Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Hakuna ubishi waandishi wa habari wana nafasi kubwa sana ya
kuipatia jamii viongozi bora na sio bora viongozi, kama wataweka mbele
uzalendo na kuacha kuchukua hongo kutoka kwa wagombea kwenye Uchaguzi
Mkuu wa 2015.
Nafahamu wapo waandishi wengi wenye uadilifu,
lakini kwa sababu kwenye msafara wa mamba na kenge wamo, si ajabu kukuta
ambao njaa yao ya muda mfupi inatupatia viongozi wabovu.
Kipindi cha uchaguzi ni wakati ambapo baadhi yetu
tunajulikana thamani zetu. Wapo wa Sh20,000, wengine Sh50,000, pia wa
Sh100,000 na wale wanaopewa hongo zaidi ya kiasi hicho.
Hongo hizi wanazopokea ili kumpamba mgombea kuliko
uhalisia wake, zimekuwa na athari kubwa kiuchumi, kisiasa na kijamii
ikiwamo kupata viongozi wasiofaa na wanaotanguliza masilahi yao binafsi
mbele.
Sote tunafahamu Uchaguzi Mkuu wa 2005 na 2010
namna ambavyo tuliwapamba baadhi ya wagombea wakiwamo wa ubunge,
tukawaaminisha wapigakura wakawachagua, lakini leo wanajuta. Natamani
utaratibu ule wa zamani urejee, kwamba kama wananchi walikuwa na hitaji
la kiongozi walimtafuta wenyewe na kumuomba ili agombee, leo mtu
anagombea tena kwa kuhonga wapigakura.
Mwaka huu huenda tukawa na uchaguzi wa Serikali za
mitaa, lakini mwakani tukawa na uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na
madiwani watakaotuongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Ni kipindi ambacho thamani ya waandishi wa habari
hupanda kwa kipindi kifupi sana na kisha wanasiasa wakishaingia
madarakani, huwatelekeza kama mafundi wanavyotumia karai la zege.
Nafahamu asilimia 75 ya wanahabari wote nchini ni
wa kujitegemea ambao kimsingi wanalipwa kulingana na habari ama makala
zitakazochapwa au kutangazwa na vyombo vya habari.
Ni ukweli malipo haya ni kidogo, lakini hiyo
haiwezi kuhalalisha baadhi yetu kujiingiza katika vitendo vya kupokea
hongo kutoka kwa wagombea ili tu wawaandike vizuri hata kama hawafai.
Maadili ya Uchaguzi Mkuu 2010 kwa wanahabari
yaliweka sharti la lazima kwa wanahabari kuwahabarisha na kutoa elimu ya
uraia kwa wapigakura ili wafanye uamuzi sahihi wakati wa kupiga kura.
Uamuzi sahihi ni kwa wapigakura kuchagua viongozi
bora na siyo bora viongozi kwa sababu tu amepandishwa chati na
wanahabari wakati dhamira yake ni kwenda kuchuma na si kusaidia jamii.
Wakati tunajiandaa na chaguzi nilizozisema, tayari
wapo wagombea ambao wamekuwa ‘mzigo’ lakini wanajiandaa kufanya kila
njia ili waweze kurudi tena bungeni kwa kipindi kingine.
Kuna taarifa zisizo rasmi baadhi yao wametenga hadi Sh200
milioni na sehemu ya fedha hizo imetengwa kwa ajili ya wanahabari
wasioheshimu maadili ili wawasafishie njia hata kama hawafai.
Wanahabari tunapaswa kuanza kujitafakari sasa kama
tumefanya nini kulisaidia taifa kupata viongozi bora, wazalendo na
wenye dhamira ya dhati ya kuwaletea Watanzania maendeleo.
Haiwezekani leo hii tuna rasilimali kibao kuanzia
madini ya kila aina, vivutio vya utalii, nishati ya gesi, wingi wa
misitu na mazao ya baharini lakini Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi
maskini.
Hapa ni lazima tutafakari kauli ya Baba wa Taifa,
Hayati Mwalimu Julius Nyerere kuwa ili nchi iendelee inahitaji vitu
vinne navyo ni ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. Ninasema
tutafakari ni kipi tunachokikosa kati ya vitu hivyo vinne hadi
Watanzania waendelee kuwa maskini licha ya kuwa moja ya nchi
zinazoongoza barani Afrika kwa kuwa na rasilimali nyingi.
Hakuna ubishi tuna tatizo la uongozi ndio maana
hatufiki kule tunakotaka kwenda na wanahabari wanalo jukumu zito la
kuirudisha nchi hii kwenye mstari.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment