Home » » Wakulima wa viazi vitamu mkoani Singida walalamikia bei wanayolazimishwa na wafanyabiashara.

Wakulima wa viazi vitamu mkoani Singida walalamikia bei wanayolazimishwa na wafanyabiashara.

E83A0368
 Makuli kumi wakipakia juu ya lori gunia moja la viazi vitamu lenye zaidi ya kilo 150 lenye thamani ya shilingi 35,000.Wakulima wa zao la viazi vitamu tarafa ya Ihanja wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida,wamelalamikia ujazo huo pamoja na bei wanayopewa kwa madai kuwa ni ya kinyonyaji.
E83A0363
Magunia ya zao la viazi vitamu katika kijiji cha Ighuka wilaya ya Ikungi,vikiwa tayari kusafirishwa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kwenda kuuzwa.
E83A0364
Lori ambalo dereva wake aliomba lisitajwe namba zake za usajili likiwa linapakia magunia ya viazi vitamu katika kijiji cha Ighuka wilaya ya Ikungi.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel  Limu.
Wakulima wa zao la viazi vitamu tarafa ya Ihanja wilaya ya Ikungi mkoani Singida wamelalamikia tabia ya wafanyabiashara ya kuwalazimisha kuuza gunia lenye uzito wa kilo zaidi ya 150 kwa bei ndogo ya shilingi 35,000.
 Wamedai kwamba ujazo huo wa gunia la viazi vitamu unaojulikana kwa jina la ‘polo’, unachangia wakulima kunyonywa mapato yao.
 Wakizungumza kwa nyakati tofauti na MO Blog, wakulima hao wamedai kuwa gharama wanazotumia katika kulima na ile ya kusafirisha hadi barabarani zao la viazi vitamu, haiwezi kurudi kwa bei wanayopewa na wafanyabiashara hao.
Mmoja wa wakulima hao Doricus Hussein, amesema wafanyabiashara hao wanaotoka katika mikoa ya Dodoma, Tanga, Dar-es-salaam, Zanzibar pamoja na visiwa vya Comoro, wamekuwa hawako tayari kununua zao hilo kwa kutumia vipimo kwa madai kuwa hakuna soko litakalonunua viazi vitamu kwa kutumia mizani.
 Alitumia fursa hiyo kuiomba serikali ya kijiji kwa ushirikiano na halmashauri ya wilaya ya Ikungi,kuangalia uwezekano wa kuwasaidia wakulima wasiendelee kunyanyaswa na kudhulumiwa na wafanyabiashara hao.
 Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji wa kata ya Pum Miraji Ntungu, amesema kuwa licha ya kupiga marufuku ujazo wa rumbesa unaolalamikiwa na wakulima hao, lakini ni wakulima wenyewe ndio wanaopingana na agizo hilo kwa madai kuwa serikali haijawasaidia kutafuta mbegu ya viazi vitamu.
 Ntungu amesema kwa siku moja magunia yasiyopungua 200 husafirishwa kutoka kijiji cha Puma pekee kwenda kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi, ambapo kila gunia hulipiwa ushuru wa shilingi elfu moja.
 Kwa upande wao wafanyabiashara hao wanaolalamikiwa, wamedai kuwa hakuna soko linaloweza kununua gunia la viazi vitamu  lisilo kuwa na ujazo wa rumbesa iliyopitiliza.
 Mmoja wa wafanyabiashara hao Bw. Shabani Hamisi Bilali, amesema pia wanawataka wakulima hao kujaza gunia ujazo huo wa rumbesa ili pamoja na mambo mengine, wao waweze kufidia gharama za upakiaji na  usafirishaji  na hivyo kupata faida inayokidhi mahitaji.
 Na Mo Blog

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa