Home » » Nyara za Serikali zawafikisha polisi

Nyara za Serikali zawafikisha polisi



JESHI la Polisi Mkoa wa Singida, linawashikilia watu wawili kwa tuhuma ya kumiliki nyara za Serikali kinyume na sheria. Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwela aliwataja watu wanaoshikiliwa kuwa ni Esinasi Stephano (36) mkazi wa Kijiji cha Chikuyui. Alisema mtuhumiwa alikamatwa kwa kosa la kumiliki meno mawili ya tembo yenye uzito wa kilo tano na thamani ya zaidi ya Sh milioni 4.4.

Alisema mtuhumiwa huyo, alikamatwa juzi jioni baada ya raia wema kutoa taarifa polisi.

Alimtaja mtuhumiwa wa pili kuwa ni, Mwanandi Amani (34) mkazi wa Kijiji cha Mitundu ambaye alikamatwa na mkia wa tembo, meno mawili ya ngiri, mafuta ya samba na sare moja ya Jeshi la Polisi.

Alisema mtuhumiwa huyo, alikamatwa baada ya raia wema kutoa taarifa juu ya umilikaji wake wa nyara za serikali kinyume na sheria.

Katika hatua nyingine, alisema wameanzisha msako mkali wa kusaka watu wanne waliomvamia mmiliki wa duka Miraji Abdallah (45) mkazi wa Kijiji cha Mtunduru na kupora simu 15 za kiganjani.

Alisema watu hao, wanaodhaniwa ni majambazi, kabla ya kupora simu hizo ambazo thamani yake bado haijajulikana, walimjeruhi vibaya Miraji na watu wengine Hamisi Hamisi (30) na Hatibu Idde (18) kwa kutumia visu.

CHANZO HABARI LEO

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa