Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmood Mgimwa amewatahadharisha
baadhi ya wafanyakazi waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali za
misitu kutokuwa kichocheo cha uharibifu wa misitu kutokana na
kutowajibika ipasavyo pamoja na kufanyakazi kinyume cha maadili.
Mgimwa alitoa tahadhari hiyo wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa
mwaka wa siku tatu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS),
uliofanyika mjini Singida.
“Katika mikakati hii hatutegemei kuona wafanyakazi waliopewa dhamana
ya kusimamia rasilimali hizi, wanakuwa kichocheo cha uharibifu wa misitu
yaani kunakotokana na kutowajibika ipasavyo na kufanyakazi kinyume cha
maadili,”alisisitiza.
Alifafanua kuwa ni jukumu la wataalamu wote kutekeleza mipango kazi
inayoanishwa katika mikakati yao ya kuongoza na kuendeleza rasilimali za
misitu na nyuki.
Kwa mujibu wa Naibu waziri huyo, TFS kwa niaba ya serikali ya
Tanzania anatakiwa ajipambanue kwa kufanya kila linalowezekana katika
kulinda rasilimali za misitu zilizopo na kuziendeleza kwa kuongeza
maeneo zaidi ya misitu.
Naye Mtendaji Mkuu wa TFS, Juma Mugoo alisema katika kipindi cha
kuanzia mwaka wa fedha wa 2010/2011 hadi 2013/2014, wameweza kutengeneza
na kusambaza mizinga ya nyuki ipatayo 19,570 katika vituo vya wakala
mizinga 5,729 na vijiji vilivyoko kando ya misitu ya Hifadhi mizinga
13,841.
Hata hivyo, Mugoo aliweka bayana kwamba vituo vya ufugaji nyuki vya
Nyandakame Kondoa, Ukimbu Manyoni, Buha Kibondo na Mwambao wa Handeni
vimewezeshwa kuwa vituo vya uzalishaji badala ya ilivyokuwa mwanzo kama
vituo vya maonesho.
“Kiasi cha tani zaidi ya 7.6 za asali na kilo 458.5 za nta
zilizalishwa na kuuzwa,vile vile wakala imeanzisha manzuki mpya 51
katika kanda za Kusini, Kaskazini, Mashariki, Kati na katika mashamba
saba ya miti,”alisema.
Raisi wa Chama cha Wataalamu wa Misitu Tanzania (TAF), Prof. Reuben
Mwamakimbullah alisema kwa kiasi kikubwa hali ya misitu nchini
inasikitisha licha ya kuwepo wataalamu wanaolipwa kwa ajili ya kusimamia
sekta hiyo.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment