Home » » WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUWADHIBITI MAKANJANJA

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUWADHIBITI MAKANJANJA

Na Nathaniel Limu, Singida
KLABU za waandishi wa habari nchini, zimetakiwa kuweka utaratibu madhubuti wa kuwadhibiti watu wanaofanya kazi ya uandishi wa habari bila kuwa na taaluma ya uandishi wa habari, maarufu kama makanjanja.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Yahaya Nawanda, wakati akifungua mkutano mkuu wa Katiba wa Klabu ya Waandishi wa Habari, Mkoa wa Singida, uliofanyika Mjini Kiomboi.

Nawanda alisema kwamba, kumekuwapo na wimbi kubwa la watu kujiingiza kwenye uandishi wa habari bila kuusomea na kwamba, hali hiyo inasababisha ukiukwaji wa maadili katika tasnia hiyo.

Pia alisema kwamba, kitendo cha watu hao kujiingiza katika taaluma hiyo, kinakuwa chanzo cha uwepo wa habari zilizopotoshwa kwa kuwa wahusika hawajui miiko na maadili ya uandishi wa habari.

“Taaluma ya habari ni taaluma muhimu sana duniani, huwezi kujiingiza katika taaluma hii na kuanza kuandika mambo ambayo huyajui na kama unayajua unayaandika bila kufuata maadili ya taaluma yenyewe.

“Hili ni kosa kubwa ambalo haliwezi kuvumiliwa na mtu yeyote na ili kuondokana nalo, lazima kuna haja ya uwepo wa nguvu za pamoja kutoka kwa kila anayehusika,” alisema Nawanda.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuna haja kwa klabu za wanahabari kuweka utaratibu wa kudhibiti tatizo hilo, ili kuhakikisha kuwa taaluma ya habari inakubalika na kuheshimika na jamii kutokana na umuhimu wake.

Alisema kuwa, kitendo cha kuwaacha baadhi ya watu wasiokuwa na taaluma waendelee kuitumikia taaluma hiyo, kunaifanya kazi hiyo ionekane kuwa ni kazi inayoweza kufanywa na mtu yeyote tena kwa ubabaishaji.

Klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Singida, yenye wanachama 25, hivi sasa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002, imefanya marekebisho ya katiba yake, ili iweze kuendana na wakati.

Pamoja na malengo hayo, marekebisho yamefanywa ili kuziba mianya ya watu wanaotaka kuitumia taaluma hiyo vibaya, kwa kuwa wanaweza kuhatarisha amani ya nchi.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa