Katibu wa CCM wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida, Joseph Rudisha akitoa mwongozo kwenye mkutano wa uchaguzi wa kuchagua mwenyekiti na makamu wake wa halmashauri ya wilaya hiyo mpya.Wa kwanza kulia ni mgombea pekee wa nafasi ya uenyekiti Celestine Yunde.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ikungi, Hassan Tati akizungumza kwenye mkutano wa uchaguzi wa nafasi za mwenyekiti na makamu wake wa halmashauri ya wilaya mpya ya Ikungi. Mkutano huo ulifanyikia kwenye ukumbi wa mikutano wa chuo cha maendeleo ya wananchi mjini Singida.Wa kwanza kulia ni mgombe wa nafasi ya mwenyekiti Celestine Yunde na kushoto ni mgombe wa nafasi ya makamu mwenyekiti, Alli Nkhangaa.
Mgombea wa nafasi ya mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ikungi, Celestine Yunde akiomba kura kwa wajumbe (hawapo kwenye picha) wa mkutano wa uchaguzi wa kuchagua wagombea watakaopambana na wagombe kutoka CHADEMA. Kulia ni katibu wa CCM wilaya ya Ikungi, Joseph Rudisha na kushoto ni mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ikungi, Hassan Tati.
Baadhi ya madiwani waliohudhuria mkutano wa uchaguzi wa CCM wilaya ya Ikungi wanaowania nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti katika halmashauri ya wilaya hiyo.Mkutano huo ulifanyikia katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha maendeleo ya wananchi mjini Singida.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Celestine Yunde wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) halmashauri ya wilaya ya Ikungi, amechaguliwa kwa kishindo kuwania nafasi ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo.
Yunde ambaye alikuwa mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Singida kabla ya wilaya hiyo kuzaa halmashauri mpya ya Ikungi, alipata kura 29 za ndio na moja ilimkataa.
Kwa ushindi huo mnono, Yunde atapambana na mgombea kutoka CHADEMA iwapo chama hicho cha upinzani, kitaamua kutoa mgombea.
CHADEMA ina madiwani wawili katika wilaya ya Ikungi.
Nafasi ya makamu mwenyekiti imenyakuliwa na Alli Nkhangaa ambaye naye alipata kura 29 za ndio na moja ilimkataa.
Mapema akizungumza kwenye mkutano huo wa uchaguzi, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ikungi Hassan Tati, amewahimiza madiwani hao kuhakikisha wanaimarisha umoja wao ili chama kiendelee kuwa na nguvu za kushinda chaguzi mbalimbali.
Wakati huo huo, Katibu wa CCM wilaya ya Singida vijijini Mwanamvua Kilo, amesema mkutano wa uchaguzi wa nafasi ya mwenyekiti na makamu wake katika halmashauri hiyo umeahirishwa hadi hapo baadae.
Amesema mkutano huo uliokuwa ufanyike juzi, pamoja na madiwani wote wa halmashauri hiyo kuhudhuria, haukufanyika kutokana na hitilafu zilizojitokeza mara tu baada ya mkutano huo kuanza.
Amesema hawezi kwa sasa kusema ni nini kilichotokea kwenye mkutano wao, ila ifahamike tu kwamba uchaguzi huo utarudiwa baadae katika siku itakayopangwa.
KWA HISANI YA MO BLOLG
0 comments:
Post a Comment