Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi ameshauri Mpango wa Kunusuru Kaya
Masikini (TASAF) uanzishe kazi za ajira za muda, kwa walengwa wa Mpango
huo kutoka jamii ya Wahadzabe waliopo Wilayani Mkalama ili uwasaidie
kuinua uchumi wao.
Dkt
Nchimbi ametoa ushauri huo mara baada ya kutembela kijiji cha Singa
Wilayani Mkalama na kuona bwawa litakalotumika kuhifandhi maji ya mvua
kwa ajili ya shughuli mbalimbali lililojengwa na walengwa wa Tasaf
Kijijini hapo kisha kutembelea kijiji cha Munguli Kata ya Mwangeza
Wilayani humo aliposhuhudia malipo ya walengwa wa kihadzabe wa Mpango wa Tasaf.
Ameeleza
kuwa jamii ya wahadzabe hawana mradi unaohusisha kazi za ajira za muda
ambazo zimekuwa zikisaidia katika kuongeza kipato, kuwafundisha thamani
ya kazi pamoja na kutekeleza miradi ambayo imekuwa ikisaidia jamii nzima
kama vile mabwawa na barabara.
“Nashauri
TASAF kabla ya msimu huu wa mvua kuisha muwaletee na hawa wahadzabe
mradi wa ajira za muda kama ambavyo walengwa wa vijiji vingine wamekuwa
wakifanya kazi hizo na zimekuwa zikichangia maendeleo kwa vijiji vyao”,
ameeleza na kuongeza kuwa,
“Miradi
ya ajira za muda zitawafundisha Wahadzabe kujituma kufanya kazi ambazo
zinachangia maendeleo ya jamii huku kazi hizi zikiwa kama darasa la wao
kujifunza kwa vitendo kuwa kama anaweza kwa mfano kushiriki kujenga
bwawa basi anaweza kufanya jambo kubwa katika familia au maisha yake”,
amesisitiza Dkt Nchimbi.
Aidha
ametoa tahadhari kwa walengwa hao wa kihadzabe kuwa wasitumie pesa
wanayopewa kwa kunywa pombe badala yake pesa hiyo itumike sawasawa na
maelekezo ya mpango huo na hatua zichukuliwe kwa wale watakaokaidi.
Kwa
upande wake Afisa Ufuatiliaji Kutoka Tasaf Makao Makuu Anna Njau ambaye
aliambatana na Mkuu wa Mkoa Dkt Nchimbi katika ziara yake ameeleza kuwa
ushauri huo ni mzuri na una lengo la kuwasaidia wananchi kama ambavyo
Tasaf imekuwa na lengo la kuinua jamii hasa kaya masikini hivyo wazo
hilo ataliwasilisha makao makuu kwa ajili ya utekelezaji.
Baadhi
ya wahadzabe waliofika kupokea fedha za Mpango wa Tasaf wameeleza kuwa
fedha hizo zimewasaidia kuwainua kiuchumi kwa kuhakikisha wana chakula
cha kutosha, watoto wameenda shule, watoto wadogo wamepelekwa kliniki
huku wakijiendeleza zaidi kiuchumi kwa ufugaji mdogo wa kuku na mbuzi
pamoja na kuboresha makazi yao.
Jamii
ya Wahadzabe waliopo Kijiji cha Munguli na hasa kitongoji cha Kipamba
Wilayani Mkalama wamekuwa wakiishi kwa kutegemea uwindaji wa wanyama
pori, kula asali, ubuyu, matunda na mizizi mbalimbali ambapo juhudi za
Serikali kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (Tasaf) umesaidia
jamii hiyo kuanza kupeleka watoto shule, kuanzisha shughuli za
uzalishaji mali kama vile kilimo na ufugaji.
0 comments:
Post a Comment