Sehemu ya wakazi wa Singida katika mkutano wa hadhara.
Na Nathaniel Limu.
Wakazi wa wa Singida mjini asilimia kubwa hawakusikiliza rasmu ya katiba iliyosomwa tarehe 3/6/2013, kwa kile walichodai kuwa kuisikiliza au kutokuisikiliza ni sawa tu, kwa madai kuwa hata wakitoa maoni yao kurekebesha baadhi ya vipengele, havitafanyiwa kazi.
Fundi cherehani Ali Soghweda.akizungumzia suala hilo amesema “Binafsi sikuona faida yo yote ya kusikiliza uwasilishaji wa rasmu ya katiba hiyo, kwa sababu imekusanya maoni ya Watanzania wengi wa ngazi mbalimbali, basi mi nipo pamoja nao katika maoni yao”.
Hata hivyo, Katibu wa TCCIA mkoa wa Singida Culvert Nkurlu, amesema rasmu hiyo haija ainisha vizuri juu ya ardhi na kwa maana hiyo, haitawanufaisha wananchi hasa wale walioishi kwenye eneo husika kwa miaka mingi.
Amesema kuiacha ardhi kwenye mamlaka ya rais, kunawanyima haki ya wananchi walioishi kwa miaka mingi kwenye maeneo hasa yanayogundulika kuwa na madini.
Amesema “Hivi sasa tunashuhudia wawekezaji wakiwatoa wananchi walikokaa kwa miaka mingi katika eneo husika, bila kuwapa fidia ya kukidhi mahitaji. Wananchi wa aina hiyo, katiba inatakiwa kuwapa umuhimu ili waweze kufaidika na ardhi yao”.
Naye Mwenyekiti wa TLP wilaya ya Singida, Athumani Nkii, ameipongeza rasimu hiyo kwa matakwa yake ya kutaka kuwepo kwa marasi watatu, Tanzania bara, Tanzania visiwani na yule wa muungano.
Nkii ambaye pia ni fundi cherehani, amepongeza pia utaratibu wa kufuta ubunge wa viti maalum na kupendekeza uwepo wa mgombea binafsi.
Ameongeza kuwa “Maoni ya kuwa spika wa bunge asitokane na wabunge, hiyo pia ni nzuri, spika na msaidizi wake atoke kwenye kamati huru ya uchaguzi ambayo haitatokana na kuteuliwa na rais”.

NA MO BLOG