuzwa.
“Kikao cha Julai 26 kilihudhuriwa na madiwani 36 madiwani 26 wa CCM walishikizwa kupiga kura ya kuiondoa Sikika madiwani 10 wa upinzani tulikataa,” alisema.
Wakijibu madai hayo, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hisdory Mwalongo na Mwenyekiti wa halmashauri, Khamis Mwenda walitetea msimamo wao na kusema kuwa hatua zilizochuliwa dhidi ya shirika hilo ni sahihi.
Chanzo;Tanzania Daima 

MGIMWA AONYA MAAFISA MISITU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmood Mgimwa amewatahadharisha baadhi ya wafanyakazi waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali za misitu kutokuwa kichocheo cha uharibifu wa misitu kutokana na kutowajibika ipasavyo pamoja na kufanyakazi kinyume cha maadili.
Mgimwa alitoa tahadhari hiyo wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa siku tatu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), uliofanyika mjini Singida.
“Katika mikakati hii hatutegemei kuona wafanyakazi waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali hizi, wanakuwa kichocheo cha uharibifu wa misitu yaani kunakotokana na kutowajibika ipasavyo na kufanyakazi kinyume cha maadili,”alisisitiza.
Alifafanua kuwa ni jukumu la wataalamu wote kutekeleza mipango kazi inayoanishwa katika mikakati yao ya kuongoza na kuendeleza rasilimali za misitu na nyuki.
Kwa mujibu wa Naibu waziri huyo, TFS kwa niaba ya serikali ya Tanzania anatakiwa ajipambanue kwa kufanya kila linalowezekana katika kulinda rasilimali za misitu zilizopo na kuziendeleza kwa kuongeza maeneo zaidi ya misitu.
Naye Mtendaji Mkuu wa TFS, Juma Mugoo alisema katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha wa 2010/2011 hadi 2013/2014, wameweza kutengeneza na kusambaza mizinga ya nyuki ipatayo 19,570 katika vituo vya wakala mizinga 5,729 na vijiji vilivyoko kando ya misitu ya Hifadhi mizinga 13,841.
Hata hivyo, Mugoo aliweka bayana kwamba vituo vya ufugaji nyuki vya Nyandakame Kondoa, Ukimbu Manyoni, Buha Kibondo na Mwambao wa Handeni vimewezeshwa kuwa vituo vya uzalishaji badala ya ilivyokuwa mwanzo kama vituo vya maonesho.
“Kiasi cha tani zaidi ya 7.6 za asali na kilo 458.5 za nta zilizalishwa na kuuzwa,vile vile wakala imeanzisha manzuki mpya 51 katika kanda za Kusini, Kaskazini, Mashariki, Kati na katika mashamba saba ya miti,”alisema.
Raisi wa Chama cha Wataalamu wa Misitu Tanzania (TAF), Prof. Reuben Mwamakimbullah alisema kwa kiasi kikubwa hali ya misitu nchini inasikitisha licha ya kuwepo wataalamu wanaolipwa kwa ajili ya kusimamia sekta hiyo. 
Chanzo;Tanzania Daima 

TUSIKUBALI KAMWE KUGEUZWA KARAI LA ZEGE 2015

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

 
Hakuna ubishi waandishi wa habari wana nafasi kubwa sana ya kuipatia jamii viongozi bora na sio bora viongozi, kama wataweka mbele uzalendo na kuacha kuchukua hongo kutoka kwa wagombea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Nafahamu wapo waandishi wengi wenye uadilifu, lakini kwa sababu kwenye msafara wa mamba na kenge wamo, si ajabu kukuta ambao njaa yao ya muda mfupi inatupatia viongozi wabovu.
Kipindi cha uchaguzi ni wakati ambapo baadhi yetu tunajulikana thamani zetu. Wapo wa Sh20,000, wengine Sh50,000, pia wa Sh100,000 na wale wanaopewa hongo zaidi ya kiasi hicho.
Hongo hizi wanazopokea ili kumpamba mgombea kuliko uhalisia wake, zimekuwa na athari kubwa kiuchumi, kisiasa na kijamii ikiwamo kupata viongozi wasiofaa na wanaotanguliza masilahi yao binafsi mbele.
Sote tunafahamu Uchaguzi Mkuu wa 2005 na 2010 namna ambavyo tuliwapamba baadhi ya wagombea wakiwamo wa ubunge, tukawaaminisha wapigakura wakawachagua, lakini leo wanajuta. Natamani utaratibu ule wa zamani urejee, kwamba kama wananchi walikuwa na hitaji la kiongozi walimtafuta wenyewe na kumuomba ili agombee, leo mtu anagombea tena kwa kuhonga wapigakura.
Mwaka huu huenda tukawa na uchaguzi wa Serikali za mitaa, lakini mwakani tukawa na uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani watakaotuongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Ni kipindi ambacho thamani ya waandishi wa habari hupanda kwa kipindi kifupi sana na kisha wanasiasa wakishaingia madarakani, huwatelekeza kama mafundi wanavyotumia karai la zege.
Nafahamu asilimia 75 ya wanahabari wote nchini ni wa kujitegemea ambao kimsingi wanalipwa kulingana na habari ama makala zitakazochapwa au kutangazwa na vyombo vya habari.
Ni ukweli malipo haya ni kidogo, lakini hiyo haiwezi kuhalalisha baadhi yetu kujiingiza katika vitendo vya kupokea hongo kutoka kwa wagombea ili tu wawaandike vizuri hata kama hawafai.
Maadili ya Uchaguzi Mkuu 2010 kwa wanahabari yaliweka sharti la lazima kwa wanahabari kuwahabarisha na kutoa elimu ya uraia kwa wapigakura ili wafanye uamuzi sahihi wakati wa kupiga kura.
Uamuzi sahihi ni kwa wapigakura kuchagua viongozi bora na siyo bora viongozi kwa sababu tu amepandishwa chati na wanahabari wakati dhamira yake ni kwenda kuchuma na si kusaidia jamii.
Wakati tunajiandaa na chaguzi nilizozisema, tayari wapo wagombea ambao wamekuwa ‘mzigo’ lakini wanajiandaa kufanya kila njia ili waweze kurudi tena bungeni kwa kipindi kingine.
Kuna taarifa zisizo rasmi baadhi yao wametenga hadi Sh200 milioni na sehemu ya fedha hizo imetengwa kwa ajili ya wanahabari wasioheshimu maadili ili wawasafishie njia hata kama hawafai.
Wanahabari tunapaswa kuanza kujitafakari sasa kama tumefanya nini kulisaidia taifa kupata viongozi bora, wazalendo na wenye dhamira ya dhati ya kuwaletea Watanzania maendeleo.
Haiwezekani leo hii tuna rasilimali kibao kuanzia madini ya kila aina, vivutio vya utalii, nishati ya gesi, wingi wa misitu na mazao ya baharini lakini Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi maskini.
Hapa ni lazima tutafakari kauli ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere kuwa ili nchi iendelee inahitaji vitu vinne navyo ni ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. Ninasema tutafakari ni kipi tunachokikosa kati ya vitu hivyo vinne hadi Watanzania waendelee kuwa maskini licha ya kuwa moja ya nchi zinazoongoza barani Afrika kwa kuwa na rasilimali nyingi.
Hakuna ubishi tuna tatizo la uongozi ndio maana hatufiki kule tunakotaka kwenda na wanahabari wanalo jukumu zito la kuirudisha nchi hii kwenye mstari.
Chanzo;Mwananchi

WAJUMBE WAUNGA MKONO PENDEKEZO LA RASIMU YA KATIBA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Shamsi Vuai Nahodha
 
Wajumbe wa kamati namba mbili wamefanya marekebisho katika ibara ya 21 (3) kwa kueleza mtumishi wa umma atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria baada ya kusimamishwa kama ilivyopendekezwa kwenye rasimu ya katiba.
Ibara hiyo inasema: “Kiongozi wa umma ambaye anatuhumiwa kwa makosa ya: (a) kimaadili; (b) udhalilishaji wa mtu au wa kijinsia; au (c) wizi au ubadhirifu wa mali za umma, atasimamishwa kazi hadi suala lake litakapoamuliwa kwa mujibu wa sheria za nchi au taratibu nyingine zinazowahusu viongozi wa umma.”

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Shamsi Vuai Nahodha (pichani), alisema wajumbe hao waliona ibara hiyo imetoa adhabu moja kwa moja na kwamba, katiba haipaswi kuadhibu moja kwa moja.

“Kifungu C tumebadilisha na kusema atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, mtu ametuhumiwa anafukuzwa halafu akienda mahakamani akashinda itakuwaje, hivyo tumeweka atachukuliwa hatua,” alisema.

Alisema kifungu hicho kitasomeka kiongozi wa umma, ambaye anatuhumiwa kwa makosa ya wizi, rushwa au ubadhilifu wa mali ya umma atachukuliwa hatua.

Nahodha alisema sheria ndiyo itaainisha hatua za kuchukuliwa kwa mtumishi kuliko katiba kutoa adhabu, ambayo itakuwa hatari.

Alisema kamati yake inabadilisha baadhi ya maeneo bila kuathiri maudhui ili kuwa na katiba yenye lugha fasaha na siyo maneno yenye maana zaidi ya moja ili kila atakayeisoma apate maana iliyokusudiwa.

Kamati 12 za Bunge hilo zimejichimbia katika kumbi mbalimbali kujadili sura 15 za Rasimu hiyo kwa muda wa siku 16, huku baadhi ya kamati zikiwa katika sura ya tano na saba.
 
CHANZO: NIPASHE

MAUAJI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
  Sungusungu wadaiwa kuwaua raia kwa kipigo
  Mmoja wamchoma akiwa mfu, mwingine hai
Kamanda wa Polisi Tarime/Rorya, Lazaro Mambosasa
Mauaji ya kutisha ya watu wawili, yanadaiwa kufanywa na kundi la askari wa jadi maarufu kama Sungusungu wilayani Manyoni Mkoa wa Singida baada ya kuwatoa nyumbani kwao usiku, kuwapeleka kichakani ambako waliwashambulia kwa kipigo, kisha kumchoma mmoja akiwa mfu na mwingine akiwa bado hajakata roho.
Waliouawa katika tukio hilo lilitokea kwa nyakati tofauti usiku wa kuamkia ijumaa iliyopita katika kijiji cha Damwelu kata ya Ipande tarafa ya Itigi wilayani hapa mkoa wa Singida ni Lameck Joshua (31), mkazi wa kijiji hicho na Doto Kindai (20), wa mkoa wa Mbeya.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kijiji hicho, ,  Agustine Raphael,  kundi la watu hao wanaokadiriwa kufikia 40 waliojitambulisha kuwa ni sungusungu,  walifika nyumbani kwa Joshua na kugonga mlango kwa lengo la kutaka awafungulie.

Raphael alisema  inasemekana Joshua hawafungulia, ndipo walipomtishia kuwa watamwagia nyumba yake petroli kisha kuilipua kwa njiti ya kibiriti.

"Baada ya tishio hilo Joshua alifungua mlango na kutoka nje na kukamatwa huku akizibwa macho kwa kufungwa usoni kwa kitambaa na baada ya hapo alipelekwa kwenye kichaka ambako alipigwa vibaya hadi kufa na mwili wake kuchomwa moto, "  alisema.

 Alisema baada ya kufanya mauaji hayo ya kinyama, sungusungu hao walikwenda nyumbani kwa Mapalala ambako nao walimkamata Kindai na kwenda naye kwenye kichaka hicho  na  kumshambulia kwa kipigo, kisha kummaliza kwa kumchoma moto.

" Taarifa zilizozagaa lijijini kwetu ni kwamba watu hao wameuawa kikatili kwa madai kwamba ni wezi wa mifugo.. hata hivyo serikali ya kijiji chetu haina taarifa kabisa juu ya watu hao kujihusisha na vitendo vya wizi wa mifugo." alisema na kuongeza kuwa:" Wameuawa kinyama, miili yao imeteketea na kubaini nyama kidogo na mifupa."

Katika hatua nyingine; Munge wa  Manyoni Magharibi (CCM), John Paulo Lwanji amesema  kuwa amepokea taarifa ya mauaji hayo ya kinyama kwa masikitiko makubwa.

Lwanji alisema kuwa analaani vikali wauaji hao kujichukulia sheria mkononi kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Aliwataka wakazi wa jimbo hilo kujiepusha na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi kwa sabababu  vitawasababishia matatizo  na usumbufu.
Alitoa wito kwao kuwa endapo watamhisi mtu au watu wanaojihusisha na vitendo hivyo viovu wasisite kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Kwa upande wake Kamanda wa polisi Mkoa wa Singida,  Geofrey Kamwela, alipotakiwa kuzungumzia mauaji hayo,  aliomba  muda zaidi ili aweze kujiweka vizuri na kutolea ufafanuzi.

Watuhumiwa watano wauawa Katika tukio jingine; watu wanne, wakiwamo raia watatu wa Kenya wameuawa kwa tuhuma za ujambazi katika kijiji cha Mriba tarafa ya Ingwe.

Kamanda wa Polisi Tarime/Rorya, Lazaro Mambosasa aliwataja  waliouawa kuwa ni raia hao wa Kenya kutoka vijiji vya Ntimaro na Girabose wilaya ya Kurya East, Mwita Rugena (30), Rogona Nyamahoyi na Machera Marwa na Sagire Gachanga (25) wa kijiji cha Itiryo tarafa ya Ingwe wilayani Tarime Mkoa wa Mara.

Mambosasa alisema kuwa mauaji hayo yalitokea  Agosti 8 mwaka huu baada ya watuhumiwa hao  waliokuwa na silaha kukutwa na wananchi wakitaka  kupora fedha na simu za wateja katika duka la Shadrack Mahenye kijiji hapo Agosti 3, mwaka huu na kuwajeruhi kwa risasi watu watatu.

Alisema baada ya taarifa hizo,  polisi wakwenda katika eneo la  tukio na kuwakuta watuhumiwa hao wameuawa kwa kushambuliwa kwa kipigo n a wananchi.

"Miili ya watu hao imehifadhiwa hospitali ya wilaya ya Tarime ikisubiri kuchukuliwa na ndugu zao. Kwa sasa tunawahoji watu nane kuhusiana na mauaji hayo,” alisema Kamanda huyo na kuwataja kuwa ni wakazi wa Kijiji cha Mriba.

Baba adaiwa kuuawa mwanawe
Wakati huo huo; Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamsaka Mkazi wa kijiji cha Kanji tarafa ya Kirua Vunjo wilaya ya  Moshi Vijijini , aliyejulikana kwa jina moja la Maurice kwa tuhuma za kumuua mwanawe mwenye umri wa miaka minne, Nicholaus Maurice (4).

“Siku mbili kabla tulimisikia baba yake  akitamka kwa jazba wakati akimuadhibu mwanawe kwa kuchelewa kupeleka kijiko ili ale chakula na mke wake," alidai mmoja wa watu kwenye familia hiyo na kuongeza kuwa:

" Nitakuuwa ili niishi na mke  wangu vema na usinipotezee  malengo  bora ufe, sikuhitaji tena," Alisema kuna  uwezekana wa  baba huyo kuwa wakati akimuadhibu  mtoto huyo alimnyonga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo  Agosti 10, mwaka huu saa 5 asubuhi.
Boaz alisema mtoto huyo  alikutwa amefariki dunia baada ya kupigwa  na baba yake mzazi  huku  mkono wake wa kushoto na makalio vikiwa vimevimba.

Alisema baada ya kufanya mauaji hayo, mtuhumiwa huyo alitokomea kusikojulikana na kwamba polisi wanamsaka kwa udi na uvumba ili akamatwe na kufikishwa mahakamani.

Mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa  hospitali ya Kilema  ukisubiri kufanyiwa uchunguzi kisha kukabiliwa kwa ndugu kwa maziko.
“Inauma sana kuona mzazi unamchapa mtoto wako tena wa kumzaa paka umauti unamkuta, huu ni unyama. Tutahakikisha tunamsaka mzazi huyo popote pale alipo ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yake” alisisitiza Kamanda Boaz.

 Vilevile alisema  Agosti 9, mwaka huu majira ya saa 6:15 usiku, Nastori Christian (60), alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu hospitali ya Huruma iliyopo Rombo- mkuu, wilayani Rombo baada kudaiwa kupigwa kichwani kwa fimbo na mtoto wake, Christofa Nestori(25).

 Kamanda  Boaz alisema chanzo cha mtoto huyo kuamua kumchapa baba yake huyo hakijajulikana, hivyo wanamshikilia kwa mahoajiano zaidi. Imeandikwa na Jumbe Ismailly, Singida, Samson Chacha, Tarime na Mary Mosha, Moshi.
CHANZO: NIPASHE

AUNGUZWA NA UJI KISA WIVU WA MAPENZI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
MSICHANA Jackline Lasway maarufu kwa jina la Pendo, mkazi wa eneo la Minga Manispaa ya Singida, amenusurika kifo baada ya kumwagiwa uji wa moto na mke wa tajiri wake wa dukani kutokana na kile kinachosadikiwa ni wivu wa kimapenzi.
Pendo amelazwa wodi namba mbili hospitali ya Mkoa wa Singida, huku akiwa na majeraha ya kuungua sehemu ya sikio la upande wa kulia na mgongoni.
Akizungumza kwa taabu katika wodi hiyo, Pendo alisema tukio hilo limetokea jana mchana wakati akiwa dukani kwa bosi wake aliyemtaja kwa jina la Charles Kamnde ‘Frarucha’.
Alisema akiwa anaendelea na kazi yake ya kuuza bidhaa mbalimbali dukani hapo, ghafla alitokea mke wa bosi wake akiwa na chupa yenye uji wa moto na kutaka kumwagia usoni.
Alisema aligeuka ili uji ule usimwagigikie usoni na ndipo ulimuunguza sikio la kulia na mgongoni, ambako baada ya mke wa bosi wake kumkosa uso, alitoa kisu kutaka kumchoma kifuani.
“Mimi sikuwa na ugomvi naye wala sijui chanzo cha yeye kufika dukani na kufanya hili tukio, maana kama ni kazi mi nafanya kulingana na maelekezo kutoka kwa bosi wangu Chale,” alisema.
Alisema katika purukushani za kujiokoa asichomwe kisu, alifanikiwa kumkamata mkono mwanamke huyo na kupiga kelele na watu walifika kumwokoa.
Hata hivyo, alisema alichukuliwa na bosi wake hadi kituo cha polisi mjini Singida na kupewa PF 3 kwa ajili ya matibabu na kuletwa katika hospitali hiyo, ambako amelazwa huku akiwa na majeraha makubwa mgongoni.
Muuguzi wa zamu katika wodi namba mbili ya wanawake, Anna Cyprian, alisema hali ya mgonjwa huyo inaendelea vizuri na anaendea kupatiwa matibabu ya majeraha ya moto aliyopata.
Kwa upande wake mmiliki wa duka hilo, Frarucha, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba hayuko tayari kulizungumzia, kwani maelezo aliyotoa binti huyo yanajitosheleza.
Baadhi ya kina mama waliohojiwa kuhusiana na tukio hilo, wameonesha masikitiko yao kutokana na hatua ya mwananmke huyo kumwagia uji msichana huyo.
Amina Ramadhani, alisema hicho ni kitendo cha kinyama kwa binti mdogo kama huyo na kwamba kama aliona kuna mahusiano ya kimapenzi na mumewe, angetumia busara na kumwondoa dukani na siyo kumuunguza kwa uji wa moto.
Veronica Masawe, alisema amesikitishwa na tukio hilo na kuwa hakiendani na haki za binadamu, kwa kuwa ni kumdhalilisha msichana huyo ambaye alikuwa akifanya kazi kwa ajili ya kujipatia kipato.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwela, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba, wanamshikilia mtuhumiwa kwa mahojiano na baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa mahakamani
Chanzo:Tanzania Daima
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa