Madereva
wa vyomo vya moto hasa bajaji na bodaboda wamewahimizwa kujiunga na
chuo kikuu huria ili waweze kujiendeleza kielimu na kuboresha huduma
zao, ambapo kwa kufanya hivyo watasaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa
ajali za barabarani.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi ametoa wito huo juzi wakati
akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama
barabarani yaliyofanyika kwenye kituo cha zamani cha mabasi cha Mjini
Singida.
Amesema
masomo ya chuo kikuu huria humwezesha mtu kujiendelea kwa kupata elimu
bora bila kuathiri shughuli zake za kila siku hasa za kujipatia kipato.
“Dereva
wa bodaboda, bajaji au mkazi yeyote mkoani kwetu, tusiridhike na elimu
tuliyonayo, kumbukeni elimu haina mwisho. Hivyo tutumie chuo chetu hiki
cha huria kujiendeleza kielimu. Tukiwa na wasomi wengi mkoa wetu kwa
vyovyote lengo la kuwa na uchumi wa kati na chini ya viwanda utalifikia kwa haraka”, amesema.
Dkt
Nchimbi amwataka madereva wa vyombo vya moto kutii na kuzingatia sheria
za usalama barabarani ili kuepusha ajali na sio tu kuendeshwa na kamera
za barabarani.
“Baadhi ya madereva wa vyombo vya moto, hawaheshimu kabisa sheria za usalama barabarani, wanaendeshwa na kamera.
Siku moja yupo dereva mmoja wa bodaboda alikuwa mbele yangu, huku
akiandika ujumbe kwenye simu yake. Utamaduni huu haufai kwa sababu ni
chanzo cha ajali”,amesema Dkt.Nchimbi.
Aidha
amemtaka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP Debora Magiligimba
kusimamia zoezi la madereva wa bajaji na bodaboda kujiunga na Chuo kikuu
Huria.
“Hebu
angalia uwezekano wa kuanzisha mfuko maalumu kwa ajili ya madereva hawa
kujiendeleza kielimu. Tunataka ifike siku tuwe na madereva hawa wana
diploma au digrii, kwa hili nina imani na wewe utaweza kuwasaidia
vizuri”, amesema.
Wakati
huo huo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amesema atagharamia
safari ya viongozi wa madhehebu ya dini kwa kutoa kiasi cha shilingi
laki tano, kwenda kufanya sala maalum kwenye maeneo yaliyokidhiri kwa vitendo vya ajali.
“Karibu
kila wilaya ina eneo ambalo ajali haziishi kutokea mara kwa mara. Nina
imani Mungu hajanipa mkoa wenye maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajali.
Nimekubaliana na viongozi wangu wa madhehebu ya dini
wataenda katika maeneo hayo, na kuomba Mungu atuondolee balaa la ajali
za barabarani kwenye maeneo hayo” amesema.
Kwa
upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP Debora Magiligimba
amewaagiza viongozi wa madereva wa bodaboda na bajaji, kusimamia vema
madereva hao ili wapunguze ajali za barabarani.
Mmoja kati ya wakazi wa Manispaa ya Singida, Njolo Kidimanda, amesema kuwa kuna haja serikali kuongeza kiwango cha faini kwa madai kiwango kilichopo, hakiwaogopeshi kabisa baadhi ya madereva.
Aidha,
Kidimanda ameshauri madereva kuwa mstari wa mbele katika kuchangia damu
salama, ili kusaidia majeruhi wa ajali barabarani wenye hitaji la damu.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida,
jumla ya watu 68 wamefariki kutokana na ajali za barabarani kati ya
Januari hadi Oktoba mwaka huu. Idadi hiyo imeonyesha kupungua kwa vifo
vitokanavyo na ajali za barabarani kwa kuwa katika kipindi hicho hicho mwaka jana, watu 152 walifariki.
0 comments:
Post a Comment