Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
BAADHI ya madiwani katika Halmashauri ya Wilaya Kondoa, wamejitokeza
kupinga uamuzi uliofikiwa na Baraza la Madiwani wa kulifukuza Shirika
la Sikika wilayani humo.
Wakizungumza na gazeti hili hivi karibuni, madiwani hao walisema
uamuzi huo hauna afya kwa maendeleo ya wilaya hiyo, kwani shirika hilo
lilikuwa likisaidia kuonyesha udhaifu uliopo katika idara ya afya.
Kwa mujibu wa madiwani hao, uamuzi wa shirika hilo kufukuzwa ulianza
kutengenezewa mazingira kwa madiwani wa CCM kufungwa na msimamo wa
kichama juu ya shirika hilo.
Diwani wa Kata ya Kondoa Mjini, Hamza Mafita (CCM), alisema Sikika ni
jicho la pili ambalo kama lingetumiwa vizuri lingeweza kuwasaidia
madiwani kuona uchafu mahala ambapo wameshindwa kuufikia.
“Kuhusu Sikika mimi nilijua shirika hili litafukuzwa tu kwa sababu ya
viongozi wetu kupenda kulinda ufisadi. Katika bajeti ya mwaka 2012/2013
miradi ya afya shughuli namba 12 ilitengewa bajeti ya sh milioni 17 kwa
ajili ya kukarabati vizimba vya kuchomea takataka.
“Ilikuwa ni kwa ajili ya vituo vya afya vya Hamai na Mrijo. Kizimba
cha Hamai kilijengwa chini ya kiwango thamani yake hata milioni mbili
hakifiki, Mrijo kule hicho kizimba chenyewe hakipo,” alisema.
Diwani wa Viti Maalumu, Hija Suru (CCM), alisema uamuzi wa shirika
hilo kufukuzwa ulikuwa na msukumo ndani yake wenye sura inayotiliwa
shaka dhidi ya madiwani.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Suruke, Jafari Ganga (CUF) alisema
uamuzi huo ulifanywa na madiwani wa CCM lakini madiwani wa upinzani
walipiga kura ya kukataa shirika hilo kufukuzwa.
“Kikao cha Julai 26 kilihudhuriwa na madiwani 36 madiwani 26 wa CCM
walishikizwa kupiga kura ya kuiondoa Sikika madiwani 10 wa upinzani
tulikataa,” alisema.
Wakijibu madai hayo, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hisdory Mwalongo
na Mwenyekiti wa halmashauri, Khamis Mwenda walitetea msimamo wao na
kusema kuwa hatua zilizochuliwa dhidi ya shirika hilo ni sahihi.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment