Naibu
Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) akiongozana na Mbunge wa Jimbo
la Nzega Vijijini, Hamis Kigwangala (kulia) mara baada ya kuwasili
kwenye Chuo cha Madini Dodoma, Kampasi ya Nzega ili kujionea hali ya
eneo hilo.
Naibu
Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia) akikagua mazingira ya Chuo cha
Madini Dodoma, Kampasi ya Nzega ili kujionea hali ya Kampasi hiyo.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Isanga, Kata ya Lusu Wilaya ya Nzega (hawapo pichani).
Naibu
Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) akiongozana na mwenyeji wake
Mbunge wa Nzega Vijijini na Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii,
Dkt. Hamis Kigwangala (kulia) walipofanya ziara kwenye Chuo cha Madini
Dodoma, Kampasi ya Nzega ili kujionesa hali ya Kampasi hiyo.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa pili kushoto) akikagua mazingira ya Chuo cha Madini Dodoma, Kampasi ya Nzega.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati) alipotembelea Chuo Cha Madini Dodoma, kampasi ya Nzega
Serikali
imetoa onyo kali kwa waliojinufaisha na kutumia ruzuku ya uchimbaji
madini kinyume na makusudio yake ambao hadi sasa hawajarejesha licha ya
kutakiwa kufanya hivyo.
Naibu
Waziri wa Madini, Doto Biteko alitoa onyo hilo Februari 26, 2018 kwenye
mkutano na wananchi na wachimbaji wadogo wa madini katika kijiji cha
Isanga, Kata ya Lusu Wilaya ya Nzega.
Awali
kabla ya kutoa onyo hilo, wachimbaji hao waliiomba Serikali kuwapatia
ruzuku ili iwasaidie katika shughuli zao za uchimbaji madini ndipo Naibu
Waziri Biteko alipoweka bayana suala hilo la ruzuku.
Alisema
Serikali ilisimamisha utoaji wa ruzuku kwa wachimbaji wadogo wa madini
nchini baada ya kubaini kwamba imeshindwa kuleta mafanikio
yaliyokusudiwa na kwamba ilikwishaagiza wale wote waliojipatia ruzuku na
kuitumia kinyume na makusudio wanapaswa kuirejesha mara moja vinginevyo
hatua kali za kisheria zitachukuliwa.
“Wapo
ambao tayari wameanza kurejesha na wengine bado hawajafanya hivyo.
Ninawahakikishia wale ambao bado, tutawachukulia hatua kali za
kisheria,” alisema Biteko.
Alisema haiwezekani watu wachache wasiokuwa na huruma kwa wanyonge wakatumia fedha ya Watanzania kinyume na makusudio yake.
Biteko
alisema kuwa lengo la Serikali la utoaji wa ruzuku lilikuwa ni
kuhakikisha wachimbaji wadogo wa madini nchini wanaweza kuendeleza
machimbo yao kwa kufanya shughuli zenye tija kwao na Taifa kwa ujumla
hata hivyo, makusudio hayo hayakufikiwa kama ilivyotarajiwa.
Alibainisha
kuwa Serikali inakuja na mpango mwingine wa kuwasaidia wachimbaji
wadogo kupata manufaa kutokana na shughuli zao lakini sio kuwapatia
fedha kama ilivyokuwa hapo awali. “Tunanunua vifaa vya uchimbaji ambavyo
vitatumika kuwasaidia na sio kuwapatia fedha,” alisema Biteko.
Aidha,
Biteko aliwataka wachimbaji kote nchini kujiunga kwenye vikundi ili
kujipatia manufaa mbalimbali ikiwemo urahisi wa kupata huduma za
kifedha, kukopesheka na kuelimishwa njia bora na sahihi ya uchimbaji.
Alisema
wachimbaji watakapojiunga wataweza kuwa na uchimbaji wenye tija na
hivyo kutoa ajira nyingi kwa Watanzania wenzao, kulipa ushuru na tozo
mbalimbali za Serikali na hivyo kujiletea maendeleo wao binafsi lakini
pia maendeleo kwa Taifa kwa ujumla.
Katika
ziara hiyo, Naibu Waziri Biteko aliambatana na mwenyeji wake Mbunge wa
Jimbo la Nzega Vijijini na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis
Kigwangala ambapo walitembelea maeneo ya Chuo cha Dodoma Kampasi ya
Nzega (MRI) ambapo zamani palikuwa ni mgodi wa Reolute.
0 comments:
Post a Comment