Picha/habari na Nathanieli Limu-Singida
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassimu Majaliwa Kassim amesema
kuna haja ya kuangalia upya mfumo wa elimu ya juu nchini ili kuuboresha
uweze kusaidia kutayarisha haraka rasilimali watu walioelimika zaidi,
watakaoliwezesha taifa kuwa na maendeleo na kufikia uchumi wa kati
ifikapo mwaka 2025.
Waziri
Mkuu Majaliwa ameyasema huyo jana wakati akizungumza kwenye kilele cha
mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu huria cha Tanzania yaliyofanyika kwenye
viwanja vya Kanisa Katoliki mjini Singida.
“Kwa
kuzingatia malengo ya dira ya taifa ya maendeleo na mwelekeo wa
serikali ya awamu ya tano, napenda nisisitize kuwa dira ya utendaji wenu
ijikite katika maeneo yaliyoainishwa chini ya mwamvuli wa kauli mbiu ya
chuo-elimu bora na nafuu kwa wote”, amesema.
Amesisitiza
kwa kusema kwa uchumi wa kati na wa viwanda, hauwezi kufikiwa au kuwa
endelevu pasipo kuwa na kiwango cha udahili katika elimu ya juu cha
angalau asilimia 23.
“Hivi
sasa kiwango cha Tanzania cha udahili katika elimu ya juu ni aslimia
nne (4). Kiwango hiki ni kidogo hata kuliko nchi kama Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo ambao licha ya hali ya vita nchini mwao kwa muda
mrefu,wamefikia asilimia saba (7)”,amefafanua.
Waziri
Mkuu Majaliwa amefafanua zaidi kwa kusema kuwa takwimu zinaonyesha
kwamba karibu nchi zote washiriki katika jumuiya ya Afrika mashariki,
ukiacha Burundi, zina viwango vya juu zaidi vya udahili katika elimu ya
juu ikilinganishwa na kiwango cha Tanzania.
Amesema
kwa mujibu wa sera ya elimu ya mwaka 2014 mfumo wa elimu na mafunzo
umetawaliwa na muundo wa kitaaluma wenye dhana ya kuchuja wahitimu kwa
kila ngazi ili kupata wachache wenye uwezo mkubwa katika taaluma.
“Hali
hii inatokana na nafasi za elimu na mafunzo ngazi za juu kuwa chache
kadri wanafunzi wanavyohitimu kuanzia ngazi ya elimu ya msingi
na kuendelea. Kwa uhaba wa nafasi za elimu ya juu na ufinyu wa bajeti
ndio unaosababisha kutumia muundo wa kuchuja badala ule wa kutoa
fursa kulingana na uwezo, vipaji na vipawa”, amesema na kuongeza;
“Huu
ndio mfumo ambao unahitaji kuhuishwa na mfumo wa elimu huria na masafa
kama alivyoeleza Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia Profesa Joyce
Ndalichako kwamba mazingira, vigezo na masharti ya mchakato huu
vimeainishwa katika sera ya elimu na mafunzo 2014’.
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali inaunga mkono azma ya
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya kuanzisha dawati maalum kwa
ajili ya kuimarisha mfumo wa elimu huria na masafa.
“Kupitia
hafla hii, ninaagiza dawati kama hili lianzishwe pia katika Tume ya
vyuo vikuu (TCU) na Baraza la elimu ya ufundi (NACTE), kwa lengo la
kuhakikisha kuwa taratibu zao za ithibati zinazingatia na kukidhi
matakwa ya viwango vya mfumo wa elimu huria na masafa”, amesema.
Katika
Mahafali hayo Mkuu wa Chuo Kikuu Huria na Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo
Peter Pinda amemtunuku shahada ya heshima ya uzamivu Balozi Nicolous
Kuhanga ambaye mchango wake umetajwa kuwa mkubwa hasa wakati wa
kuanzishwa kwa chuo hicho.
Zaidi
ya wahitimu 2200 wamehitimu katika Chuo Kikuu hicho na kutunikiwa
shahada mbalimbali ambapo mke wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Mama Mary
Majaliwa, amekuwa miongoni mwa wahitimu akitunukiwa shahada ya uzamili
katika Elimu ya Utawala, Mipango na Sera.
0 comments:
Post a Comment