WATU 12 wamekufa na wengine 22 kujeruhiwa katika ajali iliyotokea
kijiji cha Ighuka wilayani Ikungi kwenye Barabara Kuu ya Singida –
Manyoni baada ya Toyota Hiace walimokuwa wakisafiria kutoka kumchukua
bibi harusi kugongana uso kwa uso na Toyota Noah iliyokuwa imepakia watu
kutoka msibani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Debora Magiligimba alisema kuwa
ajali hiyo ilitokea juzi saa mbili usiku kwa kulihusisha gari lenye
namba za usajili T 581 BBV iliyokuwa ikitokea Singida kwenda Manyoni na T
423 CFF iliyokuwa ikitokea Manyoni kwenda Singida.
Alisema kuwa ingawa uchunguzi wa kina juu ya chanzo cha ajali hiyo
bado unaendelea, taarifa za awali zinaonesha kuwa sababu kuu ni mwendo
kasi na uzembe wa madereva.
“Baadhi ya majeruhi walituambia dereva wa Toyota Hiace aliyekuwa
anatoka Singida mjini alihama kutoka upande wake na kwenda upande wa
pili wa barabara ambako aligongana uso kwa uso na Noah iliyokuwa imebeba
watu waliokuwa wakitoka msibani na kusababisha vifo vya abiria 10 hapo
hapo na majeruhi 24,” alisema.
Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa mkoa wa Singida, Dk Ng’hungu
Kusenza alisema kuwa majeruhi wawili waliofikishwa Hospitali ya Misheni
Puma kwa ajili ya matibabu pia walikufa hivyo kufanya idadi ya watu
waliokufa kuwa 12.
Aliwataja waliokufa ambao miili yao imehifadhiwa Hospitali ya mkoa
kuwa ni John Duma, Jasson Nsunza, Abubakar Omari, Mary Kinku, Mwanaidi
Juma na Husna Juma, Wengine ambao miili yao imehifadhiwa Hospitali ya
Misheni Puma wilayani Ikungi ni Ezekiel Joseph, Mussa Daniel, Namtaki
Daniel, Hamis Omari, Jumanne Mganga na Wansola Shalua. Habari ambazo
hazijathibitishwa zinadai kuwa Bwanaharusi na madereva wa magari yote
mawili ni miongoni mwa watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment